Kanisa lachomwa Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Jengo la Kanisa la Pool Sloan Church kanda ya Zanzibar lililopo Kianga lililochomwa moto usiku wa kuamkiajana.
Jengo la Kanisa la Pool Sloan Church kanda ya Zanzibar lililopo Kianga lililochomwa moto usiku wa kuamkiajana.

WATU wasiojulikana wamevamia na kuchoma moto Kanisa la Pool Sloan Church kanda ya Zanzibar, Usiku wa kuamkia jana huko kianga mkoa wa kusini Unguja.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mlinzi wa kanisa hilo, Mussa Jackson alisema kwamba majira ya saa 4:oo Alfajiri Usiku wa kuamkia jana watu watatu walifika katika eneo la kanisa hilo wakiwa na mapanga pamoja na vipande vya nondo.

Mlinzi huyo alisema ,Watu hao walizunguka kanisa hilo ghafla Mlinzi huyo alitoka katika sehemu yake ya maficho na kukimbia huku akiomba msaada ndipo watu hao waliokuwa wamefunika vyuso zao wakaanza kumfukuza waliposhindwa wakarudi nyuma.

“Baada ya watu hao kunifukuza niliondoka nikiomba msaada kwa wakaazi waliokuwa eneo hilo,baadhi yao walijitokeza na tukaelekea kwenye kanisa tulipofika tukakuwa Kanisa limechomwa moto umeanza kushika paa la nyumba hiyo”Alisema Jackson

“Kwa kushirikiana na wakaazi wa eneo hilo tulifanikiwa kuzima ila ulikuwa ushaunguza baadhi ya vifaa katika sehemu ya mbele ya kufanyia ibada anapokaa kiongozi wa kanisa “Madhabauni”na sehemu zingine ndani ya kanisa hilo.”Aliendelea kuelezea Mlinzi
Naye Naibu Mkurugenzi wa makosa ya Jinai Zanzibar,ACP Yussuf Ilembo Alikiri kutokea kwa tukio hilo Jana Alfajiri huko Kianga Mkoa wa kusini Unguja,Alisema Jeshi la polisi Zanzibar linaendelea kuwasaka wahusika wa tukio hilo ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Kamanda Ilembo Amesema Kwamba kutokana na wingi wa matukio yanayojitokeza Zanzibar Jeshi hilo limeongeza nguvu za ziada kutoka makao makuu ya Polisi Tanzania Bara.

Kwa Upande wa Mjungaji Msaidizi wa Kanisa hilo, Penuel Wizdom  Alisema wanasikitishwa na jaribio la kuteketeza Kanisa hilo, kwani ni mara ya pili mwanzo lilibomolewa ukuta na watu wa nyuma na watu wasijulikana.

“Jambo la kusikitisha kuna waumini wa dini “hakuitaja jina”tunawasikia wakisema kwamba watahakikisha wanateketeza makanisa yote ya ukanda huo,kwani wao hawataki yawepo”Aliendelea kusisitiza Mchungaji huyo
Uchomaji wa Nyumba za ibada hasa makanisa Zanzibar yamekuwa ni matukio sugu jambo linalopelekea baadhi ya wananchi kuendelea kukosa imani na serikali.

Kuwawa kwa Pdri Mushi hakutokani na Itikadi za kidini – Askofu Shayo

Imewekwa na Nassor Khamis

Askofu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara miwili Augustino Shao akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na kuwawa kwa Padri Mushi huko Ofisini kwake Kanisa la Minara miwili.
Askofu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara miwili Augustino Shao akizungumza na Waandishi wa habari kuhusiana na kuwawa kwa Padri Mushi huko Ofisini kwake Kanisa la Minara miwili.

ASKOFU wa kanisa katoliki jimbo la Zanzibar,Augostino Shao Alisema matukio ya uhalifu yanayoendelea kujitokeza nchini hasa kwa waumini na viongozi wa kanisa hilo hayahusiani na itikadi za kidini bali yanafanywa na watu wachache  wasioitakia mema Zanzibar

Hayo yamesemwa na Askofu wa kanisa hilo  Augustino Shao wakati akizungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake Kanisa la Minara Miwili Shangani, mjini Zanzibar.

Alisema, kuongezeka kwa matukio ya uhalifu nchini, kunatokana na kutowajibika kwa watendaji wa vyombo hivyo, jambo alilosema linatoa nafasi kwa watu wenye dhamira ya kuchafua amani na utulivu uliopo nchini kutenda uhalifu.

“Matukio ya uhalifu, ubaguzi na chuki dhidi ya ukristo Zanzibar yanaendelea kushamiri kwani watu waliopewa dhamana ya kulinda na kusimamia amani na usalama wa wananchi wanaishia kukemea kwa maneno tu badala ya  vitendo.pindi kunapotokea matendo hayo”, alisema Askofu Shao.

“Siwezi kuhusisha matukio haya na tofauti za dini ya kikiristo na kiislam bali ni ukosefu wa umakini kwa watendaji wa vyombo vyenye dhamnana ya kusimamia maisha ya watu.”Aliendelea kusisitiza Askofu

Hata hivyo, alisema waumini pamoja na viongozi wa kanisa hilo hapa Zanzibar wanaendelea kuishi kwa hofu na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Aliongeza kuwa, uongozi wa kanisa hilo ulifanya juhudi za kuzungumza na watendaji wakuu wa serikali ya Zanzibar tangu lilipoanza vuguvugu la uchomaji makanisa na kufikia makubaliano ya kushirikiana katika kudhibiti hali hiyo.

Aliwataka waumini wa dini ya Kikristo na wananchi kwa ujumla kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki cha msiba wa Padri Evaristus Mushi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Mohamed, alisema jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aliwataka wananchi kushirikiana na polisi jamii kutoa taarifa zitakazosaidia jeshi hilo kukamilisha zoezi hilo kwa haraka zaidi.

“Tangu kuuwawa kwa Padri Evaristus Mushi juzi Jumapili, tuliitisha kikao cha dharura kwa maafisa mbalimbali wa Polisi, tukapeana majukumu ili kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni”, alieleza kamanda huyo.

Akizungumzia suala la umiliki wa silaha nchini, alisema kwa mujibu wa sheria za Tanzania hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kumiliki silaha ya aina yoyote isipokuwa kwa kibali maalum au taratibu zinazotambulika kisheria.

Kuuwawa kwa Padri Mushi kumeiondoshea sifa Zanzibar ya kuwa kisiwa cha amani – Maalim Seif

Imewekwa na Nassor Khamis

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa kauli nzito ya Serikali kuhusiana na mauwaji ya  Padre Evarist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar, wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF kisiwani Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akitoa kauli nzito ya Serikali kuhusiana na mauwaji ya Padre Evarist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar, wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF kisiwani Pemba.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amelaani vikali kitendo kwa kupigwa risasi na kuuliwa kwa Padre Evarist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar.

Amesema kitendo hicho kimevuruga sifa njema ya Zanzibar ya kuwa kisiwa cha amani.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF ametoa kauli hiyo kisiwani Pemba wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF inayofanyika ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi.

Amesema kwa niaba yake binafsi, chama chake na Serikali analaani vikali kitendo hicho cha kinyama ambacho kimeitia doa kubwa Zanzibar.

Amesema kitendo hicho ambacho hakikubaliki ni cha kusikitisha kwa vile Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa kuvuliana kwa kipindi kirefu bila ya kutoa vitendo hivyo.

Amesema ni wajibu wa Wazanzibari kuendeleza sifa njema ya Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuishi kwa kuvuliana na kuwapa matumaini wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa shughuli mbali mbali ikiwemo ya utalii.

Ameviomba vyombo vya dola kufanya kazi ya ziada kuwatafuta waliohusika na tukio hilo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo amesema wakati uchunguzi huo ukiendelea kufanyika, ni vyema kwa vyombo vya dola kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuepuka kuwahusisha watu wasiohusika na tukio hilo.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa kwake na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa kitendo hicho ni cha kigaidi.

Amekiri kuwa kitendo hicho ni kikubwa na kibaya, lakini hakijafikia hatua ya kuitangaza Zanzibar kuwa nchi ya kigaidi, na kwamba kufanya hivyo ni kuijengea sifa mbaya Zanzibar.

“Kauli kama hizi ukweli hazisaidii zaidi ya kutuvuruga, ni kweli ni kitendo kibaya na kikubwa, lakini ugaidi ni mkubwa zaidi na sisi hatujafikia na wala hatutofikia hatua hiyo”, alionya Maalim Seif.

Amesema ni vyema kwa viongozi wanaotokea upande wa pili wa Muungano kufanya mashauriano na viongozi wa Zanzibar kabla ya kutoa kauli ambazo zinaijengea sifa mbaya na kuitia doa Zanzibar.

Wakati huo huo Maalim Seif amesema ni lazima maamuzi ya madiwani yaheshimiwe na watendaji wengine katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema madiwani ndio wafanya maamuzi katika Serikali ya mitaa,hivyo maamuzi yao yaheshimiwe na watendaji ili kujenga mustakbali mwema katika kuwatumikia wananchi.

Amefahamisha kuwa tatizo lililopo sasa ni kuwa mfumo uliopo unatoa mamlaka makubwa kwa watendaji, hasa makatibu wa Halmashauri na  Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa.

Amesema wakati Serikali imo katika mchakato wa kuleta mageuzi  katika Serikali za Mitaa Zanzibar, ni vyema mageuzi hayo yakarekebisha hali isiyoridhisha iliyopo sasa.

Ametoa wito kwa Madiwani  kuchapa kazi kwa bidii, na kuhakikisha wanayafahamu, kuyasimamia na kuyatekeleza ipasavyo majukumu waliyokabidhiwa.

Aidha Maalim Seif amewasihi Madiwani wa CUF kutokubali kuburuzwa na watendaji, na kuhakikisha kuwa maamuzi yao katika Mabaraza na Halmashauri yanaheshimiwa na kutekelezwa kwa ukamilifu.

“Lazima mujue matumizi ya kila senti moja. Lazima muhakikishe kuwa hakuna upendeleo katika ugawaji wa rasilimali kwa Shehia zilizomo katika Halmashauri au Baraza”, alisema Maalim Seif na kuongeza,

“Endapo Katibu au Mtendaji hafuati maagizo ya Madiwani na anafanya atakavyo, lazima mumuarifu Waziri anayehusika, na kama Waziri atapuuza wasilisheni ripoti kwa Makamu wa Pili wa Rais”,

Amefahamisha kuwa ili malengo ya utekelezaji yaweze kufikiwa ni vyema kwa madiwani kufanya kazi bega kwa bega na watendaji wengine wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Masheha, kwa vile kazi na maeneo yao ya kazi yanalingana.

Jumla ya madiwani 83 wa CUF kutoka Pemba na Unguja wanashiriki semina hiyo ya siku 6 ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji madiwani, inayofadhiliwa na Taasisi ya Friedrich Naumann Foundation (FNF) ya Ujerumani.

Hassan Hamad, OMKR

“Tutahakikisha Magaidi hawa tunawatia mikononi” asema Dkt, Nchimbi

Imewkwa na Nassor Khamis

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt, Emmanuel Nchimbi akizungumza na Waandishi wa Habari Makao makuu ya Polisi Zanzibar.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt, Emmanuel Nchimbi akizungumza na Waandishi wa Habari Makao makuu ya Polisi Zanzibar.

Na Nassor Khamis

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt, Emmanuel Nchimbi amesema serikali inafanya juhudi kuhakikisha inawakamata watu waliomuua kwa kumpiga risasi Padre Evaristus Gabriel Mushi wa kanisa katoliki Parokia ya Minara miwili Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Makao makuu ya Polisi Zanzibar Dkt, Nchimbi amesema serikali imesikitishwa na tukio hilo na tayari Jeshi la Polisi zanzibar kwa kushirikiana Makao makuu ya Polisi Dar es salaam wameanza uchunguzi wa tukio hilo.

Alisema kuwa tukio la kushambuliwa kwa Padre Mushi  si tukio la ujambazi bali ni tukio la kigaidi hivyo serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha magaidi hawa wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tutahakikisha magaidi hawa tunawatia mikononi kwa nguvu zote na kuwapeleka katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake” alisema Dkt, Nchimbi

Alisema kuwa watu waliofanya uhalifu huo wana lengola kuipeleka nchi katika machafuko yasiyo na lazima kwani uhalifu wao wamelenga kushambulia viongozi wa dini na kuwatia hofu wananchi jambo ambalo ni hatari kwa taifa.

Alisema kuwa tukio la kuuwawa kwa Padre Mushi linafanana na tukio la kushambuliwa kwa risasi Padre Ambrose Mkenda wa kanisa katolilki Parokia ya Mpendae mwishoni mwa mwaka jana kutokana na mazingira yaliyotumika kumshambulia Padre Mkenda ndio mazingira yaliyotumika kumuua Padre Mushi.

“Waliomshambulia Padre Ambrose Mkenda mwishoni mwa mwaka jana ndio waliohusika na mauaji ya  Padre Mushi kwani aina ya silaha na mazingira yaliyotumika yanafanana” alisema Dkt, Nchimbi.

Aidha alifahamisha kuwa katika kukabiliana na matukio ya kihalifu yanayoendelea kutokea Wizara imeomba kibali cha kushirikiana na Mashirika ya kimataifa ya upelelezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete ili kuwabaini wahalifu hao haraka iwezekanavyo.

Alisema kuwa serikali inalipa uzito mkubwa suala hili hivyo itagharamia gharama zote zitakazo hitajika kuendelea na upelelezi wa tukio hilo utakaofanyika kwa kushirikiana na mashirika hayo.

“Serikali haijashindwa kulishughulikia tatizo hili bali inalipa uzito mkubwa kutokana na hali ya nchi inavyoelekea” alisema Waziri Nchimbi.

Dkt, Nchimbi aliwataka Watanzania kutokujiingiza katika mitego ya kuchukiana katika misingi ya kidini na kuwataka kuwa wavumilivu katika kipindi hichi ambacho Jeshi la Polisi linaendelea na Uchunguz

Padre Evaristus Mushi aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana ambao walikua wamepanda pikipiki aina ya Vespa leo asubuhi wakati akielekea kuongoza ibada ya misa katika kanisa la Mtakatifu Theresia lililopo Beit el Rass mjini Zanzibar.

CCM yalaani mauaji ya Padri Mushi

Imewekwa na Nassor Khamis

Afisi kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
Afisi kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.

 

Chama Cha Mapinduzi kimetaja kusikitishwa kwake na tukio la kinyama lililofanywa na watu wasiojulikana kumpiga risasi na kumuua Padri wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya Beilt Ras Padri  Evaristy Mushi Viswani Zanzibar leo asubuhi.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamatiwa Maalum ya MNEC Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi Waride Bakari Jabu na kulitaja tukio hilo na mengine yakijumuishwa katika orodha yavitendo vya ukatili na uhalifu kunakoongeza taharuki Zanzibar.
Waride alisema mfululizo wa mashambulizi kwa viongozi wa dini  kuijengea taaswira chafu Zanzibar huku watuhumiwa wa matukio hayo bado wakiwa hawajawakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Chama Cha Mapinduzi kwa upande wake kimeyalinganisha  matukkio hayo yote kama yanayosimama  katika ukatili wa kutisha ,ukijenga sintofahamu, kuleta mgawanyiko , kuathiri mashirikiano, umoja wa kitaifa na sifa njema ya visiwa hivyo.
“Tunavitaka vyombo vya upelelezi kufanya kila linalowezekana kwa mwendo wa haraka kuhakikisha vinayadhibiti matukio hayo pamoja na   watuhumiwa kuwakamata,nilazima wachululiwwe hatua , chimbuko lake lijulikane na kukomeshwa kwa  uharamia huu “AlisemaWaride
Alisema ukimya wa vyombo vyenye dhamana ya upepelezi na kutokuwepo kwa uchunguzi dhidi ya matukio yanayowaandama viongozi wa dini kukatisha tamaa na kutotoa picha halisi ya utendaji wa kazi zao.
“Matumaini ya watu na maisha yao yako mikononi mwa vyombo hivyo, tunataka wafanye kazi zao kwa utaalam ,umakini na kuwakamata wahalifu wa matukio hayo bila urasimu, amani yetu ni zaidi ya rasilimali yeyetote”Alisema
Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar aliyataja matukio yanayotokea hivi sasa na yale ya nyumba za ibada kuchomwa moto,kiongozi wa kiislam sheikh Fadhil Sotraga  kumwagiwa tindikali, Padri Ambrose Mkenda kujeruhiwa kwa risasi na sasa Pdri Mushi kuuawa, hakuletei muonekano mwema Zanzibar.
‘Vitendo hivyo vimekosa kuthamini  utu huku vikikiuka ustaarabu uliozooeleka  kwa karne nyingi ha0pa hapa Zanzibar, CCM  tunalaani vikali  kushamiri na kujitokeza kwa vitendo vya kihalifu na kiharami,wote ni lazima tushirikiane kuwafichua na kupinga ukatili huu”.Alisema
Hata hivyo Chama Cha Mapinduzi kimetoa wito na kuwaomba wananchi ,viongozi wa kiroho na waumini wa dini mbalimbali kuwa wastahamilivu hivi sasa huku vyombo vyenye dhamana vikifanya kila linalostahili kuwatia nguvuni wahusika wa matukio hayo .

Padri wa Kanisa Katoliki auwawa kwa kupigwa risasi Zanzibar

Padri Evaristus Mushi alieuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Padri Evaristus Mushi alieuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

PADRI wa kanisa katoliki jimbo la Zanzibar,amepigwa risasi za kichwa na kifuani na kuuwawa na watu wasiojulikana.

Padri huyo aliyetambuliwa kwa jina la Evaritus Gabriel Mushi wa kanisa katoliki parokia ya mtakatifu Joseph Shangani mjini , Zanzibar

Watu hao ,ambao hawajafahamika wala kukamatwa ,walifanya unyama huo leo majira saa moja na nusu asubuhi nje ya kigango cha  mtakatifu theresia kanisa la mtoni,wakati akijiandaa kushuka kwenye gari kuingia kanisani kufanya maandalizi ya ibada ya jumapili.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake, kamishna wa jeshi la polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa Alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa jeshi hilo Padri Mushi ,alipigwa risasi akiwa kwenye gari na kujeruhiwa vibaya sehemu za kichwa na kifua.

Alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo punde baadhi ya waumini wa kanisa hilo waliofika katika kanisa hilo  kwa ajili ya ibada walimpeleka Padri Mushi katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu baada ya muda mchache Akafariki dunia.

“Kutokana na uzito wa tukio hili jeshi la polisi Zanzibar linaendelea na upelelezi wa kina kuhakikisha wahusika wote wanafikishwa katika vyombo vya kisheria.”Alisema kamishna Mussa
“Natoa wito kwa wananchi washirikiane na maafisa wetu juu ya taarifa zozote zinazohusiana na tukio hili ili tuweze kutekeleza majukumu kwa wakati.” Aliendelea kusisitiza

Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ,ACP Aziz Mohamed alisema kwa sasa jeshi la polisi linaendelea na doria katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Zanzibar ili kuhakikisha wale wote wanaohusika katika mauaji ya padri huyo wanakamatwa.

Wakati huo huo ,Naye Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Abdallah Mwinyi Amefika katika Viunga vya Hospitali ya Mnazi Mmoja Mnamo wa Saa 4 Asubuhi  kwa ajili ya kuwafariji Jamaa,ndugu na waumini wa dini hiyo waliofika katika eneo hilo kwa ajili ya kufuatilia hatima ya kiongozi wao.

Akizungumzia tukio hilo,msemaji wa kanisa hilo ambaye pia ni katibu mkuu wa kanisa katoliki jimbo la Zanzibar padri Cosmas Shayo aliwataka waumini wa kanisa hilo,kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki hadi suala hilo litakapotafutiwa ufumbuzi.

Alisema Uongozi wa kanisa hilo,umepokea suala hilo kwa masikitiko makubwa pia kufariki kwa padri huyo ni miongoni mwa pigo kubwa kwa waumini na kanisa kwa ujumla.

“Tukio hili si la kufumbia macho kwani viongozi na waumini wa kanisa katoliki Zanzibar kwasasa tunaishi kwa mashaka hali ya kuwa,mtu ukitoka asubuhi huna uhakika wa kurudi jioni ukiwa hai”Alisema padri Shayo.

“Kwa nini matukio haya yanaandama waumini na viongozi wa  kanisa katoliki hapa kuna agenda ya siri hadi tunafikia hatua ya kuishi kama watumwa tukiwa na hofu juu ya usalama wa maisha yetu,serikali na vyombo vya ulinzi vikiwa vinakaa kimya.”Aliendelea kusema Padri shayo.

Alisema Kanisa linathamini mchango mkubwa uliotolewa na marehemu wakati wa uhai wake,katika kuliendeleza kanisa kwenye huduma za kiimani na kiroho kwa waumini wa kanisa.

Baadhi ya mashuhuda ,waliozungumza kwa nyakati tofauti katika eneo la tukio ambapo walisema kwamba walifika mapema katika Kanisa hilo kwa ajili ya maandalizi ya ibada,pembeni mwa kanisa hilo kulikuwa na watu watatu ambao hawakujulikana kwa haraka ghafla baada ya kufika padri Mushi walisikia milio ya risasi wawili wakaondoka mbio na pikipiki aina ya vespa na mmoja akatokomea Vichochoroni.

Wananchi wamesikika wakitupia lawama jeshi la polisi kwa kushindwa kudhibiti uharifu na umiliki wa silaha kinyume cha sheria,kwani matukio ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini mbalimbali Zanzibar yameshamiri

Dkt, Bilali aongoza zoezi la uteketezaji wa silaha haramu Jijini Dar

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Simon Siro, wakati wakipita kukagua sihala hizo, haramu kabla ya kuanza kwa zoezi la uteketezaji wa silaha hizo, lililofanyika Ukonga, jijini Dar es Salaam leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Simon Siro, wakati wakipita kukagua sihala  haramu kabla ya kuanza kwa zoezi la uteketezaji wa silaha hizo, lililofanyika Ukonga, jijini Dar es Salaam leo.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, ameongoza zoezi la uteketezaji silaha haramu na kuwataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kuwafichua wanaomiliki silaha hizo, mapema kabla athari haijawa kubwa zaidi.

Akizungumza katika zoezi hilo, la kuteketeza silaha haramu, ambalo limefanyika pamoja kwa  nchi  wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye viwanja vya Magereza, Ukonga Jijini Dar es Salaam leo, Dk. Bilal alisema  kila mwananchi ni mlinzi wa kwanza wa amani ya nchi yake  na  wanaomiliki silaha haramu ni wazi kuwa siyo raia wenye malengo mema na amani ya nchi zao.

“Naomba kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanikisha zoezi hili ambalo linalenga kutukumbusha kuwa ili tuwe na Jumuiya bora yenye kupiga hatua, hatuna budi kuhakikisha eneo letu linabaki kuwa salama na kwamba wananchi wetu wanapata nafasi ya kufanya kazi zao za kujiongezea kipato bila kuwa na hofu ya usalama wa maisha yao,”

Alisema ndani ya Jumuiya kumekuwa na migogoro mbalimbali sambamba na matukio ya kihalifu ambayo mengi huchangiwa na uwepo wa silaha ndogo na kubwa ambazo hazimilikiwi kihalali.

Alisema takwimu zilizopo zinabainisha kuwepo kwa silaha haramu zipatazo 500,000 (laki tano) katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki hali ambayo inaonesha kuwa kuna kazi kubwa ya kukabiliana na migogoro ya aina mbalimbali ya uhalifu inayojitokeza katika jamii.

Alisema kufuatia raia wasio waaminifu kumiliki silaha haramu kumekuwepo na ongezeko la matukio ya kihalifu yanayotumia silaha na matukio mengi katika ukanda wa Afrika Mashariki yanatokea katika maeno ya mipakani na yale yanayohusisha muingiliano wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, matukio ya ujambazi,  uvamizi na mengine ya aina hiyo.

Alisema ongezeko la silaha haramu lina athari nyingi katika maisha na maendeleo kwa ujumla na kutaja athari ya wazi kabisa inayotokana na ongezeko la silaha hizo kuwa ni ile inayojitokeza katika sekta ya Utalii ambako watu wameshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ujangili unaofanywa katika mbuga za wanyama ambao unahatarisha kwa kiasi kikubwa mafanikio katika sekta ya Utalii.

“Tusipowadhibiti majangili mapema, siku wanyama wakipungua watahamia katika sekta nyingine. Kazi hii itakuwa rahisi kama tukiifanya kama Jumuiya na sio nchi moja moja,” alibainisha Makamu wa Rais.

Dkt. Bilal alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia Jumuiya ya Afrika Mashariki kukabiliana na tatizo la silaha haramu na hasa Shirika la Maendeleo la Ujerumani GTZ ambalo limesaidia katika kufanikisha zoezi hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini Klaus Brandes alisema  Serikali ya Ujerumani itaendelea kuisaidia Jumuiya katika kukabiliana na tatizo la silaha haramu ili kuhakikisha eneo la ukanda wa Afrika Mashariki linabaki kuwa na amani na salama.

Alielezea kufurahishwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kutatua migogoro kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Na Ofisi ya Makamu wa Rais, Dar es salaam

Yatima abakwa miaka 10 kwenye danguro Dar

  •   Alawitiwa na kuambukizwa virusi vya ukimwi
  •   Polisi naye adaiwa kumbaka akiwa kituoni

Imewekwa na Nassor Khamis

Nyumba inayoonekana ni ghorofa inayodaiwa kutumiwa kama danguro iliyopo Mwananyamala Magengeni jijini Dar es Salaam
Nyumba inayoonekana ni ghorofa inayodaiwa kutumiwa kama danguro iliyopo Mwananyamala Magengeni jijini Dar es Salaam

Msichana yatima, mkazi wa mkoani Manyara, amefungiwa kwenye danguro  kwa zaidi ya miaka 10 akinyanyaswa kingono, kuteswa na kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi  (VVU).

Msichana huyo aliyeondolewa nyumbani kwao Oysterbay mjini Babat,i  alilaghaiwa na mwanamke aliyejifanya kuwa msamaria mwema, akitangaza  nia ya kumsaidia kielimu na kimaisha, kufuatia kifo cha mama yake mzazi.

Msichana aliyefikwa na masahibu hayo ni  Sara Tarimo (27) ambaye aliangukia mikononi mwa  mwanamke mwenye danguro hilo, Abia Lucas (44) anayeishi Mwananyamala Magengeni.

Ilikuwa ni baada ya kifo cha mama yake  Magreth Kitinati, aliyekuwa akiishi naye  Oysterbay huko Manyara.

Sara anasema mwanamke huyo alimtoa kijijini kwao hadi jijini Dar es Salaam, na kumshinikiza kwenye `utumwa wa ngono’ kwa kipindi cha miaka 10 akiwa amefungiwa ndani.

Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, mama yake mzazi alifariki, hivyo ujio wa msamaria huyo ulikuwa faraja na tumaini jipya kwa maisha yake. Haikuwa hivyo.

Sara alisema  alipoteza bikra yake baada ya kumlazimisha kufanya ngono  na mwanamume mtu mzima, aliyembaka na ukawa mwanzo wa kutumiwa kingoni na wanaume wa kila aina.

Sara alisema alifanywa unyanyasaji huo akiwa na miaka 13 na kwamba hilo lilikuwa   tukio lake la kwanza kukutana na mwanaume.

Baada ya kufanikiwa kutoroka na kuwataarifu polisi nyendo za mama huyo ambaye sasa anashikiliwa kwa mahojiano, Sara anasimulia kumbukumbu za kusikitisha za miaka aliyoipoteza katika himaya ya danguro la ‘msamaria.’

HISTORIA YAKE

Sara ni mmoja wa watoto watatu katika familia yao. Kaka  yake  Emmanuel Tarimo (31) na dada yake Neema Tarimo.

Wakati akipochukuliwa na ‘msamaria’ alimuacha kaka yake huko Babati akijitafutia riziki kwa kubeba mizigo na dada yake akiendelea na masomo ya shule ya msingi.

Anasikitika kuwa katika maisha yake hakubahatika kumfahamu baba yake, lakini aliwahi kuelezwa na mama yake kuwa ni mwenyeji wa Kilimanjaro.

Mama yake ndiye aliyekuwa anatunza familia yao licha ya  kwamba hakuwa na ajira rasmi, wala biashara za kudumu.

Mazingira hayo, yalimlazimisha kukatisha masomo  akiwa darasa la tatu katika shule ya Msingi Idangunyii.

Anasema alikuwa na ndoto ya kupata elimu zaidi, lakini kifo cha mama yake kilisababisha ajione kuwa  hana bahati.

MAISHA KWENYE DANGURO

Alisimulia kuwa,  baada ya ‘msamaria ‘ kujitokeza na kumwahidi  kuwa atamtafutia shule na kugharamia elimu alimsikiliza na kumfuata hadi jijini  Dar es Salaam.

Sara alieleza kuwa mwanamke huyo alipofika nyumbani kwao Babat, alieleza kuwa anatafuta wasichana 10  kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwa familia za  Dar es Salaam.

“Aliiambia  familia yangu kuwa, hata kama wasichana watakaopatikana watakuwa wanasoma wataendelezwa mara baada ya kufika mjini wakati wakiendelea na kazi ,’’ anasema na kuongeza:
“Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa mwaka 2003, tuliondoka kwa usafiri wa basi tukiwa 10  ingawa sikuwatambua wenzangu kwa sababu alituchukua kutoka katika vijiji tofauti.”

Alisimulia kuwa walifika nyumbani kwa mwanamke huyo Mwananyamala Magengeni kwenye ghorofa mbili, ambayo juu linaonyesha ujenzi unaendelea.

Alisema wakiwa nyumbani kwa mama huyo, walibadilishwa mavazi kutoka yale waliyotoka nayo kijijini na kupewa nguo nyingine- sketi fupi, kaptula na  blauzi maarufu kama ‘vitop’.
Alikumbuka kuwa  baada ya kupewa nguo hizo, walitakiwa kila mmoja akajipumzishe kwenye chumba chake vilivyokuwa ghorofa ya kwanza.

 KUBAKWA MARA YA KWANZA

Alieleza kuwa siku hiyo akiwa chumbani kwake mlango uligongwa na alipouliza ni nani, alijibiwa na sauti ya kiume kuwa ni mlinzi.

Alipofungua,  mwanaume mtu mzima alimwambia wakati huo sio wa kulala bali ni wa kazi na kumtaka avue nguo huku akimtisha na  bisibisi.

Vitisho  vilitawala akilazimishwa kufanya ngono kwa nguvu na  mwanaume huyo  aliyetumia bisibisi kumchoma  mdomoni  na mkononi  karibu na kiwiko.

“Nilipiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna aliyekuja kunisaidia hadi yule mzee alipomaliza haja yake  na kuniacha nikiwa kwenye maumivu makali.”

Anasema  hakuamini kilichotokea na kulalamika kwa mwenyeji wake….“Nilimfuata yule mama kumweleza yaliyonitokea cha ajabu aliniambia hiyo ndiyo kazi niliyofuata mjini.”

Anasema “baada ya kupewa maneno hayo makali nilipelekwa  kwa daktari wa  hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi.”

Anasema aliendelea kuwa mtumwa wa ngono kwa sababu baada ya matibabu akawa anaendelea na kazi hiyo.

Sara anasema katika hospitali hiyo ndiko walikokuwa wanatibiwa na mwanamke huyo alimweleza kuwa huyo ni daktari wao.

Anasema aliwahi kudhalilishwa kingono na wanaume zaidi ya 10  kwa siku moja, wakiwa wa rika, tabia  na maumbile  tofauti.

“Nakumbuka siku moja alikuja mteja aliyekuwa amelewa,  akaniambia amelipa fedha nyingi kwa mama na anachotaka ni kunitumia kinyume cha maumbile.”

“Sijawahi kufanya hivyo, nilipokataa alitoa kisu na kunitishia…alinilazimisha nivue nguo na kulala  kitandani kabla hajanijeruhi.” Anasema.

“Nikiwa kitandani alidondosha kisu  tumboni mwangu, akakilalia na kunijeruhi, nikakimbizwa Mwananyamala na kutibiwa na yule daktari wa mwanzo niliyeambiwa ni  tabibu  wetu ambaye alinishona  sehemu nilizojeruhiwa na alikuja nyumbani kunitoa  nyuzi,” anasema
MALIPO
Sara anasema hakuwahi  kulipwa japo   wakati wakiendelea na kazi hiyo, mwanamke huyo aliwaeleza kuwa malipo yao ni Sh. 30,000 kwa mwezi na kwamba wangelipwa baada ya kukamilisha alichokitaka.

Akielezea faida waliyomtengenezea mama huyo alisema alikuwa akitoza kati ya Sh. 10,000 hadi 15,000 kwa wateja waliofanya ngono kwa njia ya kawaida na wale waliokuwa wakiwaingilia kinyume cha maumbile ilikuwa aliwalipisha  kati ya Sh. 30,000 na 50,000.
Anaeleza kuwa walikuwa  wakipatiwa  matibabu, chakula na kununuliwa mavazi lakini hawakuruhusiwa kutoka nje ya nyumba hiyo.

“Niliwahi kumhoji mama kwa nini alitudanganya unatuleta mjini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na kutusomesha?”

“ Nilimuomba anirudishe nyumbani, lakini alikataa na kuniambia kazi yake itakapokwisha nitarudi  sikuyaelewa majibu haya,” anasema.
ALIVYOTOROKA
Alisema baada ya kutumikishwa  kwa muongo mmoja, Februari 4, 2013,  siku  aliyofanikiwa kutoroka baada ya mwanaume aliyefanya naye mapenzi siku ya kwanza  kufika kwenye danguro hilo akihitaji huduma yake.

“Alilipia  na kuja chumbani kwangu na kunieleza kuwa lile embe lililokula kipindi kile  lilikuwa bichi, hivyo amekuja kwa mara nyingine  likiwa limeiva na baada ya kumaliza haja zake.”

“Aliniambia anataka kunipa zawadi hivyo niliporuhusiwa na mama tuliondoka naye, tukipita maeneo tofauti akinielekeza majina ya mitaa na mwishowe tuliingia sokoni Kariakoo,” anasimulia.

Waliondoka na gari aina ya Volkswagen  hadi Kariakoo na  wakati huo alihisi njaa  na kumuomba kabla ya  kumnunulia zawadi,  wanunue kwanza chakula.

Mteja huyo katika mazungumzo yake alimfahamisha kuwa ni mwanasheria anayefanya kazi manispaa japo hakutaja jina.

“Tukiwa njiani alikokuwa amekusudia kunipeleka nilikuwa nikitembea nyuma yake,   hapo ndipo nilipotoroka nikikimbia bila kujua ninaelekea wapi, nilizunguka na hatimaye giza liliingia na watu walipungua kwenye eneo nililokuwapo.”

“Sijui ilikuwa saa ngapi, lakini  niliona gari la polisi niliamua kuwafuata nikamueleza askari wa  kike  mkasa mzima,” alisema.

Anasema walikwenda kituo kikuu cha polisi na kuchukuliwa maelezo lakini pia alimpatia nguo nyingine kwa vile alikuwa amevaa mavazi yasiyo na staha.

“Siku iliyofuata niliambiwa kuna dawati la kushughulikia masuala ya wanawake, lakini kwa wakati huo wahusika hawakupo. Ilipofika Alhamisi nilikabidhiwa kwa askari mwingine anaitwa Happy.”

Aliongeza: “tuliondoka naye hadi Oysterbay polisi, huko walitoka askari kadhaa kwenda  Mwananyamala nyumbani kwa  mama huyo.”

Sara alisema walifanya upekuzi kwenye vyumba walivyokuwa wakilala bila mafanikio, walishuka chini na kumuamuru afungue moja ya vyumba vilivyokuwa vimefungwa lakini mwanamke huyo alikataa na  polisi walimuagiza aende kituoni kuandika  maelezo dhidi ya  tuhuma hizo.

Alieleza kuwa wakati mtuhumiwa huyo akiwa mahabusu watoto wake anaoishi nao mmoja mwanaume mwenye  miaka 27 na mwingine wa kike walimsihi afute kesi hiyo, lakini alikataa na kuongeza kwa alifungua jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu  RB/2468/2013  la Februari 7.

VYOMBO VYA HABARI

Alisema amefikisha suala hili kwenye vyombo vya habari akiomba msaada wa nauli ili aweze kurudi kwao pamoja na chakula.
“Kabla sijafika NIPASHE nilitoa taarifa kwenye Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambacho kimeahidi kulifanyia kazi suala langu,” anasema.

AFYA YAKE

Sara analalamikia kuwa na vivimbe mbavuni  na sehemu za siri na anahofu kuwa huenda ameambukizwa magonjwa ya ngono na Ukimwi.

Anasema ana wasiwasi  kwa vile aliwahi kupata vipele vingi  mwilini japo  daktari wao alimueleza kuwa vilisababishwa na joto lakini sasa  vimekuwa uvimbe mkubwa.

Anasema wakiwa kwenye danguro hilo daktari wao alikuwa anawapa dawa mara kwa mara ambazo hawafahamu zilikusudiwa kutibu nini na zilipomalizika aliendelea kuzileta japo hakuwahi kutumia tiba hiyo.

KONDOMU

Anasema baadhi ya  wanaume wenye ndoa walitumia kondomu wakati wa kufanya ngono lakini asilimia kubwa ya wateja wa danguro hilo walikuwa hawatumii mipira hiyo ya kiume.

“Walikuwa wananiambia nina mke ninampenda hivyo natumia kondomu lakini wengine walikuwa hawatumii, chumbani tulikuwa tunawekewa kondomu lakini  ukiwaambia wazitumie wanakataa.”

KUGUNDULIKA NA VVU
Sara anasema Jumatatu Februari 11,  akiwa  polisi Oysterbay, aliamriwa kuondoka eneo hilo kwani si sehemu ya kuishi nail kufungua mashtaka.

“Nilikwenda kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo lakini usiku nilizidiwa ilipofika  asubuhi nilikwenda zahanati ya Mwenge nilikotibiwa na kuelezwa kuwa nimeambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kutakiwa kuanza kutumia dawa.”

KULAWITIWA NA  POLISI
Wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Abia  ukiendelea, inadaiwa kuwa usiku wa Jumatano  polisi wa kituo cha Oysterbay alimlawiti Sara eneo lenye migomba kituoni hapo.
Akizungumza na NIPASHE kwenye kituo cha trafiki kilichopo kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo,  alisema  alifanyiwa unyama huo baada ya polisi kumfuata akiwa amelala kwenye maegesho ya magari.

Anasema alikwenda Ubungo kuchukua nguo  alizozificha hapo na akiwa huko alikutana na  askari huyo ambaye alimueleza matatizo yake, ndipo akamtaka wakale chakula.

“Baada ya chakula wakati tunarudi kituoni, aliniambia nimlipe kwa kumruhusu kunifanyia tendo hilo lakini nilikataa na askari huyo alinishika kwa nguvu na kunilawiti.”

Anaongeza kuwa kutokana na kitendo hicho aliondoka kituoni hapo  saa 12:00 asubuhi na kufikisha taarifa ITV kwa vile aliona polisi hawakuwa na msaada kwake.

Baada ya kutoa malalamiko yake na kusaidiwa na wafanyakazi wa ITV alijitokeza  polisi mwanamke na kumchukua kwa matibabu kwenye zahanati ambayo Sara alisema haifahamu na baadaye kupelekwa kituo cha mabasi Ubungo ili kurudishwa nyumbani kwao Manyara.
Alimweleza Mwandishi Wetu kuwa aliomba simu kutoka mtu aliyekuwa kituoni hapo ili awasiliane naye kabla hajasafirishwa na polisi hao.

Baada ya mwandishi kufika Ubungo na kufanya mahojiano na Sara gari la polisi   lenye namba PT 2083  lilifika na kumpeleka  polisi  Oysterbay  na kuandikisha  maelezo.
MAELEZO YA POLISI

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, John Mtalimbo,  alipofuatwa alisema taarifa zipo kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kinondoni (OCD).

Aidha, alisema kwa mujibu wa OCD msichana huyo amekuwa akitangatanga maeneo ya  Buguruni na sehemu nyingine ambazo hakuzitaja.

“Naona lengo lake ni kutuchafua, kwa nini asubuhi alikuja ITV na sio kutoa taarifa kwetu kama amelawitiwa na askari wetu, anatuchafua,” alisisitiza  Kamanda Mtalimbo.
Alikiri kuwa siku mbili zilizopita polisi ilimtafutia tiketi ili kumrudisha kwao lakini haikufanikiwa.

Kamanda alipoulizwa sababu za kumsafirisha Sara wakati amefungua kesi ya kuuzwa kimwili  kwenye danguro alisema ni kutokana na kukosa makazi.

Awali, Mwandishi Wetu alinasa mawasiliano ya simu ya Kamanda Mtalimbo na mtu aliyeelezwa kuwa  ni OCD   akimwelekeza jinsi yakuandika maelezo dhidi ya binti huyo.
Alisikika akisema: “Inabidi tujipange, hapa watakuja waandishi wa habari, (bila kujua kama mwandishi wetu alikuwepo eneo hilo), watataka kujua kinachoendelea na kumshauri andike kuwa walikubaliana kufanya ngono.”

Licha ya kusikia kilichozungumzwa juu ya mlalamikaji huyo  alipoingia ofisi kwake na   kujitambulisha  na kuuliza habari za Sara Mtalimbo alimweleza kuwa hana taarifa hizo na kwamba anasubiri zitoke kwa OCD.

Akisoma maelezo ya OCD wa Kinondoni,  Mtalimbo alisema Februari 2, mwaka huu Sara  aliripoti kituo hapo kuwa alikuwa akiishi Mwananyamala alikokuwa akifanyishwa kazi za kuuza mwili na mtuhumiwa aliyemtaja kwa jina la Abia.

Alisema baada ya polisi kupokea  malalamiko hayo  walikwenda Mwananyamala kuonyeshwa danguro hilo na polisi walipomkamata Abia mlalamikaji alishindwa kumtambua na kuongeza kuwa walifungua jalada la uchunguzi na kwa sasa mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana na Sara aliendelea kubaki kituoni hapo hadi alipoonekana ITV jana asubuhi.

Kamanda alielezwa kuwa katika mahojiano ya Sara na OCD alimfahamisha kuwa  Jumatano wiki hii akiwa Ubungo alitongozwa na askari aliyemuahidi kumpatia Sh. 10,000 baada ya kumlawiti.

“Walikwenda kwa makubaliano migombani na  baada ya kufanya kitendo hicho, askari alimpa Sh. 20,000 ,” alisema na kuhoji sababu za  msichana huyo kutofikisha  tukio hilo kituoni badala yake alikimbilia ITV.

Hata hivyo alipoulizwa iwapo mlalamikaji amemtambua askari huyo kupitia gwaride la utambuzi na iwapo alichukuliwa hatua alisema bado na kuongeza:”Maelezo niliyokupa ndiyo mambo mengine yatafuata baadaye.”
NYUMBANI KWA ABIA

Gazeti hili likafika nyumbani kwa Abia na kukutana na  binti  alijitambulisha kuwa anafanyakazi za ndani na kueleza kuwa mwenye nyumba  hakuwepo na hajui alikokwenda.
Alipoulizwa kuhusu danguro binti huyo mwenye miaka kati ya 13 na 20  alisema hafahamu kinachoendelea kwani mwajiri wake anamkataza kutoka nje kukutana na  majirani lakini akadokeza kuwa Jumatatu wiki hii walikuja polisi wakamkamata mama huyo ambaye  siku iliyofuata alirudi nyumbani.

KUWEPO MADANGURO
Majirani wa mtuhumiwa  walikataa kutoa ushirikiano kwa kuhofia wanazungumza na  polisi lakini Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Kata ya Makumbusho, Said Muhunzi,  alisema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo kwa danguro hilo.

“Nimebaini wapo wasichana wenye umri mdogo ambao wanaonekana na majirani wakiingizwa hapo kila mara na baadhi ya watu, majirani wamethibitisha hili,” alisema.

Aliongeza kuwa, Jumatano iliyopita kikundi chake cha ulinzi shirikishi, kilifika kwenye nyumba hiyo saa 7:00 usiku na  kumkuta mtuhumiwa Abia  na watu wengine wakiwa  nje na  kuwataka waingie ndani kwa kwani haukuwa  muda wa kukaa nje.

“Ijumaa iliyopita niliwaambia walinzi waende tena saa 8:00 usiku kuangalia kama watawakuta nje, waliona watu watano wakinywa pombe nje,” alisema na kuongeza:
Aliongeza kuwa watu hao ni Abia, Salome,  mtoto wa marehemu mumewe  na wanaume watatu na kuongeza kuwa kijana mmoja anayeitwa Juma alifahamika baada ya wenzake kumtaja kutokana na kuwatishia walinzi hao kwa bastola.

Muhunzi alisema Salome  anatumiwa na Abia kutafuta mabinti kwa ajili ya danguro hilo na kwamba kufuatia tukio hilo la walinzi kutishiwa walifungua kesi tatu katika kituo cha polisi Minazini alizozitaja kuwa ni  kukutwa nje wakinywa pombe  usiku,kutishia kuua na  kuzuia ulinzi usifanyike

Alisema walifungua jalada lenye kumbukumbua RB/118/2013 na kesi hiyo ilifikishwa kituo cha polisi Oysterbay na kukuabidhiwa kwa mpelelezi aliyemtaja kwa jina moja la Mwesiga
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo, alisema eneo lake moja ya changamoto zilizopo ni kuibuka kwa madanguro na baadhi ya wasichana wenye umri mdogo kujiuza kwenye baa nyakati za usiku.

Alitaja baadhi ya baa (majina tunayo ) kuwa zinaongoza kwa kuwa na wasichana wengi wanaojiuza na kwamba wanatoa elimu kupitia kamati ya Ukimwi na kufanya msako lakini tatizo ni kubwa.

Alitaja danguro maarufu liitwalo  ‘kwa wahaya’  lililopo Minazini na kusema kuwa  ofisi yake inawajua watuhumiwa kwa majina.

Habari zilizozifikia gazeti hili jana asubuhi, Sara alikuwa amewekwa mahabusu kituoni hapo.

Maandamano yatikisa, zaidi ya watu 90 wanaswa

Imewekwa Nassor Khamis

Askari wa kikosi maalum cha kupambana na uhalifu, wakiwasaka waumini wa dini ya kiislamu  kwa kutumia pikipiki katika mtaa wa Ohio na Samora, waliojipenyeza katikati ya jiji la Dar es Salaam, ili kwenda Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  kushinikiza kuachiwa kwa dhamana kwa Sheikh Issa  Ponda Issa anayekabiliwa  na makosa mbali mbali.
Askari wa kikosi maalum cha kupambana na uhalifu, wakiwasaka waumini wa dini ya kiislamu kwa kutumia pikipiki katika mtaa wa Ohio na Samora, waliojipenyeza katikati ya jiji la Dar es Salaam, ili kwenda Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kushinikiza kuachiwa kwa dhamana kwa Sheikh Issa Ponda Issa anayekabiliwa na makosa mbali mbali.

SHUGHULI katika Jiji la Dar es Salaam jana zilisimama kwa muda baada ya wafuasi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, kuandamana huku wakipambana na askari polisi waliotanda katika maeneo mengi ya mji.

Wafuasi hao waliotawanywa mara kwa mara na kwa mabomu ya machozi na askari polisi, walitumia stali mpya kuandamana hadi kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kufikisha ujumbe wao.

Vurugu hizo za polisi kupambana na waandamanaji hao zilianza mchana baada ya swala ya Ijumaa hadi saa 9:00 alasiri huku mitaa mingi katika jiji la Dar es Salaam ikiwa wazi kutokana na watu wengi kuondoka maeneo hayo.

Watu hao waliandamana kushinikiza Ponda ambaye yupo ndani akikabiliwa kesi ya wizi na uvunjifu wa amani aachiwe kwa dhamana.

Watu hao walitokea katika misikiti mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam baada ya swala ya Ijumaa ikiwemo, Kwamtoro, Magomeni na Buguruni kuelekea ofisi za DPP zilizopo barabara ya Ohio na Sokoine eneo la posta wakiwa katika vikundi vidogovidogo, tofuati na mandamano ambayo yamezoeleka kufanyika.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya  Dar es Salaam inawashikilia zaidi ya watu 90 ambao walishiriki kuhamasisha na kufanya maandamano.

Kaimu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mohamed Msangi alisema kati ya watu hao watawahoji ili kuwabaini wahusika wakuu na kufikishwa mahakamani.

“Kama inavyofahamika wazi kwenye  msafara wa mamba kenge hawakosekani sasa tutawahoji ili tuweze kuwapata wahusika wakuu na tuweze kuwachukulia hatua za kisheria kwani hao ni wavunjifu wa amani,”alisema.

Msangi alisema jeshi hilo lilipiga marufuku maandamano hayo lakini watu hao wamekaidi amri hiyo na kwamba sasa watachukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kulikuwa na vikundi vya watu katika maeneo ya Buguruni, Mnazi Mmoja na Kariakoo ambao walikuwa katika makundi huku wengine wakiandamana katika makundi

“Tumeweza kuchukua hatua kwa watu waliyokuwa wanataka kujaribu kuvunja amani kwa kufanya maandamano  kwani tumedhibiti hali hiyo na kuweza kuwakamata watu 80 ambao wapo katika kituo cha Polisi Kati  na Msimbazi,”alisema Msangi.

Alisema hali sasa ni shwali na kwamba vurugu ambazo zilitaka kujitokeza zimedhibitiowa.

SMZ itaendelea kuthamini jitihada za Cuba katika kuisaidia Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na  Uongozi wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Shirikisho la Ujerumani unaofanya ziara ya siku sita Nchini Tanzania Kuangalia miradi iliyofadhiliwa na Nchi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Shirikisho la Ujerumani unaofanya ziara ya siku sita Nchini Tanzania Kuangalia miradi iliyofadhiliwa na Nchi hiyo.

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuthamini jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Cuba katika kusaidia uimarishaji wa  huduma za afya hapa Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania Bwana  Jorge Luis Lopez Tormo hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Wananchi walio wengi hapa Zanzibar wamekuwa akielezea faraja yao kutokana na huduma mbali mbali wanazozipata kutoka kwa Wataalamu  na Madakari bingwa wa Cuba waliopo hapa Nchini.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi Lopez Tormo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwajengea mazingira bora ya makaazi  Wataalamu  na madaktari hao ili watekeleze vyema jukumu lao.

Balozi Seif alifahamisha kwamba ipo haja kwa uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu  wa Cuba  ukaendelezwa zaidi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Cuba kuangalia uwezekano wa  taasisi na makampuni yake ya  Kitalii nchini humo kutumia fursa iliyotolewa na Zanzibar katika uwekezaji vitega uchumi kwenye  Sekta ya Utalii.

Alisema Cuba imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika uwekezaji ndani ya sekta ya Utalii na kuipatia mapato makubwa, hivyo ni vyema kwa Nchi hiyo kuangalia jinsi inavyoweza kutanua wigo wake hadi Zanzibar.

Naye Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Cuba Nchini Tanzania Bwana  Jorge Luis Lopez Tormo  ameelezea kuridhika kwake  na huduma bora wanazopatiwa Wataalamu na Madaktari Bingwa wa Nchi yake wanaofanya Kazi hapa Zanzibar.

“ Nimepata fursa ya kutembelea makaazi ya Wataalamu na Madaktari Bingwa wa Nchi yangu na kuridhika na mazingira mazuri waliyowekewa na Serikali ambayo sina budi kuipongeza SMZ kwa hatua hii niliyoishuhudia”. Alifafanua Balozi huyo mpya wa Cuba Nchini Tanzania.

Balozi  Lopez Tormo ambae aliwahi kushika wadhifa huo Nchini Botswana alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano kati ya pande hizo mbili utaimarishwa na kuendelezwa zaidi.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alionana na Kamati ya Bajeti ya Bunge la Ujerumani ikiongozwa  na Mheshimiwa Claude Peter Willsch hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Ujumbe huo wa Viongozi kumi wa Kamati ya Bajet ya Ujerumani upo  Nchini Tanzania kwa ziara ya siku sita kuangalia miradi mbali mbali ya maendeleo, Kijamii na Uchumi iliyopo Nchini ambayo imefadhiliwa na Serikali ya Shirikisho la Ujerumani.

Katika mazungumzo yao Kiongozi wa Ujumbe  Huo Bwana Claude Peter Willsch alieleza kwamba Nchi  imejipanga kutumia Euro Milioni 4,000,000  kusaidia  miradi minane iliyojipangia kuitekeleza Nchini Tanzania katika  kipindi kijacho.

Bwana Claude aliutaja mradi uliotekelezwa  na Ujerumani hapa Zanzibar wa Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } uliopo Bububu ambao unaongezewa vifaa vya umeme unaotumia jua utakaosaidia hospitali hiyo kufanya kazi muda wote.

“ Tumeona ipo haja kwa Hospitali hiyo kuwa na umeme wa Solar utakaokidhi mahitaji ya operesheni wakati wote endepo umeme wa kawaida utazimwa au kuwa na hitilafu ya kiufundi”. Alifafanua Bw. Claude Peter.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo kwamba Hospitali ya Jeshi iliyopo Bububu imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananachi wa Zanzibar katika kujipatia huduma za Afya.

Alisema  mradi huo  mbali ya   kuiongezea nguvu Hospitaki kuu ya Mnazi Mmoja lakini pia unakwenda sambamba na ile azma ya Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwa na sehemu za huduma za afya kila baada ya kilo mita tano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishauri Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Ujumbe huo katika mipango yake ya baadaye kufikiria kuwa na mradi mwengine wa Kijamii Kisiwani Pemba.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Vitendo vya uchimbaji mchanga kiholela vya kithiri Kwarara

Eneo lililochimbwa mchanga karibu na nguzo kubwa ya umeme
Eneo lililochimbwa mchanga karibu na nguzo kubwa ya umeme

 

Na Nassor Khamis

Wakaazi wa shehia ya Kwarara wamelalamikia kukithiri kwa vitendo vya uchimbaji wa mchanga karibu na vianzio vya umeme katika shehia yao.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi hao wamesema uchimbaji huo umekithiri zaidi katika njia kuu zinazopitisha umeme unaotoka Fumba kuelekea Mtonokidatu.

Wamesema kuwa vitendo hivyo ni vya muda mrefu na hufanyika zaidi nyakati za usiku ambapo vijana wenye magari ya ng’ombe huvamia kuchimba mchanga na kuwauzia watu wanaojenga pamoja na wenye kuendesha biashara ya kuuza matofali.

“Hawa vijana hungojea usiku wa saa nne na tano ambapo watu wamelala na kuvamia katika maeneo haya na kuanza kuchimba mchanga” alisema mmoja wa wananchi hao.

Aidha wamefahamisha kuwa mashimo yanayochimbwa yamekuwa makubwa  jambo linalo hribu mazingira pamoja kuhatarisha usalama wa wakaazi wa maeneo hayo.

Nae msaidizi wa sheha wa shehia ya kwarara Bw, Haruna Haji Ame amesema katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo  wameamua kumwaga taka katika mashimo yaliyochimbwa ili kuzuia uchimbwaji wa mchanga usiendelee.

Aidha amefahamisha kuwa licha ya juhudi za kufukia mashimo hayo kwa kumwaga taka bado hawajafanikiwa kutokana na vijana hao kuanza kuchimba maeneo mengine pamoja kuto taka zilizowekwa katika mashimo hayo.

Pia amesema kuwa katika kipindi cha karibuni vijana wanne waliohusika na vitendo hivyo walikamatwa na wananchi kwa kushirikiana na jeshi la polisi na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Akizungumzia tatizo hilo mtendaji wa baraza la Manispaa la mji wa Zanzibar Bw, Khamis Mcha Mosi amesema baraza hilo limepitisha mpango wa kutupa taka katika mashimo yaliyochimbwa mchanga kwa lengo la kuyafukia ili kudhibiti uharibifu wa mazingira pamoja na kuzuia kuanguka nguzo za umeme.

Aidha amefahamisha kuwa wananchi wana jukumu la kulinda mazingira yanayo wazunguka kwa kuzuia vitendo kama hivyo kwani waathirika wakubwa wa vitendo hivyo ni wananchi wenyewe.

Pia amewata wale wanao fanya vitindo hivyo kuacha ili kuweza kulinda mazingira pamoja na kuepusha maafa yanayoweza kutokea kutokana na vitendo hivyo.

Dkt, Shein azindua ugawaji wa vitambulisho vya taifa awamu ya kwanza Zanzibar

Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mh, Pereira Ame Silima akimkabidhi kitambulisho cha tifa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Ali Mohammed Shein katika sherehe za ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa awamu ya kwanza Zanzibar katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi.
Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mh, Pereira Ame Silima akimkabidhi kitambulisho cha tifa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Ali Mohammed Shein katika sherehe za ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa awamu ya kwanza Zanzibar katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi

Na Nassor Khamis

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi Dkt, Ali Mohammed Shein amewtaka Wazanzibari kujisajili katika vitambulisho vya Taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza katika sherehe za ugawaji wa vitambulisho vya Taifa awamu ya kwanza kwa upande wa Zanzibar katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi Dkt, Shein amesema vitambulisho hivyo vina faida kubwa kwa Taifa ikiwemo ulinzi na usalama wa wananchi.

Amesema kuwa pia vitambuliosho hivyo vitasaidia kutanua wigo wa serikali katika ukusanyaji wa kodi za mapato kwa wananchi pamoja na mashirika mengine.

Aidha amefahamisha kuwa kumekuwa na ongezeko la wahamiaji haramu nchini hivyo kupitia vitambulisho hivyo kutaisadia serikali kuatambua raia wake pamoja kudhibiti uingiaji wa wageni kiholela.

“kumekuwa na ongezeko la watu hapa nchini ambao wengine ni wageni hivyo vitambulisho hivi vitaiwezesha serikali kujua raia wake kutokana na alama za vitambulisho hivyo” alisema Dkt, Shein.

“Vitambulisho hivi ni tofauti baina ya wanavyo pewa raia na ambao si raia hivyo kwa njia hii itakuwa ni rahisi kutambulika” ailongeza Dkt, Shein.

Dkt, Shein amewataka wananchi kutosikiliza maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya watu juu ya lengo la vitambulisho hivyo na kuwataka kuyapuuza kwani hayana nia njema na taifa.

“Wananchi nakunasihini musisikilize maneeno yoyote ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya watu juu ya vitambulisho hivi kwani hao hwatitakii mema nchi hii” aliasa Dkt, Shein.

Hata hivyo amefahamisha kuwa Zanzibar ina uzoefu mkubwa katika kutambua umuhimu wa vitambulisho kutokana kuwepo kwa kitambulisho cha mzanzibzri mkaazi ambacho kitaendelea kuwepo na kutumika kama ilivyokusudiwa.

Pia amewataka vingozi wa kisiasa na taasisi mbalimbali za kini na kiraia kusaidia kutoa taaluma kwa kwa wananchi juu ya umuhimu wa vitambulisho hivyo kwa taifa.

Aidha amewataka watendaji wa mamlaka ya usajili wa vitambulisho vya taifa (NIDA) kushirikiana na taasisi nyengine wakiwemo viongozi wa shehia ili kuahakikisha taarifa zinazotolewa zinakuwa sahihi ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo kw wananchi.

Pia amewataka watendaji hao kutunza taarifa zinazotolewa na kutumiwa na wale wenye mamlaka ya kuzitumia taarifa hizo ili kuepuka usumbufu kwa wananchi.

Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya usajili wa vitambulisho vya taifa Bw, Dikson Maimu amesema usajili wa vitambulisho hivyo unakabiliwa na baadhi ya matatizo yakiwemo kukusekana kwa vielelezo muhimu katika kuchukua taarifa za wananchi wakati wa usajili pamoja na baadhi ya wageni kutaka kusajiliwa kama wageni jambo linalorudisha nyuma zoezi hilo.

Katika sherehe hizo viongozi mbalimbali wa serikali na na mashirika ya umma pamoja na wananchi wa kawaida walikabidhiwa vitambulisho vyao.

Miongoni mwa waliokabidhiwa vitambulisho hivyo ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt, Ali Mohammed Shein, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Mwinyihaji Makame, Mufti mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi pamoja na viongozi wengine na wananchi.

Balozi Seif ataka mifuko ya Pencheni kuwekeza kwenye kilimo

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa tatu wa wadu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } katika Hoteli ya Maount Meru Mjini Arusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa tatu wa wadu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } katika Hoteli ya Maount Meru Mjini Arusha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Mifuko ya Pencheni Nchini kuwekeza katika sekta ya Kilimo pamoja na Viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa kwa lengo la kuongeza ajira hasa kwa vijana ili kuondosha ukali wa maisha na kupunguza umaskini.

 Wito huo ameutoa wakati akiufungua  Mkutano wa Tatu wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa  Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } unaofanyika katika  Ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru Mjini Arusha.

Balozi Seif alisema haifurahishi kwa Taifa hili kubarikiwa kuwa na rasilmali nyingi lakini matokeo yake malighafi ya mazao mengi yanayotokana na rasilmali hizo  husafirishwa nje ya Nchi hali ambayo inasababisha Serikali kupata mapato madogo.

Alisema pamoja na kazi nzuri ya uwekezaji katika kilimo inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania lakini bado Mifuko mengine ya Pencheni ina wajibu wa kufanya jitihada za kuzuia usafirishaji huo na badala yake wanayasarifu hapa nchini ili mbali ya kuongeza thamani lakini pia kutoa ajira kwa wananchi walio wengi.

“ Ikiwa  Nchi ya India imeweza  kupiga marufuku kusafirisha mali ghafi kama pamba ipo haja na sisi Tanzania kufanya jitihada za makusudi kabisa ya kuzuia kusafirisha mazao yetu kwa namna hiyo” Alisisitiza Balozo Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na mikakati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } ya kuwekeza kwenye Viwanda  vya kuongeza thamani ya mazao ambao utatoa fursa zaidi kwa wakulima  kupata soko la uhakika wa mazao yao.

Balozi Seif alitoa mfano wa  uwekezaji huu wa NSSF ambao umetoa fursa nzuri kwa wakulima wadogo wadogo wa  miwa Mkoani kagera kuvuna Tani 40,000 za miwa ambazo zina thamani ya shilingi Bilioni 1.6 hali iliyoimarisha kipato cha jamii iliyo karibu na Kiwanda cha Sukari Mkoani huo.

  Uzuri wa Serikali kuwa na Mashirika makubwa na yenye fedha kama NSSF Ndio huu kwani shirika hili kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani limeweza kujenga Vyuo vikuu pamoja na miradi mengine bila ya mikopo ya Kimataifa”. Alifafanua Balozi Seif.

Akizungumzia umuhimu wa utafiti na elimu ya kuongeza idadi ya wanachama Balozi Seif  alisema ipo haja kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufanya utafiti katika sekta isiyo rasmi ambayo mchango wake katika Uchumi wa Taifa ni mkubwa.

Alisema sheria ya marekebisho ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii nambari 5 ya mwaka 2012 bado hayajasaidia kupanua wigo wa wanachama bali kinachoonekana hivi sasa ni kwa Mifuko hiyo ikishindana kwa kubadilishana wanachama wale wale.

Alieleza kwamba ni vyema kwa Mifuko hiyo ikaweka mikakati ya makusudi ya kuongeza wanachama kupitia mabadiliko ya sheria hiyo ili kuruhusu wanachama wapya wanaojiunga na mifuko kuchagua wenyewe ule mfuko wenye mazingira mazuri ya kuvutia wanachama.

Akimkaribisha mgeni rasmi Balozi Seif Waziri wa Kazi na Ajira wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Gaudensia Kabaka alisema Tanzania imefikia vigezo saba kati ya Tisa vilivyoainishwa na Shirika La Kazi Duniani { ILO } Katika  Mkataba nambari 102 kuhusu mafao ya Jamii.

Waziri Gaudensia alivitaja baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni pamoja na Uzee, Kifo, Ugonjwa, Ukosefu wa Ajira na Uzazi ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ile ya Pencheni.

Hata hivyo Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Gaudensia Kabaka alieleza kwamba bado kipo kilio kikubwa kwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ile ya pencheni ambacho ni ufinyu wa kukidhi mahitaji ya mafao.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania Dr. Ramadhan Dau alisema bado zipo baadhi ya changamoto zinazozorotesha utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo.

Dr. Ramadhan Dau aliitaja moja ya changamoto hiyo kuwa ni ucheleweshaji wa ukusanyaji wa michango ya wanachama  ambapo mpango maalum uko tayari kutumika wa makusanyo ya michango hiyo kwa kutumia njia ya M. Pesa.

Ujumbe wa mwaka huu wa Mkutano huo wa Tatu wa Wadau wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } Hifadhi ya Jamii Tanzania iko njia panda.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar