CHINA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA VIWANDA ILI KUZALISHA MAZAO YA BAHARINI

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa  katika Idara ya Biashara ya Jimbo Heilongjiang Nchini China Bwana Li Leyu Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Idara ya Biashara ya Jimbo Heilongjiang Nchini China Bwana Li Leyu Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Idara ya Biashara kupitia kitengo chake cha ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Jimbo la Heilongjiang Nchini China inakusudia kuwekeza katika sekta ya Viwanda vitakavyozalisha  Mazao ya Baharini hatua ambayo imekuja kufuatia mazingira mazuri yaliyopo ya Bahari ya Hindi iliyovizunguuka Visiwa vya Zanzibar.

Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa  katika Idara ya Biashara ya Jimbo hilo Bwana Li Leyu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Li Leyu aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Idara hiyo alisema kwamba mradi huo wa uwekezaji utakwenda sambamba na utoaji taaluma kwa wavuvi wadogo wadogo ukilenga kuwa na  uzalishaji wa kimataifa  kwa kushirikisha pande zote mbili.

“ Mradi wetu utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kutoa ajira zisizopunguwa mia tano kwa wavuvi wazalendo na ndio maana tukasisitiza zaidi suala la Taaluma kabla ya kuanza kwa mradi na hatimae uzalishaji. Tumekusudia Mradi wetu uwe wa mfano, bora na wa mwanzo katika mwambao wa Afrika Mashariki “. Alifafanua Bwana Li leyu.

Mkuu huyo wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Nje katika Idara ya Biashara ya Jimbo la Heilongjiag Nchini China Bwana Li alifahamisha kwamba wataalamu wa kufanya utafiti wa kuendesha mradi huo watafika Nchini mara baada ya kuridhiwa pamoja na kukamilika kwa taratibu zilizowekwa za uwekezaji Nchini.

Bwana Li Leyu alieleza kuwa Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango kikubwa cha mazao ya Baharini ikiwemo samaki na Kamba mazao ambayo yana pato kubwa katika masoko ya kimataifa hasa eneo la Bara la Asia.

Alieleza  kwamba mradi huo mkubwa ulioelekezwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki ukiilenga zaidi Zanzibar unaweza kuwa tayari ndani ya kipichi cha kati ya miaka miwili hadi mitatu tokea utapoanza ujenzi wa Viwanda vyake.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Idara hiyo ya Biashara ya Jimbo la Heilongjiang Nchini China kwa mtazamo wake wa kuiona Zanzibar ndio mahali panapostahiki kuwekezwa mradi huo wa mazao ya Baharini.

Balozi Seif alisema huo ni mradi mzuri utakaoleta faraja kwa Serikali katika harakati zake za kuongeza ajira kwa wananchi na hasa lile kundi kubwa la vijana wanaomaliza masomo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Idara ya Baishara ya Jimbo la Heilongjiang kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar   itakuwa tayari kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuona mradi huo unasimama na kufanya kazi hapa Zanzibar.

“  Bidhaa za Kamba na Samaki tumekuwa tukizishuhudia ughali wake katika masoko ya Kimataifa. Sasa kuwepo kwa mradi huu hapa Nchini kutasaidia kuongeza pato la Taifa na kupunguza ukali wa maisha kwa wavuvi watakaobahatika kufanya kazi katika kiwanda hicho “. Alisisitiza Balozi Seif.

WAKULIMA WA MIKARAFUU WATAKIWA KUZINGATIA USHAURI WA WATAALAMU WA KILIMO

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza Umuhimu wa Mashamba ya Mikarafuu kulimwa kwa Kitaalamu ili kukidhi mahitaji halisi ya soko la Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza Umuhimu wa Mashamba ya Mikarafuu kulimwa kwa Kitaalamu ili kukidhi mahitaji halisi ya soko la Kimataifa.

Na Othman khamis Ame –  OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa wakulima wa mashamba ya Mikarafuu kukubali kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa Kilimo hicho ili kujenga nguvu za uzalishaji wa uhakika wa zao Karafuu Nchini.

Balozi Seif alitoa sisitizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua baadhi ya Mashamba ya Serikali ya Miti ya Mikarafuu ambayo yako chini ya usimamizi wa baadhi ya wakulima ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema bado ipo dhana kwa baadhi ya wakulima wa Mikarafuu kujilimbikizia miti mingi ya zao hilo wakiwa na mawazo na fikra za kupata uzalishaji mkubwa zaidi jambo ambalo ni ndodo Kitaalamu.

Balozi Seif ambae amekuwa na utaratibu wa kutembelea mara kwa mara mashamba ya Mikarafuu hasa Kisiwani Pemba alieleza kwa kuwa Serikali Kuu inaendelea na Mikakati ya kuimarisha zao hilo Wananchi pamoja na Wakulima wa Kilimo hicho wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.

“ Hivi sasa tunapaswa kuwa makini katika uzalishaji wa zao la Karafuu kitaalamu kwani wakati wa kuvuna karafuu mpeta umepitwa na wakati kulingana na mazingira yaliyopo ya soko la Dunia “ Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wakulima Abdulla Masoud Abdulla wa Kijiji cha Shungi na Mkulima Ali Othman Ali wa Kijiji cha Minazini kwa uamuzi wao wa kujikubalisha kuyahuisha mashamba ya Mikarafuu ya Serikali yaliyomo katika maeneo yao.

Balozi Seif alisema juhudi hizo zimeleta faraja kwa Serikali na kuwaahidi kwamba wao ndio wanaostahiki kupewa upendeleo wa kukodishwa wakati unapofikia msimu wa zao la karafuu.

Naye Mkulima Ali Othman Ali wa Kijiji cha Minazini alimueleza Balozi Seif kwamba shamba hilo la Serikalio lilikuwa pori tupu kwa muda mrefu na kulazimika kuliomba kulihuisha kutoka kwa Taasisi husika ili kulirejesha katika hali yake.

Mkulima Ali Othman alifahamisha kwamba alilazimika kutumia nguvu za ziada katika kulihuisha shamba hilo lenye ukubwa unaokadiriwa kufikia ukubwa wa Eka moja.

Alisema hatua hiyo hivi sasa imempa faraja kwa vile tayari mazao ya Mihogo na Migomba aliyoiotesha ndani ya miti ya Mikarafuu iliyomo ndani ya shamba hilo imeanza kumpatia faida cha chakula sambamba na fedha za kujikimu kwa mambo mengine ya maisha.

Naye Mkulima Abdulla Masoud Abdulla wa Kijiji cha Shungi amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzingatia ushauri wa wataalamu katika harakati za kuendesha kilimo hicho.

Mkulima Masoud alieleza kuwa ufinyu wa taaluma ya kilimo hicho ndio uliokuwa ukiwapa  ukaidi na kupelekea kuleta mgongano kati yao na wataalamu wa kilimo hicho.

Mapema Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Hemed Salum alisema kasi ya wakulima wa Mikarafuu kujitokeza kufyekea mashamba yanayomilikiwa na Serikali hivi sasa imeongezeka zaidi.

Nd. Hemed alisema hatua hiyo imeleta faraja kwa Watendaji wa Taasisi yake kupata muda wa kuendelea na majukumu yao ya kawaida badala ya kushughulikia zaidi mashamba hayo.

 

BALOZI SEIF AZINDUA KAMPENI ZA CCM KUWANIA UBUNGE JIMBO LA CHAMBANI

Imewekwa na Nassor Khamis

Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akimnadi Mgombea wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama hicho kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chambani Nd, Matar Sarhani Said.
Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akimnadi Mgombea wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama hicho kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chambani Nd, Matar Sarhani Said.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amesema Wananchi wa Jimbo la Chambani Mkoa Kusini Pemba wanapaswa kujenga Historia mpya ya kumsimamia kushinda Kijana wa CCM atakayeungana nao katika kujiletea Maendedleo yao kwa haraka.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua Mkutano wa Kampeni za CCM kuelekea  kwenye uchaguzi mdogo wa Kiti cha Ubunge wa Jimbo la Chambani hapo katika uwanja wa Michezo wa Skuli ya Ukutini Wilaya ya Mkoani.

Uchaguzi huo unakuja kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo  Mh.  Salim Hemed Khamis kufariki Dunia kutokana na Maradhi ya Moyo mnamo Tarehe 26 mwezi wa machi mwaka huu wa 2013.

Balozi Seif ambae pia alipata fursa ya kumnadi Mgombea wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Mattar Sarhan Said kwenye Mkutano huo wa uzinduzi ya Kampeni  alisema  wakati wa kujipima mawazo yao na yale wanayopewa na kuletewa umefika ili watoe maamuzi sahihi yatakayoleta  maslahi kwao na vizazi vijavyo.

Alieleza kwamba Wananchi wa Jimbo la Chambani wamekuwa mashahidi wakubwa wa kuona Ilani za Vyama vya siasa zinaponadiwa wakati wa kampeni za uchaguzi tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwakumbusha wanachi hao kwamba CCM iliyopata ridhaa ya kuongoza Dola Bara na Zanzibar imekuwa ikiendelea kutekeleza ilani yake kama ilivyoahidi ambapo  Jimbo la Chambani limefarajika na Ilani hiyo hasa katika sekta ya Elimu, Afya na Mawasiliano.

Akizungumzia  amani Balozi Seif alisema kwa vile suala hilo limo ndani ya Ilani ya uchaguzi ya CCM Serikali zote mbili zitaendelea kuwa imara katika kuhakikisha zinadhibiti amani iliyopo hivi sasa.

Alisema vipo baadhi ya vikundi na watu wanaojaribu kuichezea amani iliyopo kwa visingizio vya uhuru wa kusema ambavyo kamwe Serikali haitakuwa na mzaha katika kukabiliana navyo.

“  Katika suala la amani tuko wazi kabisa, hatutamvumilia Mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuhatarisha amani ya Nchi. Lazima Jamii ichunge amani ya Nchi iliyopo “. Alitahadharisha Balozi Seif.

Kuhusu suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif alisema kwamba Wazanzibari ndio wanaoendelea kufaidika zaidi  Muungano uliopo ambao uliasisiwa na Hayati Mwalimu Julius K.Nyerere pamoja na Mzee Abeid Amani  Karume.

Alisema huduma za Kiuchumi na biashara zimepanuka na kushamiri zaidi kwa pande zote mbili ikilinganishwa na wakati wa kabla ya Uhuru hali iliyowafanya   Wazanzibari walio wengi kuendelea Kibiashara.

Aliwatahadharisha Wananachi kujiepusha na kasumba wanayoendelea kupewa kuhusu mfumo wa Muungano unaotakiwa na kuwashauri kuiachia Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kufanya kazi hizo kwa niaba yao.

Katika Risala yao iliyosomwa na Katibu Msaidizi Mkuu wa CCM Wilaya ya Mkoani Nd. Abdulla Yussuf wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Chambani wameelezea kujivunia kwao kwa kuendelea na shughuli zao za kimaisha bila ya hofu wala vikwazo.

Nd. Abdulla  alisema Wananchi hao wameahidi kuilinda kwa nguvu zote amani iliyopo  Nchini na kusisitiza kwamba  wakati wa kusikiliza na kuunga mkono propaganda za watu binafsi umekwisha na wameamua  kuzipa kisogo.

Walifahamisha kwamba Chama cha Mapinduzi ni nahodha wa Demokrasia kwa kuleta mambo mengi ya maendeleo ambayo yameenea na kuchanua kila pembe ya Nchi hii likiwemo  Jimbo la Chambani.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua Mkutano huo wa Kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chambani kwa Kiti cha Ubunge alisema CCM imedhamiria kushinda katika uchaguzi huo.

Nd. Vuai aliwaomba Wananchi wa vijiji vilivyomo ndani ya Jimbo hilo wanawake, wazee na Vijana kumuunga mkono mgombea wa CCM ili apate fursa ya kusimamia vyema Ilani ya Chama hicho katika Jimbo hilo.

DHAMIRA YA MAPINDUZI NI KUWAWEZESHA WAZANZIBARI KUJITAWALA WENYEWE – MAALIM SEIF

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika ufunguzi wa Kongamano la pili la maridhiano ya kitaifa katika ukumbi wa Salam Hall Bwawani.
Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia katika ufunguzi wa Kongamano la pili la maridhiano ya kitaifa katika ukumbi wa Salam Hall Bwawani.

Na Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amesema dhamira ya msingi ya ukombozi wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya Januari 12, 1964, ni Zanzibar kuweza kujitawala yenyewe na kuwa na mamlaka kamili.

Maalim Seif ameeleza hayo katika ukumbi wa salama hoteli ya Bwawani, wakati akifungua kongamano la pili la kitaifa linalohusu Maridhiano ya Wazanzibari.

Amesema dhamira hiyo ya Mapinduzi ilianza kukiukwa baada ya kutiwa saini kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao uliipunguzia Zanzibar mamlaka yake.

Amesema wakati Wazanzibari wanapodai kuwa na mamlaka kamili wanatetea haki na maslahi ya nchi yao, na kwamba hakuna sababu ya kubezwa wala kupuuzwa.

Amefahamisha kuwa akiwa ni kiongozi wa Zanzibar, atasimamia na kutetea mawazo ya wazanzibari waliowengi katika kupata haki zao za msingi ndani na nje ya Zanzibar.

Akifafanua zaidi kuhusu msimamo wake amesema hiyo haina maana kuwa Wazanzibari hawataki Muungano, bali wanataka kuwepo kwa Tanzanyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili, halafu kuwepo na muungano wa mkataba, ili kila nchi iweze kuendesha mambo yake kwa uhuru.

“Kuwa na mamlaka kamili sio kwa maslahi ya watu wachache bali kwa watu wote, ni kama mvua, yaani inaponyesha mimea yote inanawirika”, alifafanua Maalim Seif na kuongeza,

“Tunataka kurejesha heshima ya nchi yetu, tuwe na sera na Wizara yetu ya mambo ya nje, bendera yetu ipepee nchi za kigeni, Umoja wa Mataifa na Jumuiya nyengine za Kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki”.

Amewataka wanakongamano hao kuwaongoza wajumbe wa mabaraza ya katiba katika kutetea maoni na maslahi ya Zanzibar.

Akizungumzia kuhusu mafanikio ya maridhiano amesema yamerejesha umoja wa wazanzibari na kuondosha uhasama na chuki miongoni kwa wananchi.

Ameipongeza kamati ya maridhiano chini ya Mwenyekiti wake Mzee Hassan Nassor Moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuyaendeleza maridhiano hayo na umoja wa wazanzibari.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ambaye ni mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar Mzee Hassan Nassor Moyo amesema maridhiano hayo yaliyoasisiwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar dkt. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, yameondoa fitna na chuki zilizodumu kwa muda mrefu miongoni mwa wananchi.

Amesema kamati yake inaisubiri kwa hamu kubwa rasimu ya Katiba mpya itakayotolewa, ili waweze kuichambua kuona kama imezingatia maoni ya wananchi na maslahi ya Zanzibar.

Akiwasilisha mapendekezo ya kamati hiyo Mzee Moyo amesema kila nchi katika Muungano inapaswa kuwa na uraia wake, sera yake ya mambo ya nje na Muungano uwe na JINA la “Muungano wa Jamhuri za Tanzania” au “United Republics of Tanzania”.

BALOZI SEIF AIOMBA NORWAY KUISADIA ZANZIBAR KATIKA SEKTA YA UVUVI WA BAHARI KUU

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Inguun Klepsvik Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar na kuiomba Norway kuangalia uwezekano wa kusaidia utaalamu wa Uvuvi wa Bahari Kuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Inguun Klepsvik Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar na kuiomba Norway kuangalia uwezekano wa kusaidia utaalamu wa Uvuvi wa Bahari Kuu.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiomba Norway kuangalia uwezekano wa kuisadia Zanzibar kitaaluma katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu kwa vile Nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo.

Akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klepsvik hapo ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar imezunguukwa na bahari pembe zote rasilmali ambayo ikitumika vyema inaweza kusaidia kutoka ajira katika kiwango kikubwa zaidi na kusaidia pia uchumi wa Taifa sambamba na kupunguza umaskini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania kwamba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha uchumi sekta ya Uvuvi imepewa msukumo na kinachoangaliwa zaidi wakati huu ni kuwashawishi washirika wa Maendeleo na Nchi hisani kuunga mkono sekta hiyo.

Aliipongeza Norway kwa juhudi zake za kuendelea kuunga mkono harakati za maendeleo za Zanzibar kupitia Shirika lake la Maendeleo la Norad ambapo Zanzibar tayari inaendelea kufaidika  na sekta za nishati na mawasiliano ya bara bara kutokana na mchango wa Taifa hilo Hisani.

Naye kwa upande wa Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klepsvik alimuhakikishia Balozi Seif kwamba  Nchi yake itahakikisha kwamba sekta zilizopata msaada wa Nchini hiyo zitaendelea kuungwa mkono zaidi.

Balozi Ingunn alizitaja baadhi ya sekta  zilizoungwa mkono na Serikali yake hapa Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya mawasiliano ya Bara Bara Kisiwani pemba pamoja na Sekta ya Nishati Vijijini.

 

MADAKTARI BINGWA KUTOKA CHINA WAMALIZA MUDA WAO WA UTUMISHI ZANZIBAR

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwashukuru Madaktari Mabingwa wa China  kwa mchango wao mkubwa wa  huduma bora za afya ndani ya kipindi chao cha miaka Miwili ambao wanatarajiwa kumaliza muda wao ifikapo mwezi  ujao wa Juni mwaka huu. Hafla hiyo ya chakula cha usiku aliwaandalia hapo katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resor Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwashukuru Madaktari Mabingwa wa China kwa mchango wao mkubwa wa huduma bora za afya ndani ya kipindi chao cha miaka Miwili ambao wanatarajiwa kumaliza muda wao ifikapo mwezi ujao wa Juni mwaka huu. Hafla hiyo ya chakula cha usiku aliwaandalia hapo katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resor Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Na Othman Khamis Ame – OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Timu ya Madaktari  Bingwa wa Jamuhuri ya Watu wa China kwa umakini wake wa kutoa huduma za Kiafya katika Hospitali mbali mbali hapa Zanzibar.

Pongezi hizo alizitoa wakati wa hafla maalum ya Chakula cha Usiku alichowaandalia Madaktari hao ambao wanatarajia kuondoka Nchini Mwezi ujao baada ya kumaliza muda wao wa kutoa huduma za afya wa miaka miwili hapa Zanzibar.

Hafla hiyo fupi iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji ilifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakifarajika kutokana na huduma nzuri wanazozipokea kutoka kwa madaktari Bingwa wa China wakati wanapofuata huduma za Afya katika Hospitali tofauti kubwa hapa Zanzibar.

Alifahamisha kwamba huduma za afya ndani ya Visiwa vya Zanzibar zimekuwa zikipanuka siku hadi siku kutokana na kuimarishwa kwa  mbiundo mbinu katika sekta ya  Afya kunakotekelezwa  kwa pamoja kati ya Wananchi na Serikali.

Balozi Seif alieleza kuwa mfumo huo wa miundo mbinu umekuwa ukipata nguvu za ziada za misaada ya vifaa, Utaalamu pamoja na uwezeshaji unaofanywa na mashirika, wahisani  na Mataifa rafiki miongoni mwao likiwemo la Jamuhuri ya Watu wa China.

“ Tumekuwa tukishuhudia kwa muda mrefu ndugu zetu wa China wanavyotuunga mkono katika masuala mbali mbali ya Maendeleo na Uchumi lakini Sekta ya Afya wameipa umuhimu zaidi Kivifaa na hata uwezeshaji “.  Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Watu China imekuwa ikiipatia Zanzibar  Madaktari Mabingwa wa fani tofauti katika mpango maalum iliyouweka Nchi hiyo kusaidia huduma za Afya mara tu baada ya   mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema hatua hiyo imeendelea kujenga nguvu za Kihistoria kwa wananchi na Viongozi wa Pande hizi mbili zinazoimarisha  zaidi uhusiano uliopo wa kidugu wa mataifa haya rafiki.

Balozi Seif aliwahakikishia Madaktari Mabingwa hao wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila msaada kwa Timu za Madaktari wa chi hiyo wanaopangiwa kuja kutoa huduma za afya hapa Zanzibar.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Timu hiyo ya Madaktari Mabingwa wa China Afisa wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Zhang Zhiqiang alisema juhudi zilizochukuliwa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea mazingira mazuri madaktari hao zimewawezesha kutekeleza vyema majukumu yao kwa  kiwango kikubwa.

Bwana Zhang alisema uungwana huo utabakia kuwa chachu ya upendo kati ya Madaktari hao na Zanzibar itakayoendelea kudumu ndani ya nyoyo zao katika uhai wote wa maisha yao.

Timu hiyo ya Madaktari Mabingwa 12 kutoka Jamuhuri ya Watu wa China ikiongozwa na Dr.  Lu Jian Lian inatarajiwa kuondoka Nchini Tarehe 18 mwezi ujao wa Juni kurejea nyumbani  mara baada ya kuwasili Timu nyengine mpya katika ule mpango maalum wa Wataalamu wa afya wa China kuja kutoka huduma za afya Zanzibar.

MAALIM SEIF AWATAKA WAKULIMA KUONGEZA UFANISI KATIKA SHUGHULI ZAO ZA KILIMO

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia bidhaa zitokanazo na nntta, wakati akikagua shughuli za kikundi cha ufugaji wa nyuki Vitongoji.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia bidhaa zitokanazo na nntta, wakati akikagua shughuli za kikundi cha ufugaji wa nyuki Vitongoji.

Na Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wakulima kisiwani Pemba kuyatumia mafunzo wanayopewa katika kujiongezea ufanisi wa shughuli zao.

Akizungumza wakati akitoa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili katika Wizara ya Kilimo na Maliasili kwenye ukumbi wa kituo cha mazunzo ya Amali Fidel Castro, Maalim Seif amesema mafunzo hayo yanayotolewa kwa wakulima pamoja na utafiti shirikishi ni miongoni mwa juhudi za serikali katika kuwakomboa wakulima.

Amesema iwapo mafunzo hayo yatatumika vizuri, yatawasaidia wakulima kuweza kulima kilimo cha kisasa, kutumia mbegu bora na pembejeo kama inavyotakiwa.

Amepongeza juhudi za Wizara ya kilimo katika kuwashirikisha wakulima na wafugaji katika utafiti wa mazao mbali mbali, hatua ambayo inakuza uelewa kwa wakulima na kuweza kuongeza kipato chao.

Hata hivyo amesema Wizara ya Kilimo bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi hasa mabwana na mabibi shamba, hali inayopelekea mtendaji mmoja kuhudumia hadi shehia tatu.

Katika majumuisho hayo Maalim Seif ameigiza Wizara hiyo kufanya utafiti wa pembejeo na mahitaji ya wakulima kwa kila shehia ili kuwawezesha wakulima kupata mahitaji kamili, sambamba na kusambaza matokeo ya tafiti za kilimo kwa wakulima wote.

Kwa upande mwengine Maalim Seif ameitaka Wizara ya kilimo kufikiria namna ya kuirejesha miti ya asili ikiwemo mifuu na mizambarau, ili kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa nchi ya kijani.

Kuhusu misumeno ya moto, amewataka wananchi kushirikiana kuifichua misumeno hiyo ambayo ni adui wa mazingira na binadamu.

Akiwa katika ziara ya kutembelea shughuli za kilimo Mkoa wa Kusini Pemba, wakulima waliomba kupatiwa mikopo ili waweze kuendeleza shughuli zao kwa uhakika.

Katika Mkoa wa Kusini Pemba ambako pia aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mtumwa Kheri Mbarak na Katibu Mkuu Affan Othman Maalim, alitembelea maendeleo ya shmaba darasa la wakulima wa migomba Kuukuu Kangani, vitalu vya mikarafuu Mjimbini na Chanjaani pamoja na uzalishaji wa mbegu za muhogo Mfikiwa Chake chake.

BALOZI SEIF AMTEMBELEA SHEHA ALIYEMWAGIWA TINDIKALI

Imewekwa na Nassor Khamis

Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini Magharibi Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu } akielezea mkasa uliompata wa kumwagiwa Tindi kali { Acid } mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kumfariji. (Picha na Haasn Issa wa –OMPR – ZNZ.)
Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini Magharibi Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu } akielezea mkasa uliompata wa kumwagiwa Tindi kali { Acid } mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kumfariji. (Picha na Haasn Issa wa –OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis Ame – (OMPR)

Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Bwana Mohd Omar Said        { Maarufu Kidevu } anaendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa Tindi kali { Acid }  na mtu asiyejuilikana.

Mkasa huo umempata jana usiku mara baada ya kurejea ibada ya sala ya Isha wakati akiendelea na harakati za kutafuta huduma za maji na kumwagiwa tindi kali hiyo iliyoathiri eneo la kifua chek, Bega pamoja na sehemu za jicho la kulia.

Hili ni tukio la tatu kutokea ndani ya mkoa wa mjini Magharibi likiwahusisha aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma pamoja na Katibu wa Fufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.

Sheha huyo wa Tomondo Bwana Mohd Omar Kidevu akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali hapo kumfariji pamoja na kumpa pole alisema alijikuta akimwagiwa tindi kali majira ya saa 2.00 za usiku na mtu asiyemfahamu.

Bwana Mohd Kidevu alisema Mtu huyo alianza kutimua mbio baada ya kufanikiwa kufanya dhambi hiyo kitendo ambacho akalazimika kuomba msaada kwa wasamaria wema lakini hatimae ilishindikana kutokana na kuzidiwa kwa maumivu makali yenye kuchoma kama moto.

Sheha huyo wa Shehia ya Tomondo aliendelea kumfahamisha Balozi Seif kwamba hali yake hivi sasa inaendelea vyema na ameshaanza kupata matumaini kufuatia jicho lake kuanza kuona ingawa bado anakabiliwa na maumivu katika sehemu yake ya usoni. 

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alimuomba Sheha huyo wa Tomondo kuwa na moyo wa subra wakati wa kipindi hichi kigumu cha huduma za matibabu.

Balozi Seif alimuhakikishia Bwana Mohd Kidevu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufuatilia ushauri utakaotolewa na Madaktari kuhusu   tiba ya afya yake na kutoa msaada wowote utakaohitajika ili kuendeleza nguvu za huduma ya tiba yake.

“ Tutafuatilia ushauri watakaotupa Madaktari kuhusu afya yao. Na kama kuna wazo la kukusafirisha iwe Hospitali ya Rufaa Muhimbili au Nje ya Nchi basi sisi kama Serikali tuko tayari  kulitekeleza hilo “. Balozi Seif alimuhakikishia Sheha  Mohd Kidevu.

Akizungumza na vyombo vya Habari nje ya Wodi ya Mapinduzi Kongwe katika Hospitali Kuu ya Mmnazi Mmoja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali  Iddi alisema Serikali Kuu imesikitishwa na vitendo hivi viovu vinavyoleta athari kwa Binaadamu.

Balozi Seif alisema tabia hii mbaya inayoonekana kuanza kuchipua hapa Nchini ikibeba ufinyu wa imani inaanza kuleta hofu miongoni mwa wananchi katika kuendelea na harakati zao za kimaisha za kila siku.

Alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea na uchunguzi wa kufuatilia matukio hayo na haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuwafikisha katika mkondo wa sheria.

SHEHA WA SHEHIA YA TOMONDO AMWAGIWA TINDIKALI

Imewekwa na Nassor Khamis

Sheaha wa Shehia ya Tomondo Unguja akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa Tindikali na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake.
Sheaha wa Shehia ya Tomondo Unguja akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa Tindikali na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake.

 

Vitendo vya uhalifu vinaendelea kujitokeza hapa nchini kila kukicha uku mamlaka zinazohusika na suala la ulinzi na usalama zinaonekana kukaa kimya kwa kushindwa kudhibiti vitendo hivyo.
Hayo yamebainika baada ya sheha wa shehia ya Tomondo Mohammed Saidi Kidevu jana amemwagiwa tindi kali akiwa nyumbani kwake Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja.

 

Tukio la kumwagiwa kwa tindi kali sheha huyo lilitokea mnamo  majira ya saa 2:30 usiku, wakati akiwa katika harakati za kuchota maji.

 

Akizungumza katika hospitali ya Mnazimmoja ambayo ndio anayopatiwa matibabu sheha huyo alisema kabla ya tukio hilo kutokea alitokea kijana mmoja ambae hakumfahamu na kusalimiana  nae na baadae kumwagia.

 

Alisema mara baada ya kumwagia asid  alimfukuza kijana huyo huku akimnadia mwizi lakini alishindwa kupata msaada wowote kutoka kwa wananchi.

 

Awali sheha  huyo alikua akipokea vitisho kutoka kwa watu mbalimbali ambao hawafahamu, ambavyo vimeanza wakati wa chaguzi za wilaya za kuwapata wajumbe wa baraza la katiba.

 

Nae daktari anaempatia matibabu hospitalini hapo dk saidi ali amesema amepata majeraha katika jicho la upande wa kulia ,kifuani na mgongoni  na hali yake inaendelea vizuri huku akisisitiza kuwa ataendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo mpaka Serikali itakapoamuwa kama asifirishwe au la.

MAALIM SEIF ATEKETEZA MISUMENO YA MOTO KISIWANI PEMBA

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiichoma moto misumeno ya moto 23 katika eneo la Kizimbani Pemba, ikiwa ni kampeni ya kutokomeza misumeno hiyo Zanzibar. (Picha, Salmin Said, OMKR).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiichoma moto misumeno ya moto 23 katika eneo la Kizimbani Pemba, ikiwa ni kampeni ya kutokomeza misumeno hiyo Zanzibar. (Picha, Salmin Said, OMKR).

Na Hassan Hamad, OMKR.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wananchi kushirikiana kuisaka misumeno ya moto popote ilipo ili iweze kutokomezwa kabisa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Ameeleza hayo katika kampeni maalum ya kutokomeza misumeno ya moto ambapo misumeno 23 imechomwa moto mbele ya kiongozi huyo, baada ya kukamatwa na maofisa wa Idara ya misitu.

Amesema kila mtu ana wajibu wa kushirikiana na jamii katika kufichua misumeno iliyobakia, ili kuhakikisha kuwa haitumiki tena na kusababisha athari za kimazingira.

“Kila mtu ana wajibu wa kuwafichua watumiaji wa misumeno hii, lakini mashena na polisi jamii muna jukumu kubwa zaidi, na nina hakika mukiamua munaweza kuwabaini wote wenye misumeno ya moto”, alisema Maalim Seif.

Amesema iwapo misumeno hiyo haitodhibitiwa inaweza kuiathiri nchi kwa kiasi kikubwa kutokana na uwezo wake wa kukata miti kwa muda mfupi.

Uchomaji huo wa misumeno ya moto 23 umefanyika katika ofisi za Idara ya misitu iliyoko Kizimbani Kisiwani Pemba.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya kilimo na maliasili Affan Othman Maalim amesema misumeno ya moto ipatayo 270 bado inakisiwa kuwepo Zanzibar, na kwamba kampeni hiyo itasaidia kuitokomeza.

Kwa mujibu wa Affan, kisiwa cha Pemba kinaongoza kwa kuwa na misumeno mingi ya aina hiyo ipatayo 150, huku Unguja kukiwa na misumeno zaidi ya 120.

Amefahamisha kuwa takriban ekari 1000 za miti hupotea kila mwaka visiwani Zanzibar kutokana na kukatwa ovyo na kuongezeka kwa kasi hiyo kutokana na matumizi ya misumeno ya moto.

Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili Mtumwa Kheir Mbarak, amesema misumeno hiyo ambayo ni adui wa muda mrefu wa mazingira, inaweza kuiweza kuifanya nchi kuwa jangwa kwa muda mfupi na ni hatari pia kwa afya ya binadamu.

Maalim Seif yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambako anatembelea shughuli za kilimo kwa lengo la kuwahamasisha wakulima kuendeleza kilimo chenye tija kwa kutumia utaalamu wa kisasa na mbegu bora.

Katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambako alianza ziara yake alitembelea shamba la utafiti wa uzalishaji wa mpunga wa mbegu ya nerika liloko Gombeume mchangamdogo, skuli ya wakulima iliyoko Kiongweni Kambini, shamba la viazi vitamu Makangale na skuli ya wakulima juu ya nishati mbadala iliyoko Kinyasini.

MAAGIZO YA VIONGOZI WA SERIKALI HAYATEKELEZWI IPASAVYO NA WATENDAJI WA NGAZI ZA CHINI

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mh. Saleh Nasson Juma { Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Chake chake Pemba } akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya Kamati yake kupokea Taarifa ya kazi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mh. Saleh Nasson Juma { Mwakilishi wa Jimbo la Wawi Chake chake Pemba } akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya Kamati yake kupokea Taarifa ya kazi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa imeelezea kusikitishwa kwake na tabia  ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuendelea  kudharau  Maagizo yanayokuwa yakitolewa na Viongozi Wakuu wa Serikali katika Taasisi na maeneo tofauti Nchini.

Wajumbe wa Kamati hiyo waliokuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wake Mh. Saleh Nassor Juma Mwakilishi wa Jimbo la Wawi walieleza hayo wakati wakizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kukutana na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupokea Taarifa ya utendaji ya Ofisi hiyo.

Walisema wamekuwa wakishuhudia uzorotaji mkubwa wa kusimamia maagizo hayo hasa katika masuala ya migogoro ya ardhi jambo ambalo huendelea kuleta malalamiko kwa wananchi wanaokumbwa na matatizo ya migogoro hiyo.

Walieleza kwamba baadhi ya watendaji hao wa Serikali wamekuwa wakionyesha chuki za wazi  dhidi ya Waheshimiwa wakati wanapofuatilia au kulalamikia utendaji mbovu.

Walifahamisha kwamba wao sio polisi bali wanachokifanya ni kutekeleza majukumu waliyopangiwa ndani ya Kamati zao ambazo zimeteuliwa kwa mujibu wa taratibu na Kanuni za Baraza la Wawakilishi lililoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali.

Wajumbe hao wameipongeza Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake ambayo yameleta faraja kwa Kamati hiyo na kusisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano wa sehemu zote mbili ili lile lengo la kuwahudumia Wananchi lifanikiwe vyema.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliwakumbusha Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa wakali wanapotekeleza wajibu wao wa kila siku.

Balozi Seif alisema  Kamati za Baraza la Wawakilishi zimeundwa kwa lengo la  kufuatilia mwenendo wa shughuli za Serikali katika Taasisi zake ili zishauri, zikosoe na hata kuelekeza njia ya kuleta ufanisi utakaostawisha na kunufaisha Jamii Nchini.

“ Hili suala la kufuatilia maagizo yanayotolewa na Viongozi wakuu wa Serikali limo ndani ya mamlaka yenu na kamwe hakutakuwa na kiongozi mwengine atakayekuwa na mamlaka ya kujipangia utekelezaji huu “. Alisisitiza Balozi Seif.

Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifanya ziara fupi ya kukagua matengenezo ya majengo ya  Kiwanda cha Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali kinachotarajiwa kuhamia hapo Maruhubi Nje kidogo ya Mji Zanzibar.

Uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukihamisha Kiwanda hicho hapo Mtaa wa Mkele na kuhamia Maruhubi umekuja kufuatia kiwanda hicho baadhi ya wakati kufungwa kutokana na mashine zake kuharibika kwa sababu ya mafuriko ya maji wakati wa msimu wa mvua za masika.

Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Ndugu Mohd Mzee alimueleza Balozi Seif kwamba matengenezo ya majengo hayo chini ya Kampuni ya Kimataifa ya CRJ ya Nchini China yalipangwa kukamilika mwezi huu lakini yatachelewa kidogo kutokana na ufinyu wa bajeti yake.

Hata hivyo Ndugu Mzee alifahamisha kwamba Kampuni ya CRJ imethibitisha kwamba upatikanaji wa fedha za kukamilishia matengenezo yaliyobaki zikipatikana kwa wakati harakati hizo zinaweza kuchukuwa muda miezi miwili au mitatu kuanzia sasa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alisema matengenezo ya majengo hayo ya Kiwanda cha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali yanatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi Bilioni mbili kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana na Uongozi wa Kampuni ya Mafuta Tanzania { State Oil Tanzania } ukiongozwa na Bwana Bjorn Rasmussen  hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Uongozi huo wa mafuta ambao umekuwa ukiendesha mafunzo mbali mbali ya uhifadhi wa mazingira kwa kushirikisha wadau wa mafuta na wana taaluma wa vyuo vikuu Nchini umekuwa ukisisitiza umuhimu wa suala hilo.

Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Mafuta Tanzania Bwana Bjorn alifahamisha kwamba harakati za miradi ya mafuta na gesi hufanikiwa vyema na kuleta faida kubwa pale wahusika na wadau wakuu wa sekta hiyo wanapozingatia vyema msingi mkuu wa mazingira.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitahadharisha jamii nchini kufahamu kwamba rasilmali yoyote inayopatikana popote pale huwa ni ya taifa na wala si ya wakaazi wa eneo husika pekee.

Balozi Seif alieleza kwamba upo ufinyu wa mawazo kwa baadhi ya wananchi kuhisi kuwa rasilmali inayopatikana katika maeneo yao haiwahusu wananchi wengine jambo ambalo ni kosa.

Othman Khamis Ame.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

MAALIM SEIF AHIMIZA KUIMARISHWA ULINZI KATIKA MIPAKA YA BAHARI NA NCHI KAVU

lmewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, alipofika ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, alipofika ofisini kwake Migombani.

Na Hassan Hamad (OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amevitaka vyombo vya ulinzi nchini kusimamia vyema majukumu yake ili kuhakikisha kuwa bahari na mipaka ya nchi inakuwa salama.

Amesema Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa, inakabiliwa na changamoto moto nyingi za kiulinzi na usalama kuhakikisha kuwa magaidi hawaingii nchini, sambamba na kukabiliana na vitendo vya uharamia na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Maalim Seif ameeleza hayo ofisini kwake Migombani alipokuwa na mazungumzo na Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman.

Amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa ni tishio la vitendo vya kigaidi katika Pembe ya Afrika, jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa ili vitendo hivyo visije kuiathiri Zanzibar.

“Suala la ulinzi halina mbadala, kitu cha msingi ni kwa vyombo vya ulinzi na dola kushirikiana kuhakikisha kuwa nchi iko salama kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla”, alisisitiza Maalim Seif.

Kuhusu vitendo vya uharamia vinavyofanywa katika bahari ya hindi, Maalim Seif amesema vinaathiri shughuli za kibiashara na uchumi na vinastahiki kupigwa vita kwa nguvu zote.

Kwa upande wake, Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali S S Othman, amesema suala la ulinzi ndio jukumu la msingi kwa vyombo vya ulinzi, na kuahidi kushirikiana na vyombo vya dola na wananchi katika kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi zaidi.

Jererali Othman ambae pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Zanzibar, amesifu mashirikiano anayoyapata kutoka kwa viongozi wa nchi na watendaji wengine katika kufanikisha jukumu hilo la kiulinzi.

 Jererali Othman pia amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji na kubadilishana mawazo juu ya majumu ya ofisi hiyo.

Waziri Fereji amesema katika kukabiliana na majukumu ya ofisi hiyo, wanahitaji mashirikiano ya karibu na vyombo vya ulinzi katika kukabiliana na na vitendo viovu vikiwemo udhalilishaji wa watu wenye ulemavu, uchafuzi wa mazingira na matumizi ya dawa za kulevya.

Amevishauri vyombo vya ulinzi kujiimarisha zaidi ili kuweza kukabiliana na makundi ya kihalifu yakiwemo yale yanayojihusisha na uchimbaji wa mchanga kinyume na utaratibu.

“Ukweli ni aibu kusema kuwa jeshi la polisi linashindwa kuwakamata wachimbaji wa mchanga kwa sababu wana pamanga na marungu au mawe, wakija wakiamua kuingia barabarani je mutawafanyaje?”, alihoji Waziri Fereji.

Kuhusu UKIMWI, Waziri Fereji amesema licha ya kuwa kiwango cha maambukizi bado ni chini ya asilimia moja, lakini athari kubwa inajitokeza kwa makundi hatarishi likiwemo lile linalojihusisha na biashara haramu ya ukahaba.

UCHUMI WA MATAIFA MACHANGA UTAKUWA KWA KUZINGATIA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA KISASA – BALOZI SEIF

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Vifaa vya Mtandao wa Teknolojia ya Kisasa ya Zhong Xing Telecommunication Equipment  { ZTE } ya Nchini  China Bwana Chen Jinsong.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Vifaa vya Mtandao wa Teknolojia ya Kisasa ya Zhong Xing Telecommunication Equipment { ZTE } ya Nchini China Bwana Chen Jinsong.

Uchumi wa Mataifa machanga yanayolenga kuelekea kwenye maendeleo ya haraka utazidi kuimarika  iwapo Mataifa hayo yatajikita  zaidi katika matumizi ya Mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano ya moja kwa moja kati yao au hata kushirikiana pamoja na yale Mataifa yaliyoendela.

Hayo yaliibuka wakati wa mazungumzo kati  ya Ujumbe wa Kampuni ya Vifaa vya Teknolojia ya Mawasiliano  { Zhong Xing  Telecommunication Equipment } {ZTE }  yenye Makao Makuu yake Nchini China ulioongozwa na Makamu wa Rais  wa Kampuni hiyo Bwana Chen Jinsong pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Chen Jinsong ambae Kampuni yake ya ZTE ndiyo inayojenga na kusimamia mradi wa Mkongo wa Taifa hapa Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuwa mfumo huu wa mawasiliano hutoa fursa kwa wataalamu wa pande mbili walio Nchi tofauti kufanya kazi pamoja kwa kutumia mtandao wa kisasa wa mawasiliano ya Teknolojia.

Alifahamisha kwamba hatua za Kiuchumi , Biashara, Afya  pamoja na harakati za maisha ya Jamii za kila siku zina nafasi na fursa nzuri ya kutumia Mtandao wa Serikali  { E. Government } wakati utakapokamilika matengenezo yake Mfumo huo.

“ Uwezo wa Wataalamu mfano wa sekta ya Afya unaweza  kukua mara dufu kwa kushirikiana katika masuala ya mikutano { Group Discution } na hata baadhi ya operesheni za wagonjwa wakiwa nchi tofauti kwa kutumia mitandano ya     Kisasaya Teknolojia “. Alifafanua Makamu wa Rais huyo wa Kampuni ya ZTE.

Bwana Chen alieleza kwamba katika kuunga mkono Mataifa ya Bara la Afrika kuingia katika mfumo huu wa mawasiliano ya Kisasa ya Teknolojia Uongozi wa Kampuni yake umeshaanza kusambaza huduma zake katika Baadhi ya Mataifa hayo ya Bara la Afrika.

Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Zhong Xing Telecommunicationa Equipement tayari  imeshafungua Ofisi yake Nchini Tanzania likiwemo pia tawi lake moja hapa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba miradi inayoanzishwa na Kampuni hiyo mbali ya kuongeza ushirikiano na Mataifa hayo lakini pia umelenga kusaidia kutoa ajira kwa wazalendo walio wengi kwenye Mataifa hayo rafiki.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alisema mradi mkubwa ulioanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Mtandao wa Serikali { E. Government } chini ya Kampuni hiyo ya ZTE utaisaidia kuirusha Zanzibar kuingia katika mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano Duniani.

Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo ya ZTE kwa kusimamia kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi huu wa Mtandao wa Serikali hapa Zanzibar hatua ambayo itazidi kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa China.

“ Tunashukuru na kufarajika kuona kwamba Nchi zetu mbili Zanzibar na China bado zinaendelea kushirikiana kwa karibu miaka 50 sasa  mara tuu baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 “. Alisisitiza Balozi Seif.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni  inayoendesha Miradi ya Hoteli za Kimataifa Afrika Mashariki iitwayo Mada Hotels yenye Makao Makuu yake Mjini Nairobi Nchini Kenya Bwana Tinu Mhajan.

Bwana Tinu Mhajan ambae amefika Zanzibar kuangalia uwezekano wa Kampuni yake kutaka kuwekeza Vitega uchumi vyake hapa Zanzibar katika maeneo ya Hoteli alisema Utalii utaendelea kukua na kuimarika kwa kupitia mfumo wa kubadilisha vivutio vitakavyowapa ushawishi zaidi watalii kupenda kutembelea eneo hili.

Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya Mada Hotels alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwamba Taasisi yao imelenga kutoa huduma zake ndani ya Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar bado ina fursa nzuri za uwekezaji katika maeneo ya Utalii ambayo Mada Hotels inaweza kuzitumia ipasavyo fursa hizo.

Balozi Seif alimfahamisha Mwenyekiti huyo wa Mada Hotels kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya Utalii ili isaidie uchumi wa Taifa ambao hadi sasa unategemea zaidi zao la Karafuu.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar