Warioba amshukia Prof Shivji

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa gazeti hili, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa gazeti hili, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dar es Salaam. Mjadala wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.

Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.

Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.

Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika pande hizo mbili za Muungano.

Pia alisema suala la maadili kwa viongozi halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar, Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.

Katika majumuisho yake, Profesa Shivji, ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba walikuwa na nia njema.

Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema “the road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.

Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.

“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa matumizi ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana jioni.

“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”

Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa Zanzibar.

“Shivji alikuwa anasema Tanganyika imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi isijifiche,” alisema Jaji Warioba.

“Na Shivji amechochea hilo… wote wale waliokuwa wanamnukuu walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi yake na kwamba mpaka leo hii kuna watu wa Zanzibar wanaamini Muungano huu si halali kisheria kutokana na Shivji ambaye alisema Baraza la Mapinduzi halikuridhia articles (ibara) za Muungano.”

Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma hizo za uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na Utanganyika, Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia Jaji Warioba akizungumzia hilo.

“Hey, amezungumza lini?” alihoji. “Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe.”

Lakini Jaji Warioba alisema watu walitumia msingi huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji amesababisha hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa yanatokana uchochezi huo.

“Hata kabla ya sisi kuanza mchakato huu, Shivji alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na akawaambia issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa leo anaona kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea nationalism (utaifa),” alisema Jaji Warioba.

Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema mara ya kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu muundo wa Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa 47,000, huku watu 27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka Zanzibar.

 “Safari hii ametaja zile za Tanzania Bara na kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu 300,000 waliotoa maoni,” alisema Warioba.

Alisema Tume ilitumia takwimu zinatokana na watu waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na si kwa ujumla na ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa makusudi.

Warioba alimuelezea Profesa Shivji kuwa sasa ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda Rasimu ya Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio unaoifaa Tanzani kwa sasa.

Aidha, Warioba alisema msimamo wa Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010.

“ Nimeshangazwa na Shivji kusema kwamba kitendo cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa ‘Zanzibar ni Nchi’ halikuwa jambo la ajabu,” alisema Warioba.

Alisema Shivji ni msomi ambaye anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika muundo wa Muungano.

“Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi, alijibu kuwa Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka,” alisema.

Alisema lakini msomi kama Shivji haoni kama suala hilo la ‘Zanzibar ni nchi’ lina madhara makubwa katika mstakabali wa taifa letu.

Jaji Warioba alisema kama serikali tatu hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili Katiba yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo haiwezekani.

“Maana kama ni kusahihisha, ni lazima kwanza Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba ya Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,” alisema.

“Zanzibar wakubali Rais wa Muungano ana madaraka nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka yake.”

Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu hazionyeshi uhalisia wa maoni ya wananchi.

“Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro linakuwa na watu 100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu 20,000 na waliopiga kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake utakuwa katika watu waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,” alisema Warioba

CHANZO: MWANANCHI

Bunge la Katiba kuanza kazi rasmi leo

Wabunge wakiwa Bungeni mjini Dodoma
Wabunge wakiwa Bungeni mjini Dodoma

Dodoma. Wakati Bunge la Katiba leo linaanza kujadili sura mbili za Rasimu ya Katiba ambazo zitalenga Muundo wa Muungano, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umewataka wajumbe wake kutokuondoka Dodoma hadi kumaliza kujadili sura hizo.

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge iliyotangazwa Ijumaa iliyopita na makamu mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Saluhu, leo wajumbe wataanza kujadili sura ya Kwanza ya Rasimu ambayo inahusu Jina, mipaka, alama, lugha na Tunu za Taifa.

Sura ya sita, inahusu muundo wa Muungano, vyombo vya utendaji na mamlaka ya Serikali, nchi washirika na uhusiano wa nchi washirika.

Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema utaratibu wa kujadili rasimu kwa kuanza na sura hizo umetolewa na Kamati ya Uongozi kwa kuzingatia kanuni ya 58 ya Bunge la Katiba.

Kanuni hiyo ya 58 (3) inasema kamati ya uongozi itakuwa na majukumu ambayo ni “(a) kujadili na kuamua mambo yote yanayohusu uendeshaji bora wa shughuli za BungeMaalumu na kamati zake.

“(b) kujadili na kupanga ratiba ya utekelezaji wa shughuli za Bunge na (c) kujadili na kufanya uamuzi kuhusu masuala yatakayohitaji usuluhishi na maridhiano”.

Tamko la Ukawa

Mjumbe wa Bunge hilo, John Mnyika akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alisema kuanzia leo Bunge litaanza kujadili muundo wa Muungano ambao alisema ndiyo moyo ya Rasimu ya Katiba hivyo wajumbe wote wa Ukawa watashiriki.

“Tumewaomba wajumbe kutokuondoka wakati wa kujadili sura hizi mbili kwani ndiyo roho ya rasimu na tunaonya ikifikia hatua CCM wakachakachua, tutachukua maamuzi (uamuzi) mazito na kwa gharama zozote,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema tayari wamepata taarifa kuwa wajumbe kutoka CCM wataingia na mapendekezo yao na yatapigiwa kura kwa kujua wao wapo wengi pamoja na uteuzi wa wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete .

Hata hivyo alisema wakati wa kupitisha vifungu vya rasimu hiyo ni wazi kuwa CCM haina theluthi mbili kwa Zanzibar na kama wakipeleka mapendekezo ya kutaka kuvunja sheria na kanuni kwa masilahi yao hawatakubali.

Mnyika alisema licha ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kueleza upungufu wa mfumo wa Serikali mbili na hivyo kupendekeza Serikali tatu ambayo ni maoni ya wananchi, bado CCM inashinikiza na kutetea msimamo wao.

Mnyika alionyesha waraka aliodai wa siri wa CCM kuhusu jinsi ya kupinga mapendekezo ya Sura ya Kwanza na ya sita katika rasimu hiyo.

Alionya kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya kupitisha sura katika rasimu, ni lazima ipatikane theluthi mbili kwa upande wa Tanzania Bara na kwa Zanzibar.

Tamko hilo la Ukawa limekuja siku chache baada ya wajumbe wake kadhaa, akiwapo Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema kutangaza nia ya kuondoka Dodoma, akipinga mwenendo wa Bunge hilo hasa upigaji wa kura za wazi na siri kwa wakati mmoja.

Lema alidai kwa mazingira yaliyojengwa bungeni amepoteza imani ya kupatikana kwa Katiba ya wananchi.

CHANZO: MWANANCHI.

Sitta ‘amkataa’ Warioba bungeni

Mwenyekiti wa Bunge maalumu la katiba, Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge maalumu la katiba, Samuel Sitta

 

Dodoma. Jaribio la kutaka kumrejesha bungeni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili ajibu masuala yaliyoibuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya kufungua Bunge limegonga mwamba.

Uamuzi wa kukataa ombi hilo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mjumbe wa Bunge, Julius Mtatiro, akisema hadhani kama ni sahihi ombi hilo kutekelezwa.

Awali Mtatiro aliomba mwongozo kwa mwenyekiti, akitaka kujua iwapo kuna haja ya kumrejesha Jaji Warioba kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya hoja za Rais Kikwete ambazo zimekinzana na maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.

Mtatiro alisema: “Mtoa hoja mahususi alikuwa ni Jaji Warioba na Rais Kikwete alialikwa kama mgeni rasmi kufungua Bunge, lakini badala yake alikuja kujibu hotuba ya Warioba.

“Kwa sababu Rais alikaribishwa kama mgeni rasmi, lakini  alijibu  hoja za Warioba, je, hatuoni kama kuna haja ya kumrejesha mtoa hoja mahususi aje kujenga hoja  kutokana na alichosema Rais Kikwete?” alihoji Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF.

Katika ufafanuzi wake, Sitta alisema tayari amepokea kwa maandishi kutoka kwa baadhi ya wajumbe kuzungumzia suala hilo, jambo ambalo litafanyika lakini si kwa kumwita tena Jaji Warioba.

“Tunapenda kupata muda wa kuzungumzia  suala hili ili kuliweka sawa, hotuba zote mbili ambazo ni muhimu zitaandaliwa ili kupitiwa kuona kama malalamiko yanayotolewa yana hoja,” alisema Sitta.

Tangu Rais Kikwete ahutubie Bunge Ijumaa na kutoa hoja kinyume na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, hasa muundo wa Muungano, kumeibuka mijadala ya ama kuipinga au kuiunga mkono, huku wengine wakieleza kuwa imekiuka sheria.

CHANZO: MWANANCHI

Hotuba ya Warioba yazidi kugusa hisia

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akipongezwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Katiba na Sheria, Asha-Rose Migiro mjini Dodoma. Picha na Salim Shao
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akipongezwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Katiba na Sheria, Asha-Rose Migiro mjini Dodoma. Picha na Salim Shao

 

Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi na watu wa kawaida, wameunga mkono hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliyoitoa bungeni mwanzoni mwa wiki hii, lakini wakitia shaka kama wajumbe wa Bunge hilo wataunga mkono.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema hotuba hiyo imetoa mwelekeo na mustakabari wa taifa katika masuala nyeti yenye kugusa hisia za wengi.

Walisema kwamba mambo muhimu waliyosikia katika hotuba hiyo ni ufafanuzi wa muundo wa Muungano, mamlaka ya Rais na haki za binadamu. Mambo haya yamekuwa yakijadiliwa sana bungeni na hata mitaani.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Ruaha, Iringa, alisema siyo mara ya kwanza tume hiyo kutoa ufafanuzi, ila ana hofu Bunge linaweza kuvunjika kutokana na misimamo ya wajumbe.

“Kama Rais Kikwete hataweza kuingilia kati misimamo ya makundi, Bunge linaweza kuvunjika. Naomba atumie nafasi yake kushawishi ili kuunusuru mchakato huo,” alisema Profesa Mpangala.

Dk. Alexander Makulilo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema ufafanuzi wa Jaji Warioba, umeongeza uwezo wa kujenga hoja katika msimamo wa serikali tatu na kubadili mtazamo kwa serikali mbili.

“Wajumbe wengi walikuwa hawafahamu kuhusu mfumo huo, lakini baada ya hotuba ya ufafanuzi ya Jaji Warioba, sasa anaweza kujenga hoja na kushawishi mfumo gani utumike,” alisema Dk. Makulilo.

“Ni lazima sasa wajumbe wakubali kupima hoja zilizotolewa na kufanya uamuzi sahihi kuliko kuendelea kubaki na misimamo isiyo na tija kwa taifa,” alisema.

Mbashiru Ali, alisema jambo kubwa lililowagawa wabunge ni muundo wa Muungano. Hata hivyo Jaji Warioba alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu umuhimu wa muundo wa serikali tatu kuliko huu huu wa sasa.

Ali alisema ni vyema pande zote zikajitokeza na kueleza aina ya Muungano wanaoutaka ili kupima uzito wa hoja kabla ya kufanya uamuzi.

Mpaka sasa wanaounga mkono serikali tatu (tume), wametoa hoja zao na zimeeleweka, lakini hakuna wa kujitokeza kutetea muundo wa serikali mbili au moja kama ambavyo baadhi wanataka. “Hatuwezi kujadili mambo mengine kabla suala la Muungano halijawekwa sawa. Hata kama tunapigania haki za watoto na wanawake, tutazipata wapi kama hakuna nchi inayojitambua?” alihoji Ali.

Alisema ana matarajio kuwa katika hatua hii ya kujadili rasimu yenyewe, wabunge watatumia busara katika kujadili na kutoa uamuzi.

“Wajumbe wako Dodoma kama nchi moja, tunaomba warudi pia tukiwa na nchi moja. Watumie busara kujenga nchi moja yenye Katiba moja kwa manufaa yetu sote,” alisema Ali.

Naye Dk. Aidan Mutembei alisema hoja ya kuongezeka kwa gharama za uendeshaji pindi tutakapokuwa na Serikali tatu, hazina mashiko kwani wananchi bado wanaumia katika muundo tulionao sasa.

Dk. Mutembei alisema bora wananchi waumie kwa muda mfupi, lakini wakawa na uhakika wa maisha yao na vizazi vyao vijavyo.

“Nina matumaini wabunge watatumia busara kuimarisha Muungano. Ikiwa Muungano utavunjika, kila kitu katika nchi hii hakitasimama. Muungano ni shina la mti lililoshika kila kitu,” alifafanua Dk. Mutembei.

CHANZO:MWANANCHI

Zanzibar wawekwa kitimoto

 

Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali tatu na kwamba kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo yao. PICHA|MAKTABA
Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali tatu na kwamba kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo yao. PICHA|MAKTABA

 

Dodoma.Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) juzi jioni walipata wakati mgumu katika kikao cha ndani cha wabunge wa chama hicho wakituhumiwa kwa ‘usaliti wa Muungano’.

Kilichowaponza wajumbe hao ni kupitisha mabadiliko ya Katiba mwaka 2010 yanayoitaja Zanzibar kuwa ni nchi na hivyo kuvunja Katiba ya Muungano na kitendo cha baraza hilo kupendekeza Serikali tatu mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Kikao hicho kilifanyika muda mfupi baada ya Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba akieleza kuwa changamoto kubwa za Serikali mbili ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, uliotokana na Mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Katika hotuba yake, Jaji Warioba alisema pia kuwa baraza hilo lilipendekeza mfumo wa Serikali tatu kutokana na maelezo kuwa linataka Zanzibar huru, Tanganyika huru na Serikali ya Muungano huru na kila chombo kuwa na mamlaka yanayotambuliwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, zinaeleza kuwa wabunge wa CCM hasa wa Bara walielekeza lawama kwa viongozi wa Zanzibar hasa Baraza la Wawakilishi kutokana na kuwasaliti.

Chanzo chetu kimemtaja mmoja wa wazungumzaji, Christopher Ole Sendeka kwamba alieleza kwa uchungu kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Zanzibar ni usaliti mkubwa kwa Serikali ya Muungano.

“Sendeka aliongea kwa uchungu kuhusu Zanzibar kuvunja Katiba ya Muungano na alisema lazima chama kichukue hatua ili kunusuru Muungano,” alisema mjumbe mmoja wa kikao hicho.

Alipoulizwa kuhusu kauli hizo, Sendeka hakukanusha wala kukubali, bali alisema hayo ni masuala ya kikao cha ndani na hawezi kuyazungumzia.

Mbunge mwingine aliyetajwa kuzungumza ni Silivester Mabumba wa Jimbo la Dole, ambaye alieleza wazi kuwa ni vyema kuacha unafiki kuwa mnataka Serikali mbili wakati kuna mabadiliko ambayo mmepitisha kuwa Zanzibar ni nchi. Hata hivyo, Spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho baada ya kushambuliwa alieleza kutofautiana na kile ambacho kimeelezwa katika hotuba ya Jaji Warioba.

Kificho, licha ya kukiri kuwa mmoja wa waliosaini taarifa ya baraza hilo, alisema bado msimamo wa baraza ulikuwa ni Serikali mbili. Kauli hiyo ilithibitishwa jana baada ya kufafanua katika kituo kimoja cha televisheni kuwa msimamo wa baraza haujawahi kuwa ni Serikali tatu.

Baada ya lawama nyingi, inadaiwa wajumbe hao, walifikia azimio la kuandaa utaratibu wa kufanyia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kupitia kura ya maoni.

“Tumewaambia waone uwezekano wa kuifanyia marekebisho Katiba yao kama ukipitishwa muundo wa Serikali mbili,” alisema mjumbe mmoja.

Wawakilishi CUF wapinga

Hata hivyo, akizungumza na mwananchi jana, Ismail Jussa, ambaye ni mwakilishi kutoka CUF, alisema wamesikia maazimio ya kikao cha CCM lakini hawatakubali Katiba kufanyiwa marekebisho.

Jussa alisema mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, yalifuata sheria na kanuni na siyo rahisi kubadilishwa kama viongozi wa CCM wanavyofikiri.

Naye Mbunge wa Ole (CUF), Mohamed Mbaruku alisema iwapo CCM ikishinikiza kufanyika mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar, suala hilo watalifikisha mahakamani.

“Tumepata taarifa ya kikao chao, lakini tunawaonya wasilete vurugu Zanzibar. Makubalino ya mabadiliko ya Katiba ni sehemu ya mwafaka wetu, sasa wakileta hoja zao tutafika mahakamani,” alisema Mbaruku.

Hotuba ya Warioba yawatibua

Kinachoonekana wazi ni kuwa hotuba ya Jaji Joseph Warioba imelivuruga baraza hilo hasa baada ya kueleza kwamba kiini cha tume kupendekeza Muungano uwe wa Serikali tatu ni pamoja na maoni ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kificho jana alikana maoni hayo ya kutaka serikali tatu na kwamba kilichoelezwa na Jaji Warioba siyo tafsiri sahihi ya mapendekezo yao.

“Hii inaonyesha kwamba Tume yenyewe ilishakuwa na mwelekeo wa serikali tatu kwa sababu kama alivyoeleza Jaji Warioba kwamba walitafsiri maoni yetu kuwa ni yenye kuhitaji serikali tatu, na wakati mwingine, tafsiri inaweza kukupa maana tofauti na maana halisi,” alieleza Kificho alipohojiwa na TBC1.

Kificho alisema baraza hilo linaundwa na wawakilishi kutoka vyama mbalimbali – CCM na CUF na msimamo wa CCM ni serikali mbili na hana uhakika kwa upande wa CUF, ingawa anadhani ni msimamo wa serikali tatu. Hivyo ni vigumu kudai Baraza la Wawakilishi limepeleka mapendekezo yenye msimamo mmoja.

Maoni ya Kificho yalipingwa na Mwakilishi Rufai Said Rufai aliyesema kuwa alichosema Jaji Warioba ndicho kilichomaanishwa na baraza.“Ingawa sikuwa mjumbe katika Kamati ya Uongozi, kwa nafasi yangu ya uwakilishi, naafikiana kuwa maoni yaliyosomwa na Jaji Warioba bungeni ndiyo haswa tuliyopeleka na jinsi alivyoyatafsiri ndivyo tulivyomaanisha,” alieleza Said.

“Unaweza vipi kukana kudai serikali tatu, wakati unatoa maoni yanayodai kuwapo kwa mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya Muungano yaliyowekwa wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya kila mamlaka? Wanaokataa, wanakataa wanachokubali,” alifafanua Said.

Mjumbe mwingine ambaye yumo kwenye Kamati ya Uongozi, Abdallah Juma Abdallah alisema anayekana kauli ya Jaji Warioba hana akili na anajikanyaga.

CHANZO:MWANANCHI