Rushwa na Ufisadi Chanzo cha kuporomoka kwa majengo nchin – Mtatiro

: Naibu katibu mkuu wa Chama cha Wananchi CUF MH, Julius Mtatiro akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea eneo lililo poromoka jengo la ghorofa 16 Posta jijini Dar es salaam
: Naibu katibu mkuu wa Chama cha Wananchi CUF MH, Julius Mtatiro akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutembelea eneo lililo poromoka jengo la ghorofa 16 Posta jijini Dar es salaam
Na Nassor Khamis, Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Tanzania Bara Mh, Julius Mtatiro amesema matukio ya kuanguka kwa majengo mbalimbali hapa nchini kunatokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watendaji mbalimbali katika sekta za ujenzi.
Akizungumza na Waandishi wa habari kufuatia kuanguka kwa jingo la ghorofa 16 lililopo Posta mtaa Morogoro/Indiragandhi jijini Dar es salam amesema kumekuwa na utaratibu wa kugawana asilimia Fulani za mapato ya ujenzi ili kuweza kupatikana vibali pamoja na kutofanya ukaguzi wa majengo yanayojengwa.
Amesma majengo mengi yamekuwa yakijengwa chini ya viwango vinavyohitajika na hatimae kuporomoka na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi.
“Chanzo cha ghorofa hii kuanguka, ni rushwa, ufisadi na uzandiki mkubwa. Watu washachukua 10% zao sasa raia wasio na hatia wanateketea. Wizara wamekula chao, mkandarasi chake, watathmini chao, mtoa kibali kaka alichokula, sasa rushwa imetamalaki.”alisema Mtatiro
Aidha amesema kuwa serikali bado haipo makini katika kukabiliana na maafa yanapojitokeza kutokana na ucheleweshwaji wa kupeleka vikosi vya uokozi pamoja na vifaa vya kisasa katika maeneo ya tukio.
“Inasikitisha kuwa hata vifaa vya uokozi hatuna, serikali haiwezi kuokoa maisha ya raia wake. Hadi sasa hakuna mipira ya oksijeni inayoweza kupenyezwa kwenye vifusi ili walau kupeleka hewa kwa wale wanaopigania uhai huko chini, bila kupeleka mipira hiyo tutaokoa maiti tu.” Alisema Mtatiro.
Amesema kuwa licha ya kuzungumza na viongozi kadhaa wa serikali waliokuwepo eneo la tukio umuhimu wa kuleta vikosi vya jeshi ili kuongeza kasi katika uokoaji bado wameachiwa raia wasio na ujuzi wowote wa kupambana na majengo huku maisha ya watu yakiangamia.
Amesema kuwa licha ya ndugu wa wtu waliopatwa na maafa hayo kuomba usaidizi wa uokoaji kutoka shirika linalosaidia katika uokoaji kwa gharama zake la Nchini Israel na kukubali kusaidia serikali imeshindwa kutoa kibali kwa shirika hilo hivyo kupelekea kuzorota kwa shughuli za uokoaji.
Kufuatai kuanguka kwa ghorofa hiyo watu kadhaa wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya ambapo hadi mchna wa leo watu wapatao ishirini na moja (21) wamefariki dunia huku shughuli za uokoaji zikiwa bado zinaendelea.

Chuo cha utumishi wa Umma Zanzibar chafanya Mahafali yake ya tano

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimzawadia Mwanafunzi bora zaidi  Iddi Muhsin Bakar kati ya wanafunzi 25 waliofanya vizuri katika mafunzo yao ya Stashahada katika chuo cha Utawala Bora Tunguu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimzawadia Mwanafunzi bora zaidi Iddi Muhsin Bakar kati ya wanafunzi 25 waliofanya vizuri katika mafunzo yao ya Stashahada katika chuo cha Utawala Bora Tunguu.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema usimamizi uliobora na utekelezaji wenye ufanisi wa mipango ya Serikali hupatikana kutokana na taaluma bora wanayopewa watumishi wa umma.

Alisema maendeleo ya nchi yanategemea watumishi wa umma waliopikwa vizuri kitaaluma ambayo inayokwenda sambamba na mabadiliko ya wakati hasa yale ya karne hii ya Sayansi na teknolojia.

Akizungumza katika Mahafali ya Tano ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar hapo katika Viwanja vya majengo yake Mapya yaliyopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema mtumishi wa umma ndie msimamizi na mtekelezaji wa mipango sahihi ya Serikali.

Balozi Seif alisema  ipo haja kwa chuo cha Utawala wa Umma kutilia mkazo mafunzo mafupi ya kuwajengea uwezo watumishi na watendaji tofauti ili wafanye kazi zao za kutoa huduma kwa ufanisi unaokubalika na jamii.

“ Kwa vile chuo hichi kina dhima ya kuleta mabadiliko na mageuzi ya utumishi wa umma, si vibaya mkatumia uwezo wa vyuo vya nchi tofauti ili kuona jinsi wanavyoendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo na kukuza maadili ya watumishi”. Alisisitiza Balozi Seif.

“ Wenzetu hawa wa vyuo vya nje tayari wameshapiga hatua kubwa katika mageuzi ya utumishi , hivyo hatuna budi nasi kujifunza kutoka kwao”. Aliongeza kusisitiza zaidi Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikiomba chuo hicho kusaidia katika upandaji wa fikra mpya kwa umma jinsi ya kuwahudumia wananchi wanapohitaji huduma kutoka kwa watumishi wa Umma.

Alisema wananchi wanapohitaji huduma hizo ni vyema kwa watumishi hao wakaelewa kwamba wananchi hao ndio waliosababisha uwepo wao kutokana na kodi wanazolipa.

Akizungumzia suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema utendaji kazi katika sekta za umma hauko kwenye kiwango kinachokubalika.

Alisema tabia hiyo inayochangia kuzorotesha ufanisi wa kazi inakwenda sambamba na kuporomoka kwa maadili ya kazi pamoja na kukithiri kwa wizi katika taasisi kadhaa za umma.

Balozi Seif alishauri elimu ya sasa ya utumishi iweke mkazo wa kuendesha Taasisi na Idara za umma kama zinavyoendeshwa katika Taasisi Binafsi kwa kuheshimu uwajibikaji na udhibiti madhubuti wa matumizi ya fedha.

“ Moja kati ya sifa kubwa ya sekta binafsi ambayo wengi wetu tunaielewa ni udhibiti madhubuti wa matumizi ya fedha. Sasa sekta binafsi isipofanywa hivyo maana yake ni kufilisika kunakopelekea Taasisi kushindwa kutoa huduma. Kwa bahati mbaya mwamko kama huo haupo katika sekta za umma hapa Nchini”. Aliasa Balozi Seif.

Aliupongeza Uongozi pamoja na Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma kwa juhudi zao za maandalizi ya mahafali hayo ya tano ambayo ni ya kihistoria kwa vile kwa mara ya kwanza yamefanyika katika jengo lao jipya liliopo Tunguu.

Halkadhalika Balozi Seif  alitoa pongezi maalum kwa mwanafunzi Maryam Hassan Vuai ambae ni mlemavu wa viungo kwa moyo wake wa kujiendeleza uliomuwezesha kukamilisha ndoto yake na kumaliza mafunzo ya Rasilimali watu katika ngazi ya Stashahada chuoni hapo.

Katika risala yao wahitimu hao wa chuo cha Utawala wa Umma wameelezea faraja yao  kutokana na jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali kupitia wizara inayosimamia Utumishi wa Umma kwa kujenga jengo la kudumu la chuo hicho.

Walisema ujenzi huo umesaidia kuondosha kero na matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wanafunzi hao kwa kipindi kirefu hali ambayo ilikuwa ikiwakosesha utulivu wa mafunzo kutokana na ukosefu wa sehemu ya uhakika ya kupata taaluma.

Walisema licha ya hatua nzuri ya upatikanaji wa jengo hilo na uhaba wa vifaa na changamoto nyengine zinazoendelea kukikabili chuo hicho, lakini wameiomba Serikali kupitia chuo hicho kufikiria uamuzi wa kuanzisha mafunzo ya shahada ya kwanza hapa Zanzibar kwa vile vijana wengi wenye sifa za kujiunga na kiwango cha elimu hiyo wapo wa kutosha.

Mapema Mkurugenzi wa chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar Bibi Arusi Masheko alisema jumla ya wahitimu elfu 1455 wa fani tofauti katika ngazi ya Msingi, Cheti na Stashahada wamekamilisha mafunzo yao na kufanikiwa kupata vyeti na stashahada.

Bibi Arusi Masheko alifahamisha kwamba kati ya wahitimu hao wanafunzi 424 ni wa ngazi ya Msingi,  1312 ambao ndio wengi walikuwa ngazi ya Cheti na 190 wa ngazi ya Stashahada.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Jeshi la Polisi lamtia mbaroni anaedaiwa kumuua Padri Mushi

Imewekwa na Nassor Khamis

Hayati Padri Evarist Mushi
Hayati Padri Evarist Mushi

MTU mmoja alietajwa kwa jina la Omar Mussa Makame (35), mkazi wa Mwanakwerekwe Zanzibar, amekamatwa na Jeshi la Polisi Zanzibar, kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Padri wa Kanisa Katoliki Zanzibar, Evaristus Mushi. Taarifa hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Kamishna wa Jeshi hilo Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Kamishna Mussa, mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 13, mwaka huu, katika Mtaa wa Kariakoo, Zanzibar na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu zote kukamilika.

“Huu ni mwanzo tu, kwani Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa kitaalamu ili kuhakikisha watu wote wanaohusika na matukio ya uhalifu hapa Zanzibar, wanakamatwa na kufikishwa katika mkondo wa sheria.

“Jalada la mtuhumiwa huyu tayari limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria kwa sababu yeye ndiye atakayetupa mwongozo juu ya suala hili.

“Kabla mtuhumiwa hajakamatwa, tulifanya upelelezi kwa kutumia michoro na alipokamatwa, watu waliokuwa eneo la tukio siku ambayo padri aliuawa, walimtambua kwamba ndiye aliyekuwapo.

“Lakini, kwa kuwa tulikuwa tumeahidi zawadi ya shilingi milioni kumi kwa atakayesaidia kukamatwa kwa watuhumiwa na kwa kuwa mtuhumiwa huyu amekamatwa kwa msaada wa wananchi, aliyesaidia kukamatwa, atakabidhiwa fedha zake katika mazingira ya usiri kwa ajili ya kulinda usalama wake.

“Pamoja na kazi nzuri tunayoifanya kwa kushirikiana na wananchi, bado tunahitaji msaada wao katika harakati zetu za kukabiliana na uhalifu,” alisema Kamishna Mussa.

Padri Mushi aliuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi kichwani Februari mwaka huu, wakati akiingia katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Mtakatifu Theresia, Zanzibar.

Baada ya watu hao kufanya mauaji hayo, walitoweka kwa kutumia pikipiki waliyokuwanayo wakati wanamsubiri padri huyo awasili kanisani hapo.

Kutokana na uzito wa tukio hilo, Jeshi la Polisi nchini, lilifanya upelelezi kwa kuwashirikisha wataalamu wa masuala ya upelelezi kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ambao waliwasili Kisiwani Zanzibar na kuchora michoro kuonyesha jinsi mauaji hayo yalivyofanyika.

Juzi, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuonyesha jinsi asivyoridhishwa na ukimya wa upelelezi wa kuuawa Padri Mushi na kujeruhiwa kwa risasi, Padri Ambrose Mkenda.

Ghorofa laanguka na kusababisha maafa Dar

Imewekwa na Nassor Khamis
Wananchi mbalimbali wakiendelea na shughuli za uokoaji ili kupata watu waliokwama kwenye kifusi kufuatia kuporomoka kwa ghorofa liyo kuwwa inajengwa maeneo ya Posta Jijini Dar es salaam.
Wananchi mbalimbali wakiendelea na shughuli za uokoaji ili kupata watu waliokwama kwenye kifusi kufuatia kuporomoka kwa ghorofa liyo kuwwa inajengwa maeneo ya Posta Jijini Dar es salaam.
Na Nassor Khamis, Dar es salam
Watu kadhaa wanahofiwa kufa kufuatia ajali ya kufunikwa na kifusi baada ya jengo walilokuwa wakijenga kuporomoka ghafla.
Jengo hilo lenye urefu wa ghorofa kumi na sita linaalomilikiwa na ndugu watatu wa familia moja lilianguka likiwa na watu kadhaa ndani yake ambao walikuwa ni wafanyakazi katika jengo hilo.
Akithibitisha kutokea kwa tokeo hilo Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova amesema tukio hilo limetokea majira ya saa mbili na nusu asubuhi ya leo mtaa wa Morogoro na Indira Gandhi.
Amesema kuwa Juhudi za uokozi wa watu walio nasa ndani ya kifusi hicho zinaendelea na tayari wamefanikiwa kuokoa maiti za watu wawili na majeruhi kumi na saba akiwemo mwanamke mmoja na watoto wane.
Amesema kuwa tayari jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa awali ili kubaini chanzo cha ajali hiyo kwa kuwahoji baadhi ya wahusika wamasuala ya ujenzi kutoka katika manispaa ya Ilala.
“Uchunguzi wa awali ili kubaini chanzo cha ajali hii tayari umeanza na taunawahoji baadhi ya wahusika wanao husika na masuala ya ujenzi ili kubaini chanzo cha ajali.
Aidha amewataja baadhi ya watu wanaohojiwa kuwa ni pamoja na Mkandarasi wa halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Muhandisi mkuu wa majengo pamoja na Mkaguzi mkuu wa majengo wa Manispaa ya Wilaya hiyo.
Wakizungumza Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa watu wapatao hamsini ambao ni walikuwa ni wafanyakazi wa jengo hilo pamoja na baadhi ya watoto ambao walikuwa wkicheza karibu na jengo hilo.
Aidha wamesema kuwa vifaa duni vya ujenzi wa jengo hilo vikiwemo uhaba wa saruji pamoja na nondo dhaifu ndio chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo.
“Hili jengo limejengwa chini ya kiwango kwani wakati wa kujengwa unaona jinsi wanavyojenga mchanga unakuwa mwingi na saruji kidogo na zile nondo si unaziona zilivyo nyembamba hasa pale unategemea nini kama si kuporomoka na kuua watu.” Alisena  mmoja wa mashuhuda hao aliejitambulisha kwa jina la Othman Nassor.
“Yaani huwezi amini ghorofa zote kumi na sita zimejengwa kwa miezi sita tu hasa wewe umeona wapi ujenzi wa haraka kiasi hicho tena jengo kubwa kama hili.” Aliongezea.
Hata hivyo jitihada za uokoaji ili kuwapaa wahanga waliosalia katika ajali hiyo bado zinaendelkea na hakuna idadi kamili iliyothibitishwa juu ya waliyoikuwemo kwenye jengo hilo.

Balozi Seif azitaka Kampuni za Nje kuwekeza kwenye sekta ya Maji na Nishati

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji yenye makao makuu yake nchini Qatar. Kushoto yake ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Bwana Adnan Harb na kulia yake Balozi ni Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya Nchini Ras Al- Khaimah Bwana Kamal Ahaya ambaye ndie aliyeratibu ujio wa Ujumbe huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji yenye makao makuu yake nchini Qatar. Kushoto yake ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Bwana Adnan Harb na kulia yake Balozi ni Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya Nchini Ras Al- Khaimah Bwana Kamal Ahaya ambaye ndie aliyeratibu ujio wa Ujumbe huo.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema bado Makampuni na Taasisi mbali mbali za Ndani na nje ya Nchi zina fursa ya kuwekeza katika sekta za Maji na nishati ili Zanzibar iwe na uhakika kamili wa kujitosheleza kwenye mahitaji ya sekta hizo muhimu.

Alisema licha ya baadhi ya makampuni na taasisi tofauti kujitokeza kuonyesha nia hiyo lakini mlango uko wazi kwa washirika wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono hatua hiyo.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe  wa Kampuni ya Kimataifa  inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji safi na salama yenye makao yake makuu Nchini Qatar mazungumzo yaliyofanyika hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Aliueleza Ujumbe huo unaoongozwa na Meneja Mkuu wake Bwana Adnan Harb kwamba Zanzibar inahitaji kuwa na vianzio vingi vya nishati ya umeme kwa vile imelenga kujiimarisha zaidi katika sekta ya viwanda pamoja na miji mipya.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar hivi sasa ina kianzio kimoja tuu cha umeme wakati mahitaji ya huduma hiyo yanabadilika kila mara kutokana na ongezeko la miradi ya kiuchumi kama Hoteli na Biashara ambayo yote hiyo inakwenda sambamba katika matumizi ya nishati hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo ya EMEQ  kwa kuonyesha shauku ya kutaka kuwekeza miradi yake hapa Zanzibar jambao ambalo litasaidia ushawishi wa uwekezaji katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

“ Kwa vile tayari mmeshapata fursa ya kutembelea na kukutana na watendaji wa Wizara zinazohusika na Nishati pamoja na Maji kuelezea fursa mlizonazo katika miradi yenu, nitajitahidi kuhakikisha wahusika hao wanawasiliana na nyinyi ili kufanikisha lengo hilo”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa  inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji salama Bwana Adnan Harb alisema Kampuni yao imefanikiwa kuendesha miradi ya umeme wenye uwezo wa kufikia Kilowati 100 ambao hutumia Gesi.

Bwana Adnan alimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Gesi inayotumika kuzalishia Umeme huo unaouwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 20 haina sumu katika matumizi yake baada ya kufanyiwa utafiti wa kitaalamu.

Naye Mkuu wa Idara ya uhandisi wa Kampuni hiyo Bwana Ibrahim Raymond Nassar alieleza kwamba Kampuni hiyo imelenga kutoa huduma za kutibu maji ili kuondoa vijidudu vinavyosababisha maradhi mbali mbali.

Bwana Ibrahim alisema dawa maalum za vidonge zimetengenezwa ili kutumika katika miradi hiyo ambayo imekusudiwa kwa jamii iliyokubwa zaidi hasa vijijini ambayo umezo wao ni hafifu kwa kutumia mamlaka zinazohusika na huduma hiyo.

Ujumbe huo wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji salama yenye makao yake makuu Nchini Qatar umekuja Nchini kupitia uratibu wa Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya Ras Al- Khaimah Bwana Kamal Ahaya.

Othman Khamis Ame

0fisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Mbunge wa Chambani afariki dunia

Imewekwa na Nassor Khamis

Mbunge wa Jimbo la Chambani Mh, Salim Hemed Khamis akikimbizwa Hospitalini mara baada ya kuanguka ghafla katika kikao cha Kamati ya Wizarz ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa jana.
Mbunge wa Jimbo la Chambani Mh, Salim Hemed Khamis akikimbizwa Hospitalini mara baada ya kuanguka ghafla katika kikao cha Kamati ya Wizarz ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa jana.

 

Na Nassor Khamis, Dar es Salam

Mbunge wa Jimbo la Chambani Mh, Salim Hemed Khamis amefariki dunia mchana wa leo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili aliko lazwa tokea jana.

Mbunge huyo aliefikishwa Hospitalini hapo baada ya kuanguka ghafla katika kikao cha kamati ya kudumu ya Bunge inayosimamia Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mh, Edward Lowassa.

Mh, Salim alikutwa na masahibu hayo jana na alikimbizwa hospitalini kwa matibabu ambako alilazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU). Hata hivyo, hali yake ilizidi kuwa mbaya huku akizungumza kwa tabu kuwa alikunywa dawa za shinikizo la damu (BP) kabla hajala chochote na hivyo kuzidiwa.

Tartibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kuelekea Kisiwani Pemba zinafanyika na mazishi yanatarajiwa kufanyika leo saa kumi jioni huko Kisiwani Pemba.

Sisi sote ni Allah na kwake tutarejea, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema Peponi AMIN.

 

Hukumu ya Sheikh Ponda Aprili 18

Imewekwa na Nassor Khamis

Katibu wa jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda.
Katibu wa jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda.

 

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Aprili 18, mwaka huu inatarajiwa kutoa hukumu katika kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda (55) na wenzake 49.

Mbali na kupangwa kwa tarehe ya hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa jana aliutaka upande wa mashtaka na utetezi kuwasilisha hoja zao kama washtakiwa hao watakuwa na hatia ama la, Aprili 3, mwaka huu.

Juzi wakati Sheikh Ponda akijitetea aliieleza mahakama hiyo, kuwa yeye hana nyaraka za umiliki wa Kiwanja cha Malkazi Chang’ombe bali historia ya eneo hilo inawafanya wao kuwa wamiliki.

Sheikh Ponda na wenzake hao 49, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kuingia kwa jinai, kuvamia ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali, wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni na uchochezi.

Akijitetea dhidi ya mashtaka hayo, Sheikh Ponda, akiongozwa na wakili wake, Juma Nassoro, alidai kuwa awali kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na Taasisi ya Jumuiya ya Kiislamu ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS) ambayo ilivunjwa na Serikali mwaka 1958 na Serikali kuunda chombo kingine kilichosajiliwa kama Bakwata.

Alidai kuwa Bakwata iliundwa ili kusimamia shughuli zilizokuwa zikiendeshwa na Taasisi ya Jumuiya ya Kiislamu ya East African Muslim Welfare Society na siyo mali kama majengo, viwanja na hata shule.

“Tulitumia njia ya mazungumzo ya kidiplomasia kurejesha kiwanja cha Malkazi Chang’ombe kwa kuzingatia kuwa itatatua mgogoro huo katika njia nyepesi” alidai Sheikh Ponda.

Alidai Sheikh Ponda.Nyerere sasa tusilete mijadala isiyokuwepo.”

Hata hivyo, Sheikh Ponda alikubali kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliohusika kutoa taarifa kwa maimamu wa misikiti mbalimbali kuwaeleza waumini wao kushiriki kujitolea katika ujenzi wa msikiti wa muda uliojenga katika eneo la Malkazi Chang’ombe Oktoba 11 na kukamilika Oktoba 14, mwaka jana.

Alidai kuwa walijenga msikiti huo baada ya kufanya makubaliano na mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Agritanza Ltd, Hafidhi, na kukubaliana kuweka alama ambayo kila Muislamu akiiona ataiheshimu na kutofanya shughuli zake binafsi katika eneo hilo na kupendekeza kujenga msikiti huo wa muda.

Kuhusu kukamatwa kwake

Sheikh Ponda alidai kuwa yeye alikamatwa Oktoba 16, 2012, nyakati za saa 4 kasoro usiku alipokuwa akijiandaa kuingia katika Msikiti wa Tungi Temeke , akipanda ngazi alitokea mtu mmoja aliyekuwa kwenye gari nyeusi aina ya Toyota Harrier akimtaka amfuate.

Alidai kuwa na yeye pia alimshauri pia amfuate na baadaye alimua kuachana naye na kuingia ndani ya msikiti huyo, lakini alisikia kishindo cha gari na alipogeuka nyumba aliona gari tatu deffender zilizojaa askari wa FFU wakiwa wamebeba silaha.

Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Nchini Tanzania { Tamta } kuadhimisha miaka 51 toka kuanzishwa kwake

Imewekwa na Nassor Khamis

 Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Tanzania             { Tamta  }  Sheikh Mohammed Abdull Dhikri akitoa maelezo ya maandalizi ya Sherehe za Jumuiya yao  kuadhimisha miaka 51 tokea kuanzishwa kwake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Kati kati yao  ni Mwenyekiti wa Jumuiya  Hiyo ya Tamta Maalim Sheikh Mudhhir
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Tanzania { Tamta } Sheikh Mohammed Abdull Dhikri akitoa maelezo ya maandalizi ya Sherehe za Jumuiya yao kuadhimisha miaka 51 tokea kuanzishwa kwake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Kati kati yao ni Mwenyekiti wa Jumuiya Hiyo ya Tamta Maalim Sheikh Mudhhir

Viongozi wa Jamii popote pale walipo wataendelea kuwa wahimili wa kusimamia malezi na elimu kwa kizazi chao kilichowazunguuka ili kujenga Taifa lenye heshima, Utii, Maadili na nguvu ya uwajibikaji kwa mfumo wa kitaaluma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi sita wa Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Nchini Tanzania { Tamta } uliofika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema suala la kumfinyanga mtoto halihitaji mjadala na litaendelea kuwa jukumu la wazazi kwa kufuata sheria, taratibu sambamba na maamrisho yaliyoelekezwa katika vitabu vya dini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Jumuiya hiyo ya Walimu wa Kiislamu Tanzania  kwa jitihada zake za kuendeleza elimu ya Dini kwa watoto wa rika tofauti ambazo zinahitaji kuungwa mkono na waumini wengine ndani na nje ya Nchi.

Aliufahamisha Uongozi wa jumuiya hiyo kwamba katika kuunga mkono jitihada zao atajitahidi kuangalia uwezekano wa kuunga mkono hatua yao hiyo kwa kuwashawishi wahisani na washirika wa masuala ya dini kusaidia Jumuiya hiyo muhimu kwa hatma ya Umma wa Kiislamu.

“ Sisi Viongozi ndio wahimili wakubwa wa kusimamia elimu iwe ya dunia au akhera kwa watoto wetu waliotuzunguuka na tukielewa kuwa hii ni dhima inayotukabili wazazi sote”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Tanzania { Tamta } Sheikh Mohammed Abdull Dhikri alisema utaratibu wao wa kuendesha sherehe za Madrasa ya Jumuiya hiyo unalenga kuamsha ari na hamasa kwa wanafunzi kuelekea katika kudumu vyema mafunzo yao.

Hata hivyo sheikh Mohammed Abdul Dhikri alisema zipo changamoto kadhaa zinazochangia uendeshaji wa madrasa ya Jumuiya hiyo akazitaja kuwa ni pamoja na uwezeshaji wa walimu wanaojitolea, uchakavu wa majengo pamoja na huduma za Umeme.

Alieleza kuwa katika kukabiliana na changamoto hizo Uongozi wa Jumuiya hiyo pamoja na kujiendesha kwa baadhi ya misaada ya wahisani lakini umelenga kujiendesha wenyewe  kwa kuamua kuwekeza katika Kilimo cha alizeti.

Katibu Mkuu huyo wa Tamta amewakumbusha waislamu popote walipo kuandaa mazingira ya kuunga mkono jumuiya hiyo ili lile lengo la kuujenga kitaaluma Umma wa Kiiislamu lipatikane.

Jumuiya hiyo ya Walimu wa Kiislamu Tanzania { Tamta } ifikapo Juni 27 mwaka huu inatarajiwa kuadhimisha miaka 51 tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1962.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

ZECO latakiwa kufanya matengenezo katika mfumo wa Umeme

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara ya kukagua nguzo ya umeme mkubwa iliyoanguka katika kijiji cha Pete Wilaya ya Kusini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara ya kukagua nguzo ya umeme mkubwa iliyoanguka katika kijiji cha Pete Wilaya ya Kusini.

 

Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } limeagizwa kuufanyia matengenezo makubwa mfumo wa umeme uliopo katika Kijiji cha Michamvi Kilichopo Wilaya ya Kati ambao uko katika mazingira ya hatari kwa wananchi wapitao kwenye  maeneo hayo.

Agizo hilo limetolewa na Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara ya ghafla katika eneo hilo kuangalia waya za umeme zilizoanguka chini ya ardhi pembezoni mwa Hoteli za Utalii Beach Resort na Kilele Beach Vila Michamvi kufuatia nguzo zake kung’oka kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Balozi Seif alifanya ziara hiyo kufuatia malalamiko ya Wananchi wa Michamvi waliyoyatoa kupitia Kipindi maalum cha Mawio kinachotolewa na Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } kila siku asubuhi.

Balozi Seif akiambatana na Wakuu wa Wilaya za Kati na Kusini alisema wahandisi wa Shirika la umeme wanapaswa kufanya marekebisho hayo haraka iwezekanavyo ili kukinga athari zinayoweza kuleta maafa hapo baadaye.

Alisema haipendezi kuona watendaji hao wanaripotiwa matukio mbali mbali ya hitilafu za umeme katika maeneo mbali mbali lakini utekelezaji wa hatua hizo huchukuwa muda mrefu jambo ambalo linavunja moyo wale wanaotoa taarifa hizo.

Balozi Seif alifahamisha kwamba uchelewaji wa hatua hizo husababisha baadhi ya watu kujiungia wenyewe huduma hizo bila ya kuzingatia athari za baadaye pamoja na wengine kutumia fursa hiyo kwa kufanya wizi na hujuma zinazopelekea kulitia hasara shirika hilo.

“ Kumekuwa na uchelewaji wa kuchukuliwa hatua kunakofanywa na wahandishi wa Shirika la Umeme wakati inapotokea hitilafu ya kiufundi. Na hili hata mimi mwenyewe nimelishuhudia katika makazi yangu ninayoishi Mazizini. Hebu jitahidini kupunguza malalamiko ya wananchi mnaowapatia huduma za Umeme”. Balozi Seif aliwasa wahandisi hao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kati Nd. Vuai Mwinyi alimueleza Balozi Seif kwamba tatizo hilo amelirithi kwa Mkuu wa Wilaya aliyemtangulia na kuchukuwa hatua za kuwaandikia Barua ya kuwakumbusha watendaji hao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif pia alipata fursa ya kuangalia Waya nyengine zilizoanguka za umeme mkubwa katika njia inayokwenda Wilaya ya Kusini ambayo ni miongoni mwa mradi wa umeme uliofadhiliwa na Serikali ya Norway kupitia Shirika lake la Misaada la Norad .

Kwa mujibu wa taarifa za wakaazi wa Kijiji cha Pete walimueleza Balozi Seif kwamba nguzo zilizobeba waya hizo zimeanguka kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Hata hivyo baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wameamua kuzitumia waya hizo kwa kuanikia nguo zao jambo ambalo ni hatari kwa mujibu wa kanuni na taratibu za sekta ya umeme.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Tume ya Pinda yatoa matokeo ya awali sakata la kufeli Wanafunzi wa Kidato cha nne

Imewekwa na Nassor Khamis

WaziriMkuu wa Tanzania Mh, Mizengo Pinda.
WaziriMkuu wa Tanzania Mh, Mizengo Pinda.

 

HATIMAYE tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, imetoa taarifa yake. Tume hiyo imebaini sababu zilizochangia matokeo hayo kuwa mabaya ni upungufu wa walimu na matumizi ya vitabu vilivyopitwa na wakati.

Sababu nyingine ni usimamizi dhaifu katika sekta ya elimu, pamoja na uhaba wa bajeti, sababu ambazo zimezoeleka na zilikuwa zikijulikana kabla ya tume hiyo kuundwa.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome, wakati akitoa matokeo ya awali yaliyofanywa na tume hiyo kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam.

Profesa Mchome alisema tume hiyo haitadharau kutumia maoni yalitolewa bungeni na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kwa ajili ya kunusuru sekta ya elimu.

“Tume imepata maandiko, taarifa na nyaraka mbalimbali kutoka ofisi ikiwamo mikoa na wilaya ambazo tayari zimeshafanya vikao kwa ajili ya suala hili na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali, ili kusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya tume.

“Hadi sasa tumepokea ujumbe mfupi wa maandishi zaidi ya 300, email hazihesabiki, maoni kwenye tovuti zaidi ya 300, simu zaidi ya 1,000 na walimu na wanafunzi zaidi ya 40 katika kila shule, kwa mantiki hiyo ni zaidi ya maelfu ya watu wametoa maoni yao kwa upande wa Dar es Salaam pekee.

“Tulifanya mahojiano na chama cha wamiliki wa shule binafsi, Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) Kanda ya Dar es Salaam, Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

“Wengine ni viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kama vile kaimu kamishana wa elimu, wakurugenzi wa idara za elimu ya msingi na elimu ya sekondari.

“Tumefanya mahojiano ya awali na Baraza la Mitihani Tanzania, Taasisi ya Elimu Tanzania, wakuu wa shule, baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo Ilala, Kinondoni na Temeke na wananchi mbalimbali.

“Kutokana na mahojiano hayo ya awali tumebaini kuwa tatizo la uhaba wa walimu, uhaba na uchakavu wa majengo sambamba na nyumba za walimu pia ni chanzo cha kushuka kwa ufaulu.

“Kuhusu mitaala tumechukua sample kwa mamlaka husika na tunaendelea kuzifanyia kazi, huku tukiendelea kusubiri watupatie taarifa tulizowaagiza.

“Pia tumebaini usimamizi duni katika sekta hii pamoja na uhaba wa bajeti ni mojawapo ya chanzo cha kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mtihani huo,” alisema Profesa Mchome.

Alisema kwa sasa wajumbe wa tume yake wamesambaa mikoani kulingana na ratiba ambayo ni Mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Manyara, Arusha, Morogoro, Pwani, Simiyu, Shinyanga na Mbeya.

Alisema maoni yote yanayoendelea kutolewa na watu mbalimbali yanaendelea kufanyiwa kazi, hivyo akawataka wananchi wasisite kuendelea kutoa maoni yao kwa ajili ya kunusuru sekta ya elimu nchini.

 

Nyerere, Karume watajwa kesi ya wafuasi wa Ponda

Imewekwa na Nassor Khamis

Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere.
Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere.

 

Shahidi wa utetezi  na Mwanzilishi wa Baraza la Misikiti Tanganyika, Bilali Waikela (87), amedai mahakamani katika kesi inayomkabili Sheikh Issa Ponda na wenzake 49, kwamba  Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Shekhe Abeid Karume, walivunja Umoja wa Waislamu wa Afrika Mashiriki.

Waikela alidai kuwa umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuwatetea na kuwasaidia Waislamu na kwamba Tanzania ilipata kiwanja cha Chang’ombe Marcas kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Misri.

Waikela ambaye ni shahidi wa 48 wa upande wa utetezi katika kesi hiyo alidai kuwa, umoja huo ulifutwa baada ya Karume kudanganywa kuwa wana mpango wa kufanya mapinduzi na kuwarudisha Waarabu Zanzibar.

“Mwalimu Nyerere ndiye aliyemtuma Karume afanye hivyo na mwaka 1964 nilifungwa baada ya kukataa kupokea Shilingi 40,000 ili nikubali kuvunja umoja huo, na  Kassim bin Juma, Adam Simba na Salehe Masasi waliotumiwa kuhamasisha watu kuvunja umoja huo,” alidai.

Alidai kuwa ofisi za umoja huo zilifungwa hadi mwaka 1968 lilipoundwa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na kukabidhiwa ofisi pamoja na mali zote kikiwamo kiwanja cha Chang’ombe markazi kilichokuwa kimejengwa shule ya Waislamu.

CHANZO: NIPASHE

 

Wanafunzi washinda danguroni Dar

Imewekwa na Nassor Khamis

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Yasinta Assey akionyesha baadhi ya nguo na viatu vya wanafunzi vilivyokutwa katika eneo linalodaiwa kuwa danguro linalotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo, jana. (Picha na Pamela Chilongola  )
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Yasinta Assey akionyesha baadhi ya nguo na viatu vya wanafunzi vilivyokutwa katika eneo linalodaiwa kuwa danguro linalotumiwa na wanafunzi wa shule hiyo, jana. (Picha na Pamela Chilongola )

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Majani ya Chai iliyopo Kipawa jijini Dar es Salaam, wametajwa kujiingiza katika kashfa ya ngono, kuvuta na kuuza bangi katika moja ya nyumba zinazozunguka shule hiyo.

Hilo ni tukio lingine jipya, kwani mwishoni mwa mwaka jana, kuliibuka matukio ya ajabu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi, Ruaruke, Rufiji mkoani Pwani ambao walielezwa kujihusisha na uvutaji bangi hata kukonyeza na kubaka walimu wao.

Mkuu wa Sekondari hiyo, Jasinta Assey alikiri na kusema kwamba vitendo vya uvutaji bangi na biashara ya ukahaba kwa wanafunzi wake, vinachangiwa na askari wa Kituo kidogo cha Stakishari ambao alidai wanachukua rushwa kwa wauzaji wa bangi na nyumba bubu za wageni. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Shule hiyo, Jasinta Assey alisema ni kawaida ya polisi hao kwenda kwenye nyumba hizo kunakofanyika biashara hizo na kuchukua rushwa badala ya kutatua tatizo.

Alisema ongezeko la utoro katika shule hiyo ni tatizo kubwa na wanafunzi wa kidato cha nne wanaosoma masomo ya sanaa ndiyo wanaoongoza kwa kuvuta bangi na kwenda kufanya ngono katika nyumba zilizo jirani na eneo la shule hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema hajapata taarifa za hali hiyo.
“Ngoja nimtume Mkuu wa Kituo cha Polisi Stakishari afuatilie kwa karibu,” alisema Minangi na kuongeza: “Lakini ngoja nikwambie, hili suala nakumbuka liliwahi kuripotiwa 2011 wakati nikiwa mkuu wa kituo hicho; nililishughulikia na tulibaini kuwa hakuna mwanafunzi ambaye alikuwa anaenda kwenye nyumba hizo kuvuta bangi wala kufanya ngono.

“Kilichotokea kwa wakati huo ni kwamba, tuliwachukua baadhi ya wanafunzi ili watupeleke mahali walipokuwa wakifanyia vitendo hivyo kutokana na maelezo na vielelezo vyao, lakini hatukubaini hizo sehemu.
“Inawezekana basi haya mambo yameibuka upya baada ya kuona kuna mkuu wa kituo mwingine mpya,” alisema Kamanda Minangi.
Kutokana na matendo hayo, wanafunzi wengi walifanya vibaya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka jana.
“Walifeli sana mwaka jana hawa, walimu wapo, tunawapa nyenzo lakini hawataki, ninaiomba Serikali kuingilia kati suala hili kwani ni la muda mrefu na ni faida ya vijana hawa,” alisema.
Shule ya Majani ya Chai ilishika nafasi ya 61 kimkoa kati ya shule 226 wakati ngazi ya taifa, ilishika nafasi ya 543 kati ya shule 3,392.
Wanafunzi 274 walijisajili kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana na kati yao 130 walipata sifuri, wakati waliopata daraja la nne ni 85, waliopata Daraja la Tatu ni 18 wakati waliopata daraja la pili ni watano. Hakukuwa na daraja la kwanza na wanafunzi 36 hawakufanya mtihani.
“Baada ya kuona utoro umekithiri shuleni hapo, nilikwenda kutoa taarifa kituo kidogo cha Polisi Stakishari, lakini hawakuonyesha ushirikiano matokeo yake wanakwenda kwa wenyeji hao na kuchukua rushwa.
“Hili inaonekana kama ni dili la hawa askari, kwani wapo walionifuata na kunieleza niache kufuatilia, lakini mimi niliwaambia nitafuatilia tu na ilifikia hatua nikatishiwa maisha.
“Baada ya kuona nazidi kutishiwa maisha, niliogopa, nikaacha…na hivi ninavyoongea na wewe, najua tu watanifuata kwani nimeshaambiwa nikipita peke yangu eneo wanakofanyia biashara zao watanifanyia kitu kibaya,” alisema Assey.

Mwalimu huyo alisema kwamba, wanafunzi wa kidato cha nne wanaosoma masomo ya sanaa wapo 54, lakini wakati mwingine utakuta wanafunzi watano tu darasani na waliobakia wanakwenda kuvuta bangi na kufanya vitendo vya ngono.
Assey alisema kuwa iliwahi kutokea wasamaria wema waliwapelekea baadhi ya nguo na viatu vya wanafunzi wa shule hiyo vilivyokutwa eneo wanakofanya biashara hiyo ya haramu.
“Hili darasa linaongoza kwa utovu wa nidhamu na limeshindikana…Nilikuwa nawategemea sana polisi, lakini hawaonyeshi ushirikiano wowote ule…Unaona hizi nguo za wanafunzi zililetwa na mama mmoja baada ya kuzikuta kwenye danguro ‘bubu’,” alisema Assey huku akionyesha sare hizo za shule.

CHANZO: MWANANCHI.

Jiajirini wenyewe musisubiri kuajiriwa na serikali – Mama Asha Balozi

Imewekwa na Nassor Khamis

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akiyafunga mafunzo ya miezi sita ya ushoni hatua ya awali ya ushoni kwa kikundi cha hatubaguani cha jimbo la Kitope hapo Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B. (Picha na Hassan Issa OMPR - Zanzibar)
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akiyafunga mafunzo ya miezi sita ya ushoni hatua ya awali ya ushoni kwa kikundi cha hatubaguani cha jimbo la Kitope hapo Ofisi ya Jimbo hilo iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B. (Picha na Hassan Issa OMPR – Zanzibar)

 

Na Othman Khamis Ame  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Wanavikundi vya ushirika wanaojishughulisha na kazi za amali Nchini wanapaswa kuzingatia fani yao katika dhana nzima ya kujipatia ajira badala ya tabia ya kufikiria ajira hupatikana Serikalini pekee.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo wakati akiyafunga mafunzo ya miezi sita ya ukataji nguo katika Fani ya Ushoni kwa Kikundi cha Ushirika cha  Hatubaguani cha Jimbo la Kitope  hafla iliyofanyika hapo Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “ B “.

Mama Asha alisema Ushoni ni miongoni mwa kazi pekee inayotoa ajira ya uhakika hasa kwa vikundi vya ushirika. Hivyo wanavikundi hao wana wajibu wa kuhakikisha mafunzo yao wanayaendeleza lengo likiwa kujiongezea mapato sambamba na kusaidia Familia.

Alisema zipo familia na vikundi vinavyoendesha maisha yao kwa kutegemea sekta ya ushoni na matokeo yake familia hizo zimekuwa zikiendesha maisha yao bila ya kutetereka.

“ Tumeshuhudia baadhi ya Familia zimekuwa zikiyakabili  matatizo yao yanayowazunguuka bila ya msaada wa utegemezi wa waume zao jambo ambalo limekuwa faraja kwao pamoja na watoto wao”. Alisisitiza Mama Asha.

Aliwalaumu baadhi ya wanachama wa Kikundi hicho cha Hatubaguani waliokuwa na tabia za kupangilia ushiriki wa mafunzo yao jambo ambalo litasababisha kuwavunja moyo Viongozi waliojitolea kudhamini mafunzo hayo.

Alisema walimu na Viongozi wa Jimbo hilo walijitolea kwa hali na mali kuhakikisha mafunzo hayo ya ushoni yanaendelea na kuleta tija ya kutoa ajira kwa wana kikundi hicho.

Katika kuunga mkono harakati za mafunzo hayo Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi mchango wa Shilingi Laki Tano  Taslim { 500,000/- } kusaidia gharama za ufundishaji wa wana kikundi hicho.

Akitoa nasaha zake Mkurugenzi wa Chuo cha Ushoni kiliopo Magomeni Mjini Zanzibar { Modern Tailoring Academy } ambacho ndicho kilichosimamia kuendesha mafunzo hayo Mwalimu Rashid Makame Shamsi aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Kitope kwa hatua zake za kuwajengea uwezo wa ajira wananchi wake.

Nd. Rashid alisema Uongozi huo umeonyesha moyo wa kuwatafutia ujuzi Wana Kikundi hao na katika kuunga mkono juhudi hizo aliahidi kwamba Uongozi wa Chuo chake utakuwa tayari kuwaendeleza tena wana kikundi hao kwa hatua ya Pili na ya tatu endapo utaratibu wa mafunzo hayo utaandaliwa.

Mapema Mwenyekiti wa Kikundi cha Hatubaguani Bibi Sichana Said Haji amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kwa moyo wake wa kujitolea kusimamia uanzishwaji wa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujipatia ajira ya kudumu.

Bibi Sichana kwa niaba ya wana kikundi wenzake wameahidi kwamba mafunzo waliyoyapata ya miezi sita yakijumuisha wanafunzi 30 watayatumia vyema kwa manufaa yao na vizazi vyao.

Hata hivyo wanafunzi waliofanya mtihani wao ambapo wanatarajiwa kupatiwa vyeti vya  Modern Tailoring Academy walikuwa 17 kati ya 30 na kufikia asilimia 50% ya wanafunzi hao.