BALOZI SEIF AZINDUA JENGO JIPYA LA KISASA LA SKULI YA MSINGI MIWANI

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idakizindua rasmi jengo jipya la kisasa la Skuli ya Msingi ya Miwani iliopo katika Jimbo la Uzini Wilaya ya Kusini Unguja.
Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idakizindua rasmi jengo jipya la kisasa la Skuli ya Msingi ya Miwani iliopo katika Jimbo la Uzini Wilaya ya Kusini Unguja.

Na Othman Khamis Ame – OMPR,

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema  wakati umefika kwa Wananchi kuwa na hadhari katika kuangalia Mtu mwenye muelekeo wa kuwafaa katika kuwasimamia kusukuma mbele maendeleo yao wanayoyahitaji kwenye maeneo yao.

Kauli hiyo aliitowa wakati akizindua rasmi jengo jipya na la kisasa la Skuli ya Msingi  ya Miwani ndani ya Jimbo la Uzini lililojengwa ndani ya kipindi cha miezi miwili na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mohd Raza Hassan.

Balozi Seif alisema ile tabia ya baadhi ya wananchi kukumbatia watu wanaoendeleza ubinafsi inafaa kupigwa vita kwa hali yoyote ile kwa vile inachangia kuzorotesha kasi ya Maendeleo ya Wananachi.

Aliwahimiza Viongozi, washirika na wahisani zikiwemo Taasisi za Kijamii na zile za maendeleo zilizomo katika Halmashauri za Wilaya kujikita zaidi katika kuunga mkono juhudi za Wananachi kwenye sekta za Mendeleo na Kiuchumi wakiangalia zaidi ile sekta muhimu ya Elimu.

“ Siku zote tunasema tuwekeze kwenye elimu ambayo watoto wetu itawasaidia wao wenyewe kwa kupata muelekeo na mafanikio ya maisha yao sambamba na kusaidia familia zinazowazunguuka “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza kwa hatua yake aliyochukuwa ya ujenzi wa Jengo hilo la madarasa mawili lililokamilika huduma zote ikiwemo vikalio ambalo limesaidia kuiepusha Skuli ya Miwani kuchukuwa wanafunzi katika mikondo miwili.

Balozi Seif alisema juhudi za Mwakilishi huyo ni miongoni mwa utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ya CCM pamoja na kukamilisha ahadi alizotowa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza Jimbo hilo.

Aliwakumbusha Viongozi wengine wa Jimbo, Wilaya na hata mkoa kuunga mkono jitihada za Wananachi wa Miwani katika kukamilisha jengo jengine la Madarasa  Sita la Skuli hiyo ambalo linahitaji nguvu za ziada za Viongozi hao likiwa limekwama kwa  miaka minne sasa.

Alisema katika kuunga mkono juhudi hizo za Wananchi ambapo zinahitajika kiasi cha shilingi Milioni Tisa { 9,000,000/- } kukamilisha hatua ya linta ili likabidhiwe  Wizara ya Elimu  na Mafunzo ya Amali kwa Ukamilishaji aliahidi kuchangia Shilingi Milioni Mbili { 2,000,000/- }.

“ Sisi viongozi kuanzia Wawakilishi wa kuteuliwa, Mbunge, Madiwani na hata halmashauri za Wilaya tunalazimika kuunga mkono juhudi hizi ili kutowavunja moyo wananchi tunaowaongoza katika Majimbo yetu “. Alikumbusha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akitoa salamu za Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } iliyosaidia Vikalio vyote vya jengo hilo Meza 100 na Viti 100 vyenye thamani ya shilingi Milioni 16,000,000/-  Msaidizi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki  hiyo  Ame Haji Makame amesema benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Wananchi popote pale.

Nd. Ame alisema benki ya Watu wa Zanzibar inajali maendeleo ya Jamii na wakati mwengine kushawishika kusaidia miradi yao tofauti ikiwemo zaidi sekta ya elimu ambayo ndio mkombozi wa Taifa lolote.

Naye kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bibi Mwanaidi Saleh amempongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Raza kwa juhudi zake za kusaidia nguvu za Wizara hiyo katika ukamilishaji wa majengo  ya Skuli.

Bibi Mwanaidi alisema juhudi za Mwakilishi huyo za kukamilisha majengo mawili ya Skuli ndani ya Jimbo hilo limeipunguzia mzigo mkubwa Wizara ya Elimu wa kukamilisha majengo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na wizara hiyo.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu amewakumbusha Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini kuhakikisha kwamba majengo ya skuli wanayoyaanzisha yanatengewa vyumba maalum kwa ajili ya vitengo vya Kompyuta.

Alisema Wizara imeanzisha mfumo maalum wa mafunzo ya kompyuta kuanzia elimu ya msingi kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa Zanzibar kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia yaliyopo Duniani.

Akitoa shukrani zake katika hafla hiyo ya uzinduzi wa jengo jipya la Skuli ya Miwani iliyomo ndani ya Jimbo la Uzini Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mohd Raza Hassan alisema kwamba uwepo wa Viongozi katika Jamii upo kwa ajili ya kusimamia matakwa ya Wananchi.

Mh. Raza alisema tabia ya baadhi ya Viongozi kuigonganisha vichwa jamii ni kutowafanyia haki Wananachi wanaowaongoza na hatimae inaviza maendeleo yao na kuwaongezea chuki na fitna baina yao.

Mapema katika Risala yao iliyosomwa na Mwalimu  wa Skuli ya Msingi ya Miwani Juma Abdulla wananchi hao wa Kijiji cha Miwani walisema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ndani ya Kijiji hicho.

Mwalimu Juma alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa bara bara, mashine za uchapaji , ukosefu wa Daktari katika kituo chao cha Afya pamoja na umaliziaji wa jengo lao la madarasa sita ambalo linaweza kusaidia muendelezo wa mkondo mmoja tu skulini hapo.

Jengo jipya  la  madarasa mawili la Skuli ya Msingi ya Miwani litakalokuwa na uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 122 ambapo wanafunzi  56 kwa kila chumba  lilijengwa ndani ya kipindi cha miezi miwili kwa gharama za shilingi Milioni 30,000,000/- .

Katika hafla hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Uzini pia alikabidhi Mchango wa Shilingi Milioni Mbili kwa ajili ya Kusaidia maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi Mtukufu ya Zanzibar hapo mwaka 2014.

Fedha hizo zitasaidia katika Ofisi ya Mkoa Kusini Unguja, Wilaya ya Kati, Jimbo la Uzini Kichama pamoja na kukabidhi pia mipira kwa ajili ya Timu za Skuli 12 zilizomo ndani ya Jimbo la Uzini.

SHEHA WA TOMONDO APELEKWA INDIA KWA MATIBABU ZAIDI

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuaga Sheha wa Shehia ya Tomondo Mohd Omar Said { Kidevu }  anayekwenda Nchini  India kwa Uchunguzi na Matibabu zaidi baada ya kumwagiwa Tindi kali usiku wa Tarehe 22 Mei 2013. Sheha Kidevu alikuwa akipatiwa  huduma ya matibabu katika Hospitali Kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja kwa takriban Mwezi mmoja baada ya tukio hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuaga Sheha wa Shehia ya Tomondo Mohd Omar Said { Kidevu } anayekwenda Nchini India kwa Uchunguzi na Matibabu zaidi baada ya kumwagiwa Tindi kali usiku wa Tarehe 22 Mei 2013. Sheha Kidevu alikuwa akipatiwa huduma ya matibabu katika Hospitali Kuu ya Rufaa Mnazi Mmoja kwa takriban Mwezi mmoja baada ya tukio hilo.

Na Othman KhamisAme – OMPR

Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu } ameondoka Zanzibar kuelekea Nchini India kwa ajili ya Uchunguz na matibabu zaidi baada ya kumwagiwa Tindi kali { Acid }  na mtu asiyejuilikana Usiku wa tarehe 22 Mei Mwaka huu wa 2013.

Sheha Mohd Kidevu alikuwa akipatiwa huduma zamatibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kwa takriban Mwezi Mmoja sasa kutokana na kuathirika sehemu ya kulia ya kifua chake, Bega pamoja na baadhi ya maeneo ya mapaja.

Mgonjwa huyo ameondoka na Ndege ya shirika la ndege la Oman kwa kupitia Muscut na amewasili Mjini Chenai Nchini India mapema leo tarehe 21/6/2013 saa 12.30 za asubuhi akiambatana na Daktari wake.

Akimuaga sheha huyo hapo katika wadi yake ya Mapinduzi Kongwe Mnazi Mmoja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi alimuombea sheha Mohd Kidevu  safari ya mafanikio itakayomletea hafaja njema.

Bwana Mohd Kidevu alisema Mtu huyo alianza kutimua mbio baada ya kufanikiwa kufanya dhambi hiyo kitendo ambacho akalazimika kuomba msaada kwa wasamaria wema lakini hatimae ilishindikana kutokana na kuzidiwa kwa maumivu makali yenye kuchoma kama moto.

Sheha huyo wa Shehia yaTomondo aliendelea kumfahamisha Balozi Seif kwamba hali yake hivi sasa inaendelea vyema na ameshaanza kupatamatumainikufuatiajicho lake kuanzakuonaingawabadoanakabiliwanamaumivukatikasehemuyakeyausoni.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimuomba Sheha huyo wa Tomondo kuwa na moyo wa subra wakati wa kipindi hichi kigumu cha huduma za matibabu.

Balozi Seif alimuhakikishia  Bwana Mohd Kidevu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufuatilia matibabu ya afya yake hadi atakapopata nafuu na kurejea nyumbani kuendelea na harakati zake za kimaisha kama kawaida.

Naye sheha wa shehia ya Tomondo Mohd Omar Said { Kidevu } aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada zake zilizosaidia kufanikisha kwa safari yake ambayo imempa faraja kubwa.

Sheha Kidevu alisema maumivu yaliyokuwa yakimkabili ndani ya wiki hii hasa wakati wa kula imepunguwa kidogo kufuatia huduma za karibu alizokuwa akipatiwa na madaktari wanaomuhudumia.

Akizungumza na vyombo vya Habari nje ya Wodi ya Mapinduzi Kongwe hivi karibuni wakati alipomkagua sheha huyo kwa mara ya kwanza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali  Iddi alisema Serikali Kuu imesikitishwa na vitendo hivyo viovu vinavyoleta athari kwa Binaadamu.

Balozi Seif alisema tabia hiyo mbaya inayoonekana kuanza kuchipua hapa Nchini ikibeba ufinyu wa imani inaanza kuleta hofu miongoni mwa wananchi katika kuendelea na harakati zao za kimaisha za kila siku.

Alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea na uchunguzi wa kufuatilia matukio hayo na kamwe haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuwafikisha katika mkondo wa sheria wale wote watakaobainika kuhusika katika vitendo hivyo.

Hili ni tukio la tatu kuwahi kutokea la kumwagiwa watu tindili kali ndan ya mkoa wa mjini Magharibi likiwahusisha aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma pamoja na Katibu wa Fufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.

SMZ YAIPONGEZA BADEA KWA KUSAIDIA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII ZANZIBAR

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpatia zawadi ya mlango Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (BADEA) Mhandisi Youser Ibrahi Albassam kama ishara ya Benki hiyo kukaribishwa rasmi Zanzibar. Zawadi hiyo alimpatia katika hafla fupi ya uzinduzi waujenzi wa  Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kampasi ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpatia zawadi ya mlango Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (BADEA) Mhandisi Youser Ibrahi Albassam kama ishara ya Benki hiyo kukaribishwa rasmi Zanzibar. Zawadi hiyo alimpatia katika hafla fupi ya uzinduzi waujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kampasi ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Na Othman KhamisAme -OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeupongeza Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } kwa hatua zake kubwa ilizoonyesha katika kusaidia maendeleo ya Kiuchumi na kijamii hapa Zanzibar.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili  wa Rais wa Zanzibar Balozi  Seif  Ali Iddi katika hafla fupi  ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } awamu ya kwanza uliopata ufadhili mkubwa kutoka kwa Benki hiyo ya Badea hapo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Baloz Seif ambae alimuwakilisha Rais wa Zanzibar kwenye uzinduzi huo alisema Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } imekuwa mshirika mkubwa wamaendeleo wa  Zanzibar  hasa katika sekta ya Elimu hatua ambayo inaijengea mazingira ya mfumo mzuri wa miundo mbinu ya Kielimu hapa Zanzibar.

Alisema sekta ya Elimu ni moja kati ya mambo yaliyopewa msukumo mkubwa ndani ya dira ya maendeleo ya Zanzibar ya 2020 katika muelekeo wa kuwajengea uwezo wa Kielimu vijana wanapomaliza masomo yao wakubalike kuingia moja kwa moja katika soko la ajira.

“ Chuo chetu Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } tunakusudia kukijengea uwezo mkubwa zaidi utakaowapa fursa pana wanafunzi wetu kuingia katika soko la ajira sio Tanzania na Afrika  Mashariki bali popote pale Duniani “. Alifafanua BaloziSeif.

Balozi Seif alisisitiza kwamba licha ya ongezeko kubwa la idadi ya watu liliopo hivi sasa Nchini lakini bado Serikali imejikita kuongeza Skuli zaidi nyengine za Sekondari Unguja na Pemba kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili kuwajengea mazingira bora wanafunzi yatakayowawezesha kupata fursa ya uhakika ya kujiunga na vyuo vya Elimu ya juu.

Akitoa salamu za Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Mhandisi Youser Ibrahim Albassam alisema ujenzI wa vyuo Vikuu ni moja ya hatua nzuri kwa Taifa lolote katika kuelekea kwenye maendeleo ya uhakika.

Mhandisi Albassam ambe pia ni Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia alisema Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo za  Zanzibar.

Alisema kupitia Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Hiyo Mhandisi Albassam alieleza kwamba Uongozi wa Benki hiyo umeahidi kusaidia tena Dola za Kimarekani Milioni kumi  { U$ Dolla 10,000,000 } kwa ajili ya kuendeleza awamu ya pili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA } katika Kampasi yaTunguu.

“ Tumefarajika na ukarimu wa watu wa Zanzibar na mazingira yake mazuri yaliyopelekea kuushawishi Uongozi wa Benki yetu ya Badea kusaidia Sekta ya Elimu, Bara bara na Nyanja nyengine za maendeleo “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Badea Mhandisi Albassam.

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUSA } Profesa Idriss Rai alisema ujenzi huo umeongeza program nyengine na kufikia nane kutoka Nne kutokana na mabadiliko ya mahitaji Kiuchumi sambamba na Kijamii hapa Nchini.

Profesa Rai alizitaja baadhi ya program hizo kuwa ni pamoja na masomo ya Sayansi ya mazingira ,Biashara, Utalii na Kilimo pamoja na kuanzishwa kwa vituo viwili vya utafiti vya mazingira na Kiswahili.

Makamu Mkuu huyo wa Suza alifahamisha kwamba muelekeo wabadae wa chuo hicho kikuu cha Taifa cha Zanzibar ni kukiwezesha kuhudumia wanafunzi kutoka kanda ya Afrika Mashariki na maeneo mengine ya mbali.

Alieleza kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia Zanzibar kubarikiwa kuwa na bahati ya kupokea wanafunzi wengi kutoka sehemu mbali mbali nje ya Tanzania kwa ajili ya kujakujifunza hasa masuala ya lugha.

“ Tutalazimika kujikita pia katika kuwajengea mazingira bora ya makazi wanafunzi wetu hasa  wale wa kigeni na hili linahitaji pia kuungwa mkono na wadau wetu wa elimu “. Alieleza Profesa Rai.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alisema msaada wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha awamu ya kwanza ya mradi huo.

Katika ujenzi huo wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } awamu ya kwanza Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { Badea } imechangia Dolla za Kimarekani Milioni 5.6  wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa Shilingi za Kitanzania Bilioni 5.5.

Wakati huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini  Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo unaoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Mhandisi Youser  Ibrahim Albassam kwamba Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar itahakikisha awamu ya pili ya Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Suza unaanza mara moja.

Alisema uungaji mkono wa Uongozi wa Benki hiyo kwenye ahadi iliyotolewa katika uzinduzi wa kwanza umekuwa chachu ya maandalizi ya awamu inayofuatia .

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Mhandisi Youser Ibrahim Albassam alisema Badea daima itaendelea kusaidia Mataifa machanga katika kujinasua kiuchumi ikilenga zaidi Mataifa ya Bara la Afrika.

 

SMZ: Kuna njama za kugombanisha waumini Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi Mh, Omar Yussuf Mzee.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi Mh, Omar Yussuf Mzee.

Matukio ya kupigwa risasi na kumwagiwa tindikali viongozi wa dini na serikali Zanzibar yalilenga kuleta fitina na kugombanisha waumini wa madhehebu ya dini Visiwani Zanzibar, imefahamika jana.

 

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi Omar Yussuf Mzee, Wakati akiwasirisha makadirio na matumizi ya bajeti ya serikali katika mwaka wa Fedha wa 2013/20 14.

 

Waziri Mzee, alisema vitendo vya hujuma dhidi ya viongozi wa dini na serikali vinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu na kuwataka waumini na wananchi kuendelea kuwa na moyo wa subira na kulinda amani na Umoja wa kitaifa kwa manufaa ya Zanzibar.

 

Waziri Mzee alisema bila ya busara na hekima za viongozi wa dini na wananchi Zanzibar ingeweza kuingia katika machafuko makubwa na kuathiri kuathiri usitawi wa maendeleo ya wananchi wake.

 

Viongozi waliohujumiwa kwa kumwagiwa tindikali ni Katibu wa Mufti Sheikh Fadhili Soraga na sheha wa Tomondo Mohamed Kidevu,  wakati Padiri Ambrose Mkenda alipigwa risasi na mwezake Padri Evaristus Mushi, alipoteza maisha baada ya kupigwa risasi Febuari 17 mwaka huu wakati akienda kuongoza misa ya Jumapili huko Kibweni mjini Zanzibar.

 

“Mheshimiwa Spika serikali bado inaendelea na jitihada za kuwapeleka wahusika katika mikono ya sheria, tuendelee kunasihiana katika kudumisha utulivu tuliouonesha wakati wachache wetu walipotutia majaribuni,” Alisema Waziri Mzee.

 

Alisema mwenyezi Mungu atawalipa wote waliotenda uovu na dhuluma dhidi ya viongozi wa dini na kusisitiza nchi yoyote duniani haiwezi kufanikiwa kimaendeleo bila ya kuwepo kwa misingi ya amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.

 

Kuhusu mabadiliko ya katiba mpya alisema kwamna ni jambo la faraja kuona mchakato huo unaendelea kufanyika katika mazingira ya amani na utulivu kwa wananc hi wa Tanzania bara na Zanzibar.

 

Aidha alisema kwamba jambo la muhimu ni kuhakikisha mageuzi ya katiba mpya ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hayafarakanishi wananchi wake wa pande mbili za muungano huo.

 

Kuhusu bajeti, waziri Mzee aliserma SMZ  imepanga kutumia asilimia 37 ya bajeti kuu kufanikisha vipaumbele vine ikiwemo kuimarisha kiwango cha ubora wa elimu, afya, hasa upatikanaji wa dawa muhimu za binadamu, huduma za maji safi pamnoja na kufanikisha mpango kazi wa ajira kwa vijana ambapo  serikali imepanga kutumia shilingi Bilioni 113 .2 kufanikisha vipaumbele hivyo.

 

Tangu baadhi ya wanasiasa na wana harakati kuanza kampeni za kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kumekuwepo na matukio mengi ya hujuma dhidi ya viongozi wa dini kupigwa risasi na kumwagiwa tindikali Visiwani Zanzibar.

 

CHANZO: NIPASHE

 

CHANGIENI DAMU ILI KUOKOA MAISHA WATU – BALOZI SEIF

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu duniani zilizofanyika kitaifa  katika kituo cha huduma za Damu salama Sebleni Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wachangiaji damu duniani zilizofanyika kitaifa katika kituo cha huduma za Damu salama Sebleni Mjini Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Wananchi kujiunga na jumuiya ya wachangiaji Damu Nchini ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kupatiwa huduma za Damu.

Wito huo ameutoa katika maadhimisho ya siku ya wachangia damu Duniani zilizofanyika katika Kituo cha Huduma za Damu salama kiliopo pembezoni mwa nyumba za Wazee Sebleni Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema kuwepo kwa utaratibu wa kukusanya damu kutoka kwa wachangiaji wa hiari chini ya Mpango wa damu salama kutasaidia kupunguza vifo ambao unakubaliana na dira ya maendeleo ya Milenia ambapo lengo moja wapo ni kupunguza vifo vya akina mama  na watoto.

Aliiomba jumuiya ya wachangia damu iendelee kuwa ya kudumu na ili kufikia lengo hilo wanachama wake hawana budi kubuni mikakati ya kuingiza wanachama wengi zaidi mjini na vijijini.

“ Nyinyi ndio benki ya damu na bila ya nyinyi benki hiyo itabakia kuwa ni jiengo lenye wafanyakazi pamoja na mitambo yake, lakini isingekuwa na damu “. Alifafanua Balozi  Seif.

Alieleza kwamba damu ni uhai kwa kiumbe yoyote yule, hivyo kujitolea kwao wachangiaji damu hao kwa hiari kumeonyesha upendo walionao kwa Wananchi wenzao wenye kuhitaji damu hizo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wachangiaji damu wote kwa moyo wao wa huruma na upendo wanaoendelea kuuonyesha ambao umepelekea kuwepo kwa ukusanyaji mkubwa wa damu Unguja na Pemba  unaotia moyo.

Aliwashauri wafanyabiashara na Taasisi tofauti Nchini kuisaidia Serikali kwa kuziunga mkono huduma za uchangiaji Damu kwa hiari ili kuzifanya huduma hizo zidumu zaidi pamoja na kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya Nchi.

Balozi Seif pia aliwapongeza wapiganaji wa vikosi vya Ulinzi vya Serikali ya Muungano wa Tanzania, vile vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wanafunzi wa Skuli za Sekondari Nchini  kwa mashirikiano yao mazuri wanayo toa kwa Kituo cha Damu salama katika kuhakikisha damu ya kutosha inapatikana wakati wote.

Katika risala yao wana jumuiya ya uchangiaji damu salama { JUWADAHIZ } iliyosomwa na Katibu wao Hamad Bakari Magarawa  wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Afya kwa juhudi zake za kusaidia jumuiya hiyo.

Hamad Magarawa alisema jumuiya hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Damu imekuwa ikiendelea kuishajiisha jamii kujenga  tabia ya kukubali kuchangia huduma za damu salama.

Alisema ushajiishaji huo umesaidia kuibua wimbi kubwa la wachangiaji damu na kufikia mia 850 wakiwa jinsia tofauti Unguja na Pemba kupitia vilabu tofauti hapa Nchini.

Hata hivyo Hamad Magarawa alieleza kwamba jumuiya hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazochangia kuzorotesha Utekelezaji  wa majukumu ya jumuiya hiyo.

Alizitaja baadhi ya changa moto hizo kuwa ni pamoja na ufinyu wa ufadhili kwa jumuiya hiyo pamoja na baadhi ya watendaji wa sekta ya afya kutokuwa waaminifu kutokana na tabia yao mbovu ya kuuza damu kwa kushirikiana na baadhi ya wachangiaji damu.

Mapema Meneja  Mkuu wa Mpango wa Damu salama Zanzibar Dr. Mwanakheir Ahmed Mahmoud alisema kuzuka kwa maradhi ya ukimwi nchini katika miaka ya tisini  kulichangia upungufu wa uchangiaji damu ambao ulikuwa ukifanywa na familia za wagonjwa.

Dr. Mwanakheir alisema watu wengi walikuwa wakikwepa kuchangia damu kwa kuhofia kudhaniwa kuwa na virusi vya ukimwi na kusababisha usumbufu wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Meneja Mkuu huyo wa Mpango wa Damu salama alieleza kwamba takwimu zinaonyesha  kuwa vifo vingi vilivyokuwa vikiwapata watoto na akina mama vinatokana na upungufu wa damu.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya siku ya wachangia damu Duniani  Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji aliihakikishia jamii kwamba Wizara hiyo haitovumilia kumchukulia hatua za kinidhamu mtendaji  wake ye yote atakayebainika kuwa na tabia ya kuuza damu.

Wachangiaji damu salama wapatao 850 Unguja na Pemba wamejitokeza  kujiunga na vilabu mbali mbali vya uchangiaji damu kupitia Vikosi vya ulinzi vya SMT na SMZ, Wanafunzi wa skuli za Sekondari pamoja na vikundi vya kiraia.

Baadhi ya wachangiaji damu katika kiwango kikubwa wamepatiwa zawadi maalum katika maadhimisho hayo ambapo Ujumbe wa mwaka huu wa siku ya wachagiaji damu Duniani ifikapo tarehe 14 mwezi Juni ya kila mwaka unaeleza “ Uchangiaji Damu ni zawadi ya Maisha”.

WATU WATATU WAFARIKI KWA KUANGUKIWA NA UKUTA WA TENKI LA MAJI PEMBA

mewekwa na Nassor Khamis

ASKARI wa vikosi vya Ulinzi na Usalama kisiwani Pemba, wakiwa katika zoezi la kuokoa miili ya Marehemu waliopoteza maisha katika ajali ya kuangukiwa na Ukuta wa tangi la Maji Machomanne Chake Chake Pemba leo
ASKARI wa vikosi vya Ulinzi na Usalama kisiwani Pemba, wakiwa katika zoezi la kuokoa miili ya Marehemu waliopoteza maisha katika ajali ya kuangukiwa na Ukuta wa tangi la Maji Machomanne Chake Chake Pemba leo

JUMLA ya watu watatu wamefariki ndunia papo hapo na watatu kujeruhiwa baada yakuangukiwa na ukuta mnara wa tangi la maji uliopo machomanne chake chake pemba, majira ya saa tatu za asubuhi ya leo.Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Suleiman Hassan Suleima, amesema kuwa, merehemu hao walifikiwa na mauti wakiwa katika kazi ya kuteremsha ukuta wa mnara wa tangi la maji ambao walikuwa wameshaukata.

Kamanda Suleimana alisema kuwa, ukuta huo ulikuwa tayari umeshafanya ufa wa kupasuka, hivyo wakati wakiwa kazini kuuteremsha ukuta huo, ulianguka na kuwaelemea marehemu hao pamoja na mejeruhi waliokuwa juu wakiuteremsha ukuta huo.

Kamanda alisema kuwa idadi ya mafundi waliokuwepo kazini hapo, walikuwa ni watu 12 ambapo watatu wamepoteza maisha papo hapo na watatu kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya chake chake na wengine sita walikimbia na jeshi la polisi liko katika utaratibu wa kuwatafuta kwa ajili ya kuelewa hali zao.

Aliwataja marehemu hao kuwa, ni Juma Rashid Juma (35)mkaazi wa chanjaani, Suleiman Mohammed Abdiadi “maarufu golo” (55) mkaazi wa kwale na Salum Muhidini Vuai “Bandudu” (35) mkaazi Madungu wote ni wakaazi wa wiliya ya chake chake mkoa wa kusini Pemba.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Jakson John (26) mzaliwa wa Iringa mkaazi wa msingini, Ali Saleh Ali (35) mkaazi wa michakaeni na Yohana Richerd (25) mkaazi wa machomanne Chake Chake Pemba.

“baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi tulifika katika eneo la tukio na tukashirikiana kikamilifu na wenzetu wa vikosi vya ulinzi na usalama wote wa pemba katika kuokoa maisha ya wananchi wetu waliokuwepo hapo”alisema kaimu kamanda Suleiman.

Aidha aliwataka wananchi kutoa mashirikiano pale panapotokea majanga kama hayo, ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, DK Hilali Juma Mohammed, wa Hospitali ya Chake Chake, amesema kuwa kati ya marehemu hao watatu, wawili waliumia kichwa, Kifua na Mikono.

Alisema kuwa merehemu Suleiman Mohammed Abdiadi “maarufu golo” aliumia sehemu za kichwa ambacho kilikatika moja kwa moja, Kifua na Mikono, hivyo baada ya kumaliza taratibu za uchunguzi waliweza kuzikabidhi maiti hizo kwa ndugu na Jamaa zao.

“Tulishirikiana kikamilifu na vikosi vya ulinzi na usalama vyote pamoja na uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba, katika kuwakabidhi miili hiyo kwa jamaa wa marehemu kwa ajili ya Mazishi”alisema Dk Hilali.

Akitoa tamko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mhammed, aliwataka wananchi waliopoteza ndugu zao katika aji ya kuangukiwa na ukuta huo, kuwa na subra katika kipindi hichi kigumu kwao. 

Alisema kuwa msiba huo, sio wao pekeyao bali ni wataifa kwa ujumla, hivyo Serikali iko pamoja nao katika msiba huo na itashirikiana nao kwa mazishi na madawa kwa wale ambao wamepata majeruhi na kulazwa katika hospitali.

“Nimepokea habari ya kusikitisha kutoka kwa viongozi wenzangu, kuhusu kuanguka kwa ukuta na kupelekea kupoteza maisha ya wananchi watatu, na wengine watatu kujeruhiwa”alisema Mohammed Aboud.

Kwa upande wake mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Wawi kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohammed, alisema kuwa kukosekana kwa taaluma kwa wananchi juu ya vifaa vitakavyo tumika pamoja na athari zake zitakazo tokea imechangia kutokea kwa tukio hilo.

Alisema kuwa, hilo lililotokea ni funzo tosha kwa serikali na kuitaka serikali kuwa makini wakati wote na kabla ya kufanya kitu chochote waangalie athari yake ili kuweza kuepusha majanga kama hayo.

Aidha alisema kuwa, kutokea kwa tuki hilo ni funzo kwa tasisi zote za umma pale wanapotaka kufanya kitu lazima wajuwe athari yake inayoweza kutokea hapo baadae, ambamba na kuwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kifupi.

“Nawashukuru sana vikosi vyetu vya Ulinzi licha ya kukosa zana za kisasa, walipopewa taarifa tu wamefika na kuanza kuokoa maisha ya wananchi, hilo ni jambo la kuwapongeza, wananchi tuwe pole katika kipindi hiki kigumu cha msimba kwani ni msiba wetu sote huu.”alisema Hamad Rashid.

Naye mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, aliwashukuru wananchi wa maeneo ya Machomanne kwa juhudi zao kubwa walizozionyesha kabla ya kufika kwa vikosi vya uokozi katika tukio hilo.

Aliwataka wataalamu wanaotoa tenda kutumia taaluma zao wakati wanapotoa tenda kwa kuchukuwa wafanya kazi wenyetaaluma, kwa kuangalia wafanyakazi wao taaluma zao wakati wanapotaka kufanyiwa kazi zao.

Aliwapa pole familia zote zilizopoteza ndugu na jamaa zao katika eneo la tukio hilo, katika kipindi hicho kigumu. “ Sina budi kuwapongeza wananchi wote waliofika katika tukio hilo, na kuweza kusaidia uokozi kabla ya kufika kwa vikosi vya uokozi katika tukio hili”alisema Tindwa.

Kwa upande wake Mkuu wa kikosi cha Zimamzoto na Uokozi Pemba, ACF Iddi Khamis Juma, alisema kuwa katika tuko hilo changamoto kubwa iliyowakabili ni kukosekana kwa vifaa vya kisasa vya uokozi, hali iliyopelekea kuchukuwa muda mwingi kwa kutumia vufaa vya kienyeji.

Alisema kuwa, licha ya kutumika kwa vifaa vya kienyeji lakini waliweza kuziopoa marehemu zilizokuwa zimekwama katika mnara huo, sambamba na kuwataka wananchi pindi likitokea tukio kutoa taarifa kwa wakati muafaka kwa vyombo vya Sheria.

“Tulipopata taarifa tu tuliweza kupeana taarifa makamanda wote na kufika katika eneo la tukio na kuweza kuziopoa maiti zilizokuweko juu ya Mnara huo, ila kikwazo ni zana za uokozi kwani tumetumia dhana duni”alisema.

Naye mmoja kati ya wafanyakazi katika mnara huo, Said Mohammed , alisema kuwa katika kazi hiyo jumla wako vijana 12 ambao ndio wanofanya kazi ya ubomoaji wa mnara huo.

Said alisema kuwa, wanapofika asumuhi huchonga kuta hilo kwa kutumia drili ili kuweza kuliangusha au kuvunja kidogo kidogo, na baadae hushuka chini na kuuvuta kwa gari huo ukuta.

“Leo kabla ya hawajateremka chini, ukuta uliwaangukia na tukaamua kupanda juu kwa lengo kuwaokoa merejeruhi kwanza waliokuwepo hapo juu”alisema kiongozi huo.

Ujenzi huo wa mnara wa tangi la maji Machomanne Chake Chake Pemba, unaendeshwa na kampuni wa Serengeti Limited ya Tanzania Bara.

CHANZO: ZANZINEWS

KUDAI MAMLAKA YA ZANZIBAR SI DHAMBI – MAALIM SEIF

Imewekwa na Nassor Khamis

atibu Mkuu wa CUF Taifa ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamadi, akihutubia maelfu ya wananchi waliofika kiwanjani hapo leo jun 06 2013. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.)
atibu Mkuu wa CUF Taifa ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamadi, akihutubia maelfu ya wananchi waliofika kiwanjani hapo leo jun 06 2013. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.)

Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ameunga mkono kauli iliyotolewa na Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar Eddi Riyami ya kuwataka Wazanzibari wasiotaka mamlaka kamili ya Zanzibar wajitokeze hadharani kama wanavyofanya wale wanaodai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF ameeleza hayo katika viwanja vya Kibanda maiti mjini Zanzibar katika mkutano wa hadhara uliolenga kusherehekea “Umoja wa Wazanzibari”ulioasisiwa kufuatia maridhiano ya kisiasa.

Amesema hatua ya Wazanzibari kudai mamlaka ni haki yao, na kwamba hakuna dhambi ya kudai jambo hilo.

Amefahamisha kuwa wazanzibari walio wengi wameungana kudai mamlaka ya nchi yao kwa njia ya amani na demokrasia, na kutoa wito kwa wale wasiotaka mamlaka ya Zanzibar wajitokeze hadharani.

Amewahakikishia wananchi kuwa hatorudi nyuma katika kuitetea Zanzibar kuwa na mamlaka yake, ili iweze kutambulika kimataifa na kuweza kuratibu na kushughulikia mambo yake ya nje.

Kwa upande wake Katibu wa kamati ya maridhiano Ismail Jussa Ladhu, amewaomba viongozi wa vyama vyote kushirikiana na wananchi katika kudai mamlaka ya nchi, ili wazanzibari waweze kujikomboa kutokana na kile alichokiita ukoloni wa Tanganyika.

Katika risala ya wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar iliyosomwa na Ameir bin Ameir kutoka Bwejuu, amesema pamoja na mambo mengine, katiba mpya izingatie uwepo wa Jamhuri ya Zanzibar na uraia wake.

Mambo mengine waliyotaka yatolewe katika orodha ya mambo ya Muungano ni pamoja na sarafu, benki kuu, mambo ya nje, vyama vya siasa, baraza la mitihani pamoja na mafuta na gesi.

 

BALOZI SEIF AKAGUA UJENZI WA HOTELI YA DARAJA LA SABA

Imewekwa na Nassor Khamis

Ramani halisi  itakavyokuwa Hoteli ya Daraja la Saba ya Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s inayojengwa katika eneo la ilipokuwa Starehe Club Pembezoni mwa Fukwe ya Forodha Mchanga.
Ramani halisi itakavyokuwa Hoteli ya Daraja la Saba ya Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s inayojengwa katika eneo la ilipokuwa Starehe Club Pembezoni mwa Fukwe ya Forodha Mchanga.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Hoteli Mpya ya Daraja la Saba { Grand Hayert } inayomilikiwa  na Kampuni   ya Kimataifa ya ASB Holding’s ambayo inajengwa katika eneo lililokuwa Starehe Club ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar inatarajiwa kufunguliwa rasmi katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar za mwaka 2014.

Ujenzi wa Hoteli hiyo unaofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya CRJ kutoka Nchini china unatazamiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu ambapo zaidi ya ajira za wazalendo kati ya 60 na 100 zitatolewa wakati itakapoanza kazi zake rasmi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli hiyo ili kupata sura halisi ya Ujenzi huo kufuatia kupokea malalamiko mengi kutoka kwa  baadhi ya watu na taasisi dhidi ya ujenzi huo kwa dhana ya kukiukwa kwa matakwa ya hifadhi ya Mji Mkongwe.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Balozi Seif kwamba Jengo la Hoteli hiyo litakalokuwa na ghorofa tatu linazingatia kubakisha sura ile ile ya haiba ya nyumba zilizomo ndani ya Mji mkongwe.

Nd. Sarboko alisema Uongozi wa Kampuni ya ASB utapaswa pia kuzingatia ujenzi wa ukuta maalum wa mita tatu kama yalivyo majengo mengine ya Mji mkongwe yaliyo pembezoni mwa bahari ili kusaidia kunusuru athari yoyote ya maji, Mazingira  au matukio ya dhoruba  yanapotokea wakati wowote.

Alisema hatua zote hizo zinachukuliwa sambamba na matakwa ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Elimu sayansi na Utamaduni { UNECSO } juu ya hifadhi ya Mji mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika makubaliano ya Hifadhi ya Kimataifa.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s Bwana  Ali Al-Bwardy alifahamisha kwamba Uongozi wa Hoteli hiyo utazingatia matumizi bora na sahihi ya fukwe iliyopo pembezoni mwa Hoteli hiyo bila ya kuathiri  matumizi ya Wananchi kwa utaratibu maalum utakaoandaliwa.

Bwana Ali Al – Bwardy alisema uongozi wa Kampuni yake ya ASB  unaelewa kwamba eneo la fukwe ni la Serikali ambalo Jamii inafursa ya  kulitumia wakati wowote wanapolihitaji kwa shughuli zao za kila siku ikiwemo michezo au hata mapumziko.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha zake mara baada ya kuangalia harakati hizo za ujenzi alieleza kuridhika kwake na taratibu za ujenzi zinazochukuliwa na Kampuni hiyo ya ASB Holding’s.

Balozi Seif alisema kwamba amechukuwa hatua hiyo ya kukagua ujenzi huo kufuatia malalamiko aliyokuwa akiyapokea kutoka kwa baadhi ya Watu na Taasisi tofauti yakiishutumu  Kampuni hiyo kukiuka taratibu za ujenzi ndani ya eneo la hifadhi ya Mji Mkongwe.

“ Nimeridhika na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Kampuni yenu ya ASB Holding’s katika ujenzi huu wa Hoteli kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe. Sina shaka nao na mnaweza kuendelea na Ujenzi kama kawaida. Sasa kama kuna asiyeridhika mnaweza kumuelekeza kuja  kwangu “. Alisisitiza Balozi Seif.

Ujenzi wa Hoteli hiyo  ya Daraja la Saba { Grand Hayert } iliyopo baina ya Tembo Hoteli  na Nyumba Iliyokuwa ikiandikisha Vizazi na Vifo ya Mambo Msiige itakapomalizika itakuwa na uwezo wa kulaza wageni wapatao 65 kwa wakati mmoja.