Featured

Masheikh wana wajibu wa kuisaidia jamii katika kukuza elimu

Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar akiufungua  Msikiti wa Kijiji cha Kajengwa utakaotoa huduma za ibada za sala na madrasa kwa waumini wa Kijiji hicho.
Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar akiufungua Msikiti wa Kijiji cha Kajengwa utakaotoa huduma za ibada za sala na madrasa kwa waumini wa Kijiji hicho.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Wanazuoni, Masheikh na wazee wote nchini wana wajibu mkubwa wa kuisaidia Serikali Kuu katika jitihada zake za kukuza elimu, kujenga jamii iliyo bora, kulinda amani pamoja na kukataza maovu vikiwemo vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – hajj Dr. Ali Mohamed Shein wakati akiufunguwa msikiti wa Kijiji cha Tasani  Makunduchi unaokadiriwa kusaliwa na waumini wapatao 200 kwa wakati mmoja wa sala.

Dr. Shein ambae Hotuba yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema katika msaada huo Masheikh wana fursa nzuri ya kuzungumza na waumini wao hasa kupitia hotuba za sala za ijumaa ili kujenga jamii iliyo bora.

Alisema Dini imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa zaidi kwenye suala zima la kukuza maadili mema , malezi ya watoto sambamba na kuendeleza hali ya kuishi kwa upendo miongoni mwa jamii  yote.

Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali imedhamiria kutilia mkazo mfumo wa Utawala bora unaozingatia utii wa sheria na kuendeleza mikakati katika kuimarisha uwajibikaji kwa kupiga vita ubadhirifu wa mali za umma.

Alifahamisha kwamba uimarishwaji wa mafunzo ya dini katika misikiti na hata madrasa una mchango mkubwa katika kuisaidia Serikali kuimarisha lengo lake hilo la usimamizi wa Utawala bora pamoja na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Al Hajj Dr. Ali Mohamed Shein amewapongeza Waumini na Wananachi wa Makunduchi kwa jitihada zao walizochukuwa na hatimae kufanikiwa kupata nyumba mpya ya Ibada.

Alisema Jamii imekuwa  ikushuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa misikiti mikubwa yenye nyenzo za kisasa katika pembe zote za Visiwa vya Unguja na Pemba neema ambayo Mwenyezi Muungu anaendelea kuishusha ndani ya Nchi hii.

Alieleza kwamba ujenzi wa Misikiti mipya ni ishara ya kuendelea kwa imani na mapenzi baina ya waislamu pamoja na kuongezeka kwa nguvu za kiuchumi miongoni mwa wananchi.

Dr. Shein aliikumbusha jamii kujitokeza zaidi katika kuwekeza katika mambo ya kheri kama hili la ujenzi wa misikiti ili kujitengenezea maisha bora ya baadaye na kuachana haya ya duniani ambayo ni ya mpito.

“ Na simamisheni sala na mtoe zaka na mkatieni Mwenyezi Muungu sehemu njema { katika mali yeni iwe ndio zaka na sadaka } na kheir yoyote mnayoitanguliza kwa ajili ya nafsi yenumtaikuta kwa mwenyezi mungu imekuwa bora zaidi na ina thawabu kubwa sana “. Dr. Shein aliikariri suratul Muzzammil aya ya 20.

Alisema ni vyema kwa waliojaaliwa uwezo kuangalia maeneo wanayoishi namna bora ya kutoa sadaka inayoendelea katika kupitia usambazaji wa huduma zinazohitajika na jamii iliyowazunguuka.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitekeleza dhamira ya kuhakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma muhimu katika maeneo wanayoishi.

Hata hivyo alisema zipo sababu tofauti zinazochangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wananchi kuendelea kukosa huduma hizo muhimu kwa maendeleo yao ya kijamii ya kila siku.

Aliwapongeza waislamu wote waliochangia pamoja na kushiriki kwenye ujenzi wa msikiti huo juhudi ambazo lazima ziambatane na kuendelea kuutunza  msikiti huo ili uendelee kubakia katika haiba yake ya kupendeza.

Katika kuunga mkono juhudi za waumini hao Balozi Seif  Ali Iddi Binafsi aliahidi kusaidia pampu ya kusukumia maji katika msikiti huo mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mnara wa tangi la maji.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alilifungua jengo la Madrasatul Shafiat liliopo katika Kijiji cha Kajengwa Makunduchi.

Akizungumza na waumini hao Dr. Shein alisema ufunguzi wa madrasa hiyo ni kielelezo cha jitihada za wananchi wa kajengwa kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutilia maanani haja ya kuwapatia elimu ya dini watoto wao jambo ambalo limefaradhishwa na mwenyezi mungu.

Alisema elimu nizawadi na urithi bora kwa watoto ambao huwajenga kuwa na ucha mungu, kujua utu, kuheshimu haki za watu wenye  imani za dini nyengine sambamba na kumtukuza mola anayeteremsha neema kwa viumbe wote.

Alitoa wito kwa uongozi wa Madrasatul Shafiat kufanya juhudi za makusudi kuisajili Madrasa hiyo ili ifuate taratibu zilizopo pamoja na kutambulika rasmi kiserikali.

Alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kupitia kitengo kinachosimamia elimu ya maandalizina madrasa huzisajili madrasa ili kuzitambua , kusimaia taaluma inayotolewa , kuzipatia misaada ya kitaaluma vikiwemo pia vifaa.

Katika juhudi za kuunga mkono waumini hao wa Kajengwa Makunduchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein aliahidi kuchangia mafeni yote ya Madrasat Shafiiya, Meza ya Mwalimu, pamoja na Makabati ya Vitabu vya Madrasa hiyo.

Akisoma risala ya walimu na Wanafunzi hao wa Madrasat Shafiiya Mwalimu Abou Simai Mussa alisema madrasa hiyo yenye wanafunzi karibu 150 inatoa mafunzo ya elimu ya Dini na Dunia.

Mwalimu Abou alisema madrasa hiyo hivi sasa imekuwa chem chem. Kubwa ya utoaji wa walimu na masheikh mbao wamekuwa wakitoa mafunzo ya kuongoza ibada katika misikiti mbali mbali ya Jimbo la Makunduchi.

Alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi kwa jitihada zake za kuchangia ujenzi wa msikiti huo zilizofikia zaidi ya asilimia 99% ukigharimu zaidi ya shilingi Milioni 21.3.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi na waumini hao wa Jimbo la Makunduchi Mwakilishi wa Jimbo Hilo Al Hajj Haroun Ali Suleiman alisema Uongozi wa Jimbo hilo utaendelea kushirikiana na wananchi hao katika kuhakikisha kwamba kero zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Al – Haroun alisema tatizo la huduma za maji safi na salama ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi hao hasa katika eneo la ibada la Msikiti atalishughulikia kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa jimbo hilo.

Mapema Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali aliwakumbusha waumini hao kwamba Madrasa lazima zitumiwe kwa juhudi zote katika kujenga hatma njema  ya dunia na sfari ya milele.

Featured

DUNI: Mahujaji hawakuipigia kura katiba inayopendekezwa

Wanachama wa Chama cha Wananchi CUF wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho , Mh, Juma Duni Haji (hayupo pichani) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Amani kwa mabata.
Wanachama wa Chama cha Wananchi CUF wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa Chama hicho , Mh, Juma Duni Haji (hayupo pichani) katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Amani kwa mabata.

Na Nassor Khamis.
Suala la wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliokuwa kwenye ibada ya Hijja katika miji ya Makka na Madina chini Saudi Arabia, kupigia kura rasimu ya katiba inayopendekezwa na Bunge hilo sikweli.

Hayo yalielezwa na Makamo mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF taifa Mh, Juma Duni Haji wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya Amani kwa mabata wilaya ya Magharibi Unguja.

Mh, Duni ambaye pia ni Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisema, kulingana na hali ilivyokuwa katika ibada ya hijja ni vigumu kwa wajumbe hao kupiga kura kwa njia yoyote kutokana na muda wote kuwa katika ibada.

“Suala la kupigwa kura kwa njia ya mtandao ni uongo kwani hakuna hata mtu mmoja aliyepiga kura kutokana na muda wote kuwa katika ibada” alisema Mh, Duni

“Mimi nilikuweko wakati tupo katika mabanda yetu mahujaji nilimuuliza mmoja wa wajumbe vipi ndio utapigia kura katiba hapa” aliongezaMh. Duni.

Pia alisema kuwa licha ya mahujaji hao kushindwa kupiga kura kwa njia ya mtandao, hakuna afisa yoyote aliyeweza kuendesha zoezi la upigaji kura kutokana na kutokuruhusiwa kuingia kwa mtu yoyote asiyekuwa mwenye kufanya ibada hiyo ya hijja.

Aidha amesema kuwa kutoka na mahujaji hao kutokupiga kura na wengine waliyoikata hadharani theluthi mbili ya wazanzibari ya kupitisha katiba inayo pendekezwa haikutimia.

Akizungumzia Katiba inayopendekezwa alisema, katiba hiyo haina maslahi kwa Zanzibar kwani Katiba inayopendekezwa inafuta utambulisho wa Zanzibar pamoja na kuinyima Zanzibar mamlaka yake ya kujiendesha wenyewe.

Alisema kuwa baadhi ya vipengele vinavyoonyesha kuipa mamlaka Zanzibar ni sawa na kupewa kitu kwa mlango wa mbele na kisha kunyang’anywa kwa mlango wa nyuma kwani vipengele hivyo vipo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vipengele hivyo amevitaja kuwa ni pamoja na Zanzibar kujenga mashirikiano na mashirika ya kimataifa pamoja na uwezo wa kukopa fedha kutoka taasisi mbali mbali za kifedha hadi ipate udhamini kutoka kwa Serikali ya Muungano.

“Eti wanasema sasa Zanzibar inaweza kukopa pamoja na kujiunga na mashirika ya kimataifa baada yakupata udhamini ikiwa huo udhamini haukutolewa pamepatikana kitu hapo?” alihoji Mh, Duni.

Pia alisema kuwa kutokana katiba mpya inayopendekezwa kubainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atachaguliwa kwa kupata zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote ni vigumu kwa Mzanzibari yoyote kushika wadhifa huo kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura walioko Tanzania Bara.

Alisema kuwa ili kupata uhalali wa Rais wa Muungano, Katiba inayopendekezwa iweke kifungu kinacho onesha kiwango maalum cha kura kutoka kwa wapiga kura wa pande zote za Muungano.

Mh. Duni pia alizungumzia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji unaofanywa na jeshi la polisi kwa watuhumiwa makosa ya ugaidi huku viongozi wa serikali wakikaa kimya, ni kushindwa kusimamia haki za wananchi wanaowaongoza.

Akitolea mfano wa vitendo vya udhalilishaji kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali yaliyowahi kufanyika huko nyuma askari waliofanya vitendo hivyo walichukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufukuzwa kazi.

Amesema kuwa wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa Jamhuri Muungano wa Tanzani vitendo vya udhalilishaji wa watuhumiwa waliokuwa mahabusu jijini Mwanza Mwalimu Nyerere aliwawajibisha maafisa wa jeshi la polisi kwa kuwafukuza kazi huku aliyekuwa Waziri wa Mambo ya ndani wakati huo Mzee Ali Hassan Mwinyi kulazimika kujiuzulu wadhifa wake.

“leo wanakuja raia mahakamani wanaonesha suruali zinavyovuja chini kutokana na vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa na Polisi wewe husemi kitu Rais gani wewe” alisema Mh. Duni.

Aidha mh, Duni ametaka sheria zilizotungwa zifuatwe kama inavyostahiki pamoja na kuheshimiwa na watu wote.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mh, Nassor Ahmed Mazruy alisema kifungu cha thalathini na nne cha sheria ya mabadiliko ya katiba inayosema kuwa katiba inayopendekezwa itapitishwa kwa zaidi ya asilimia hamsini ya kila upande kimelenga kuchakachua kura za maoni ya kupitishwa kwa katiba hiyo.

Alisema kuwa kifungu hicho pia kinawataka Wazanzibari walioko Tanzania Bara kupiga kura upande wa Zanzibar jambo ambalo haliingia akilini na ina lengo la kuvuruga idadi ya wazanzibari ili waweze kupitisha katiba hiyo.

Aidha alisema kuwa chama cha CUF pamoja na vyama vyengine vya upinzani vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA kwa pamoja wamesaini mkataba wenye lengp la kushirikaiana katika chaguzi mbalimbali ukiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa lengo la kuindoa CCM madarakani.

Mapema Mjumbe wa Baraza kuu la Uongozi la CUF Taifa ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mh, Hamad Massoud Hamad amewataka wanachama wa chama hicho kujiweka tayari kwa uchaguzi mkuu ujao kwa lengo la kuiondoa CCM madarakani.

Amesema kuwa uchaguzi unaofuata chama cha CUF hakitofanya makosa kama chaguzi zilizopita kwa kukubali matokeo yasiyo halali yanayo tangazwa na tume ya uchaguzi Zanzibar kwa kutoa ushindi usiostahiki kwa CCM.

“Uchaguzi wa safari hii CUF haifanyi makosa kama yaliyopita viongozi wa juu tayari wameshajiandaa na nyinyi wananchi jiandaeni tuhakikishe tunaing’oa madarakani CCM ifikapo mwakani” alisema Mh, Hamad huku akishangiriwa na wanachama waliohudhuria mkutano huo.

Featured

Wazanzibari watakiwa kuipigia kura yandio Katiba inayopendekezwa

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar Dkt, Ali Mohammed Shein (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara Kibanda maiti mjini Unguja.
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar Dkt, Ali Mohammed Shein (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara Kibanda maiti mjini Unguja.

Na Nassor Khamis, Zanzibar.
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuipigia kura ya ndio Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba kwani imezingatia maslahi ya Zanzibar ikiwamo masuala ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja.
Dkt. Shein ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mnzi Mapinduzi amesema katiba inayopendekezwa imetatua kero zote za Muungano zilizokuwepo na kuzitafutia ufumbuzi ikiwamo kero ya muda mrefu kuhusu suala la mafuta na gesi.
Amesema kuwa suala la mafuta na gesi limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaka litolewe katika orodha ya mambo ya Muungano ili Zanzibar iweze kukua kiuchumi.
“Suala hili la mafuta na gesi limekuwa likizungumzwa kipindi kirefu na serikali ya Zanzibar tokea nikiwa Makamo wa Rais kule bara na likakubaliwa litolewe na mimi nilipokukuja nimekuta limekubaliwa na mimi nikakubali” alisema Dkt. Shein.
Amesema kuwa kupitia katiba inayopendekezwa suala la hilo tayari limesahatolewa na kuwa chini ya mamlaka ya serikali ya mapinduzi Zanzibar ili kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua kiuchumi.
Amesema kuwa makampuni kadhaa ya mafuta yakiwemo kutoka Uholanzi na Ras Al-khaimah yameonesha nia ya kufanya utafiti wa mafuta katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na hatimae kuyachimaba na tayari makubaliano ya awali ya kazi hiyo yamefikiwa.
Mbali na suala hilo Dkt Shein amezungumzia maswala ya ushirikiano wa Zanzibar na taasisi pamoja na Mashirika ya kimataifa kuachwa katika mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jambo litakalo saidia katika maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Aidha amesema kuwa, kupitia katiba inayopendekezwa Zanzibar imeruhusiwa kukopa fedha katika mashirika na taasisi mbalimbali ikiwemo kupata udhamini wa Serikali ya Muungano pale itakapohitajika na itapatiwa udhamini huo.
Akizungumzia mchakato wa katiba mpya Dkt. Shein amesema mchakato huu umeendeshwa kawa mashirikiano makubwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea uundwaji wa sheria ya mabadiliko ya katiba hadi hatua iliyofikia.
Pia amewataka wananchi kuendeleza amani iliyopo na wasikubali kugawiwa kwa misingi ya katiba mpya kwani katiba inayoandikwa imetokana na makubaliano ya pande zote.
Pia amesisitiza kuwa serikali haitafumbia macho vitendo vyovyote vinavyo ashiria uvunjifu wa amani na itailinda amani ya nchi kwa gharama yoyote.
Nae Waziri wa fedha na uchumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Saada Salum Mkuya amesema katiba inayopendekezwa imezingatia maslahi ya Zanzibar katika masuala yote yakifedha ikiwemo mapato ya serikali yatokanayo na kodi ya mambo ya Muungano.
Amesema kuwa mapato yote yanayokusanywa kama kodi ya mfanya kazi wa taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar yatabakia katika serikali ya Zanzibar kwa maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh, Samia Suluhu Hassan amesema katiba inayopendekezwa imetoa fursa sawa za kiuongozi kati ya Tanzania bara na Zanzibar hasa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani endapo Spika wa Bunge hilo akitoka bara Naibu wake atatokea Zanzibar.
Mh, Samia ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais anaeshughulikia Muungano amesema, inayopendekezwa imetoa fursa kwa wanawake kwa kutoa haki sawa katika nafasi zote za uongozi wa nchi kwa asilimia hamsini kwa hamsini baina ya wanawake na wanaume pamoja haki ya uzazi salama kwa kina mama.
Mapema akizungumza katiaka mkutano huo Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Mzee Hamid Ameir amemtaka Mzee Hassan Nassor Moyo aache kuwapotosha Wazanzibar kuhusu Mapinduzi ya 1964 kutokana nakuwa hakuwa mshiriki wa Mapinduzi hayo.
Mapema katika Risala yao wanachama wa CCM wa mikoa minne ya kichama ya Unguja wameunga mkono mapendekezo yaliyomo katika Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba lililomalizika mwanzoni mwa mwezi huu mjini Dodoma.
Mkutano wa CCM umekuja baada ya mikutano miwili tofauti iliyofanywa na Chama cha Wananchi CUF hivi karibuni katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja na viwanja vya Gombani ya kale kisiwani Pemba.
Mikutano yote hiyo ilihutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho ambae pia ni Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi kadhaa wa Chama hicho.

Featured

Maalim Seif: Katiba inayopendekezwa inainyima mamlaka Zanzibar

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Zanzibar.

Na Nassor Khamis.

Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kupiga kura ya hapana kwa Rasimu ya katiba inayopendekezwa kutokana na kutozingatia maslahi ya Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja.

Akivizungumzia baadhi ya vifungu Maalim Seif amesema katiba inayo pendekezwa imepunguza mamlaka zaidi ya Zanzibar tofauti na ilivyoelezwa na wanaounga mkono katiba hiyo.

Amesema kuwa katiba inayopendekezwa imetoa mamlaka zaidi kwa Serikali ya Muungano kwa kusema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye mamlaka kamili hivyo kuinyang’anya Zanzibar mamlaka iliyo nayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar toleo la 2010.

Maalim Seif amesema kuwa Katiba ya Zanzibar inampa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika Mikoa na maeneo mengine ya kiutawala ambapo kwa sasa mamlaka hayo yamewekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha amesema kuwa rasimu hiyo bado haijatoa uhuru kwa Zanzibar kushirikiana na Mashirika na Jumuiya za kikanda pamoja na Kimataifa kutokana na mashirika hayo kutoa uwanachama kwa nchi zenye mamlaka kamili ya kiuongozi jambo ambalo kwa Zanzibar bado halijapatikana.

“Shirika kama la Chakula duniani, UNESCO na mashirika mengine hatoi uanachama kwa nchi ambazo hazina mamlaka ya kujiendesha wenyewe na kwa Katiba hii inaqyopendekezwa bado Zanzibar haijapata mamlaka kamili” alisema Maalim Seif.

Aidha amesema kuwa Rasimu iliyotolewa na Tume ya jaji Warioba ilipunguza idadi ya mambo ya Muungano kutoka 22 hadi kufikia saba badala yake Rasimu inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba imeyaongeza kutoka saba hadi 14.

Pia amesema kuwa Rasimu inayopendekezwa bado imeifanya Ta nganyika kuendelea kuvaa koti la Muungano kutokna na mambo yake yasiyokuwa ya Muungano kuendelea kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amesema kuwa katiba inayo pendekezwa imekosa uhalali wa kisheria kutokana na kutopatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar waliyoinga mkono rasimu hiyo wakati wa upigaji wa kura.

Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba Yahya Khamis Hamad wajumbe waliopiga kura ya ndio hawakufikia theluthi mbili badala yake matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na lengo la kuipitisha rasimu hiyo kinguvu kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha amesema kuwa endapo katiba inayopendekezwa itapitshwa itasababisha mgogoro wa kikatiba kutokana na na katiba hiyo kukinzana na katiba ya Zanzbar hivyo kulazimisha kufanyiwa marekebisho katiba ya Zanzibar jambo ambalo halitawezekana.

Amesema kuwa ili kuifanyia marekebisho katiba ya Zanzibar kutahitajika theluthi mbili ya Wajuumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunga mkono ambapo wajumbe watokanao na chama cha CUF hawatakubali jambo hilo kutokea.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mh, Nassor Ahmed Mazrouy amewataka Wazanzibar kuikataa katiba inayo pendekezwa pamoja na kuwakataa Wabunge na Wawakilishi wote waliopiga kura ya ndio kwa katiba inayo pendekezwa.

Naye Mjumbe wa kamati ya maridhiano Mansour Yussuf Himid amesema kuwa ataendelea kuitetea Zanzibar ipate mamlaka yake kamili hivyo ataendelea kupingana na mfumo wa Muungano wa CCM uliojaa ukatili dhidi ya Wanzibari.

Alisema kuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini mbali mbali vinaeleza kila nafsi itaonja mauti je wao wanaogopa nini kilichobakia ni kuingia mitaani kuwambia Wazanzibar wasikubali kuipitisha katiba hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Maridhiano Zanzibar,Mzee Nassor moyo alisema kuwa Wazanzibar waliungana na Tanganyika kwa hiari yao hivyo hakuna mtu yeyote wa kuwalazimisha kufanya mambo yanayokwenda kinyume na matakwa ya Wazanzibar.

Mapema mkurugenzi wa habari na uenezi wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema kuwa rasimu inayopendekezwa sio ya wazanzibar na haitofika Zanzibar bali itaishia Kisiwa cha Chumbe .

Na aliwataka wazanzibari kuungana pamoja na kuikataa kwa nguvu zote rasimu ya Chenge na wenzake kwani imekuja kuangamiza Zanzibar.

Featured

Kura ya hapana yatikisa Bunge Maalumu la Katiba

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta,  akiwaonyesha wajumbe wa bunge hilo, karatasi za kupigia kura zitakazotumika kupitishia vifungu vya Rasimu ya Katiba,  bungeni,Dodoma jana.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, akiwaonyesha wajumbe wa bunge hilo, karatasi za kupigia kura zitakazotumika kupitishia vifungu vya Rasimu ya Katiba, bungeni,Dodoma jana.

Wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba jana walianza kupiga kura za kuamua ibara za Katiba inayopendekezwa, huku kura za wajumbe kutoka Zanzibar zikiibua wasiwasi wa iwapo theluthi mbili itapatikana au la.

Dalili za kupiga kura za hapana kutoka upande wa Zanzibar zilianza kujionyesha mapema baada ya taarifa za ndani kueleza kuwa zikikosekana 10 kutoka upande huo wa Muungano hakuna katiba.

Hata hivyo, mapema Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alisema idadi ya kura zinazohitajika kukidhi theluthi mbili kwa upande wa Zanzibar ni 140 na jana jioni waliokuwamo bungeni walikuwa 142.

Mjumbe wa kwanza kufungua pazia kwa kura ya hapana alikuwa ni Adil Mohamed Adil aliyepiga ibara zote 157 kwa sura ya kwanza hadi 10.

Wengine waliopiga kura ya hapana kwa sura zote ni Dk Alley Soud Nasoro na Salma Said.

Waliopiga kura za hapana ni Fatuma Mohamed Hassan na Jamila Abeid Saleh, huku baadhi ya wajumbe wakipiga kura za siri.

Kwa upande wake, Ali Omary Juma, alikubaliana na sura za 2, 4, 5 na 9 lakini akizikataa sura za 1,3,6,7,8 na 10.

Kwa upande wa Tanzania Bara, wajumbe Abia Nyabakari na Dk Ave-Maria Semakafu walipiga kura za ndiyo kwa baadhi ya sura na zingine kuzikataa.

Mjumbe Ali Keissy Mohamed aliushangaza ukumbi kwa kupiga kura ya ndiyo kwa sura zote tofauti na wakati akiwa katika vikao vya kamati ambapo alikataa muundo wa serikali mbili.

Watakaopiga kura kwa faksi

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana alitangaza orodha ya wajumbe 22 wanaotarajiwa kupiga kura kwa njia ya faksi au mtandao wakiwa nje ya Bunge hilo.

Katika orodha hiyo, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, wajumbe tisa wako Saudi Arabia kwa ajili ya Hijja, wawili India kwa matibabu, mmoja yuko masomoni Uholanzi na wengine nje ya Dodoma lakini yuko hapa nchini.

Orodha ya wajumbe

Wajumbe walioko Uarabuni ni Dk Abdalah Kigoda, Mussa Yusuph Kundecha, Hamza Mustapha Njozi, Mohamed Raza, Dk Maua Daftari, Shawana Bukheri Salum, Asha Dodo Mtwangi, Amina Andrew Clement na Riziki Lulida.

Wajumbe walioko India kwa matibabu ni Beatrice Shelukindo na Salum Hassan Turk.

Wajumbe wengine waliko nje ya nchi ni Fredrick Msigala, Waziri wa Afya, Dk Seif Suleiman Rashid, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela.

Waliopo nchini ni Esther Bulaya, William Lukuvi, Profesa Esther Mwaikambo, Dk Athman Mfutakamba, Saada Salum Mkuya, Dk Henry Nyamubi, Sixtus Mapunda na Dk Natujwa Mvungi.

Mwananchi.

Featured

Mahakama ya Kadhi yalitafuna Bunge

Wabunge wakiwa Bungeni mjini Dodoma
Wabunge wakiwa Bungeni mjini Dodoma

Suala la Mahakama ya Kadhi limechafua hali ya hewa bungeni mjini Dodoma baada ya wajumbe Waislamu kutishia kupiga kura ya hapana kama halitaingizwa katika Rasimu inayopendekezwa.

Wakati Waislamu wakishikilia msimamo huo, wajumbe ambao ni Wakristo nao wamejipanga kupiga kura ya hapana endapo Mahakama ya Kadhi itaingizwa katika Katiba inayopendekezwa.

Dalili za mpasuko huo zilianza kujitokeza jana asubuhi baada ya mjumbe mmoja, Jaku Ayub Hashim kuwasha kipaza sauti akitaka kuzungumza akisema ana jambo muhimu.

“Mheshimiwa tangu jana (juzi) ulisema utanipa nafasi ya mwanzo nizungumze,” alisema Jaku, lakini Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu alimtaka aketi chini na suala lake limesikika.

Suluhu akaendelea kuwapa wajumbe wengine kuendelea kuchangia na baadaye alimpa Jaku muda wa dakika saba ili kuwasilisha kile alichotaka kukizungumza ndani ya Bunge hilo.

Jaku alisema walipendekeza kifungu kinachotaka uamuzi unaohusu ndoa, talaka na mirathi iliyoamuliwa kwa misingi ya dini ingizwe kwenye Katiba inayopendekeza lakini hakimo.

“Ni kitu kidogo kabisa tuliomba kiongezwe lakini cha kusikitisha kikundi cha sanaa kimeingizwa. Mimi binafsi yangu sitaunga mkono wala mguu wala sitaipigia kura hii,” alisema Jaku.

Suluhu akamweleza kuwa angalizo lake limechukuliwa, na uongozi wa Bunge pamoja na kamati ya Uandishi wanajitahidi kuingiza kila kitu kinachowezekana, lakini kwa misingi na sheria za nchi.

Baadaye Sheikh Masoud Jongo alipopewa nafasi ya kuchangia, naye alitahadharisha kuwa mambo yaliyopendekezwa na Waislamu yasipoingizwa kama ilivyo kwa sasa, hawatakuwa tayari kwa lolote.

“Msimamo wetu sisi Waislamu kama mambo yetu tuliyoleta katika mapendekezo hayataingizwa, basi yatabomokea hapa na hatutakuwa tayari tena,” alisema Sheikh Jongo, kauli iliyowashtua wajumbe.

Akihitimisha majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge alisema kamati yake imefanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwa masilahi ya Watanzania. Akiahirisha Bunge, Suluhu alisema kesho Bunge litaanza kwa kupitia baadhi ya mambo yaliyoibuka katika uhakiki kisha kupitisha azimio la upigaji wa kura. Kura zitapigwa kati ya kesho hadi Oktoba 2.

Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Sheikh mwingine, Hamid Jongo alimwendea Askofu mstaafu Donald Mtetemela na kumkumbatia, kisha kumvuta pembeni na kisha kuteta kwa dakika tano.

Katika viwanja vya Bunge, hali ilikuwa tete kwani kulikuwa na makundi tofauti tofauti ya Wakristo na Waislamu kila moja likijadili na kutafakari suala la Mahakama ya Kadhi kuingizwa kwenye Katiba.

Mjumbe wa kundi la 201 Dk Aley Nassoro alisema kuwa suala la Mahakama ya Kadhi lisipoingizwa katika Katiba inayopendekezwa, atakuwa wa kwanza kuhamasisha wenzake ili wagome kupiga kura.

Dk Nassoro alisema Waislamu wamechoka kudanganywa kwani tangu kipindi cha kampeni za mwaka 2010, waliahidiwa kuwa jambo hilo lingeshughulikiwa mapema lakini watawala wamekuwa kimya.

“Hii Katiba itakuwa ni mbovu kuliko ile ya mwaka 1977 na italeta migongano baada ya miezi sita tu tangu kuzinduliwa. Bora iachwe kwani mambo mengi ya msingi kwa Wazanzibari yameachwa,”alisema.

Akiwa viwanja vya Bunge Askofu Mtetemela alionekana akishauriana na wajumbe mbalimbali na baadaye alisema analaani kauli hizo na kusema kuwa hazilengi kujenga nchi badala yake zinabomoa.

“Kinachotakiwa ni amani, sasa tukianza kutishiana mambo hayatakwenda maana na sisi Wakristo tutataka mambo yetu yaingizwe humo, tunachohitaji ni amani na si vinginevyo,” alisema Mtetemela.

Askofu Mtetemela alisema kikubwa kinachotakiwa kwa wajumbe ni maridhiano na isiwe vitisho kwa kuwa walianza pamoja hivyo wanapaswa kumaliza pamoja.

Aliitaka Kamati ya Uandishi kutoingiza kabisa jambo hilo katika Katiba na akasema hali ikifikia hapo itasababisha mgogoro wa kimasilahi kwa kila mtu kudai haki yake ndani ya Katiba.

Hata hivyo, aliitaka Serikali kutunga sheria za kutambua uamuzi wa Waislamu wa ndoa, mirathi na umiliki wa rasilimali kwa Waislamu ili yakubaliwe kwenye sheria siyo kwenye Katiba.

Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, John Cheyo, alitaka Watanzania kuendelea kuheshimu Katiba ambayo imeweka wazi kuwa Serikali haina dini bali wananchi wake ndiyo wenye dini.

“Kwa sababu ukienda njia hiyo hakuna atakayeshinda. Na sisi Wakristo tuseme bila ‘Canon Law’ (Sheria za Kanisa) hakuna hatupigi kura, tutafika wapi? Ndiyo maana tuliyatenganisha haya mambo,”alisema.

Wakati makundi hayo yakiwa na msimamo tofauti, jana katika viwanja hivyo vya Bunge walisikika Waislamu wakihamasishana kwamba kama ikifika kesho hakuna Mahakama ya Kadhi wasusie Bunge.

Suala la Mahakama ya Kadhi, linaonekana kuwapasua kichwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ambayo juzi na jana zilikutana kutafuta njia ya kulinusuru Bunge hilo na mpasuko huo mkubwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe walipendekeza kuitishwa kwa Kamati ya Maridhiano ili kutafuta njia bora itakayonusuru Katiba Mpya kukwama kesho.

Mwananchi.

Featured

Warioba: Nitaendelea kuitetea Rasimu, sitakimbilia Ukawa

Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba.
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema uamuzi wake wa kuitetea Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na tume aliyoiongoza, pamoja na kauli yake ya juzi ya; ‘Tutakutana mtaani’, havimaanishi kwamba atakihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Jaji Warioba amesema jana kwamba baada ya kutoa kauli hiyo katika maadhimisho ya miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), baadhi ya watu wakiwamo makada wa CCM wanaodhani kuwa atajiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika maandamano ya kudai Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi.

Katika kongamano hilo, Jaji Warioba alisema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba Septemba 24 mwaka huu bungeni mjini Dodoma, imeondoa mambo manne muhimu na mengine mengi yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.

Akizungumza na gazeti hili Jaji Warioba alisema: “Juzi (jana) niliposema kuwa tutakutana mtaani, nilikuwa namaanisha kwamba tutakutana na Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika midahalo, makongamano, semina na katika vyombo vya habari. Sisi tutaendelea kuitetea rasimu tuliyoitoa Desemba mwaka jana. Wao (wajumbe wa Bunge la Katiba), tutakutana nao huko huko ili wawaeleze wananchi sababu za kuondoa maoni yao.”

Jaji Warioba aliyeiongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa miezi 20 ikiratibu na kukusanya maoni ya wananchi na mabaraza ya katiba ngazi mbalimbali, alisema kuwa kamwe hawezi kujiunga na Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na DP kwa sababu vyama vya siasa viliuteka mchakato huo na kuuharibu.

“Ieleweke kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inasimamia katika maoni ya wananchi na haiwezi kuyumba katika hilo. Tutaendelea kusisitiza kuheshimiwa kwa maoni hayo na wale waliyoyabadilisha, lazima wawaeleze wananchi sababu za kufanya hivyo,” alisema.

Aliongeza: “Inashangaza kuona watu wakihusisha kauli yangu ya juzi na kujiunga na Ukawa au vyama vya siasa. Tusubiri tu, ikifika wakati wa kupiga kura ya maoni ili tuone wananchi watakubali rasimu ipi.”

Katika ufafanuzi wake, Jaji Warioba alisema kuwa hata suala la mgombea huru limewekwa masharti mengi yanayoweza kuwa kikwazo kwa mgombea.

“Mgombea huru kawekewa masharti ambayo binafsi naona kama ni ya kumkataa kistaarabu. Suala la muungano nalo pia ni tatizo na bado halijapatiwa ufumbuzi,” alisema.

Mwananchi.

Featured

ZLS: Katiba ya wananchi imeporwa na watawala

Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) Awadh Ali Said
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) Awadh Ali Said

Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said amesema Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba imepora mamlaka ya wananchi kutokana na kitendo cha kubadilisha vifungu muhimu ikiwamo mfumo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza jana na gazeti hili mjini Zanzibar, Awadh alisema kitendo cha kubadilisha mfumo wa Muungano wa serikali tatu kama ilivyokuwa imependekezwa na rasimu ya awali ya Jaji Joseph Warioba ni kuvunja msingi wa nyumbani na kinakwenda kinyume na maoni ya wananchi.

Alisema kwamba mfumo wa Muungano wa Serikali mbili na marekebisho yake yaliyofanyika umekuwepo katika miaka ya nyuma na katika kipindi cha miaka 50, lakini umeshindwa kuondoa kero za Muungano.

“Bahati mbaya mchakato wa katiba umeporwa kutoka kwa wananchi na kumilikiwa na watawala kinyume na matakwa ya wananchi, hatuwezi kupata katiba bora kwa kuweka masilahi binafsi ya vyama.” alisema Awadh.

Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema kitendo cha kubadilisha vifungu vilivyokuwa vimependekezwa katika Katiba ya awali ni sawa na kuondoa maoni ya wananchi kwa vile rasimu ya Warioba ilitokana na maoni ya wananchi wa pande mbili za Muungano kabla kuwasilishwa bungeni Febuari mwaka huu.

Aidha, alisema kwamba wabunge wa Bunge la Katiba kupitia vyama vya siasa wamezingatia masilahi yao binafsi badala ya masilahi ya Taifa na wananchi wake, ndiyo maana wamefuta vifungu muhimu kama kuwapo kwa ukomo wa kugombea ubunge, kiwango maalumu cha taaluma, wananchi kuwa na mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa mbunge asiyewajibika kwa madhumuni ya kuimarisha uwajibikaji na misingi ya utawala bora nchini.

“Jambo la msingi Bunge la Katiba livunjwe, liundwe bunge jipya lisiloshirikisha wabunge wanaotokana na vyama vya siasa ili tupate katiba bora na yenye manufaa kwa wananchi wa pande mbili za Muungano wetu,” alisema Awadh.

Akifafanua, alisema hatua ya wabunge kuingiza mambo ya bahari na ardhi katika orodha ya mambo ya Muungano kutaibua kero nyingine mpya, kwa sababu haiwezekani kuondoa mambo ya mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano wakati rasilimali hizo zinapatikana chini ya ardhi katika mwambao wa bahari.

Hata hivyo, upande wake Mwanasheria Mkuu wa zamani, Hamid Mbwezeleni alisema kwamba rasimu ya mwisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano siyo mbaya baada ya kufanyiwa marekebisho mbalimbali na kutaka wabunge wa Bunge la Katiba kupewa nafasi ya kukamilisha majukumu yao.

Alisema kwamba, iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati ikitekeleza majukumu yake hakuna mhimili ambao uliingilia majukumu yake na kushangazwa na kitendo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo kugeuka msemaji mkuu wa Watanzania.

Mwananchi.

Featured

Majambazi wapora milioni 30.6 wajeruhi Polisi, Mfanyabiashara

Sajenti Hija Hassan Hija akipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mara baada ya kujeruhiwa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni mjambazi maeneo ya Mlandege.
Sajenti Hija Hassan Hija akipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mara baada ya kujeruhiwa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni mjambazi maeneo ya Mlandege.

Na Tatu Makame, Laylat Khalfan

WATU wawili akiwamo askari mmoja wamenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, waliofanikiwa kupora mfuko wa fedha unaosadikiwa kuwa na zaidi ya shilingi milioni 30.
Tukio hilo, lilitokea jana mchana majira ya 8:30 katika Mtaaa wa Mlandege Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo majambazi hao walimvamia mmoja wa wafanya biashara wa Mchele hapa nchini aliyetambulika kwa jina la Salum Issa Suleiman (50), Mkaazi wa Baghani Mjini Unguja ,, ambaye walimpora mfuko wake wa fedha hizo wakati akiwa njiani kuzipeleka benki.
Mfanyabiashara wakati akiwa njiani alijikuta akizingirwa na mojaya gari ndogo na kuanzakushambuliwa kwa risasi ambazo zilimjeruhi sehemu zake za miguuni na ghafla kuanguka na ndipo majambazi hao walipowezakufanikiwa kumpora fedha hizo.
Wakati tukio hilo likitokea mmoja wa askari  polisi wa Kituo cha Malindi Sajenti Hija Hassan Hija, alijaribu kupambana namabambazi hao, lakini alishindwa kufanikiwa baada na yeye kujeruhiwa sehemu ya mkononi na mguuni kutokana kushambuliwa kwa risasi.

Wakizungumza na gazeti hili, waathirika wa tukio hilo,  Mfanya biashara Salum alisema, wakati alipokuwa akielekea maeneo ya Benki hiyo  ndipo ilipotokea gari ndogo mbele yake na kumnadia mwizi na hapo ndipo walipompiga risasi ya mguu wa kulia na kumnyang’anya fedha hizo na kuondoka nazo .
Kwa upande wake askari Hija alisema, alipofika maeneo hayo ndipo alipomkuta Mfanyabiashara huyo akiwa katika harakati za kujinasua na  hali  na ndipo askari huyo alipokwenda kumuokoa lakini na yeye alishambuliwa na majambazi hao na kufanikiwa kuondoka na kitita hicho cha fedha zamfanyabiashara huyo,,
Hata hivyo,  majeruhi hao bado wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazi mmoja na hali zao walieleza kuwa zinaendelea vizuri.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,  Mkadam Khamis Mkadam, alisema ni kweli tukio hilo limetokea  na aliyeporwa fedha hizo ni  Mfanyabiashara   wa Mchele katika maeneo ya Bandarini ambae alikuwa akielekea katika Benki ya PBZ tawi la Mlandege.
Alisema mfanyabiashara huyo alikuwa na fedha zenye thamani ya shilling milioni 30,6,00,000, ambazo ni mali ya tajiri wake anafahamika  kwa jina la Yussuf Mohamed, ambazo alikuwa anakwenda kuziweka katika Benki hiyo.
Hata hivyo, Kamanda Mkadam, alitoa wito kwa Wananchi wakati wanapokwenda kuweka pesa kuacha kwenda kwa miguu na kuwatumia askari kwani askari wapo kwa ajili yao ili kuimarisha usalama wa raia.

 

Featured

Shirika la UNFPA Yakabidhi magari ya Wagonjwa Zanzibar.

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Rashid Seif  wakati akilijaribu moja ya gari hilo zilizotolewa na UNFPA katika hafla ilizofanyika  Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Rashid Seif wakati akilijaribu moja ya gari hilo zilizotolewa na UNFPA katika hafla ilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Na RAMADHANI ALI /MAELEZO ZANZIBAR

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) limekabidhi  msaada wa magari manne ya Ambulance  kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ambayo yatatumika katika Hospitali nne.

Mwakilishi wa UNFPA Tanzania  Dkt. Natalia Kanem alimkabidhi Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman magari hayo katika sherehe zilizofanyika   Wizarani Mnazimmoja.

Dkt. Natalia alitaka  magari hayo yatumike kwa uangalifu ili  kufikia malengo ya millennia  ya kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wanaozaliwa hasa katika maeneo ya vijijini.

Alisema moja ya sababu inayopelekea vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ni tatizo la usafiri ambalo linachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya familia hasa katika maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa  msaada huo ni  sehemu ya Mpango maalum wa Shirika la Umoja wa  Mataifa  ulioanza  mwaka 2011 na kumalizika Juni 2015  ambao  huenda ukaendelea hadi mwaka 2016 kusadia  masuala ya Afya na Lishe.

Amesema  mpango huo wa miaka minne  ambao unahusisha maeneo  makuu saba unaendeshwa kwa pamoja na Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa  ambayo ni WHO, UNFPA, UNICEF na WFPA.

Mwakilishi huyo wa UNFPA amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Jakaya Mrisho Kkwete na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Muhamed Sheina kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuimarisha huduma za  mama wajawazito na watoto wachanga.

Aliesema UN inathamini juhudi hizo na  juhudi za kuimarisha uchumi hivyo aliahidi  kuwa wataendelea  kuunga mkono kuhakikisha mama wajawazito na watoto wanaozaliwa wanaendelea kuishi katika mazingira yaliyo  salama.

Waziri wa Afya  Rashid Seif Suleiman, alilishukuru Shirika la UNFPA kwa misaada mbali mbali inayotoa kwa Wizara hiyo  na ameahidi kuwa magari hayo yatatumika katika malengo yaliyokusudiwa.

Amekiri kuwa tatizo la usafiri kwa  mama wajawazito Zanzibar limekuwa likiwasumbua wananchi wengi na inafikia wakati akinamama hujifungua wakiwa kwenye gari  wakati wa kupelekwa Hospitali ambazo hazina stara wala hazifai kwa kazi hiyo.

Alieleza matarajio  yake kuwa tatizo hilo kwa sasa litapungua kwa kiasi kikubwa baada ya kupatiwa msaada huo ambao umekuja wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelekeza juhudi zake kuimarisha  huduma za afya mijini na vijijini.

Gari hazo za ambulance ambazo zitapelekwa katika Hospitali ya Kivunge, Mwembeladu, Mkoani na Micheweni zimegharimu shilingi milioni 245,000,000 za kitanzania.

CHANZO: ZANZINEWS.

Featured

Sitta apokea meseji za matusi

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Samuel Sitta.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Samuel Sitta.

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amesema anapokea meseji za simu zaidi ya 50 kwa siku za kumtukana na kusisitiza ataendelea kupambana kuhakikisha Katiba inayopendekezwa inapatikana.

Sitta alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana wakati akielezea kutoridhishwa kwake na kile alichodai ni namna hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Saed Kubenea inavyopotoshwa na wanaomchukia.

“Kuna baadhi ya vyombo vya habari wananichukia mimi binafsi. Wasichanganye chuki hizo na mchakato wa Bunge Maalumu,” alisema Sitta na kuongeza;

“Mimi napokea matusi kila siku. Meseji zisizopungua 50 viongozi wa Chadema wameweka namba zangu katika tovuti nitukanwe kila siku hilo mimi niko tayari na mnaniona niko safi tu wala sihangaiki nalo.”

“Lakini sasa Bunge Maalumu ni chombo cha kikatiba,  kiko tofauti na mwenyekiti wake. Huwezi kuliadhibu Bunge Maalumu kwa sababu hupendi sura ya mwenyekiti wake,” alisema.

Sitta alienda mbali zaidi na kusema, “Kwa hiyo wale wanaoendeleza hayo mapambano tuendelee na tutaendelea kupambana, lakini kazi ya Bunge Maalumu itaendelea na ndugu zangu Watanzania mjue tunaandaa Katiba safi na rafiki kwa wananchi na itapatikana.”

Sitta alisema baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo ya kesi ya Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kumekuwa na tafsiri alizosema ni potofu.

Baada ya maelezo hayo alimpa ruksa AG, Jaji Frederick Werema kutoa ufafanuzi.

Jaji Werema alisema Mahakama Kuu, katika kutafsiri kifungu cha 25(1) (2) inakiri kwamba kuna tofauti kati ya kifungu kilichoandikwa Kiswahili na kile kilichoandikwa Kiingereza.

Alisema Mahakama Kuu katika hukumu hiyo imesema mamlaka ya kuandika Katiba Mpya ina maana ni mamlaka ya kuandika na kupitisha katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Mwananchi.

Featured

Jaji Warioba: Tutakutana mtaani

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dar es Salaam jana.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dar es Salaam jana.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.

Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma,  madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na muungano. “Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na rasimu iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.

“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda Katiba iliyoboreshwa. Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge Maalumu haitapigiwa kura hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano,  rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,” alisema.

Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka kesho Katiba Mpya itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato ukaanza upya.”

Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati yake imefuta ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha ibara 47, kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.

Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa kuwa si mambo ya muungano.

Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili kama ilivyo sasa na kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia saa 1:02 kufafanua umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu iliyotolewa na Bunge la Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la Katiba wana msemo wao kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa watakapomaliza vikao vya Bunge hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea mtaani walipo wananchi ndiyo watajua nani ni ‘shida’, kati yake na wao.

Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili kanuni ili kuruhusu wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo kwa baruapepe (e-mail) na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba alisema, “Utaratibu huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata mimi nimeanza kukata tamaa.”

Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu waliohudhuria kongamano hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila mjumbe wa tume hiyo alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini waliweka kando mawazo yao baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya Katiba wanayoitaka.

Katika maadhimisho hayo,  Jaji Warioba pia alizindua kitabu cha marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi anapumua Katiba’. Dk Mvungi  aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja wa waanzilishi wa LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini alikopelekwa kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani kwake.

Maadili ya Viongozi wa umma

Kuhusu maadili ya viongozi wa umma alisema, “Wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi. Kutokana na maoni ya wananchi Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani.”

Alisema kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa ambayo ni;  utu, usawa, umoja na mshikamano na kwamba wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye katiba ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa (Kiswahili ).

“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe mzalendo, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania anatakiwa aenzi umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alihoji.

Alisema tunu za taifa ndiyo msingi wa utamaduni na maadili ya taifa, kwamba mwelekeo wa taifa utategemea jinsi wananchi wanavyoenzi misingi mikuu na tunu.

Aliponda kitendo cha Bunge la Katiba kutoweka miiko ya uongozi kwenye Katiba wakati kila siku viongozi wanalalamika juu ya rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi.

“Katika bara la Afrika, nchi kama Afrika Kusini, Namibia na Kenya zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba. Hapa kwetu sheria tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi. Sijui kwa nini Bunge la Katiba wameondoa hili,” alisema.

Madaraka ya Wananchi

Jaji Warioba alipinga kitendo cha Bunge la Katiba kuondoa kipengele cha wananchi kuwa na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhishwi na uwakilishi wake bungeni, mbunge kutokuwa waziri ili aweze kuwawakilisha vizuri na ukomo wa mbunge kuwa vipindi vitatu .

“Bunge lina kanuni za kuwawajibisha wabunge na wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo. Vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa wabunge wao katikati ya kipindi. Wananchi nao wanataka watumie madaraka yao,” alisema.

Mgawanyo wa madaraka

Akizungumzia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya Bunge, Serikali na Mahakama, alisema pendekezo lao la kumwondoa rais na mawaziri kutoka kwenye Bunge linakataliwa kwa sababu nchi imezoea mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi nyingi za jumuiya ya madola.

“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge. Kwenye mfumo wa kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji. Madaraka hayo yako mikononi mwa Waziri Mkuu ambaye ni mbunge. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India, Canada, Australia, New Zealand,” alisema.

Akitolea mfano mwingiliano huo alisema wakati wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bunge lilitunga sheria lakini baadaye Rais alifanya mazungumzo na watu nje ya bunge na baadaye bunge likalazimika kubadili uamuzi.

 “Tanzania ina mfumo wa urais ambapo rais ni mkuu wa nchi, mtendaji mkuu na amiri jeshi mkuu. Rais na mawaziri wake kuwa sehemu ya bunge ni kuchanganya mamlaka. Hali hii inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya bunge na pia bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,” alisema.

Aliongeza, “Nchi nyingi zimebadili Katiba zao ili kutenganisha madaraka ya mihimili. Jirani zetu wa Msumbiji na Kenya wamefanya hivyo. Kenya imefanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.”

Muungano

Huku akitaja kero 20 za muungano, 11 za Zanzibar na 10 za Tanzania Bara zilizotajwa na wananchi wakati wa kukusanya maoni, Jaji Warioba alisema, “Ingawa Rasimu ya Bunge Maalumu limerudisha madaraka ya rais kuigawa nchi hiyo peke yake haitoshi. Mambo haya ni magumu kubadilika kwa upande wa Zanzibar.”

Aliongeza kuwa ili kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ni lazima mabadiliko yapitishwe kwa theluthi mbili au zaidi ya Wawakilishi.

Mwananchi.

Featured

Vitisho vyaanza Kamati ya Uandishi

Makamo wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddi akisoma moja miongoni mwa ujumbe wa vitisho kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokea Zanzibar unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii alipokuwa akizungumza na Wandishi wa hababri jana Dodoma.
Makamo wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddi akisoma moja miongoni mwa ujumbe wa vitisho kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokea Zanzibar unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii alipokuwa akizungumza na Wandishi wa hababri jana Dodoma.

MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ameitaka jamii kuacha kutumia mitandao ya kijamii kutishia maisha ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Balozi Iddi aliyasema hayo Mjini Dodoma jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya vitisho vilivyotolewa kwa wajumbe wa Bunge hilo wa Kamati ya Uandishi katika mitandao ya kijamii.

Alisema si vizuri kuwatishia wajumbe hao kwani waliteuliwa kwenye kamati hiyo kwa mujibu wa sheria.

“Wajumbe wa kamati hii, wanaitwa wasaliti, sijui kwanini wanaitwa hivyo na sijui msaliti ni nani kati ya waliobaki kuandika katiba au waliotoka nje,” alisema.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewahakikishia usalama wa kutosha wajumbe hao ili wasidhurike.

“Vyombo vya dola vipo na vitafanya kazi yake, niwahakikishie kwamba, wajumbe hawataendelea kuwa salama hata watakaporudi Zanzibar,” alisema.

Alisema Serikali ya Zanzibar, imeridhishwa na Rasimu inayopendekezwa na Bunge hilo iliyosomwa juzi bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Bw. Andrew Chenge.

“Baadhi ya mambo machache yaliyokuwa na ukakasi upande wa Zanzibar, yamefanyiwa marekebisho katika Katiba inayopendekezwa.

“Katika hoja 17 zilizowasilishwa kwenye Kamati ya Uandishi na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, zote zimeingizwa kwenye Katiba isipokuwa tatu ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa kujiuzulu kwa Bw. Othman kwenye Kamati hiyo akisema alitakiwa kushiriki kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hivyo kutokuwepo kwake si kikwazo cha kupatikana Katiba

“Waliokuwepo katika kamati hii upande wa Zanzibar, walikuwa wanatosha,” alisema.

Majira.

Featured

Mahakama yajivua mipaka ya Bunge

Mahakama haina mamlaka ya kuamua ni kwa kiwango gani cha maboresho au marekebisho ambayo Bunge la Katiba linaweza kuyafanya katika Rasimu ya Katiba.” Mahakama
Mahakama haina mamlaka ya kuamua ni kwa kiwango gani cha maboresho au marekebisho ambayo Bunge la Katiba linaweza kuyafanya katika Rasimu ya Katiba.” Mahakama

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imejivua katika mgogoro wa mamlaka ya Bunge la Katiba kuhusu ni kwa kiwango gani bunge hilo lina  mamlaka ya kufanya  marekebisho au kuboresho Rasimu ya Katiba Mpya iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Badala yake, mahakama hiyo imesema hayo ni masuala ya kisiasa zaidi kuliko kisheria. Mahakama hiyo ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa amri kuhusiana na kesi ya kuhoji mamlaka ya Bunge la Katiba, chini ya kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.

Hata hivyo, haikutoa sababu za amri hiyo na badala yake ilisema kuwa itatoa sababu hizo Oktoba 7. Kesi hiyo ilifunguliwa na mwanahabari, Saed Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa niaba ya Serikali.

Katika kesi namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea alikuwa anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu hicho kuhusu mamlaka ya Bunge na pia, itamke kama lina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Wakili wa Kubenea, Peter Kibatala akisaidiana na Mabere Marando walisema kwa mujibu wa kifungu hicho, bunge hilo lina mipaka na halina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu hiyo.

Akijibu hoja hizo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alidai kuwa bunge hilo lina mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote na kwamba, halifungwi na Rasimu hiyo kwa kuwa ni nyaraka ya kazi tu kwa bunge hilo.

Katika amri yake jana, Mahamaka ilisema imebaini kuna utata na mkinzano wa maana katika kifungu hicho katika lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiingereza.

Hivyo, mahakama kupiti jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo, Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Dk Fauz Twaib na Aloysius Mujulizi, ilitoa tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hilo baada ya kusoma Sheria yote ya Mabadiliko ya Katiba

Ilisema licha ya utata huo, mamlaka ya kutengeneza masharti ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamaanisha mamlaka ya kuandika na kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura na wananchi wa Tanzania.

Pia, ilisema mamlaka hayo yatatekelezwa kwa msingi wa Rasimu ya Katiba baada ya kuwa imewasilishwa mbele ya Bunge la Katiba na mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Kwa kufanya hivyo, Bunge la Katiba linaweza kuboresha au kuirekebisha Rasimu ya Katiba,” alisema Jaji Mwarija alipokuwa akisoma amri hiyo.

Aliongeza: “Mamlaka hayo yana mpaka tu kama ilivyokuwa kwa shughuli za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika misingi ya kitaifa na maadili yaliyotolewa katika kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.”

Ilisisitiza kuwa hayo ni masuala zaidi ya kisiasa kuliko ya kisheria, isipokuwa tu bila kukiuka kifungu cha 9 (2).

Kifungu hicho kinasema: “Tume ya Mabadiliko ya Katiba itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya Jamii  na kinataja mambo ambayo ni sharti yahifadhiwe na kudumishwa, ikiwamo Jamhuri ya Muungano.”

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema wameridhishwa na jinsi Mahakama ilivyoweza kutekeleza jukumu lake kwa wakati na wamefurahi kuwa imeitambua Rasimu ya Katiba tofauti na mdaiwa alivyodai kuwa hiyo ni nyaraka ya kazi tu kwa bunge hilo.

Alisema bado Mahakama haikuweza kukata kiu yake na ya mteja wake.

Mwananchi.

Featured

Balozi Seif akanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mtanzania

2.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo m bali mbali nchini hapo katika Ukumbi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
2. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo m bali mbali nchini hapo katika Ukumbi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.

Na Othman Khamis OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekanusha Habari  iliyochapishwa katika Gazeti litolewalo  kila siku la Mtanzania iliyotolewa siku ya Jumatano ya tarehe 24 Septemba, 2014 likiwa na  Kichwa cha Maneno kisemacho

“SIRI ZAVUJA ZA AG ZANZIBAR KUJIUZULU “.

Kanusho hilo limetolewa na Makamu  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa Vyombo mbali mbali vya Habari katika Ukumbi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.

Balozi Seif  alisema Serikali inakanusha suala la sintofamu lililoandikwa na gazeti hilo ambayo imedai kwamba Viongozi wa juu wa CCM walikutana kwa dharura na kuazimia kufukuzwa kazi kwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ  kwa kile walichodai kwamba amekisaliti Chama cha Mapinduzi

Alifahamisha kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatakiwi kuwa muumini wa Chama chochote cha siasa na ndio maana hata vikao vya chama hatakiwi kuhudhuria.  Hivyo uteuzi wa Kiongozi huyo anayesimamia masuala ya kisheria hufanywa na Rais wa Zanzibar ambae ndie mwenye maamuzi ya kumuweka na kumuondoa.

Akigusia hoja 17 za Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alizotaka ziingizwe katika Katiba Balozi Seif alisema suala hilo ni kweli na Mjumbe huyo alitakiwa aziwasilishe katika Kamati jambo ambalo alilitekeleza.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziar alielezea faraja yake kutokana na masuala hayo kuingizwa katika Rasimu ya Katiba ambapo hadi sasa Hoja 4 kati ya hoja hizo 17 bado zinafanyiwa kazi.

Alieleza kwamba kuchaguliwa kwa Mjumbe katika Kamati na kukataa kuhudhuria kama alivyofanya Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ ni maamuzi yake binafsi kwa vile hakuna ulazima wa mjumbe kuchaguliwa huko ikaonekana kama kifungo ingawa atakuwa na wajibu wa kuendelea kufanya kazi katika kamati hadi mwisho wake.

Balozi Seif alisema kwamba Mh.Othman Masoud alitakiwa ashiriki katika kamati kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wa Zanzibar.

Alisema hata hivyo kutokuwemo kwake katika kamati sio kikwazo cha kupatikana kwa rasima ya katiba, kwa vile waliokuwamo ndani ya kamati kwa upande wa Zanzibar walitosheleza kuiwakilisha Zanzibar kikamilifu.

Akigusia upotoshaji mwengine ulioandikwa na gazeti hilo la Mtanzania juu ya masuala 17 aliyotaka Mwanasheria Mkuu wa SMZ yaingizwe katika Rasimu ya Katiba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Taarifa hiyo si ya kweli kabisa.

Balozi Seif alisema Mawaziri wa Chama cha Wanachi {CUF } hawamo katika Bunge Maalum la Katiba sasa inakuaje washiriki kuchangia masuala ambayo wao kama sehemu ya { Umoja wa Katiba ya Watanzania } UKAWA hawakubaliani na kuendelea kwa Bunge hilo.

“Wapo baadhi ya waandishi wa Habari hawafahamu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeshwa katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa ulioundwa na Vyama vya CCM na CUF na kama inavyoeleweka CUF hawamo ndani ya Bunge hilo sasa itakuaje washiriki kuchangia masuala hayo? “ Aliuliza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba suala hilo liliripotiwa sambamba na upotoshaji mwengine wa gazetui hilo la mwanasheria huyo kuwasiliana na Rais wa Zanzibar alisema ni uzushi mtupu usio na maana.

Alisema Mh. Othman Masoud kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wowote na uwezo wa kuwasiliana na Rais au Makamu wa Pili wa Rais kwa mashauriano ya jambo lolote analoona linafaa.

Balozi Seif alithibitisha wazi kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati anaamua kujiuzulu wadhifa wa Ujumbe wa Kamati ya Uandishi Rais wa Zanzibar Dr. Shein alikuwa nje ya Nchi kwa kiziara rasmi ya Kiserikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi pamoja na Chama cha Mapinduzi bado kinawaamini wana Habari wa vyombo vyote, hivyo amewaomba waandhishi kujiepusha na tabia ya kuzusha baadhi ya mambo ambayo hayana ukweli wowote.

Balozi Seif aliwataka Wana Habari wote Nchini kujitahidi kutumia kalamu zao vyema kwa kuwaelimisha wananchi masuala ya ukweli badala ya kuwapotosha kwa kuwalisha mambo ya kubabaisha.

Akijibu baadhi ya maswali ya wana Habari hao Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitegemei kuchukuwa hatua yoyote ya kisheriaadhidi ya Gazeti hilo. Lakini ikauomba Uongozi wa Gazeti hilo kuzingatia maadili ili kuendelea kutoa Habari zenye usahihi.

Wakati mwengine tunaelewa kwamba kalamu za waandishi huwaponyoka wakati wanapoandika Habari zao. Lakini kuponyoka huko kusiwe ndio muendelezo wa uchapishaji wa Habari zisizo na nuchunguzi “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameiasa mitandao ya kijamii kujiepusha na tabia ya kuendeleza vitisho wanavyovielekeza kwa wajumbe wa Kamati za Bunge Maalum la Katiba hasa kutoka Zanzibar kwa visingizio vya kuizamisha Zanzibar.

Balozi Seif alisema kilichofanyika na kuendelea kufanywa na Kamati hizo chini ya Bunge hilo ni kutekeleza jukumu walilokabidhiwa na watanzania na inapaswa kuheshimiwa na kila Mwanadaamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wajumbe wa Kamati hizo kwamba Serikali kupitia vyombo vya Dola vitazingatia usalama wao na vitakuwa tayari wakati wowote kumchukulia hatua za kisheria mtu ye yote atakayetishia maisha ya wananchi wakiwemo wajumbe hao.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed aliwaeleza Wanahabari hao wa vyombo mbali mbali Nchini kwamba Katiba ni mchakato ambao masuala yote yanafanyiwa uhakiki wa kina.

Mh. Aboud alifahamisha kwamba suala lolote zito linalohusu mambo ya Muungano haliwezi kutekelezwa bila ya kuhusishwa viongozi na wataalamu wa pande zote mbili.

Featured

Waraka wa Warioba kwa Wasira

Jaji Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba.
Jaji Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameandika waraka kumjibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira kwa kauli yake kuwa ndiye aliyemkimbiza CCM kwenda upinzani mwaka 1995.

Katika waraka wa maandishi alioutuma kwa gazeti hili, Jaji Warioba alisema maelezo ya Wasira dhidi yake katika mahojiano maalumu na gazeti hili hayakuwa sahihi na hivyo akamtaka ajifunze kusema ukweli kwa kuwa mambo anayosema yanaweza kumrudia baadaye.

Waraka wenyewe

Tarehe 22 Septemba 2014, Gazeti la Mwananchi lilitoa taarifa ya mahojiano kati yake na Mheshimiwa Steven Wasira. Katika mahojiano hayo, Mheshimiwa Wasira alisema mimi ndiye niliyemkimbiza CCM.

Tangu mchakato wa Katiba Mpya kuanza nilikuwa napata taarifa kwamba Mheshimiwa Wasira alikuwa amenifanya mtaji wake katika kutetea msimamo wake. Wakati mmoja kuna kiongozi mwenzake aliniuliza kama nina ugomvi binafsi na Mheshimiwa Wasira kwa sababu kila akipata nafasi kwenye vikao vyao ananishambulia. Wakati wa mabaraza ya Katiba nilipata taarifa za aina hiyo. Nilichofanya ni kuwaarifu viongozi wake wa CCM.

Mengi aliyosema Mheshimiwa Wasira siyo ya kweli. Napenda nitoe ufafanuzi kwa machache yafuatayo:-

Niligombea mara mbili na Mheshimiwa Wasira. Baada ya Uchaguzi wa 1990 ambao nilishinda kwa kura nyingi sana, uchaguzi huo ilitenguliwa kwa sababu nilifanya kampeni kwa kutumia gari la Waziri Mkuu.

Uchaguzi ulirudiwa mwaka 1992. Niliunda timu ya kampeni, Mheshimiwa Wasira akiwa kiongozi. Aliniomba atangulie jimboni kuandaa mazingira. Alipofika huko akaanza kampeni dhidi yangu na kutangaza kwamba anagombea. Wakati huo kura za maoni zilikuwa zinapigwa na wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya. Wajumbe walikuwa kama 600. Nilipata kura 400 na Mheshimiwa Wasira alipata kura chache akiwa mtu wa tatu au nne. Baada ya matokeo akatangaza anajitoa kwenye mchakato na jina lake lisipelekwe NEC. Alikataliwa kwa sababu kufuatana na kanuni, muda wa mtu kujitoa ulikuwa umepita.

Mwaka 1995, kura za maoni zilikuwa zinapigwa kwenye kata. Tulianza na Kata ya Sarama ambayo iko upande wa mashariki, siku ya tatu tulifika Nyamuswa ambacho ndicho kijiji ninachotoka. Nyamuswa ilikuwa kituo cha tano kati ya vituo 12.

Baada ya hapo tulielekea magharibi ya jimbo anakotoka Mheshimiwa Wasira. Baada ya kura kupigwa katika Kata ya Guta, Mheshimiwa Wasira alijitoa kwa sababu aliona hawezi kunishinda hata kama angepata kura zote za kata mbili zilizobaki. Siyo kweli kwamba Nyamuswa ilikuwa ya mwisho kupiga kura na siyo kweli wananchi wa kata nzima walipiga kura. Kumbukumbu zote zinaweza kupatikana wilayani na makao makuu ya CCM.

Mheshimiwa Wasira anasema kwamba nilikuwa Jaji na kesi iliyopelekwa mahakamani ni kama kesi ya tumbili kupelekwa kwa nyani, kwa maana kwamba majaji walinipendelea. Kumbukumbu za kesi hiyo zipo. Wakati huo sikuwa jaji. Isitoshe huko nyuma uchaguzi nilioshinda 1992 ulitenguliwa. Kwa nini wakati huo sikupendelewa? Kumbukumbu za kesi zinaeleza kwa nini Mheshimiwa Wasira alifungiwa kugombea kwa kipindi.

Mheshimiwa Wasira ni kiongozi wa Taifa kwa kipindi kirefu. Ni mbunge wangu na namtambua hivyo. Tunaweza kuwa na mtazamo tofauti katika baadhi ya mambo lakini hiyo si sababu ya kusema mambo yasiyo ya kweli kwa nia ya kujijenga kisiasa.

Yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Yeye ni Waziri mwandamizi. Yeye anafikiria kugombea urais. Ni vizuri basi akajifunza kusema kweli (ambayo ni ahadi mojawapo ya WanaCCM). Akumbuke anayosema yanaweza kumrudia mbele ya safari.

J.S. Warioba

24-09-2014

MWANANCHI.

Featured

Katiba Mpya: Ni mchezo wa namba

Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba Andrew Chenge.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba Andrew Chenge.

Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba jana ilikabidhi bungeni Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ikiwa na ibara 289 kulinganisha na 271 za Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.

Rasimu hiyo pia ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Akiwasilisha rasimu hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge aliliambia Bunge kuwa Ibara 233 za rasimu hiyo zinatokana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Chenge, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema ibara 47 za Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba zimebaki kama zilivyokuwa, 186 zimefanyiwa marekebisho, 28 zimefutwa na 41 ni mpya.

Rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa imefuta kabisa muundo wa Muungano wa shirikisho ambao ungezaa muundo wa serikali tatu na badala yake imerudisha muundo wa sasa wa serikali mbili.

Chenge alisema kamati za Bunge hilo pamoja na wajumbe walio wengi, waliona kuingiza muundo wa shirikisho ilikuwa ni kukiuka makubaliano ya Muungano yaliyofikiwa mwaka 1964.

Kwa kurejesha muundo wa serikali mbili uliokuwa ukipigiwa chapuo na CCM, Rasimu hiyo imependekeza kuwapo kwa makamu watatu wa rais.

Chenge alisema uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgombea mwenza atakayekuwa makamu wa kwanza wa rais.

Chini ya muundo huo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), atakuwa makamu wa pili wa rais ilhali Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa makamu wa tatu wa rais.

Chenge alisema mapendekezo hayo yamezingatia ukweli kuwa kuwapo kwa mgombea mwenza anayekuwa makamu wa kwanza wa rais, kutafanya rais na makamu wake kutoka chama kimoja.

Rasimu hiyo inayopendekezwa, imepunguza Tunu za Taifa kutoka saba zilizokuwamo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba hadi nne huku mambo ya muungano yakiongezwa kutoka saba hadi 14.

Katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Tunu za Taifa zilikuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa; sasa zimebaki Lugha ya Kiswahili, Muungano, utu na undugu na amani na utulivu. Tunu tatu ambazo ni uzalendo, uadilifu na umoja zimeondolewa.

Mambo ya Muungano

Katika Rasimu ya Tume, mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ulinzi na usalama.

Mambo mengine yalikuwa ni uraia na uhamiaji, sarafu na benki kuu, mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.

Rasimu inayopendekezwa imetaja mambo ya muungano kuwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama, usafiri wa anga, uraia, uhamiaji, polisi, sarafu na benki kuu na kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania na kusimamiwa na idara ya forodha.

Mengine ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani, elimu ya juu, Baraza la Taifa la Mitihani, Utabiri wa Hali ya Hewa na utumishi Serikali ya Jamhuri.

Mambo mengine ambayo yalikuwa katika Rasimu ya Warioba yaliyowekwa kando ni pendekezo la wabunge kutokuwa mawaziri ikipendekezwa utaratibu wa sasa wa wabunge kuwa mawaziri uendelee kutumika.

Chenge alisema Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, imeweka ukomo wa mawaziri kuwa wasizidi 30 wakati naibu mawaziri watateuliwa kulingana na mahitaji mahsusi. Tume ya Warioba ilipendekeza mawaziri wasiozidi 15.

Rasimu hiyo inayopendekezwa imefumua muundo wa Bunge uliopendekezwa na Rasimu ya Warioba kuwa wawe 75 wa kuchaguliwa majimboni na watano kutoka kundi la watu wenye ulemavu, badala yake imesema muundo wa sasa uendelee ukiwa na wabunge 360 kwa sharti la kuwapo uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume.

Rasimu hiyo imetupilia mbali pendekezo la mtu anayetaka kugombea ubunge awe na elimu isiyopungua kidato cha nne na kurudisha kuwa ajue tu kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.

“Haki ya wananchi kumwajibisha mbunge kabla ya miaka mitano imeondolewa kutokana na mapendekezo ya kamati na wajumbe na watafanya hivyo baada ya miaka mitano,” alisema.

Rasimu hiyo imembana mgombea binafsi wa ubunge kwamba atakoma kuwa mbunge pale tu itakapotokea amejiunga na chama chochote cha siasa nchini.

Pendekezo la Warioba la kutaka Spika wa Bunge na Naibu wake wasitokane na wabunge wa Bunge la Jamhuri au kuwa viongozi wa juu wa vyama, nalo limewekwa kando na badala yake spika kupendekezwa achaguliwe miongoni mwa wabunge au kutoka kwa Watanzania wenye sifa ambao watajitokeza kuomba nafasi hiyo kama ilivyo sasa.

Hata hivyo, Chenge alisema wamependekeza Naibu Spika ni lazima atoke miongoni mwa wabunge.

Mgombea binafsi

Chenge alisema pamoja na kwamba mgombea huru wa nafasi ya urais ni haki ya kikatiba, lakini kamati yake imelazimika kuchukua tahadhari na kuweka masharti juu ya mgombea huyo.

Masharti hayo ni pamoja na kuweka kipengele katika Katiba kinacholitaka Bunge kutunga sheria itakayoweka masharti ya mgombea huru ikiwamo idadi ya watu watakaohitajika kumdhamini.

Pia sheria hiyo itaweka sharti la lazima linalomzuia kujiunga na chama chochote cha siasa, kuainisha vyanzo vya mapato vya kugharimia kampeni zake na kuweka wazi ilani yake ya uchaguzi.

Masuala ya kuingizwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuruhusiwa kwa uraia wa nchi mbili ambayo yaliwagawa wajumbe wa Bunge hilo katika makundi mawili nayo hayakuingizwa katika rasimu hiyo.

Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Chenge alisema kamati yake imezingatia mijadala ya wajumbe, taarifa za kamati za Bunge hilo na Katiba za nchi mbalimbali katika kufikia uamuzi huo.

Alisema katiba inayotungwa inahusu Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Juu hivyo masuala ya Mahakama ya Kadhi yanaweza kusimamiwa na sheria inayohusu mahakimu.

Kuhusu suala la uraia pacha, Chenge alisema waliozaliwa Tanzania lakini wakapoteza uraia na kuamua baadaye kurudi nchini, watarejeshewa uraia wao baada ya kuukana uraia wa nje. Alisema Watanzania wanaoishi nje ya nchi wakiwa na uraia wa nchi hizo, watakapokuja nchini hawatakuwa na uraia wa nchi mbili, badala yake watapewa hadhi maalumu.

Baada ya kukamilika kwa uwasilishaji huo, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alitoa fursa kwa wajumbe wa Bunge hilo kuipitia Rasimu jioni na leo watakutana kwenye kamati zao 12 kwa lengo la kuhakiki ni kwa kiasi gani waliyoyapendekeza wakiwa ndani ya kamati na kwenye mijadala yamezingatiwa.

Kesho wajumbe wote watakutana katika Bunge zima kwa lengo la kuhakiki kwa pamoja kuhusu yale yatakayoletwa na sekretarieti kutoka kwenye kamati za Bunge hilo. Septemba 28, wajumbe hao watakutana tena kwenye kamati kwa lengo la kupewa maelekezo ya namna ya kukaa ndani ya ukumbi na pia namna watakavyopiga kura siku inayofuata.

Sitta alisema upigaji wa kura utaanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 na baada ya hapo itajulikana kama rasimu hiyo imepitishwa kwa wingi wa kura wa theluthi mbili kwa pande zote za Muungano au la.

Mwananchi.

Featured

Dk.. Shein:Tutaendelea Kuhakikisha Malengo ya Elimu katika Mipango Yote ya Maendeleo Yanatekelezeka

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Walimu na Wanafunzi katika Sherehe za Miaka 50 ya Elimu bila malipo zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa Amaan Studium Mjini Unguja jana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Walimu na Wanafunzi katika Sherehe za Miaka 50 ya Elimu bila malipo zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa Amaan Studium Mjini Unguja jana.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa malengo yote katika mipango ya maendeleo ya nchi yanayohusu uimarishaji wa elimu yanafikiwa na kutoa matokeo yanayotarajiwa.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Elimu bila Malipo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Amaan mjini Unguja leo, Dk. Shein amesema Serikali inatambua kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi yanategemea kuimarika kwa kiwango cha elimu hivyo ndio maana suala la uimarishaji wa elimu limepewa kipaumbele katika mipango mbalimbali ya maendeleo.

Aliitaja mipango hiyo kuwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo 2020, Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II),Mpango wa Maendeleo ya Elimu, Malengo ya Milenia ya Elimu na Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010.

Katika kufanya hivyo, aliwaambia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuongeza nafasi za masomo katika viwango vyote kuanzia skuli za maandalizi hadi chuo kikuu ili kutoa fursa kwa kila mtoto kupata elimu katika ngazi zote.

Sambamba na kuongeza fursa za masomo, kwa upande mwingine alisema Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi zote unazidi kuongezeka kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mazingira ya utoaji elimu nchini.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuzipatia skuli vifaa na nyezo za kisasa za kufundishia ikiwemo vitabu, vifaa vya maabara, kompyuta na walimu bora ili kuwawezesha wanafunzi kufaulu masomo yao vyema.

Dk. Shein alitoa mfano wa hatua mzuri iliyofikiwa katika kuwapatia wanafunzi vitabu katika skuli za sekondari ambapo alieleza kuwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Marekani hivi sasa kila mwanafunzi katika ngazi hiyo ana vitabu vya masomo anavyovidhibiti mwenyewe na kwenda navyo nyumbani.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. shein alitoa wito kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuendeleza juhudi za ufundishaji wa taaluma ya tekinolojia ya habari na mawasiliano katika skuli za Unguja na Pemba ili Zanzibar iweze kwenda sambamba na maendeleo na mabadiliko ya karne 21 ambayo yanazingatia matumizi ya tekinolojia hiyo.

Hata hivyo ameitaka wizara hiyo kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti matumizi kwa kutunga kanuni zinazokataza matumizi mabaya ya mitandao na simu za mikononi kwa wanafunzi maskulini.

Kuhusu maslahi ya walimu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuwapatia mafunzo zaidi pamoja na kuwaongezea mishahara kadri uchumi unavyokua na hali inavyoruhusu.

Dk. Shein alizungumzia pia suala la ukosefu wa ajira kwa wahitimu wengi wanaomaliza vyuo mbali mbali huku akitambua changamoto inayowakabili wengi wa wahitimu hao ya kukosa maarifa ya kutosha kujiajiri hivyo kutegemea ajira.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Awali Bibi Zahra Ali Hamad alieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta ya elimu na kuongeza kuwa ongezeko kubwa la bajeti ya elimu mwaka hadi mwaka ni hatua inayodhihirisha umakini wa Serikali katika kuimarisha elimu nchini.

Tarehe kama leo 1964, miezi tisa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Sheikh Abeid Amani Karume alitangaza elimu bila malipo kwa kila mwananchi na kuondosha kabisa ubaguzi katika mfumo wa elimu Zanzibar.

Mapema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiri wa Baraza laMapinduzi alipokea maandamano ya wanafunzi kutoka skuli mbalimbali za Unguja na Pemba na baadae kufuatiwa na burudani za vikundi vya sanaa na michezo.

IKULU.

Featured

Siri ya AG Z’bar kujiuzulu Bunge la Katiba yabainika

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman

SIRI ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, imebainika.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kamati ya Uandishi ya Bunge hilo, kililiambia MTANZANIA kuwa wakati vikao vya kamati hiyo vikiendelea, Othman alipendekeza mambo 17 yenye maslahi kwa Zanzibar yaingizwe ndani ya Katiba inayopendekezwa na Bunge, lakini yakakatiliwa.

Kujiuzulu kwa kigogo huyo wa SMZ kulizua taharuki ya ndani ya Bunge la Katiba na hata baadhi ya wajumbe kutaka kujua sababu ya kufikia hatua hiyo.

Kikiendelea kufafanua suala hilo, chanzo hicho kilisema baada ya kukataliwa kwa maswala hayo, Othman aliamua kumwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, na kumweleza uamuzi wake wa kujiuzulu.

Kutokana na sintofahamu hiyo, iliwalazimu viongozi wa juu wa CCM kukutana kwa dharura na kuazimia kufukuzwa kazi kwa mwanasheria huyo kwa kile walichodai amekisaliti chama.

Chanzo hicho kilisema baada ya Othman kupata taarifa hiyo, aliwasiliana na Ikulu ya Zanzibar na kuomba nafasi ya kukutana na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

“Baada ya kukutana na Dk. Shein, Othman alieleza namna Kamati ya Uandishi ilivyopinga kuingizwa kwa mambo 17 ambayo yana maslahi kwa Zanzibar. Kutokana na uzito wa hoja hizo, kiliitishwa kikao cha Baraza la Mapinduzi.

“Kikao hicho kiliwashirikisha mawaziri wote wa SMZ wakiongozwa na Mwenyekiti Dk. Shein, walipewa taarifa hiyo na kuijadili kwa kina na kisha kukubaliana na hoja za Mwanasheria Mkuu juu ya masuala hayo 17.

“Kikao kile chini ya Dk. Shein kiliazimia hoja hizo 17 ziwasilishwe kwenye Baraza la Mawaziri la Muungano,” kilisema chanzo chetu.

Hatua hiyo ya Baraza la Mapinduzi kuungana na Othman, ilifanya juzi Baraza la Mawaziri la Muungano chini ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukaa, na pamoja na mambo mengine lilijadili hoja 17 za SMZ na kukataa baadhi yake.

Taarifa zilizopatikana mjini Dodoma tangu kujiuzulu kwa mwanasheria huyo, zinasema baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wamekuwa na vikao vya siri lengo likiwa ni kushinikiza mambo hayo 17 kuingizwa kwenye Katiba mpya.

Katiba hiyo inayopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa leo kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Kabla ya kujiuzulu, Othman mara kadhaa alinukuliwa na vyombo vya habari akitetea muundo wa Muungano wa Serikali tatu.

KAULI YA IKULU Z’BAR

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Hassan Hassan, alikana kuwapo kwa taarifa hizo huku akitaka atafutwe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

“Hakuna kikao chochote kilichoketi na kujadili suala la Mwanasheria Mkuu ila ninachoweza kusema mtafute Makamu wa Pili yeye ndio msemaji wa Serikali,” alisema Hassan.

Mtanzania.

Featured

Hatima ya Bunge la katiba kujulikana kesho

Wakili wa Said Kubenea, Peter Kibatara (kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Said Kubenea, Peter Kibatara (kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Hatima ya Bunge la Katiba huenda ikajulikana kesho wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar  es Salaam itakapotoa hukumu ya kesi ya kulipinga Bunge hilo iliyofunguliwa  na mwanahabari Saed Kubenea.

Uamuzi huo ulifikiwa jana baada ya kumaliza kusikiliza hoja za pande zote, upande wa mdai (Kubenea) na upande wa mdaiwa (Serikali).

Katika kesi hiyo namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea  anaiomba  mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu hicho kuhusu mamlaka ya Bunge hilo na pia itamke iwapo lina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni.

Kabla ya mahakama kufikia hatua hiyo ya kupanga tarehe ya kutoa hukumu yake kwanza, kuliibuka mvutano wa kisheria kuhusu utata wa tafsiri ya kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 katika lugha mbili zilizotumika kuandika sheria hiyo.

Utata huo unatokana na tofauti ya tafsiri ya kifungu kinachohojiwa katika toleo la lugha ya Kiingereza na la Kiswahili. Utata huo uliibuliwa na Jaji Aloysius Mujulizi. Majaji wengine katika jopo hilo ni Augustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.

Baada ya mabishano makali mahakama iliwataka mawakili wa pande zote kufika mahakamani kesho kwa ajili ya kusikiliza hukumu endapo itakuwa imekamilika na iwapo itakuwa bado, basi mahakama itatoa maelekezo mengine.

Mwananchi.

Featured

KATIBA MPYA: Bunge kutuma ofisa Saudia kusimamia kura

Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge akionyesha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kabla ya kumkabidhi Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Rasimu hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge akionyesha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kabla ya kumkabidhi Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Rasimu hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo.

Ofisi ya Bunge la Katiba itamtuma ofisa wake kwenda Makka, Saudi Arabia kusimamia upigaji kura kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa wajumbe wa Bunge hilo wanaokwenda Hijja.

Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alipotakiwa kueleza idadi kamili ya wajumbe wa Bunge hilo wanaotarajiwa kuwa nje ya nchi na jinsi watakavyopiga kura.

Juzi, Bunge hilo lilizifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwaruhusu wajumbe watakaokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge wakiwamo wanaokwenda Hijja kuipigia kura Katiba inayopendekezwa, iliyokabidhiwa kwa Kamati ya Uongozi jana.

Chini ya marekebisho hayo, mjumbe aliye nje ya Bunge, ataruhusiwa kupiga kura ya wazi au ya siri kwa njia ya fax au mtandao kama itakavyoelekezwa na katibu kwa kushauriana na mwenyekiti.

Hamad alisema hadi kufikia jana mchana walikuwa wamewatambua wajumbe wanane ambao watakwenda Hijja huko Uarabuni lakini orodha ya watakaokuwa nchi nyingine bado haijajulikana.

Hamadi alisema ofisa wake huyo atasimamia kura za wajumbe wanaokwenda Hijja katika upigaji kura unaotarajiwa kuanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 mwaka huu.

Alisema ni vigumu kutaja vituo watakavyopigia kura sasa kwa sababu bado hawajawauliza wajumbe wengine waliopo nje ya nchi ambao wangependa kupiga kura wakiwa huko.

Kuhusu iwapo watapiga moja kwa moja kwa mtandao au watapiga kwenye karatasi na kutoa vivuli, Hamad alisema suala hilo litaamuliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Samuel Sitta.

Ukawa wapinga

Wenyeviti wenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia wamelishukia Bunge hilo kwa kuruhusu upigaji kura nje ya nchi.

Akizungumza jana, Profesa Lipumba alisema kilichofanywa na Sitta na wajumbe wake ni uchakachuaji unaoweza kuliingiza Taifa kwenye mgogoro mkubwa.

“Kwanza taratibu za kura mabunge ya Jumuiya ya Madola ni kura zote zinapigwa ndani ya Bunge. Unapozungumzia akidi imetimia ni wajumbe walioko ndani ya Bunge,” alisema Profesa Lipumba.

Kanuni mpya ya 30 (1) baada ya marekebisho yaliyofanyika juzi inasomeka, “Akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalumu itakuwa ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu.”

Awali, kanuni hiyo iliweka sharti la lazima kwamba akidi ya kikao itakuwa ni nusu ya wajumbe, isipokuwa kwa kikao kinachohusu kupitisha uamuzi wa Bunge Maalumu.

“Mwenyekiti hawezi tu kutangaza kuwa akidi imetimia kwa sababu nimepata barua kuna wajumbe wako nje kwa hiyo watapigia kura huko. Ni uvunjifu wa sheria na taratibu ulio wazi,” alisisitiza.

“Hakuna maridhiano lakini zaidi ya hapo huu mchakato wote umeshaharibika. Kinachofanyika hapo ni Sitta kujaribu kuhalalisha matumizi ya Sh20 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo,” alisema.

Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema kinachofanywa na Sitta ni kuhakikisha wanatoka na Katiba hata kama haina uhalali wa kisiasa.

“Kwa hiyo inabidi lazima atoke na kitu ili aseme tumepitisha uamuzi tumetoka na Katiba hii ili kuhalalisha matumizi,” alisema Lipumba na kuhoji uharaka huo wa Sitta ni wa nini?

“Kama muda hautoshi kwenda kwenye kura ya maoni kulikuwa na sababu gani ya kuendelea na mchakato huo. Mchakato wa Katiba unakwenda katika utaratibu wa sheria,” alisema.

Profesa Lipumba alisema sheria iko wazi na iliweka utaratibu kuwa baada ya kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, isipite siku zaidi ya 120 bila kura ya maoni kufanyika.

“Ni wazi sheria yenyewe itabidi ibadilishwe. Rais atakayekuja akiwa makini hawezi kukubali kuanza na Katiba iliyowagawa Watanzania. Rais gani atakubali kuanza na migogoro ya kisiasa?” alihoji Lipumba.

“Waziri wa Katiba wa SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) hashiriki, AG (Mwanasheria Mkuu) wa Zanzibar hashiriki Katiba ya nchi, watu wa Zanzibar hawashiriki utasemaje ina uhalali wa kisiasa?”

Mbatia alisema anamshangaa Sitta kujigamba kutoka na Katiba inayopendekezwa wakati itakwenda kukaa kabatini kusubiri utashi wa rais ajaye.

“Hatuna kura ya maoni kwa hiyo haiwezi kutumika. Kwa hiyo ikishapokewa inawekwa kabatini. Rais ajaye ni mwingine, sisi tunaendelea na mikakati yetu ya marekebisho ya 15 ya Katiba,” alisema.

Kuahirishwa kwa kura ya maoni kunatokana na makubaliano kati ya viongozi wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete yaliyofikiwa Septemba 8, mwaka huu.

Mwananchi.

Featured

Kesi ya Katiba kuanza kuunguruma leo

Wakili wa Said Kubenea, Peter Kibatara (kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Wakili wa Said Kubenea, Peter Kibatara (kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo itaanza kusikiliza kesi ya msingi ya kikatiba ya Bunge Maalumu la Katiba.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi la Serikali dhidi ya shauri lililofunguliwa na Wakili Peter Kibatala kwa niaba ya Mwandishi wa Habari, Saed Kubenea.

Shauri litakalosikilizwa ni la kuomba tafsiri ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na tamko kuhusu mamlaka ya Bunge la Katiba pamoja na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kubenea, anaiomba Mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba kwa kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.

Pia, anaiomba Mahakama itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Augustine Mwarija, Dk. Fauz Twaib na Aloyisius Mujulizi, litaanza kusikiliza kesi hiyo ya msingi leo.

Awali, Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya kusimamisha kwa muda vikao vya Bunge vinavyoendelea Dodoma.

Kesi hiyo yenye namba 28 ya mwaka 2014, ilifunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

TanzaniaDaima.

Featured

Ulinzi waimarishwa mara dufu bungeni

Jeshi la Polisi likiendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma.
Jeshi la Polisi likiendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo maeneo mbalimbali ya mji wa Dodoma.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kuleta kiwewe ndani ya Bunge la Katiba ambako sasa ulinzi umeonekana kuongezwa mara dufu.

Wakati wote kumekuwa na simulizi ya ulinzi ulioimarishwa katika viwanja vya Bunge la Katiba tangu kuanza kwake Februari 18, mwaka huu, ingawa kwa sasa umeongezeka mara dufu.

Tangu Chadema walipotangaza nia yao ya kufanya maandamano ya kupinga kuendelea kwa Bunge hilo, vyombo vya ulinzi viliweka mkakati wa kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kupenya na kulifikia jengo hilo bila kibali maalumu.

Jana, Polisi waliongeza umbali wa ulinzi katika kulifikia jengo la Bunge na hakuna gari wala mtu aliyeweza kuwapita polisi hao bila ya kukaguliwa na kuulizwa vibali.

Kwa muktadha huo, ili kufikia sehemu ya ukumbi wa Bunge, kulimlazimu mtu kama mwandishi wa Habari kuvuka vizuizi vitatu ndipo afike sehemu ya kufanyia kazi zake.

Mwananchi.

Featured

Bunge lapitisha upigaji kura kwa fax, email

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu la Katiba, Pande Ameir Kificho akijibu hoja za wajumbe waliochangia mjadala wa kupitisha marekebisho ya kanuni za bunge hilo mjini Dodoma jana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu la Katiba, Pande Ameir Kificho akijibu hoja za wajumbe waliochangia mjadala wa kupitisha marekebisho ya kanuni za bunge hilo mjini Dodoma jana.

Bunge la Katiba limeingia katika historia baada ya kupitisha kanuni zinazoruhusu wajumbe wake watakaokuwa nje ya nchi kupiga kura kwa njia ya nukushi (fax) na baruapepe (email).

Uamuzi huo ulifikiwa bungeni Mjini Dodoma, baada ya wajumbe wa Bunge hilo kupitisha azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni ya 30, 36 na 38 za Bunge hilo za mwaka 2014.

Hata hivyo, wajumbe watatu kati ya 15 waliochangia azimio hilo, walipinga vikali marekebisho hayo, lakini yalipitishwa kwa wingi wa kura baada ya Mwenyekiti, Samuel Sitta kulihoji Bunge.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa raia wa Tanzania kupiga kura akiwa nje ya nchi, uamuzi ambao Sitta aliutetea akisema wanaoupinga wanachanganya kati ya kura ya uamuzi na kura ya uchaguzi.

Mwakilishi wa walimu, Ezekiah Oluoch alisema Kifungu cha 16 (6) cha Kanuni za Bunge kinamtaka mwenyekiti kuendesha Bunge kwa mujibu wa sheria walizonazo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na sheria nyingine za nchi.

“Hoja ya walioko nje ya Bunge hili kupiga kura, siiungi mkono na wengi mkiunga mkono mtakuwa mmekiuka sheria … kila raia ana haki ya kupiga, Katiba yetu inaeleza, ilimradi atimize miaka 18 lakini haki hiyo imewekewa pia utaratibu wa kisheria,” alisema.

Alisema kwa taratibu zilizowekwa nchini, hakuna unaomruhusu mtu aliyeko nje ya eneo la kupiga kura kufanya hivyo.

Hata hivyo, Sitta aliingilia kati akisema mjumbe anasema uongo, akimtaka aeleze ni kura ipi anayoizungumzia na kifungu gani kimesema hilo, naye akajibu kura anazozungumzia ni zote ikiwamo ya kufanya uamuzi ndani ya Bunge.

“Unasema uongo mtupu wewe … sheria ya uchaguzi, tunamchagua nani hapa?” alihamaki Sitta na hali kama hiyo aliionyesha pia kwa wajumbe wengine waliokuwa wakipinga marekebisho hayo.

Oluoch alisema anachoona ni kuwa si halali kwa mjumbe ambaye hayuko ndani ya Bunge kupiga kura na kutaka Bunge lisifanye mambo kwa sababu linataka kutimiza mambo ambayo si msingi wa sheria.

“Uamuzi wowote huo tunaotaka kufanya kwa lengo la kupata utashi wa kisiasa, mimi nitasimama peke yangu kukataa na itaingia kwenye hansard (kumbukumbu za Bunge) kwamba nilikataa jambo hili,” alisema.

Kwa upande wake, Said Arfi alisema hakubaliani na azimio hilo kwa sababu Kanuni ya 38 ilikuwa imeshaweka utaratibu na haoni kuwapo haja ya kufanya marekebisho.

“Jambo hili tunalofanya ni kubwa sana, kuandika Katiba ya Taifa letu ni lazima tuwe na nia zilizokuwa njema ili kulipatia Taifa Katiba ambayo itaridhiwa na Watanzania. Sioni sababu zozote za msingi kwa wajumbe ambao hawapo humu ndani kupiga kura.”

Arfi alisema uzoefu wa mabunge mengi duniani wanaopiga kura ni watu waliomo ndani ya ukumbi wa Bunge tu… “Sasa hii ya kwenda kuwatafuta watu huko waliko hauna uhakika anayepiga kura ndiye, ni shaka tupu. Kwa kweli mheshimiwa mwenyekiti Watanzania watatutazama juu ya nia zetu na dhamira zetu juu ya kulipatia Taifa Katiba maridhawa,” alisema.

Alisema kura ni hiari na mjumbe anaweza kuwapo ndani ya Ukumbi wa Bunge na kuacha kupiga kura na kuonya kuwa kuwalazimisha na kuwatafuta watu ili wapige kura si jambo la kidemokrasia.

Wakati akiendelea, Sitta aliingilia kati na kumhoji nani anayelazimisha mtu kupiga kura? Arfi akamjibu;

“Unapotuingilia katika michango yetu Watanzania wanakupima. Watanzania wanakuheshimu mwenyekiti.”

Kwa upande wake, Ali Omary Juma alisema Katiba ni maridhiano ya nchi mbili huru na si busara kuharakisha kupiga kura kwa watu ambao hawamo ndani ya Bunge.

Alisema kama hilo litaruhusiwa itakuwa ni mgongano mkubwa wa kisheria ambao utaleta ufa mkubwa kama uliojitokeza baina yao na Ukawa … “Nashauri suala la kura tulisitishe ili kutoa fursa pana ya mashauriano na kutoa muda ili wajumbe wote tuhudhurie.”

Mjumbe Paul Makonda aliunga mkono hoja hiyo akisema wajumbe zaidi 600 kuwa mahali pamoja si jambo rahisi:

“Nakumbuka tukiwa kwenye kamati yetu siku moja mtu alilazimika kutoka hospitalini. Ni mgonjwa lakini afanyeje, lakini kama kuna uhuru wa kupiga kura pale alipolala ni jambo la heri.

“Hatutafuti kura mpya. Hapa tunatafuta kupiga kura kwa wale watu ambao walishajadili jambo hili, haina maana tunatafuta kuokotaokota kama tumepungukiwa, hatujapungukiwa hata kidogo.”

Baadaye Sitta alisimama na kusema ipo dhana inayojengeka kwamba utaratibu huo unalenga kulazimisha kila mjumbe kupiga kura ili tu theluthi mbili ipatikane, hivyo akataka wajumbe waache kupoteza muda … “Hii ni dhana ya ajabu na ina nia mbaya ndani yake. Mmoja wa watu ambao ameomba apige kura yuko hospitali India, nina mamlaka gani ya kumkatalia?”

“Tumempigia Balozi atamwapisha atapiga kura ya siri italetwa na itafunguliwa humu. Zote hizo zitafunguliwa humuhumu ndani ya ukumbi na majina yatasomwa,” alisema Sitta.

“Watakaopiga kura mbele ya mabalozi wetu kwa wazi, Record (kumbukumbu) yote italetwa hapa na mtashuhudia hapa majina yatatajwa moja moja kama kanuni zinavyotaka,” alisema Sitta na kuongeza;

“Mambo haya ni ridhaa ya mtu, hakuna mtu atalazimishwa. Kama kuna hao wanasimama hapa wanasema wanalazimishwa, kama wameshindwa kuchangia hoja hii wasipoteze muda.”

Akijibu hoja za wajumbe, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho alisema wakati wa kuhakiki mjumbe halali, wale walioko watawasilisha pasi za kusafiria.

Wasomi wapinga

Akizungumzia uamuzi huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema uamuzi huo ni dalili za kupaparika kwa sababu kila kona Watanzania wanapinga kuendelea kwa vikao vya Bunge hilo.

“Tanzania hatujafikia hatua ya kuruhusu wananchi wapige kura wakiwa nje ya nchi yao, iweje leo tukubali jambo hili kirahisi namna hii, kuna nini nyuma yake? Wanachokifanya bungeni wananchi wanakifuatilia na watambue wazi kuwa hiyo Katiba watakayoipitisha itapingwa.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema, “Kama wamekubaliana kubadili kanuni sawa, ila lazima tujiulize kwa nini sasa. Kwa nini wabadili kanuni hizi ili kupiga kura tu?”

Dk Bana alisema hakuna ulazima wa kuharakisha mambo ili kupata Katiba Mpya kutokana na hali halisi iliyopo sasa.

“Nasubiri kwa hamu kuiona hiyo Rasimu wanayotaka kuipigia kura ili niilinganishe na iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kuanzia hapo tutaanza kuhoji kama mambo yatakuwa tofauti,” alisema.

Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu UDSM, Faraja Christoms alisema sheria za nchi zinatakiwa kwenda sambamba na Katiba ambayo ni sheria mama, hivyo kuruhusu upigaji wa kura wa aina hiyo ni kinyume na sheria.

Aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema, “Unaweza ukabadili kanuni lakini haitakuwa na maana kama hakutakuwa na maridhiano.”

Mwananchi.

 

Featured

Mbunge CHADEMA amuonya Turky wa CCM

MBUNGE wa viti Maalum, Mariam Msabaha (CHADEMA), amemuonya mbunge mwenzake wa Mpendae kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Turky na kumtaka aache tabia ya kutumia madaraka na kinga za kibunge kunyanyasa wananchi katika masuala yasiyohusiana na siasa.

Mbali na kumuonya kwa tabia ya unyanyasaji, pia Msabaha amesema mbunge huyo anapaswa kuwaomba radhi wabunge wenzake wa kutoka Zanzibar, kwa kile alichoeleza kuwa tabia ya kujisifu, kukebehi na kuonyesha jeuri wananchi, kwani si asili na utamaduni wa wazanzibari.

Kutokana na hali hiyo, Msabaha alisema anajiandaa kukabidhi CD za vitisho vilivyofanywa na Turky, ofisi ya Spika wa Bunge kwa ajili ya hatua zaidi.

Msabaha, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea taarifa mbalimbali zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vinavyomuonesha Mbunge Turky, akitoa lugha ya kuudhi kwa wananchi mbele ya askari Polisi.

Katika mitandao hiyo, pamoja na CD iliyogawiwa kwa waandishi wa habari na Msabaha, Turky, anakaririwa akiwaeleza washindani wake katika mgogoro wa msikiti wa Sunni, kuwa ni sawa na CHADEMA huku akiwaeleza kuwa hawana jambo lolote watakaloweza kufanya zaidi ya kupiga kelele.

Msabaha, alisema kuelezea kuwa CHADEMA haiwezi kufanya jambo lolote ni matusi na kukengeuka kwa mbunge huyo, kwa kuwa hata wananchi waliomchagua hawaujui msaada wake zaidi ya kusikia akiongoza migogoro katika matukio tofauti.

“Kwanini Turky atumie ubunge wake kama fimbo ya kuwanyanyasa wengine katika masuala ya kijamii, mfano ni hivi karibuni alipowajaza askari katika ukumbi wa uchaguzi pale Blue Pearl wakati waumini wa madhehebu ya  Sunni walipokuwa wakifanya uchaguzi, lengo lake likiwa ni kuwatisha na kuwaweka watu anaowataka yeye, huku akiwatambia wapinzani wake kuwa hawana sauti kama CHADEMA, hapa anakiingizaje chama chetu katika masuala binafsi ya kiimani,” alisema Msabaha.

Aliongeza kuwa watu wanaopewa mamlaka ya kuwaongoza wananchi na kuamua kuyatumia vibaya mamlaka hayo kwa kuwatisha waliompa nafasi hiyo, mwisho wake huwa ni machafuko makubwa na kwamba Mbunge Turky anataka kuleta hayo machafuko.

Alisema kiburi cha Turky kimepitiliza hata kwa mamlaka za Umma, kwa kile alichoeleza kuwa hivi karibuni ofisi ya msajili wa vizazi na vifo (RITA), iliagizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania ithibitishe wapiga kura wa baraza la wadhamini wa msikiti wa Sunny, lakini Mbunge huyo akalazimisha kufanyika kwa uchaguzi na kujaza polisi idadi ambayo haikutegemewa.

Jitihada za kumpata Turky kuelezea tuhuma za kutumia madaraka yake ya kibunge kuwanyanyasa wananchi na kukidhalilisha CHADEMA, zilishindikana baada ya simu yake ya kiganjani kutokupokewa na hata alipotumiwa ujumbe wa maneno hakujibu

TanzaniaDaima.

Featured

CCM wafanya vurugu mkutano wa CUF

Wafuasi wa CUF wakiwa katika Mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama hicho Buguruni jijini Dar es salam ambao ulivamiwa na CCM.
Wafuasi wa CUF wakiwa katika Mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama hicho Buguruni jijini Dar es salam ambao ulivamiwa na CCM.

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na wafuasi wao wanadaiwa kuvamia eneo la mkutano uliokuwa umeandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano wao wa hadhara.

Akizungumza na Tanzania Daima, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya, alisema, viongozi wa CUF walikuwa wameshafuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kutoa taarifa polisi na kupewa ruhusa kwa maandishi, lakini cha kushangaza walikuta eneo hilo waliloomba kukiwa na mabanda yaliyoandaliwa kwa ajili ya mkutano wa hadhara wa CCM.

“Baada ya kukuta kuna viongozi wa CCM wameweka mabanda yao wanataka kuhutubia mkutano, niliwataarifu vijana wa CUF kuondoa kwa sababu tulikuwa tumefuata sheria, CCM walikaidi hivyo kukatokea fujo, polisi wakaanza kufyatua risasi… ndipo alipokuja RCO wa Ilala, alikuja kuwakutanisha viongozi wa CUF na CCM ikabainika kuwa CCM hawakuwa hata na barua, hivyo waliambiwa waondoke wakagoma hadi polisi walipowatawanya kwa mabomu ndio nikaanza kuhutubia mkutano,” alisema Kambaya.

Taarifa zaidi kutoka eneo hilo zilisema, polisi baada ya kubaini kuwa CCM hawakuwa na barua, walianza kuwabembeleza, tofauti na kama ingekuwa chama cha upinzani kingevamia mabomu yangeanza mara moja.

Katika mkutano huo, Kambaya alivialika vyama vya CUF, NCCR, CHADEMA na NLD kujenga misingi ya kuweka bendera kwenye eneo la ofisi ya Ofisa Mtendaji Kata ya Buguruni kwa madai kuwa CCM tayari wameshajenga, na kwa kuwa hilo ni eneo la serikali ambalo hawapaswi kujenga misingi ya vyama hapo, itabidi vyama vingine navyo vipewe eneo hilo, au CCM wabomoe kwani hairuhusiwi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Mary Nzuki hakupatikana kuelezea fujo hizo zilizodaiwa kuzua tafrani kubwa kwa wakazi wa Buguruni kutokana na milio ya mabomu na risasi.

TanzaniaDaima.

Featured

CCM wafurahia matokeo ya Scotland, Uingereza

Katibu Mkuu wa CCM Mh. Abdul-rahman Kinana
Katibu Mkuu wa CCM Mh. Abdul-rahman Kinana

Kushindwa kujitenga kwa Scotland kutoka himaya ya ufalme wa Uingereza, kumetoa somo kwa wanasiasa kwamba hawana haki ya kuwafanyia uamuzi wananchi.

Akitoa maoni yake kuhusiana na matokeo ya kura iliyopigwa wiki iliyopita nchini humo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema sababu zilizoifanya Scotland kutaka kujitenga zinafanana na zile za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema ni vyema wananchi wakajifunza kuwa masuala kama hayo hayapaswi kujadiliwa kwa papara.

“Waandishi wengi wamenipigia simu wakitaka kujua maoni yangu…mimi nasema kuwa suala hili limetufundisha kuwa jambo jema ni kubaki katika Muungano,” alisema Kinana alipohutubia mkutano wa hadhara katika Mji Mdogo wa Mlandizi, wilayani Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani.

Kinana alisema wakati wa kampeni, Waziri Mkuu wa Scotland, Alex Salmon aliwashawishi watu kupiga kura ya kujitoa.

“Kulingana na kura za maoni watu wengi waliamini Scotland itajitoa katika himaya ya ufalme wa Uingereza, lakini matokeo ya kura yamekuwa tofauti. Hili ni funzo kwetu kuwa wanasiasa hawapaswi kuwa wasemaji wa wananchi au kuwafanyia uamuzi,” alisema na kuongeza kuwa wananchi wana haki ya kufanya uamuzi kwa mambo yanayohusu maisha yao.

Alisema kila Muungano una matatizo na suluhu ni kuyajadili kwa umakini ili kuyapatia ufumbuzi wenye manufaa kwa wananchi.

Kinana alisema matokeo ya kura hiyo yanaonyesha kuwa duniani kote watu wanapenda umoja kama ambavyo Watanzania wameudumisha.

Aliwataka wanaozungumzia kuuvunja Muungano, kujifunza kutoka Scotland ambayo imekuwa mshirika na Uingereza kwa miaka 307 sasa.

Awali, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema matokeo ya kura ya Scotland yamethibitisha kuwa Muungano wa hapa nchini utaendelea kudumu. “Kura hii imewakata kidomodomo wale wanaopigania kuuvunja Muungano wetu. Wameshaonyeshwa kuwa watu duniani kote wanapenda umoja,” alisema.

Mwananchi.

Featured

Wajumbe wa Z’bar watishwa

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.

Hali imeanza kuwa tete Bunge la Katiba kutokana na ujumbe unaosambazwa kwa kasi katika mitandao ya kijamii, ili kuwagombanisha na kuwafitinisha wajumbe wa kundi la 201 kutoka Zanzibar.

Ujumbe huo ambao gazeti hili limeuona, ulianza kusambazwa juzi, ukiwataka wajumbe wa kundi la 201 kutoka Zanzibar, kuondoka bungeni ili theluthi mbili ya Katiba inayopendekezwa isipatikane.

Upigaji wa kura kulingana na masharti ya Ibara ya 37 ya kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, unatarajiwa kuanza Septemba 29 na kukamilika Oktoba 2 mwaka huu.

Hata hivyo, taarifa nyingine zimedai ujumbe huo unatumwa na baadhi ya wanaCCM kama mbinu ya kuwakatisha tamaa kundi la 201 wanaoonekana kuwa na msimamo thabiti ili hatimaye warudi upande wa CCM kwa kuona wamenyanyapaliwa.

Ujumbe huo unaaminika unaweza kuwa ni sehemu ya propaganda kutoka kwa baadhi ya wanaCCM kutoka Maskani ya Kisonge Zanzibar ili wajumbe hao waanze kusalitiana na wale wenye msimamo wajenge chuki na kusalimu amri.

“Tunawaambia wazi wajumbe hao wa kundi la 201 watoke katika Bunge la Katiba mara moja kabla ya upigaji wa kura vinginevyo hatutawaelewa,” unasomeka ujumbe huo wa WhatsApp na kuongeza;

“Hatuhitaji wapige kura ya siri wala ya wazi. Tunachohitaji ni theluthi mbili ya Zanzibar isipatikane kabla hata ya huo upigaji wa kura”, unasomeka ujumbe huo ambao umeweka picha za baadhi ya wajumbe baadhi ya wanaCCM kama mbinu ya kuwakatisha tamaa kundi la 201 wanaoonekana kuwa na msimamo thabiti ili hatimaye warudi upande wa CCM kwa kuona wamenyanyapaliwa.

Ujumbe huo unaaminika unaweza kuwa ni sehemu ya propaganda kutoka kwa baadhi ya wanaCCM kutoka Maskani ya Kisonge Zanzibar ili wajumbe hao waanze kusalitiana na wale wenye msimamo wajenge chuki na kusalimu amri.

 “Tunawaambia wazi wajumbe hao wa kundi la 201 watoke katika Bunge la Katiba mara moja kabla ya upigaji wa kura vinginevyo hatutawaelewa,” unasomeka ujumbe huo wa WhatsApp na kuongeza;

“Hatuhitaji wapige kura ya siri wala ya wazi. Tunachohitaji ni theluthi mbili ya Zanzibar isipatikane kabla hata ya huo upigaji wa kura”, unasomeka ujumbe huo ambao umeweka picha za baadhi ya wajumbe.

“Na kama hawakutoka, tunawataka Wazanzibari wawatambue wasaliti hawa, wawalaani kwa nguvu zote na wawaorodheshe katika daftari la wasaliti wa Zanzibar kama wenzao akina Balozi Seif Ali Idd (Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar),” umesisitiza.

Balozi Idd ambaye ni kada wa CCM, amekuwa akitamka wazi kuunga mkono mchakato wa Katiba unaoendelea mjini Dodoma, tofauti na baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wanaotaka muundo utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili.

Watumaji wa ujumbe huo wanaotumia mtandao wa WhatsApp, wametaka ujumbe huo usambazwe kwa Wazanzibari wenzao waliopo ndani na nje ya nchi.

“Linalotusikitisha ni sehemu ya hili kundi la 201 ambao kwa nje wanaonyesha kuunga mkono madai ya Wazanzibari, lakini kwa ndani wanaonekana kumbe na wao ni mpini wanalitumikia shoka kuimaliza Zanzibar,”unadai ujumbe huo.

“Wazanzibari hatuko tayari kupoteza nchi yetu na vizazi vyetu kwa masilahi ya wanafiki wachache walioamua kwa njaa zao kufakamia mamilioni ya fedha ili kuiangamiza Zanzibar,” unasomeka ujumbe huo.

Baadhi ya kamati za Bunge zimependekeza Rais wa Zanzibar awe makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu awe makamu wa pili wa Rais wa muungano.

Hata hivyo, zipo kamati zilizopendekeza kuwapo makamu watatu wa Rais ambapo Rais wa Zanzibar anapendekezwa awe makamu wa kwanza wa Rais, mgombea mwenza awe makamu wa pili wa Rais na waziri mkuu awe makamu wa tatu.

Wajumbe wauona

Hata hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo kundi la 201 kutoka Zanzibar, Salma Said alikiri kuuona ujumbe huo na kwamba hana wasiwasi na kilichoandikwa  katika waraka huo kwa kuwa anaamini wametumia njia yao ya kidemokrasia ya kujieleza na kutoa maoni  yao  kama  wananchi ingawa njia waliyotumia siyo sahihi ya kuwaita watu wasaliti.

Alisema wakati huu ni muhimu wa kujenga umoja wa Wazanzibari na siyo kujenga uadui  kwa kushutumiana.

Naye Dk Alley  Nassoro kutoka kundi hilo alikiri kuuona ujumbe huo na akasema una lengo la kuwavuruga Wazanzibari wenye msimamo thabiti wa kutetea masilahi ya Zanzibar katika katiba.

“Baadhi yao walioandaa ujumbe huo tunawafahamu na wamefanya  mambo ya ajabu hata kule Zanzibar na nataka niwaambie Wazanzibar kuwa watu hao ndiyo  wametufikisha hapa tulipo,” alisema.

Dk Alley alisema ujumbe huo unasambazwa na maadui wa Zanzibar na lengo la kusambaza ni kuwafarakanisha wajumbe wanaotoka visiwani  wasiwe na mshikamano.

Mjumbe mmoja wa Bunge hilo anayetajwa kwenye ujumbe huo alisema ana matumaini bado ataendelea kuwapo bungeni kwa vile alishiriki mchakato huo tangu hatua za mwanzo za Bunge.

“Nataka niwahakikishie Wazanzibari kuwa watulie,  msimamo wetu ni thabiti wala hauyumbi. Huo ujumbe ni mbinu tu ya kutaka kutufitinisha na kutukatisha tamaa. Tumekuja kuwakilisha masilahi ya Zanzibar,” alisema mjumbe huyo na kuongeza;

“Tukiona ipo haja ya kuondoka na kuliacha Bunge tutafanya hivyo kwa masilahi ya Zanzibar. Sisi ni watu wazima na tunaamini hizi ni nchi mbili na zitabaki kuwa mbili na Zanzibar yenye dola kamili.”

Kanuni ya 37 ya Bunge la Katiba, inaeleza ili ibara au sura iweze kupitishwa na Bunge ni lazima iungwe mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na idadi kama hiyo ya wajumbe wa Zanzibar.

Ni kutokana na hofu ya kutopatikana kwa theluthi mbili, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta aliwataka mawaziri na naibu mawaziri kuwepo bungeni kuanzia Septemba 29.

Wito kama huo ameutoa pia kwa wajumbe wa Bunge hilo walioshiriki mjadala wa Bunge hilo, bila kuhusisha Ukawa waliosusia Bunge hilo tangu Aprili 16.

Sitta mara zote tangu kuanza kwa Bunge hilo Agosti 5 amekuwa akiwahakikishia Watanzania kuwa Bunge hilo litakamilisha kazi yake na kuwapatia Watanzania Katiba bora.

Hata hivyo, habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe zinadai kwamba ili Katiba hiyo iweze kupata theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar, CCM na washirika wake wanahitaji kura 79.

“Jumla ya Wazanzibar wote ndani ya Bunge ni 217 na theluthi mbili yake ni wajumbe 144 kwa hiyo ukitoa wajumbe 66 wa Ukawa ambao tayari hawapo ina maana theluthi mbili ni kura 78,” kilidokeza chanzo hicho.

Hata hivyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro amenukuliwa akisema wajumbe wote wa Bunge hilo ni 630 na kati ya hao, wajumbe waliotoka ni 130, idadi ambayo ni sawa na asilimia 21 ya wajumbe wote.

“Wajumbe waliobaki ndani ya Bunge ni 500 sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote na idadi hii ni pamoja na wajumbe 189 kutoka kundi la 201 ambao wamebaki bungeni,”alisema.

“Wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati ya hao 125 ni wanaotoka kundi la 201. Ukitazama takwimu zote hizi, wajumbe wa 201 ni sehemu ya Bunge hili,” alisema Dk Migiro na kuongeza;

“Kwa Zanzibar wajumbe waliobaki ndani ni 152 na kati ya hao 64 wanatokana na kundi la 201. Waliosusia Bunge kwa pande zote za muungano hawafikii theluthi moja ya wajumbe waliobaki.”

“Hii ina maana kwa kuzingatia matakwa ya kisheria kuwa uamuzi upatikane kwa majadiliano na kushawishiana kwa hoja, wajumbe waliobaki kwa wingi wao wanao uhalali wa kisiasa na kisheria,” alisisitiza Dk Migiro.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad alisema kuwa hajapata taarifa za kusambaa kwa ujumbe huo, lakini anaamini mtu anayefanya hivyo ana nia mbaya na Bunge hilo.

Pia, alisema ni rahisi mtu kuamini kuwa ujumbe huo unasambazwa na Ukawa kwa kuwa wao ndio waliotoka bungeni na kwamba wametangaza maandamano nchini nzima ya kupinga Bunge hilo.

“Ungeniambia ni Ukawa ningekuelewa kwa sababu wao ndio wametoka nje na wanatangaza maandamano nchi nzima…lakini kwa sababu bado sijaouna siwezi hasa kusema unaweza kuwa na athari kiasi gani kwenye Bunge la Katiba,” alisema.

Mwananchi.

Featured

Jeshi la Polisi lalaaniwa kwa kuwashambulia Waandishi

Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).  Kushoto ni Katibu wake, Neville Meena.
Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani). Kushoto ni Katibu wake, Neville Meena.

Wadau mbalimbali wa habari nchini wamelaani vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kuwashambulia na kuwajeruhi Wandishi wa habari wakiwa kazini juzi mbele ya Makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es salam.

Wandishi hao kutoka vyombo tofauti walishambuliwa wakati wakifuatilia taarifa za Mwenyekiti wa chama cha Demokrasi na Maendeleo Chadema Freeman Mbowe aliyekuwa akihojiwa na Jeshi la Poloisi kufuatia kauli yake ya kuitisha maandamano na migomo isiyo na kikomo nchi nzima kupinga kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.

Mbowe alitoa kauli hiyo wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Chadema mwishoni mwa wiki iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salam.

Wandishi walioshambuliwa ni Josephat Isango wa gazeti la Tanzania Daima, Shamimu Ausi wa gazeti la Hoja na Yussuf Badi ambae ni mpiga picha wa magazeti ya serikali (TSN) ambapo Issango alijeruhiwa mguuni na Ausi usoni karibu na jicho la kulia.

Miongoni mwa wadau waliyolaani kitendo hicho ni Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Umoja wa klabu za Wandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Bodi ya Taasisi za kutetea haki za binadamu (THRDC) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika kulaani kitendo hicho Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania Absalom Kibanda alisema Jukwaa la Wahariri linalaani kitendo cha kushambuliwa kwa wandishi wa habari kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na haki za binadamu.

Aidha Kibanda amemtaka Mkuu wa jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu kulifumua Jeshi la Polisi na kuliunda upya kwani limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kikazi kutokana na kuendelea kuwashambulia wanahabari badala ya kukabiliana na uhalifu.

Pia TEF wamemwandikia barua IGP juu ya kulaani tukio hilo na kumtaka kuchukua hatua dhidi ya polisi waliotekeleza vitendo hivyo kutokana na kujulikana kupitia picha za video na za mnato zilizopigwa.

“Jeshi la Polisi linapaswa kufanya kama kile kilichofanywa na polisi wenzao wa Brazil, Julai mwaka huu ambako askari polisi wanne walionaswa katika mikanda ya video wakiwashambulia waandishi wa habari, walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kufanyika,” alisema Kibanda.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari alisema MCT inaamini mashambulizi hayo hayakuwa bahati mbaya kwa kuwa ni mfululizo wa Jeshi hilo kuwanyanyasa waandishi wakati wakiwa katika kazi.

Aidha, Baraza hilo limeeleza kuwa mashambulizi hayo siyo tu yamelenga kuficha ukatili uliokusudiwa kufanywa, bali unaibua chuki baina ya taasisi hiyo na vyombo vya habari bila sababu za msingi.

“Unyanyasaji huu wa polisi ulifanyika mbele ya viongozi wakuu wa Jeshi akiwamo Kamishna wa Opereseheni na Mafunzo, MCT tunalishauri jeshi la polisi kuacha waandishi wa habari kufanya kazi zao badala ya kutumia nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na kuharibu vitendea kazi vyao,” ilisema taarifa hiyo.
Katika hatua nyengine Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Saed Kubenea alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za waandishi wa habari kuendelea kushambuliwa na polisi wakati wakitimiza wajibu wao.

Alisema kama hatua stahiki zisipochukuliwa vyombo vya habari na waandishi washikamane kwa pamoja kushinikiza mkuu wa jeshi hilo awajibike mwenyewe kwa kujiuzulu.

Nazo Klabu za waandishi habari nchini (UTPC), zimetoa tamko la kulaani kitendo cha polisi wa jijini Dar es Salaam kuwapiga baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Akizungumza na wanahabari jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Abubakar Kassan, alisema kitendo cha polisi kurudia vitendo vile vile vya kuwanyanyasa waandishi wa habari wanapokuwa kazini, hakina budi kulaaniwa.

Alisema inawezekana kitendo cha polisi kuwafukuza wafuasi wa Chadema kilikuwa sahihi, lakini wanapaswa kukumbuka wanahabari walikuwa kazini kutoa taarifa kwa jamii kuhusu mahojiano ya polisi na Mbowe.

Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimemtaka Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, ajitokeze hadharani na atoe kauli kama alitoa maelekezo mengine kwa vyombo vya dola dhidi ya vyombo vya habari mara baada ya kukutana na wahariri wa vyombo hivyo.

Pia Chadema kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, atoe kauli mbele ya umma ni hatua gani watachukua dhidi ya askari waliofanya tukio hilo baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paulo Chagonja.

“Chagonja alisimamia operesheni mbele ya jeshi na kuhakikisha kupigwa kwa waandishi wa habari, licha ya waandishi kuonyesha vitendea kazi vyao vikiwamo kamera lakini waliumizwa,” alisema.

Mwananchi, Nipashe.

Featured

Polisi wawapiga Wandishi wa Habari

Asksri wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakitembeza kipigo
Asksri wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakitembeza kipigo

Na Nassor Khamis.

Waandishi wa habari wa vyombo viwili tofauti wamejeruhiwa baada ya kupokea kipigo kutoka kwa jeshi la Polisi kufuatia purukushani ya kuwatanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Purukushani hizo zilizozuka baada Jeshi la Polisi kikosi cha kutuliza ghasia FFU kuwataka wafuasi wa Chama hicho kuondoka katika Ofisi za Makao makuu ya Polisi jijini Dar es salam walikokuwa wakimsindikiza Mwenyekiti wa Chama chao.

Waandishi hao waliojeruhiwa ni Josephat Isango kutoka gazeti Tanzania Daima na Shamimu Ausi wa gazeti la Hoja ambapo Isango alijeruhiwa mguuni na Shamimu akijeruhiwa usoni karibu na jicho la kulia.

Akizungumza mara baada ya kushambuliwa huko Isango alisema alivamiwa na askari wawili wa FFU na kuanza kumpiga hata baada ya kujitambulisha na kuonyesha kitambulisho chake cha kazi.

Nae Shamimu Ausi wa gazeti la Hoja alisema, alipigwa rungu usoni na akashangazwa na nguvu kubwa iliyotumika wakati awali aliruhusiwa kusimama katika eneo alipokuwa akiendelea na kazi yake.

Wakati huo huo Shughuli za kiserikali katika Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi za jirani, jana zilisimama kwa siku nzima kutokana na purukushani zilizoibuka baina ya polisi na wafuasi wa Chadema pale mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alipokwenda kuhojiwa na polisi.

Mbowe alikwenda Makao makuu ya Polisi jijini Dar es salam alikoitwa na jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano kufuatia kauli ya kuitisha maandamano na migomo isiyo na kikomo nchi nzima ili kupinga kuendelea kwa shughuli za Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.

Mbowe alitoa kauli hiyo katika Mkutano mkuu wa Chadema uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Purukushani hizo kati ya Jeshi la Polisi na wafuasi wa Chadema ziliibuka mara baada ya kuwasili kwa Mbowe katik Ofisi za Makao makuu ya Polisi huku akiwa ameongozana na baadhi ya Wanasheria wa Chama hicho akiwamo Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando.

Wanasheria wengine walioambatana na Mbowe ni Tundu Lissu, Peter Kibatala, John Malya pamoja na Naibu katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika.

Mara baada ya kuwasili kwa Mbowe pamoja na Wanasheria alioambatana nao barabara ya Garden inayokatiza mbele ya Wizara ya Mambo ya Ndani ilifungwa na wafuasi wa Chama hicho walizuiliwa kwa mbali.

Hali hiyo iliendelea hadi majira ya saa 9 alasiri baada ya kuhojiwa kwa Mbowe na kusababisha usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakitaka huduma katika eneo hilo nakujibiwa kuwa hakuna shughuli yoyote inayoendelea katika jengo hilo.

“Nendeni leo hakuna Shughuli yoyote inayoendelea hapa leo hadi kesho” alisikika askari aliekuwa ameshika mbwa akiwajibu wananchi waliokuwa wakihitaji huduma eneo hilo.

Licha ya wafuasi wa Chadema kuzuiliwa kufika Makao Makuu ya Polisi waliendelea kujitokeza kufuatia ombi lililotolewa juzi na naibu Katibu mkuu wa chama hicho John Mnyika kuwataka wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kumsindikiza Mbowe wakati wa kuhojiwa na Polisi.

Wafuasi hao walianza kukusanyika majira ya saa 4:00 asubuhi wakiwa mmoja mmoja na baadae kuwa wengi hadi walipoanza kutwanywa na Polisi baada ya kukaidi amri ya kuondoka maeneo hayo.

Kutokana na kukataa kuondoka Asakari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU wakiwa katika magari mawili aina ya Land Rova walianza kuwashushia kipigo wafuasi hao huku wakiwataka kukaa umbali wa miya 100 kutoka lilipo jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani.

Baada ya kuondoka eneo hilo, wafuasi wa Chadema walikwenda katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni na kupewa maelekezo na Dk Slaa na Lissu.

Lissu alisema Mbowe anatuhumiwa kwa uchochezi kutokana kauli ya kufanyika maandamano nchi nzima, huku akisisitiza kuwa tuhuma alizopewa “ni za wizi wa kuku”.

“Mbowe aliposema kufanyika maandamano alikuwa na maana kuwa maandamano hayo yatafanyika baada ya Chadema kutoa taarifa, kauli yake haikuwa ya uchochezi hata kidogo,” alisema Lissu.

Aliongeza, “Kama polisi wakitueleza ni sheria ipi inakataza maandamano, sheria ipi inalazimisha wanaotaka kuandamana lazima wawe na kibali na sheria ipi inakataza watu kugoma, watakuwa na ruksa ya kumfunga Mbowe.”

Kwa upande wake, Dk Slaa alisema, “Mbowe baada ya kutoka polisi ameomba nimwagie kwa wanachama wa Chadema. Amekwenda Afrika Kusini katika mkutano wa chama. Safari yake ilikuwa imepangwa tangu juzi na ingeahirishwa kama angenyimwa dhamana leo.”

Dk Slaa alimwagiza Kigaira kuhakikisha kuwa wanachama wawili wa chama hicho waliokamatwa na polisi wanaachiwa kwa dhamana. Zoezi la kufanya maandamano likifanyika kama hivi Taifa hili litabadilika,” alisema.

Featured

Mawakili watano wajitosa kuwatetea watuhumiwa ugaidi

Viongozi wa Jumuia ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Viongozi wa Jumuia ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Watuhumiwa 22 wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi, wakiwamo viongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki) Zanzibar, wamepata mawakili watano wa kuwatetea dhidi ya mashtaka manne yanayowakabili.

Mawakili hao walijitokeza jana wakati kesi hiyo ilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Wanasheria hao ni Salim Abubakar, Abdallah Mohamed, Rajabu Abdallah, Ubaidi Hamidu na Abdulibatah.

Miongoni mwa mawakili hao, Rajabu Abdallah aliiomba mahakama kuifuta hati ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao kwa sababu haijaweka wazi sehemu ambayo washtakiwa hao walifanya makosa hayo ya ugaidi, hivyo haikidhi matakwa ya sheria.

Abdallah alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 244 cha sheria ya makosa ya jinai (CPA), sura ya 20 na kifungu cha 135 (f) viliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, vinaitaka hati ya mashtaka kuonyesha wazi eneo, muda na taarifa sahihi ambazo washtakiwa walifanya makosa hayo ya ugaidi.

Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba iipangie tarehe nyingine ya kuitaja.

Kuhusu hoja za mawakili hao, Kweka alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya 243 na 246 vya sheria ya makosa ya jinai, kinaeleza wazi mamlaka ya Mahakama ya Kisutu kwenye kesi za ugaidi kuwa ni mshtakiwa kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yanayomkabili, kutoa amri awekwe mahabusu na kupelekwa mahakamani kila baada ya siku 14 na kumsomea maelezo ya mashahidi ili kesi iweze kuhamishiwa mahakama kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Alisisitiza kuwa hoja za mawakili hao hazina mashiko kwa kuwa hati ya mashtaka iliyopo mbele ya mahakama ndiyo sahihi.

na inajitosheleza na kwamba mahakama ya kisutu haina mamlaka ya kuongelea hati ya mashtaka hadi Mahakama Kuu.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo zote, Hakim Hellen Liwa aliwaeleza mawakili hao kuwa hoja wanazozijadili mahakamani hapo hana uwezo wa kuzitolea maamuzi na kuwashauri kuyaweka malalamiko yao katika maandishi na kuyapeleka mahakama kuu ili yaweze kujadiliwa huko na jopo la majaji na kuongeza kuwa kwa kile kilichopo mbele ya mahakama yake ni sahihi.

Mwananchi.

Featured

SMZ: Hakuna mwenye ubavu wa kuipora Pemba

Maandhari ya Kisiwa cha Pemba.
Maandhari ya Kisiwa cha Pemba.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema Kisiwa cha Pemba ni miliki ya Zanzibar na sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna nchi yoyote yenye ubavu wa kukichukua kisiwa hicho, imeelezwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia mvutano wa mipaka uliojitokeza katika usawa wa Bahari ya Hindi kwenye mwambao wa Somalia na Kenya na kulihusisha eneo la Pemba ikielezwa kuwa ni sehemu ya Kenya.

Kauli ya Waziri huyo imekuja baada ya hivi karibuni kuripotiwa kuwa Somalia imeishtaki Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa kuwa inakalia Kisiwa cha Pemba ambacho ni mali ya Kenya.

Vilevile Somalia imeishtaki Kenya katika mahakama hiyo na kwamba nayo iko katika hatari ya kupoteza umiliki wa visiwa katika Pwani ya Bahari ya Hindi.

Aboud alisema mipaka ya nchi inaonyesha wazi Kisiwa cha Pemba kimekuwa ni sehemu ya Zanzibar na hakuna sababu ya kulitilia shaka jambo hilo kuhusu mvutano uliojitokeza baina ya mataifa hayo na kuamua kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa.

“Kelele za mlango daima haziwezi kumnyima usingizi mwenye nyumba, Kisiwa cha Pemba ni mali ya Zanzibar na sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…mipaka hiyo itabaki hivyo,” alisema Waziri Aboud.

Alisema katika sura ya kwanza ya Katiba ya Tanzania (2)(1) imeeleza bayana kuwa, eneo la Jamhuri ya Muungano ni la Tanzania Bara pamoja na sehemu ya bahari inayopakana nayo.

Alisema hakuna sababu yoyote ya Wazanzibari kuwa na hofu na kwamba SMZ chini ya Jamhuri ya Muungano iko makini katika kulinda rasilimali na mipaka yake.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Mahadhi Juma Maalim alisema Serikali imeanza kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kupata ukweli kwa kile kilichoripotiwa kuhusu Kisiwa cha Pemba kuwa katika eneo la Kenya.

Dk Mahadhi alisema kwa kuwa kesi ya mipaka kati ya Kenya na Somalia iko katika Mahakama ya Kimataifa, kwanza watahitaji kufahamu madai ya pande mbili hizo katika kesi ya msingi.

walioshtakiwa na kufikishana mahakamani.

“Serikali itafuatilia ili kupata ukweli wa kuibuka kwa madai hayo ingawa mipaka yetu inafahamika kitaifa na kimataifa…hatuna wasiwasi na jambo hilo na kama kutakuwa na ulazima wa kuingia katika kesi hiyo, tutalazimika kufanya hivyo tukiwa tunajiamini,” alisema Dk Mahadhi

Hata hivyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema kwamba Kisiwa cha Pemba na Mombasa vilikuwa ni sehemu ya Zanzibar chini ya utawala wa kisultan akiwa chini ya uangalizi wa Uingereza mara baada ya ukataji wa mipaka baada ya Mkutano wa Berlin Ujerumani mwaka 1884/85.

“Ni ajabu kusikia kuwa Pemba ni sehemu ya Kenya badala ya kusikia Mombasa ni sehemu ya Zanzibar, kabla na baada ya mwaka 1963 bendera ya Sultan wa Zanzibar ilipepea huko Mombasa na maeneo yote umbali wa maili kumi toka usawa wa bahari yakiwa chini ya himaya ya Zanzibar,” alisema Awadh.

Mwananchi.

Featured

Mfanyakazi wa ndani adaiwa kumbaka bosi wake mzungu

Na Madina Issa

RAIA wa Poland mwenye umri wa miaka 31 (jina linahifadhiwa), anadaiwa kubakwa na mfanyakazi wake wa ndani.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya Septemba 14 katika kijiji cha Jambiaji Kibigija wilaya ya kusini Unguja, ambapo mtuhumiwa ni mfanyakazi wa jikoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Sadi Khamis, amethibitisha kutokea tukio hilo na kumtaja mtuhumiwa kuwa ni Kantenina Alois Jakob (34) mkaazi wa kijiji hicho.

Alisema kabla ya tukio hilo, mwanamke huyo aligombana na mume wake na kuamua kwenda kulala kwenye nyumba nyengine.

“Siku ya tukio mwanamke huyu aligombana na mume wake baada ya kurudi nyumbani wakitoka klabu ya starehe na kwenda kulala nyumba nyengine, huku mume akiendelea kulala kwenye yumba yao ya kawaida,” alisema.

Alisema mume alimjulisha mfanyakazi wao kuhusu tukio hilo, lakini ilipofika usiku mtuhumiwa alikwenda kwenye nyumba aliyolala bosi wake wa kike na kuingia ndani atakatekeleza kitendo hicho.

“Alikuta mlango uko wazi, akaingia ndani na akafanya kitendo hicho na kumsababishia maumivu makali na sasa mtuhumiwa anashikiliwa kwa upelelezi,” alisema.

Alisema mwanamke huyo alimefikishwa hospitali ya Makunduchi kwa matibabu na baadae kuhamishiwa hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Daktari wa kitengo cha mkono kwa mkono hospitali kuu ya Mnazimmoja, Salum Omar Mbarouk, alikiri kumpokea mwanamke huyo na kusema alipomfanyia uchunguzi aligundua michubuko kwenye sehemu zake za siri na mikwaruzo ya kucha kwenye mapaja na kifuani.

Aidha alisema mtuhumiwa nae alifanyiwa uchunguzi kwa kupimwa HIV na baadae kukabidhiwa jeshi la polisi kuendelea na upelelezi.

Alitoa wito kwa wananchi wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji kuwahi kufika kituoni hapo ili kupatiwa matibabu pamoja kutunza ushahidi utakaotumiwa wakati watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani,

Zanzinews.

Featured

Mipaka ya Majimbo yapingwa

Chama cha NCCR Mageuzi Zanzibar kimetangaza mpango wa kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga kazi ya kurekebisha mipaka ya majimbo inayofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Msimamo huo ulitangazwa na makamu mwenyekiti wa NCCR, Ambari Khamis Haji, akidai utaratibu huo haujazingatia uwiano wa idadi ya watu katika miji mikubwa na midogo. Chama cha Wananchi (CUF) nacho tayari kimeshatoa tamko la kupinga utaratibu huo kwa sababu hizohizo.

Haji alisema iwapo kazi hiyo itafanyika, inaweza kuibua migogoro mikubwa ya kisiasa na kuvuruga amani wakati Taifa likijiandaa na Uchaguzi Mkuu 2015. Alifafanua kuwa majimbo kisiwani Pemba hayana uwiano wa watu kulinganisha na majimbo ya kisiwani Unguja kwa vile harakati za uchumi eneo hilo ni kubwa kuliko Pemba.

Alisema Serikali ilipaswa kuimarisha miundombinu ya usafiri kama bandari, uwanja wa ndege na barabara na kusogeza huduma za maji na umeme ili kuvutia wawekezaji Pemba, hali ambayo ingepunguza wimbi la watu kuhama na kusababisha majimbo kubaki na idadi ndogo ya watu.

“Kupunguza majimbo upande mmoja na kuongeza upande mwingine, kunaweza kuvuruga amani na umoja wa kitaifa,” alisema.

“Umoja huu wa kitaifa umepatikana kwa tabu kubwa, kwani baadhi yetu wamepoteza maisha na wengine wamebaki na ulemavu wa maisha.”

Alisema NCCR Mageuzi imeamua kwenda kortini ili kuzuia Kisiwa cha Pemba kupoteza viti vingi vya ubunge na kuitaka tume iongeze majimbo badala ya kupunguza.

“Kama wameamua kwenda mahakamani ni haki yao kisheria lakini ZEC tumewapa nafasi wadau wote wa uchaguzi kutoa maoni kuhakikisha zoezi linafanyika kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwakani” alisema Jecha.

Zoezi hilo la ukataji wa mipaka ya majimbo linatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 400 ingawa chama cha CUF kinachounda serikali ya umoja wa kitaifa kimesema zoezi hilo limelenga kuibeba CCM iweze kuongeza viti katika uchaguzi wa mwakani.

Mwananchi.

Featured

Mtuhumiwa wa ugaidi atoa madai mazito mahakamani

Mtuhumiwa wa kesi ya ugaidi mkoani Arusha, Abdallah Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo, kumruhusu kutohudhuria siku za kesi na abaki magereza kutokana na maumivu makali anayopata sehemu za siri alikodai kuminywa na polisi, pamoja na kuingiziwa mti sehemu ya haja kubwa.

Mshtakiwa huyo alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devota Msofe.

“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata maumivu makali sana sehemu za siri kunauma, kwa sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,” alisema.

Alidai kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri pia mguu wake uliokatwa hospitalini bado una maumivu makali.

Maginga pia aliiomba Mahakama iagize Magereza wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5 mwaka huu lakini amezuiwa hadi sasa.

Akijibu ombi hilo, Hakimu Msofe, alisema suala la kwenda mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia alimshauri mshtakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi amweleze hakimu anayesikiliza kesi yake Mustapher Siyani, ambaye kwa siku hiyo hakuwapo.

“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza ndiyo mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema hakimu huyo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao wameshtakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi Namba 22 ya Mwaka 2002 na kwamba upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na kundi la Al-Shabaab.

Mbali na mashitaka hayo pia wanahusishwa na tukio la mlipuko wa bomu lililotokea katika baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.

Washtakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti (yupo wodini Hospitali ya Mount Meru), Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemed, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi, Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.

Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaban Musa, Athuman Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba .

Nipashe.

Featured

DW chatoa mafunzo kwa wakufunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari

Khadija Khamis na Rahma Khamis, zjmmc

Kituo cha Mafunzo cha DEUTSCHE WELLE (DW)kimeendelea kutoa Mafunzo kwa Wakufunzi wa Chuo cha Uandishi habari wa Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa Mashirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani.

Mafunzo hayo ya siku tano yana lengo la kuwajengea uwezo Wakufunzi wa Chuo hicho ili kutoa elimu sahihi ya Uandishi inayoendana sambamba na mabadiliko ya kiulimwengu.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Rashid Omar Kombo alisema Wataalamu hao watawajengea uwezo Wakufunzi wao ili kusaidia katika kufundisha wanafunzi kwa vitendo na kutumia njia za kisasa katika ufundishaji wao.

Omar amefahamisha kuwa mafunzo hayo ya vitendo kwa darasa (compelete class training) yatasaidia kutoa mbinu kwa Uandishi wa habari  wa kileo ambao unakwenda sambamba  na matarajio ya wana jami.

Ameongeza kuwa licha ya kupatiwa mafunzo pia wanatarajia kupatiwa misaada ya vifaa mbalimbali vya ufundishaji ikiwemo Camera na Komputa pamoja na kujenga majengo mbali mbali ya Chuo katika maeneo mengine.

Aidha aliongeza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa Mafunzo ambayo hutolewa na Kituo hicho cha DW kwa Chuo cha Habari ambapo Mwanzoni mafunzo hayo yalitolewa kwa wanafunzi tu wa chuoni hapo.

Jumla ya Wakufunzi 16 wa Chuo cha Habari Zanzibar wanaendelea kupatiwa mafunzo hayo kutoka kwa Wataalamu watatu wa kituo cha Mafunzo cha DW ambayo yatachukua siku tano.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

Featured

Dkt, Slaa: Maandamano ya kupinga Bunge la katiba kupanwa rasmi

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Dkt, Wilbroad Slaa.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Dkt, Wilbroad Slaa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt Wilbroad Slaa amesema maandamano yanayo tarajiwa kufanywa kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalum la Katiba yatapangiwa tarehe rasmi baada ya Viongozi wa UKAWA kukutana.

“Maandamano yatafanyika nchi nzima, tayari taratibu zimeanza kufanywa mikoani. Tutaeleza tarehe hiyo. Tumepinga kwa maneno tukitaka Bunge lisitishwe lakini wenzetu wameweka pamba masikioni. Sasa tunaonyesha chuki na hasira, polisi watambue kuwa wao wapo 35,000 na wananchi wapo milioni 45.

“Tumenyimwa vibali katika mikutano yetu iliyopita sasa safari hii wakikataa kutupa kibali tutaandamana tu. Azimio la Kamati Kuu haliwezi kuvunjwa na Chagonja kwa sababu maandamano ni haki yetu na tumeshafanya maandamano 100 ya amani nchini.”

Kuhusu ushirikiano wa vyama vinavyounda Ukawa, Dk Slaa alisema hilo ni azimio la pili la Kamati Kuu ambayo imebariki ushirikiano huo kuanzia katika Uchaguzi wa Serikali za Mtaa na Uchaguzi Mkuu 2015.

“Kamati Kuu imeunda kamati ndogo itakayoongozwa na Profesa Safari ikiwajumuisha Benson Kigaira, Mnyika na John Mrema kuangalia namna ushirikiano huo utakavyokuwa. Kamati hiyo imeanza kazi leo (jana),” alisema.

Alisema azimio la tatu la Kamati Kuu ni kuhakikisha kuwa Ukawa wanaidai Katiba ya wananchi na kwamba wanatembea nchi nzima kueleza uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba uliofanywa na CCM bungeni.

Katika hatua nyingine, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema Jeshi la Polisi limekurupuka kuzuia wafuasi wa Chadema kuandamana kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge wakati chama hicho hakijatoa taarifa rasmi kwa jeshi hilo.

Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji wa kituo hicho, Imelda Urio alisema alichofanya Mbowe ni kutangaza kusudio la kufanya maandamano na kwamba hatua nyingine za kutoa taarifa rasmi kwa jeshi hilo zingefuata baadaye.

 

Featured

Mbowe kutinga polisi na mawakili

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh. Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh. Freeman Mbowe.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe leo atasindikizwa na mawakili watano atakaporipoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam alikoitwa kuhojiwa kuhusu kauli yake ya kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.

Mawakili hao wataongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Profesa Abdallah Safari, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, Halima Mdee, Mabere Marando na Peter Kibatala, huku makada wa chama hicho wakialikwa kuandamana naye kumsindikiza.

Mbowe alitoa kauli hiyo katika Mkutano Mkuu wa chama hicho Septemba 14, mwaka huu, akisema maandamano hayo yatafanyika katika siku ambayo itapangwa katika mikoa yote.

Siku moja baadaye, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Kamishna Paulo Chagonja alimkemea akisema iwapo atafanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa. Pia, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) alimwandikia barua akimwita kuhojiwa.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema jana kwamba uamuzi huo ni moja ya maazimio matatu ya kikao cha kwanza cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliyokutana Dar es Salaam juzi.

“Mbowe ameitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kesho (leo). Polisi wameandika barua ya wito huo lakini hawajasema kosa lake ni nini. Itakuwa saa tano asubuhi na atakwenda na mawakili wote wa chama,” alisema Dk Slaa mbele ya viongozi wote wa sekretarieti mpya ya chama hicho.

Akizungumzia wito huo jana, DCI Mngulu alisema ingawa leo atakuwa Songea, ofisi yake ina watumishi wengi na kwamba ameshawasiliana naye kwa ujumbe kumfahamisha hilo.

Katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema, “Tunawaomba wanachama wa Chadema kujitokeza Makao Makuu ya Polisi ili kumsindikiza mwenyekiti atakayekuwa akihojiwa.”

Kwa upande wake, Lissu alisema katika barua ya wito, polisi wametaja vifungu vya sheria, lakini hawakueleza kosa la Mbowe ni nini, jambo ambalo linaonyesha jinsi wanavyofanya kazi nyuma ya kivuli cha chama tawala, CCM.

Akizungumzia madai hayo, Mngulu alisema Kifungu cha 10 cha Sheria ya Makosa ya Jinai kinajieleza wazi. Kifungu hicho kinazungumzia kudhamiria kutenda kosa.

Mwananchi.

Featured

Hofu ya kupatikana theluthi mbili yatanda Bunge la Katiba

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Samuel Sitta.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Samuel Sitta.

Wakati Bunge Maalum la Katiba likiwa katika hatua ya lala salama, kumeibuka hofu ya kupatikana au kutopatikana kwa theluthi mbili za kupitisha Katiba inayopendekezwa.

Kutokana na hofu hiyo, Sitta amewataka mawaziri na manaibu kuwapo bungeni kuanzia Septemba 29 ili kuweza kupiga kura ya kuipitisha Katiba inayo pendekezwa.

Sitta alisema ikiwa wajumbe watafuata kanuni za Bunge hilo zinazotaka upigaji kura uwe ibara kwa ibara, shughuli hiyo itachukua siku zisizopungua 300 kuwahoji wajumbe 460.

“Ibara naambiwa zinakaribia 300 kwa hiyo itachukua siku moja kwa ibara moja. Na kwa ibara 300 ni siku 300; haiwezekani kabisa ni kinyume cha sheria. Tumepewa siku 60 tumalize,”alisema Sitta.

Hivyo, alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge imekabidhi suala hilo kwa Kamati ya Kanuni ili kuja na mapendekezo ya njia bora ya kupiga kura hizo ili wajumbe wahojiwe sura kwa sura.

Awali, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Rose-Asha Migiro alisema wajumbe waliosalia wanatosha kupitisha uamuzi kwa kuwa ni halali kisheria na kisiasa.

Alisema wajumbe wote wa Bunge ni 630 na kati ya hao, waliotoka ni 130, idadi ambayo ni sawa na asilimia 21 tu ya wajumbe wote.

“Wajumbe waliobaki ndani ya Bunge ni 500 sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote na idadi hii ni pamoja na wajumbe 189 kutoka Kundi la 201 ambao wamebaki Bungeni,” alisema.

“Wajumbe wanaotoka Tanzania Bara ni 348 na kati ya hao 125 ni wanaotoka kundi la 201. Ukitazama takwimu zote hizi, wajumbe wa 201 ni sehemu ya Bunge hili,” alisema Dk Migiro.

“Kwa Zanzibar wajumbe waliobaki ndani ni 152 na kati ya hao 64 wanatokana na kundi la 201. Waliosusia Bunge kwa pande zote za Muungano hawafikii theluthi moja ya wajumbe waliobaki.”

Mwananchi.

Featured

Keissy alianzisha tena bungeni

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba Ally Kessy.
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba Ally Kessy.

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ally Keissy jana alilazimika kusindikizwa na askari wa Bunge kuondoka katika viwanja vya eneo hili kumnusuru na hasira za wajumbe kutoka Zanzibar waliokerwa na mchango wake kuhusu masuala ya Muungano.

Kessy alisimama bungeni hapo saa 5:52 asubuhi kutoa mchango wake kuhusu Katiba akijikita zaidi katika suala la muundo wa Muungano na kusema kwamba Zanzibar inabebwa na Tanganyika.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanganyika inabeba mzigo mkubwa ambao haubebeki, hapa tunahudumia wabunge 83 kutoka Zanzibar ambao wanatibiwa wao na wake zao na watoto kwa gharama za Tanganyika wakati hawachangii,” alisema na kuongeza kuwa haiwezekani kwa Tanganyika kubeba mzigo mkubwa kama huo wakati katika Jimbo lake la Nkasi wananchi wanalia na shida ya maji.

Alisema katika Kamati yao Namba Moja, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu alitoa semina iliyoonyesha kuwa Zanzibar haichangii chochote kwenye Muungano na kuwa hata mishahara wakati mwingine wanategemea Tanganyika.

Keissy alisema wananchi wakilijua jambo hilo, wataikataa Katiba inayopendekezwa na kuitupilia mbali kwa kuwa inatoa upendeleo kwa Wazanzibari na kuikandamiza Tanganyika.

“Mimi naweza kuwa na wanawake sita, nikazaa nao lakini kila mtoto anaendelea kutunzwa na baba yangu, jambo kama hili halivumiliki hata kidogo japo najua kuwa ukweli unawauma,” alisema huku baadhi ya wajumbe wakipaza sauti wengine kumpinga na wengine kuomba mwongozo wa mwenyekiti.

Alipinga suala la rais wa Zanzibar kuwa makamu wa rais wa Muungano kwa maelezo kuwa katika mfumo wa vyama vingi jambo kama hilo haliwezekani na kuhoji itakuwaje awe makamu wa kwanza wa rais wakati hajachaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara?

Baada ya kauli hiyo, kelele za wajumbe kutoka Zanzibar ziliongezeka baadhi wakisimama na kuwasha vipaza sauti kumshambulia Keissy, “chizi huyo, chizi huyo, hafai kwanza ni Mwarabu,” zilisikika sauti huku nyingine zikimtaka aombe radhi.

Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alimpa nafasi mmoja wa wajumbe hao, Fatuma Hamis Salehe kutoa taarifa, ndipo alisema wajumbe wa Zanzibar wapo kisheria ndani ya Bunge hilo na wala si kwa fadhila, hivyo akamtaka Keissy kuomba radhi.

Hata hivyo, Kessy alijibu akisema, “Siko tayari kuomba radhi katika jambo hili, mimi nazungumzia masuala ya Ndullu, alikuja pale katika kamati na kwamba tangu kifo cha Karume hamjawahi kuchangia, mnaposema mimi Mpemba au Mwarabu basi ninyi ni Wakongo,” alisema kwa sauti ya juu.

Alisema posho wanazolipwa bungeni hapo, zimetoka upande wa Tanganyika na Zanzibar haijachangia hata senti moja.

Baada ya hapo kelele ziliongezeka sawia na idadi ya waomba mwongozo, Mjumbe kutoka Kundi la 201, Ally Juma Khatibu, alisimama hata bila ya kupewa ruksa na kuanza kuzungumza kwa ukali akisema Kessy ni mbaguzi na mtu anayestahili adhabu kali.

Baadaye alipewa nafasi Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye aliwataka wajumbe kuwa wavumilivu na kupuuza baadhi ya mambo kwani kipindi kilichobakia ni cha kumalizia.

Alifuata Mjumbe, Mahmoud Thabit Kombo aliyesema Keissy hajui historia kwani Zanzibar ilipoteza utambulisho wake katika kiti cha Umoja wa Mataifa na kuiachia Tanzania, jambo ambalo nchi hiyo ndogo inastahili kupongezwa.

Mjumbe mwingine, Abdalla Sharia Ameir alimtuhumu Keissy kuwa ni mtu mwenye asili ya Arabuni ndiyo maana anapiga kelele kwa Waafrika na kutaka akapimwe akili.

Ameir alimtaka Keissy atoke nje kama ni mwanamume na hapo alianza kutangulia lakini alipoona hakuna wa kumfuata, alirudi hadi karibu na kiti alichokaa Keissy ndipo wajumbe wengine walipoingilia kuwatuliza.

Kwa upande wake, Hamad Rashid Mohamed alimwita Keissy mchochezi asiyejua historia ya Tanganyika na Zanzibar katika Muungano.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira alimtahadharisha Keissy kuwa mchango wake unaweza kuzua vita na kumtaka awe makini wakati wote na ndimi zake… “Japo ni maoni yake, lakini mengine yana gharama kubwa, lazima uchunge ulimi wako.”

Baadaye, Sitta alisimama akimtaka Keissy aombe radhi, jambo alilolikubali kiaina akisema, “Nilichokizungumza kina ukweli katika Bunge la Muungano lakini kama nimekosea naomba msamaha,” alisema.

Asindikizwa kutoka

Baada ya Sitta kuahirisha kikao, Keissy alifuatwa na mmoja wa wahudumu wa Bunge, Waziri Kizingiti na kumshika mkono hadi kwa wapambe wa Bunge waliomchukua na kumpeleka katika Ofisi ya Spika iliyopo kwenye jengo la Bunge na baadaye kutoka naye nje wakitumia mlango unaotumiwa na Waziri Mkuu kuingia na kutoka bungeni akiwa amezungukwa na askari wa Bunge watano hadi mlango wa kutoka nje ya eneo la Bunge ambao kwa kawaida hutumiwa na viongozi wakuu wa Serikali na Bunge.

“Mheshimiwa Keissy? Gari lako liko wapi uende ukapakie,” alisikika mmoja wa wapambe akimuuliza Keissy ambaye alisema hana gari akiwataka wamwache arudi ndani akachukue begi lake lakini alikataliwa na badala yake alipelekwa hadi sehemu ya ukaguzi katika lango la kuingilia na kupewa kiti huku akiwa amezungukwa na wapambe hao.

Nje ya Ukumbi wa Bunge, wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa wakimsubiri atoke kwa takriban dakika 30 bila mafanikio.

“Keissy yuko wapi? Kama mwanamume kweli atoke, wanamfichaficha ndani ili iweje? Tumechoka na matusi yake,” alisikika mmoja wa wajumbe akisema.

Akizungumza baada ya kufika hotelini, Keissy alisema hakuna anachoogopa kwa sababu alisimama katika ukweli katika mazungumzo yake.

“Mimi nilizungumza badala ya Watanganyika na ukweli ndiyo huo hata kama kuna watu ambao hawataki kuusikia,” alisema Keissy.

Alisema aliyasema maneno hayo kwa nia ya kutaka kuboresha Muungano katika Katiba inayoandikwa hivi sasa na si kuuvunja kama alivyotafsiriwa na Wassira.

Mwananci.

Featured

Mbowe atikisa Bunge na Polisi

Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe
Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe

Tamko la Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe la kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba imesababisha Jeshi la Polisi kumwita ili kutoa ufafanuzi wa kauli yake huku Bunge hilo likichepusha mjadala na kutumia muda mrefu kujadili hotuba hiyo.

Akizungumza jana na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho waliokuwa katika mkutano wa kuwachagua wajumbe wa Kamati Kuu, katibu mkuu na manaibu wake, Mbowe alisema ameitwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Isaya Mngulu, lakini hatakwenda hadi atakapomaliza vikao vya Chadema.

“Jana (juzi) nilitoa kauli ya kufanya maandamano nchi nzima, kauli hiyo imemfanya DCI kuniita…” alisema na kuongeza kuwa msimamo wake na Ukawa uko palepale.”

Mapema jana, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paulo Chagonja alionya kuwa endapo Mbowe atafanya maandamano kama alivyotangaza polisi hawatasita kumchukulia hatua za kisheria kwani hiyo ni mara ya pili kutoa onyo dhidi yake.

“Ni wazi kwamba siasa zina mipaka yake na zinapovuka na kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi zinageuka kuwa jinai na wala siyo siasa tena,” alisema.

Juzi, katika Mkutano Mkuu wa Chadema, Mbowe alitoa maazimio sita mazito ukiwamo utaratibu wa kuandamana nchi nzima kupinga Bunge linaloendelea.

Bunge lahama mjadala

Mjadala wa Bunge jana, ulipoteza mwelekeo baada ya wajumbe kadhaa waliopewa nafasi kuchangia, kuacha kujadili Katiba badala yake ‘kurusha makombora mazito’ dhidi ya hotuba hiyo, kwa wana Ukawa na Mbowe mwenyewe.

Baadhi ya wajumbe waliomzungumzia Mbowe na Ukawa ni pamoja na John Komba, Amos Makalla, Fahmy Dovutwa, Dk Mary Nagu na Mwenyekiti Samuel Sitta ambaye alikwenda mbali na kusema iwapo wajumbe hao wa Ukawa walimpigia kura ili awabebe katika mambo aliyoyaita ya kipuuzi, basi wasahau.

Kauli hiyo ya Sitta ilitokana na kauli ya Dovutwa kueleza kile alichodai ni kiini cha Sitta kushambuliwa na wajumbe hao wa Ukawa katika mikutano yao.

“Baada ya kuunda Ukawa, Mwenyekiti wa kikao Freeman Mbowe akasema jamani mgombea wetu ni Samuel Sitta. Huyu atalinda masilahi yetu. Tumekubaliana, lakini baadaye akasema yeyote tutakayemwona anashirikiana na CCM tutamfanyizia,” alisema Dovutwa.

Hata hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo, Vicent Mzena aliomba mwongozo wa mwenyekiti akihoji inakuwaje Bunge hilo linajadili mambo yaliyotokea nje ya Bunge badala ya kujikita kujadili utungaji wa Katiba inayopendekezwa.

Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema utayarishaji wa Katiba Mpya lazima mambo yote yanayohusiana na utungaji huo yasemwe bayana.

“Nashukuru sana Mheshimiwa Fahmy Dovutwa kwa kutupa undani wa mambo kwa sababu kama hao watu walidhani kwa kunipigia kura basi nitakubali upuuzi wowote basi kwa lugha ya siku hizi imekula kwao,” alisema Sitta.

Makala ambaye ni Naibu Waziri wa Maji, aliwafananisha Ukawa na kamati ya harusi inayogombania kupanga tarehe ya sherehe badala ya kujikita kwenye kukusanya michango kutoka kwa wajumbe.

“Nimpongeze Spika kwa kuweza kukaa na Ukawa kwa sababu kuishi na hawa ni sawa na kubeba gunia la misumari kwa namna wanavyodeka. Wamepotosha kila jambo tulifanyalo ili waonekane wana jipya licha ya ukweli kwamba wanapigania katiba ya wachache. Tunaopigania katiba ya wengi ni sisi tuliobaki.

“Nimesikia pale Profesa Lipumba (Mwenyekiti wa CUF-Ibrahim) akisema kuna ufisadi mkubwa lakini yeye mbona alipokuwapo hapa na alichukua posho? Kila tukikutana hapa anasema Makalla naona mambo yanakwenda vizuri. Wao kutoka tu imekuwa ni nongwa.”

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba alisema, “Jana Mbowe amekuwa amiri jeshi na tayari ametangaza vita kwa kuandaa maandamano ya nchi nzima bila kibali cha polisi hata kama jeshi hilo litalazimika kutumia risasi za moto. Huyu ni mtu wa aina gani?

“Aliwasalimu wanachama wake kwa kusema ‘Ukawa…’ na wao wakajibu ‘Tumaini letu…’ Naomba nitangaze personal interest (masilahi binafsi) katika hili kwa sababu mimi ni Mkatoliki na tunaposema hivyo huwa tunamaanisha imani ya hali ya juu. Kwa hili nasubiri kauli ya maaskofu… wanapaswa kulikemea hili kwa nguvu.”

Komba amvaa Warioba

Komba aliendeleza mashambulizi yake kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kumwita mchochezi akisema amekuwa akiingilia mambo ya wajumbe kuwa wanakula fedha za wananchi bila ya kukumbuka kuwa hata yeye (Warioba) alikula fedha nyingi kuliko wabunge hao.

Mwananchi.

Hatua zisipochukuliwa, tunaelekea kuwa na vipaza sauti badala ya vyombo vya habari

By Bin mazrouy

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekipiga faini ya TZS milioni 10 kituo cha TV cha ITV

ITV imepigwa faini hiyo kutokana na na kipindi kutoka bungeni kilichokuwa kinaendesha mahojiano ya moja kwa moja ambapo Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Petter Msigwa alisikika akisema “Naibu Spika amekuwa kama anavaa pampas, hataki kubanduka kwenye kiti kuongoza bunge”.

Kauli hii ya Mchungaji Msigwa imetafsiriwa kama ni kauli ya kuudhi, na imesababisha ITV kuangukiwa na rungu zito la faini badala ya mtoaji wa kauli hiyo.

TCRA wanadai katika mahojiano hayo muongozaji wa kipindi alishindwa kusimamia mjadala uliokuwa ukiendelea na kuruhusu mgeni wake kutoa kauli yenye kuudhi.

TCRA hawakuitendea haki ITV katika maamuzi haya, ukizingatia kuwa kipindi kilikuwa kinarushwa moja kwa moja (Live) na mtangazaji hajui Source wake anakwenda kuzungumza kitu gani juu ya kile alichomuuliza, hivyo kukosa nafasi yaq kuhariri kile kinacho onekana kuudhi.

Kinacho onekana katika maamuzi haya ni muendelezo wa vitisho kwa vyombo vya habari dhidi ya kile kinachoonekana kuwa ni kuwakosoa viongozi wenye mamlaka ya uendeshaji wa vyombo vya maamuzi ya wananchi.

Kwa hali hii sasa vombo vya habari vitaacha kuandaa vipindi na mijadala na mijadala yenye kuikosoa serikali na viongozi wake kwa maslahi mapana ya taifa kwa kuhofia rungu la adhabu za faini ama hata kunyimwa kabisa leseni ya kuendeshea vyombo hivyo kutoka kwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Ikiwa hali hii itaachwa iendelee tutarajie vyombo vyetu vya habari kuwa vipaza sauti tu vya watawala kufikisha ujumbe wao kwa watu wa chini badala ya kuwa majukwaa yenye kuibua hoja za kujenga taifa letu.

Ili kuepusha vyomba vya habari kuwa vipaza sauti vya watawala ipo haja kwa wadau wa habari kupingana na viashiria hivi vya vitisho vinavyo zidi kutolewa kila siku dhidi ya vyombo vya habari na watendaji wake kwa maslahi mapana ya taifa letu.