Wazanzibari watakiwa kuipigia kura yandio Katiba inayopendekezwa

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar Dkt, Ali Mohammed Shein (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara Kibanda maiti mjini Unguja.
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakimsikiliza Makamo Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar Dkt, Ali Mohammed Shein (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara Kibanda maiti mjini Unguja.

Na Nassor Khamis, Zanzibar.
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kuipigia kura ya ndio Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba kwani imezingatia maslahi ya Zanzibar ikiwamo masuala ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja.
Dkt. Shein ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mnzi Mapinduzi amesema katiba inayopendekezwa imetatua kero zote za Muungano zilizokuwepo na kuzitafutia ufumbuzi ikiwamo kero ya muda mrefu kuhusu suala la mafuta na gesi.
Amesema kuwa suala la mafuta na gesi limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutaka litolewe katika orodha ya mambo ya Muungano ili Zanzibar iweze kukua kiuchumi.
“Suala hili la mafuta na gesi limekuwa likizungumzwa kipindi kirefu na serikali ya Zanzibar tokea nikiwa Makamo wa Rais kule bara na likakubaliwa litolewe na mimi nilipokukuja nimekuta limekubaliwa na mimi nikakubali” alisema Dkt. Shein.
Amesema kuwa kupitia katiba inayopendekezwa suala la hilo tayari limesahatolewa na kuwa chini ya mamlaka ya serikali ya mapinduzi Zanzibar ili kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua kiuchumi.
Amesema kuwa makampuni kadhaa ya mafuta yakiwemo kutoka Uholanzi na Ras Al-khaimah yameonesha nia ya kufanya utafiti wa mafuta katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na hatimae kuyachimaba na tayari makubaliano ya awali ya kazi hiyo yamefikiwa.
Mbali na suala hilo Dkt Shein amezungumzia maswala ya ushirikiano wa Zanzibar na taasisi pamoja na Mashirika ya kimataifa kuachwa katika mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jambo litakalo saidia katika maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Aidha amesema kuwa, kupitia katiba inayopendekezwa Zanzibar imeruhusiwa kukopa fedha katika mashirika na taasisi mbalimbali ikiwemo kupata udhamini wa Serikali ya Muungano pale itakapohitajika na itapatiwa udhamini huo.
Akizungumzia mchakato wa katiba mpya Dkt. Shein amesema mchakato huu umeendeshwa kawa mashirikiano makubwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea uundwaji wa sheria ya mabadiliko ya katiba hadi hatua iliyofikia.
Pia amewataka wananchi kuendeleza amani iliyopo na wasikubali kugawiwa kwa misingi ya katiba mpya kwani katiba inayoandikwa imetokana na makubaliano ya pande zote.
Pia amesisitiza kuwa serikali haitafumbia macho vitendo vyovyote vinavyo ashiria uvunjifu wa amani na itailinda amani ya nchi kwa gharama yoyote.
Nae Waziri wa fedha na uchumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Saada Salum Mkuya amesema katiba inayopendekezwa imezingatia maslahi ya Zanzibar katika masuala yote yakifedha ikiwemo mapato ya serikali yatokanayo na kodi ya mambo ya Muungano.
Amesema kuwa mapato yote yanayokusanywa kama kodi ya mfanya kazi wa taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar yatabakia katika serikali ya Zanzibar kwa maendeleo ya Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mh, Samia Suluhu Hassan amesema katiba inayopendekezwa imetoa fursa sawa za kiuongozi kati ya Tanzania bara na Zanzibar hasa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani endapo Spika wa Bunge hilo akitoka bara Naibu wake atatokea Zanzibar.
Mh, Samia ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais anaeshughulikia Muungano amesema, inayopendekezwa imetoa fursa kwa wanawake kwa kutoa haki sawa katika nafasi zote za uongozi wa nchi kwa asilimia hamsini kwa hamsini baina ya wanawake na wanaume pamoja haki ya uzazi salama kwa kina mama.
Mapema akizungumza katiaka mkutano huo Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Mzee Hamid Ameir amemtaka Mzee Hassan Nassor Moyo aache kuwapotosha Wazanzibar kuhusu Mapinduzi ya 1964 kutokana nakuwa hakuwa mshiriki wa Mapinduzi hayo.
Mapema katika Risala yao wanachama wa CCM wa mikoa minne ya kichama ya Unguja wameunga mkono mapendekezo yaliyomo katika Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba lililomalizika mwanzoni mwa mwezi huu mjini Dodoma.
Mkutano wa CCM umekuja baada ya mikutano miwili tofauti iliyofanywa na Chama cha Wananchi CUF hivi karibuni katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja na viwanja vya Gombani ya kale kisiwani Pemba.
Mikutano yote hiyo ilihutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho ambae pia ni Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi kadhaa wa Chama hicho.

Maalim Seif: Katiba inayopendekezwa inainyima mamlaka Zanzibar

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti Zanzibar.

Na Nassor Khamis.

Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kupiga kura ya hapana kwa Rasimu ya katiba inayopendekezwa kutokana na kutozingatia maslahi ya Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika viwanja vya Demokrasia Kibanda maiti mjini Unguja.

Akivizungumzia baadhi ya vifungu Maalim Seif amesema katiba inayo pendekezwa imepunguza mamlaka zaidi ya Zanzibar tofauti na ilivyoelezwa na wanaounga mkono katiba hiyo.

Amesema kuwa katiba inayopendekezwa imetoa mamlaka zaidi kwa Serikali ya Muungano kwa kusema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi moja yenye mamlaka kamili hivyo kuinyang’anya Zanzibar mamlaka iliyo nayo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar toleo la 2010.

Maalim Seif amesema kuwa Katiba ya Zanzibar inampa uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika Mikoa na maeneo mengine ya kiutawala ambapo kwa sasa mamlaka hayo yamewekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha amesema kuwa rasimu hiyo bado haijatoa uhuru kwa Zanzibar kushirikiana na Mashirika na Jumuiya za kikanda pamoja na Kimataifa kutokana na mashirika hayo kutoa uwanachama kwa nchi zenye mamlaka kamili ya kiuongozi jambo ambalo kwa Zanzibar bado halijapatikana.

“Shirika kama la Chakula duniani, UNESCO na mashirika mengine hatoi uanachama kwa nchi ambazo hazina mamlaka ya kujiendesha wenyewe na kwa Katiba hii inaqyopendekezwa bado Zanzibar haijapata mamlaka kamili” alisema Maalim Seif.

Aidha amesema kuwa Rasimu iliyotolewa na Tume ya jaji Warioba ilipunguza idadi ya mambo ya Muungano kutoka 22 hadi kufikia saba badala yake Rasimu inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba imeyaongeza kutoka saba hadi 14.

Pia amesema kuwa Rasimu inayopendekezwa bado imeifanya Ta nganyika kuendelea kuvaa koti la Muungano kutokna na mambo yake yasiyokuwa ya Muungano kuendelea kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia amesema kuwa katiba inayo pendekezwa imekosa uhalali wa kisheria kutokana na kutopatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar waliyoinga mkono rasimu hiyo wakati wa upigaji wa kura.

Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba Yahya Khamis Hamad wajumbe waliopiga kura ya ndio hawakufikia theluthi mbili badala yake matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na lengo la kuipitisha rasimu hiyo kinguvu kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi.

Aidha amesema kuwa endapo katiba inayopendekezwa itapitshwa itasababisha mgogoro wa kikatiba kutokana na na katiba hiyo kukinzana na katiba ya Zanzbar hivyo kulazimisha kufanyiwa marekebisho katiba ya Zanzibar jambo ambalo halitawezekana.

Amesema kuwa ili kuifanyia marekebisho katiba ya Zanzibar kutahitajika theluthi mbili ya Wajuumbe wa Baraza la Wawakilishi kuunga mkono ambapo wajumbe watokanao na chama cha CUF hawatakubali jambo hilo kutokea.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Mh, Nassor Ahmed Mazrouy amewataka Wazanzibar kuikataa katiba inayo pendekezwa pamoja na kuwakataa Wabunge na Wawakilishi wote waliopiga kura ya ndio kwa katiba inayo pendekezwa.

Naye Mjumbe wa kamati ya maridhiano Mansour Yussuf Himid amesema kuwa ataendelea kuitetea Zanzibar ipate mamlaka yake kamili hivyo ataendelea kupingana na mfumo wa Muungano wa CCM uliojaa ukatili dhidi ya Wanzibari.

Alisema kuwa kwa mujibu wa vitabu vya dini mbali mbali vinaeleza kila nafsi itaonja mauti je wao wanaogopa nini kilichobakia ni kuingia mitaani kuwambia Wazanzibar wasikubali kuipitisha katiba hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Maridhiano Zanzibar,Mzee Nassor moyo alisema kuwa Wazanzibar waliungana na Tanganyika kwa hiari yao hivyo hakuna mtu yeyote wa kuwalazimisha kufanya mambo yanayokwenda kinyume na matakwa ya Wazanzibar.

Mapema mkurugenzi wa habari na uenezi wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema kuwa rasimu inayopendekezwa sio ya wazanzibar na haitofika Zanzibar bali itaishia Kisiwa cha Chumbe .

Na aliwataka wazanzibari kuungana pamoja na kuikataa kwa nguvu zote rasimu ya Chenge na wenzake kwani imekuja kuangamiza Zanzibar.