Hatua zisipochukuliwa, tunaelekea kuwa na vipaza sauti badala ya vyombo vya habari

By Bin mazrouy

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekipiga faini ya TZS milioni 10 kituo cha TV cha ITV

ITV imepigwa faini hiyo kutokana na na kipindi kutoka bungeni kilichokuwa kinaendesha mahojiano ya moja kwa moja ambapo Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Petter Msigwa alisikika akisema “Naibu Spika amekuwa kama anavaa pampas, hataki kubanduka kwenye kiti kuongoza bunge”.

Kauli hii ya Mchungaji Msigwa imetafsiriwa kama ni kauli ya kuudhi, na imesababisha ITV kuangukiwa na rungu zito la faini badala ya mtoaji wa kauli hiyo.

TCRA wanadai katika mahojiano hayo muongozaji wa kipindi alishindwa kusimamia mjadala uliokuwa ukiendelea na kuruhusu mgeni wake kutoa kauli yenye kuudhi.

TCRA hawakuitendea haki ITV katika maamuzi haya, ukizingatia kuwa kipindi kilikuwa kinarushwa moja kwa moja (Live) na mtangazaji hajui Source wake anakwenda kuzungumza kitu gani juu ya kile alichomuuliza, hivyo kukosa nafasi yaq kuhariri kile kinacho onekana kuudhi.

Kinacho onekana katika maamuzi haya ni muendelezo wa vitisho kwa vyombo vya habari dhidi ya kile kinachoonekana kuwa ni kuwakosoa viongozi wenye mamlaka ya uendeshaji wa vyombo vya maamuzi ya wananchi.

Kwa hali hii sasa vombo vya habari vitaacha kuandaa vipindi na mijadala na mijadala yenye kuikosoa serikali na viongozi wake kwa maslahi mapana ya taifa kwa kuhofia rungu la adhabu za faini ama hata kunyimwa kabisa leseni ya kuendeshea vyombo hivyo kutoka kwa wenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Ikiwa hali hii itaachwa iendelee tutarajie vyombo vyetu vya habari kuwa vipaza sauti tu vya watawala kufikisha ujumbe wao kwa watu wa chini badala ya kuwa majukwaa yenye kuibua hoja za kujenga taifa letu.

Ili kuepusha vyomba vya habari kuwa vipaza sauti vya watawala ipo haja kwa wadau wa habari kupingana na viashiria hivi vya vitisho vinavyo zidi kutolewa kila siku dhidi ya vyombo vya habari na watendaji wake kwa maslahi mapana ya taifa letu.