MAKALA ZA KIISLAMU

 

Nini Hikma Ya Kulala Upande Wa Kulia Kama Alivyotufundisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ?

19 Dhul-Hijjah 1428

Yote tunayoyapata kutoka katika Sunnah ya mwalimu wetu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mafunzo yenye faida kwetu ima faida ya nafsi zetu au faida katika mwili wetu au faida katika maisha yetu na kwa ujumla, bali kuna hikma kubwa kwenye mafunzo hayo:

عن البراء بن عازب رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه و قال صلى الله عليه وسلم : ((إذا أتيت مضجعك فتوضأ وضوءك للصلاة ثم ثم اضطجع على شقك الأيمن ثم قل :  أللهم  أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وَجْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ، آمَنْـتُ بِكِتـابِكَ الّـذي أَنْزَلْـتَ وَبِنَبِـيِّـكَ الّـذي أَرْسَلْـت”   واجعلهن آخر كلامك فإن مت مت على الفطرة)) – البخاري و مسلم

Kutoka kwa Al-Baraa Bin ‘Aazib رضي الله عنهما kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kasema; utakapofika wakati wa kulala, tawadha kama wudhuu wa Swalah, kisha lala upande wako wa kulia, kisha sema:  “Allaahumma aslamtu nafsiy Ilayka, wa fawwadhwtu amriy Ilayka, wa wajjahtu wajhiya Ilayka, wa aljaatu dhwahriy Ilayka, raghbatan wa rahbatan Ilayka, laa maljaa wa laa manjaa Minka illa Ilayka, aamantu bi-Kitaabikal-ladhiy Anzalta, wa bi-Nabiyyikal-ladhiy Arsalta”

[Ewe Allaah,  nimeisalimisha nafsi yangu Kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu Kwako na nimeutegemeza mgongo wangu Kwako, kwa matajarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila Kwako, nimekiamini kitabu Chako Ulichokiteremsha na Mtume Wako Uliyemtuma] Na fanya hivyo iwe ni maneno yako ya mwisho kwani utakapokufa utakufa katika Fitwrah [(Uislamu]))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

Hatuna shaka na tunaamini  na kuyafuata  mafunzo yake kadiri tuwezavyo  kwani nani msemaye kweli kuliko Allaah (Subhanaahu wa Ta’ala) na Mjumbe Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Mjumbe ambaye hasemi kwa matamanio yake ila ni wahyi utokao kwa Mola wetu Muumba Anayesema:

((وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَى)) (( إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَى))

((Wala hatamki kwa matamanio)) ((Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa)) [An-Najm: 3-4]

Basi hebu tuone hikma ya kutufunza kulala upande wa kulia

Ubongo (Brain)

Ubongo sehemu yake huwa upande wa kulia na ndio ambao unauongoza Moyo ulioko upande wa kushoto.

Mapafu (Lungs)

Pafu la upande wa kulia wa mwili ni kubwa kuliko pafu la upande wa kushoto, kwa kuwa pafu la upande wa kulia lina sehemu 3 wakati ambapo la upande wa kushoto lina sehemu 2 tu.
 

Ini (Liver)

Ini liko upande wa kulia na ndilo tezi (gland) kubwa kubwa kabisa mwilini.

Nyongo (Gall Bladder)

Nyongo nayo nipo upande wa kulia na ina majukumu ya kutengeneza utomvu ambao unameng’enyua (digest) mafuta.

Matumbo (Intestines)
 

Matumbo (Intestines) Na Sehemu Ya Mwisho Wa Utumbo (colon)

Sehemu ya ‘mwisho wa Utumbo mkubwa’ (colon) na mwisho wa matumbo (intestines) yako upande wa kulia. (Appendix)

Moyo

Moyo uko upande wa kushoto na ndio pampu la taratibu ya mzungukuo(circulatory system)

Tumeona kwamba  kwamba viungo vya mwili vikubwa viko upande wa kulia katika mwili, kwa hiyo mtu anapolala upande wa kushoto, huathiri viungo hivi na huleta madhara katika siha ya Binaadamu. Na juu ya hivyo mtu anapolala upande wa kulia huwa haileti shinikizo katika vyumba vya mapumziko ya moyo ambazo hufanya wepesi kazi ya Taratibu ya Mzunguko (circulatory cycle).

Kwa hiyo mtu anayelala upande wa kulia anapoamka asubuhi huamka akiwa mwenye nguvu na  mchangamfu.

Hadiyth za  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم tulizoamrishwa na mapendekezo ya kulala upande wa kulia

عن أبي  هريرة رضي الله عنه قال :” رأى رسول الله صلى الله عليه و سلم رجلاً مضطجعاً على بطنه فقال ((إن هذه ضجعة يبغضها الله و رسوله))”. رواه الترمذي  .

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye kasema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimuona mtu amelala kifudifudi, akasema: ((Kulala huku kunachukizwa na Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake)) [At-Tirmidhy]

عن  عائشة أن رسول الله  صلى الله عليه وسلم   “كان   إذاصلى  ركعتي    الفجر    (يعني سنتها)  اضطجع على شقه   الأيمن” – صحيح البخاري

Imetoka kwa mama wa waumini ’Aaishah رضي الله عنها  kwamba “Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  akishaswali rakaa mbili za Alfajiri, [yaani Sunnah za Alfajiri]  hulala upande wa kulia” [al-Bukhaariy]

 

 

عن أبي أمامة قال: مر النبي صلى الله عليه وسلم على رجل نائم في المسجد منبطح على وجهه فضربه برجله وقال: (( قم أو اقعد فإنها نومة جهنمية))

مسند أحمد وسنن ابن ماجه

Kutoka kwa Abu Amaamah kasema; alipita Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa mtu mmoja ambaye alikuwa amelala kifudifudi  msikitini akampiga hivi (teke) kwa mguu akasema: ((Inuka au kaa kwani kulala huku ni kama kulala kwa watu wa motoni))   [Musnad Ahmad na Sunan Ibn Maajah]

 

وعن حفصة رضي الله عنها قالت:” كان النبي صلى الله عليه وسلم إذا أخذ مضجعه جعل يده اليمنى تحت خده الأيمن” رواه الطبراني، صحيح الجامع

Kutoka kwa mama wa waumini Hafswah رضي الله عنها   ambaye kasema: “Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa anapotaka kulala huweka mkono wake katika shavu la kulia“ [At-Twabraaniy katika Swahiyh al-Jaami’y]

Amesema Imaam Ibn al-Qayyim (Allaah Amrehemu): “Kulala kwake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ubavu wake wa kulia kuna siri, nayo ni kuwa Moyo unakuwa juu kwa upande wa kushoto, kwa hivyo, ikiwa atalalia ubavu wake wa kushoto basi usingizi utakuwa mzito; kwani atakuwa katika hali ya utulivu na ushwari na hivyo kuwa usingizi wake ni mzito. Na kama atalala kwa upande wa ubavu wake wa kulia, basi atakuwa katika hali ya wasiwasi na usingizi wake utakuwa si mzito kwa kuwa moyo utakuwa katika hali ya wasiwasi na atahitajia utulie na moyo kupondokeka kwake.

…………………………………………………………………………

 Kumpenda Kikweli Mtume (صلي الله عليه وسلم)

بسم الله الرحمن الرحيم

Shams Elmi (Abu ‘Ilmi)

Leo InshaAllaah tutaangalia mada ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) kutokana na umuhimu wake katika kukamilisha imani ya mja, na kutokana na kutofahamika vyema maana halisi ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) kwa Waislamu walio wengi.

Neno محبة ni neno la Kiarabu kilugha lina maana ya; Hisia za kumili kwa moyo. Na katika Sheria, ni kumili kwa moyo kunako ambatana na kiwiliwili, hisia, akili, matakwa, na matendo ya moyo yanayothibitishwa na matendo ya viungo. Na hiyo ndio Imani.

Imani kwa mtazamo wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah ni kauli na matendo, yaani kauli ya moyo na ulimi, na matendo ya moyo na viungo. Kwa maana hii ya kisheria, mapenzi huwa na uhusiano moja kwa moja na Imani ya mtu.

Lakini kama mtu atatafsiri mapenzi kwa maana ile ya kilugha, yaani kumili kwa hisia za moyo tu, mapenzi ya mtu huyu yatakuwa na dosari kubwa, na yatakuwa yanahukumiwa na matamanio zaidi kuliko Imani, na huu ndio mtihani uliowasibu wengi katika Ummah wetu, wa kutotofautisha baina ya mapenzi ya kiimani, na mapenzi ya kumili kwa hisia za nyoyo.

Mtu anaweza kumpenda mtu mwengine kwa hisia hizo za kumili kutokana na vigezo vyake, lakini akawa bado anatofautiana naye katika mambo mengi, na wakati mwingine hakubaliani nae katika mitazamo yake na kauli zake, lakini bado moyo wake ukawa unamili kwa mtu huyo, tafsiri kama hii ya mapenzi ndio iliyowapotosha wengi miongoni mwa Waislamu kwa kudhani kuwa mapenzi ya aina hii, ni mapenzi yenye uhusiano na Imani.

Moja miongoni mwa misingi mikuu ya Imani ya Dini yetu ni kumpenda mtume wetu Muhammad (صلي الله عليه وسلم) kuliko tunavyozipenda nafsi zetu na ukimuuliza Muislamu yeyote duniani atakuthibitishia mapenzi makubwa aliyonayo kwa kipenzi chetu Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم), lakini tunatofautiana katika uelewa wa jinsi ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) kwa mujibu wa tafsiri tulizozitaja hapo juu.

Wapo miongoni mwetu ambao ukimtaja tu Mtume (صلي الله عليه وسلم) anaweza kububujikwa na machozi kwa hisia kali alizonazo juu ya Mtume wetu (صلي الله عليه وسلم), mwengine atatoa sauti kali ya kumtakia rehma na amani Mtume (صلي الله عليه وسلم) kwa kusema kwa vishindo ‘Allaahumma salim alee’, au wengineo waliozuka siku hizi na kuleta itikadi yao ya kutukana Maswahaba, utawakuta anapotajwa Mtume, huitikia kwa vishindo ‘Allaaaahumma Swaliii ‘alaa Muhammad wa aaaali Muhammad’ lakini ndio hao hao wanautukana wake zake na Maswahaba zake!! Na si ajabu ukawakuta watu hao pamoja na mapenzi makubwa wanayoyaonyesha kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) hawatimizi Swalah tano kwa siku, wake zao na mabinti zao hawajisitiri, wana vimada nje, nyumba zao zimejaa taarabu za rusha roho, zimepambwa na vinyago na mapicha, wavuta sigara, wala mirungi, wakaa mabarazani kusengenya, panapoaziniwa na kukimiwa hawasimami kwenda kuswali na Waislam,  achilia mbali kupuuza kwao baadhi ya Sunnah muhimu kama vile kufuga ndevu n.k. Watu hawa wana mapenzi makubwa kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) lakini ni mapenzi ya aina gani ? je, haya ndio mapenzi ya kiimani?

Neno mapenzi katika Uislamu lina maana nzito sana, haifai kulichukulia kwa maana nyepesi nyepesi kwani lina uhusiano mkubwa na ‘Aqiydah ya Dini yetu; Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema katika Qur-aan:

(ومن الناس من يتخذ من دون اللــه أندادا يحبونهم كحب اللــه والذين آمنوا أشد حبا للــه) البقرة 165

“Na katika watu kuna wanaofanya waungu wasiyekuwa Mwenyezi Mungu, wanawapenda kama kumpenda, lakini walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana.” 2:165

Kumpenda Allaah (سبحانه وتعالى) ni katika alama za Tawhiyd, kama ilivyobainisha Aayah, na kumpenda Allaah (سبحانه وتعالى) ndio msingi wa kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم), huwezi kumpenda Mtume kabla hujatimiza mapenzi ya Allaah (سبحانه وتعالى) na huwezi kumpenda Allaah kwa kumkwepa Mtume (صلي الله عليه وسلم).

VIGEZO VYA KUMPENDA MTUME (صلي الله عليه وسلم)

1. KUTHIBITISHA SHAHADA YA UTUME WAKE

Ni kuthibitisha utume wa Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم) kuwa ni mjumbe aliyetumwa kwa waja wote, kuthibisha kivitendo yote aliyoyaamrisha, na kujiepusha na yote aliyoyakataza na kuyakemea, kwa maana nyingine ni kumuabudu Allaah (سبحانه وتعالى) kama Alivyofundisha na kuelekeza Mtume, na Allaah Anathibitisha hayo kwa kusema:

(قل إن كنتم تحبون اللــه فاتبعوني يحببكم اللــه ويغفر لكم ذنوبكم واللـه غفور رحيم) العمران 31

“Sema, ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni, Mwenyezi Mungu Atakupendeni na Atakughufirieni madhambi yenu” 3:31

Allaah Anathibitisha kuwa, ili mja awe na Tawhiyd iliyokamilika ya kumpenda Allaah, basi ni lazima amfuate Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم) na ndio kisha Allaah Atampenda mja huyo na kumsamehe. Hivyo basi, mapenzi ya kweli yanakuwa kwa kumfuata Mtume (صلي الله عليه وسلم) katika yote aliyokuja nayo na kumtii na ndipo Allaah Atampenda mja huyo, na atakayebahatika kupendwa na Allaah (سبحانه وتعالى) hakika huyo amefaulu kufaulu kulikokuwa kukubwa.

2. KUMUIGA MTUME (صلي الله عليه وسلم)

Mapenzi ya kweli ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) yanakuwa ni kwa kumuiga kwa yote aliyokuja nayo, kumuiga katika tabia zake, katika maisha yake, katika nyumba yake, katika ibada zake, katika mahusiano yake na majirani, na katika maisha yake kwa ujumla, kama alivyotuambia Allaah (سبحانه وتعالى)

لقد كان لكم في رسول اللــه أسوة حسنة لمن كان يرجو اللــه واليوم الآخر وذكر اللــه كثيرا) الأحزاب 21

“Bila shaka mnao mfano mwema kwa mtume wa Mwenyezi Mungu kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na kumtaja Mwenyezi Mungu sana.” 33:21

Kumuiga Mtume na kumfanya kuwa ruwaza njema ndio mapenzi ya dhati ya kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم), lakini kumpenda mtume kwa kumsifu tu, na akawa hana nafasi katika maisha yako na maisha ya familia yako, basi huko si kumpenda bali ni kujifanya kumpenda na inawezekana ikawa ni kumcheza shere.

Katika Hadiyth iliyopokelewa na ‘Abdu-Rahmaan bin Quraad (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa “Mtume (صلي الله عليه وسلم) alikuwa anatawadha, na Maswahaba wakaanza kukinga maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka katika wudhuu wa Mtume (صلي الله عليه وسلم) na wakijifutia katika miili yao kutafuta baraka za wudhuu ule kutoka kwa Mtume, Mtume (صلي الله عليه وسلم) akawauliza; “kwa nini mnafanya hivi? Wakasema; ni kwa ajili ya kumpenda Allaah na Mtume Wake, Mtume (صلي الله عليه وسلم) akawaambia, anayetaka kumpenda Allaah na Mtume Wake, au kupendwa na Allaah na Mtume Wake, basi aseme ukweli anapozungumza, na atekeleze amana yake anapoaminiwa, na awe jirani mwema kwa jirani yake” Al –Albaaniy ‘Mishkaatul Maswaabiyh

Mtume (صلي الله عليه وسلم) anawaelekeza Maswahaba zake, na ndio anatuelekeza sisi jinsi ya kumpenda mapenzi ya kweli, mapenzi yenye tija na yenye kuleta mabadiliko katika tabia za mja, Mtume alikuwa anawaelekeza Maswahaba kuwa kumpenda kwa kugombea maji yake ya wudhuu peke yake ili kupata baraka, hakutoshi, na kutakuwa hamna maana kama watu hao watakuwa waongo katika mazungumzo yao, hawatekelezi amana zao, wanaudhi majirani zao, mapenzi hayo ya kutafuta baraka tu na kuacha kumfuata Mtume (صلي الله عليه وسلم) yatakuwa ni mapenzi ya kumcheza shere Mtume (صلي الله عليه وسلم).

3. KUMFANYA HAKIMU KATIKA MIZOZO YOTE

Na katika dalili za kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni kumfanya hakimu katika mizozo yetu yote, na kuridhika na hukmu yake, na katika zama tulizonazo ambazo Mtume (صلي الله عليه وسلم) hayupo nasi, basi Qur-aan na Sunnah zake ndizo zitakazotumika katika kutatua mizozo yetu, na Allaah (سبحانه وتعالى) anatuambia katika Qur-aan:

(فلا وربك لا يؤمنون حتى يحكموك فيما شجر بينهم ثم لا يجدوا في أنفسهم حرجا مما قضيت ويسلموا تسليم) النساء 65

“Naapa kwa (haki ya) Mola wako. Wao hawawi wenye kuamini (kweli kweli) mpaka wakufanye hakimu katika yale wanayokhitalifiana, kisha wasione uzito nyoyoni mwao juu ya hukumu uliyotoa, na wanyenyekee kabisa” 4:65

Katika kutafsiri Aayah hii, Imam Ibnul Qayyim katika kitabu chake cha Sharhu Al-Manaazil anasema kuwa Aayah ii imekusanya ngazi tatu za Dini, amabzo ni: UISLAM, IYMAAN, NA IHSAAN, na atakayeikanusha na kuacha kuitekeleza basi atakuwa amekanusha ngazi zote za Dini.

Jambo la kuhuzunisha ni kuwa, Waislamu tulio wengi ambao tunasema tunampenda Mtume (صلي الله عليه وسلم), haturudi kwa Mtume katika kutatua mizozo yetu, bali kila mtu, kila kundi linarudi kwa sheikh wake, kwa madh-hab yake au kwa kutumia ra’aiy zao, na unapotoa ushahidi wa kauli ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) kuhusu suala lenye mzozo basi unaweza kuambiwa mbona Imaam ash-Shaafi’iy, au Maalik kasema hivi, na mtu huyu huyu anapotajwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) humtakia rehma kwa kishindo kudhihirisha mapenzi yake kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) na unapochelewa wewe kumtakia rehma Mtume basi hudiriki kukutuhumu kuwa humpendi Mtume (صلي الله عليه وسلم).

Katika Aayah nyingine Allaah Anasema:

( فإن تنازعتم في شيء فردوه الى اللــه والرسول إن كنتم تؤمنون بالله واليوم الآخر) النساء 59

“Na kama mkikhitalifiana katika juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho” 4:59

Aidha Allaah Anatuamrisha katika Aayah nyingine kurejesha mizozo yetu Kwake na kwa Mtume, lakini asilimia kubwa ya Waislamu hawaitekelezi Aayah hii, na kwa bahati mbaya hata wale wanaojinasibisha kutetea Sunnah za Mtume (صلي الله عليه وسلم) na mwenendo wa As-Salaf As-Swaalih baadhi yao wameshindwa kuitekeleza Aayah hii, na wanaona bora kuhukumiwa na mahakama za kitwaaghuut kuliko kukaa na kuyamaliza matatizo yao kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.

Hali ya Ummah inahuzunisha, wako wanaotosheka kumsifu tu Mtume (صلي الله عليه وسلم) na kuridhika kuwa wameonyesha mapenzi yao kwa Mtume (صلي الله عليه وسلم), huku wakipinga Sunnah zake zizlizo dhaahir kwa utashi tu wa nafsi zao, na kuwatanguliza masheikh wao, na wakati mwingine kwa ajili tu ya kuwaonyesha Waislamu wenzao ukaidi wao na ubishi wao wa ushindani.

Bado hatumtendei haki Mtume wetu (صلي الله عليه وسلم), bado hatujafikia daraja ya kumpenda kwa dhati kuliko nafsi zetu, kuliko maslahi yetu, kuliko masheikh zetu, kuliko wafuasi wetu, na kuliko majina ya Taasisi na makundi yetu.

Allaah (سبحانه وتعالى) Anawasifu waumini wa kweli kwa kusema:

(إنما كان قول المؤمنين إذا دعوا الى اللــه ورسوله ليحكم بينهم أن يقولوا سمعنا وأطعنا وأولئك هم المفلحون) النور 51

“Haiwi kauli ya Waislamu wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu baina yao, ila kusema “Tunasikia na tunakubali, na hao ndio watakaofuzu” 24:51

4. KUTOTANGULIZA JAMBO MBELE YAKE, NA KUINAMISHA SAUTI

Katika kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni kutotanguliza jambo lako, au rai yako, au kauli ya sheikh wako, au madh-hab yako, mbele ya kauli ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) na kutonyanyua sauti yako, na fikra zako mbele ya mafundisho ya Mtume (صلي الله عليه وسلم), katika uhai wake na hata baada ya kifo chake (صلي الله عليه وسلم), kwa kuheshimu mafundisho yake na kuyaweka mbele na juu ya mafundisho yote, na kutonyanyua sauti yako juu ya kauli na hukmu ya Mtume (صلي الله عليه وسلم).

Siku moja Imaam Ash-Shaafi’iy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijiwa na mtu na akamuuliza mas-ala katika mas-ala ya Dini, Imaam akamwambia kuwa Mtume (صلي الله عليه وسلم). Amesema kadha, na akamsomea kipengele cha Hadiyth ya Mtume (صلي الله عليه وسلم). Yule muulizaji akamuuliza tena Imaam Ash-Shaafi’iy; na wewe Imaam unaonaje? Imaam Ash-Shaafi’iy akakasirishwa sana na yule mtu, na akamwambia, je unaniona mimi nipo kanisani hapa? Nakwambia amesema Mtume (صلي الله عليه وسلم) kadha unaniuliza rai yangu? Huku ndio kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ukweli wa kumpenda.

5. KUWAPENDA NA KUWAHESHIMU WATU WA FAMILIA YAKE

Kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni kuipenda familia yake, wakiwemo wake zake na kuwapenda Maswahaba zake, huwezi kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) na ukawa unawachukia wakeze na Maswahaba zake, bali kwa kuwachukia wake za Mtume na Maswahaba zake utakuwa unamchukia Mtume mwenyewe, na ukiwatukana utakuwa umemetukana Mtume mwenyewe

6. KUTOMSIFIA KWA SIFA ASIZOSTAHIKI

Kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) hakuwi kwa kumsifia kwa sifa ambazo hastahiki, au ambazo zimepetuka mipaka ya utume wake. Wapo Waislamu ambao wanadai kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) na wanampachikia sifa ambazo zinakaribia kufikia sifa za Allaah (سبحانه وتعالى), na unapohoji juu ya uzushi huo na shirki hizo, basi utatuhumiwa kuwa wewe ni adui wa Mtume na humpendi.

Mtume (صلي الله عليه وسلم) alitabiri hali hii na akautahadharisha Ummah wake usije ukawa kama Manaswara waliomsifu ‘Iysaa bin Maryam mpaka wakamgeuza Mungu, Mtume (صلي الله عليه وسلم) Alisema:

(لا تطروني كما أطرت النصارى ابن مريم وإنما أنا عبد فقولوا : عبدالله ورسوله )

“Msinisifie kama walivyomsifu Manaswara ‘Iysaa bin Maryam hakika mimi ni mja, niiteni mja wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.”

Lakini pamoja na tahadhari hizo za Mtume (صلي الله عليه وسلم) bado baadhi ya Waislamu hawaoni kuwa wamempenda Mtume (صلي الله عليه وسلم) mpaka wamsingizie sifa ambazo hana, na baadhi yao wamefikia hata kubadilisha Aayah ya Qur-aan ili ikubaliane na upotofu wao, Allaah (سبحانه وتعالى) aliposema kupitia ulimi wa Mtume (صلي الله عليه وسلم) katika kuthibitisha kuwa Mtume ni binadamu kama binadamu wengine isipokuwa yeye huteremshiwa wahyi, alisema:

(قل إنما أنا بشر مثلكم يوحي إلي أنما إلهكم إله واحد ) الكهف 110

“Waambie, Bila shaka mimi ni binadamu kama nyinyi (isipokuwa nimeletewa wahyi tu ndio tofauti yangu). Ninaletewa wahyi ya kwamba Mungu wenu ni mungu mmoja tu.” 18:110

Wapotoshaji hao waliona wamkosoe Allaah kwa kumshusha cheo Mtume, wao wakaona waiandike upya Aayah ili isomeke…

قل إن ما أنا بشر مثلكم يوحي إلي …

Kwa maana, sema hakika mimi si binadamu mfano wenu…

Hii ni kufru ya wazi kabisa ambayo inafanywa kwa jina la kumpenda Mtume (صلي الله عليه وسلم).

Na wengine wanadai kuwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) anajua elimu ya ghayb na anajua lini itakuwa Qiyaamah, na kuwa Mtume (صلي الله عليه وسلم) ameumbwa kutokana na nuru ya Allaah, kama isemavyo kauli inayonasibishwa na ‘Abdul-Qaadir Al-Jaylaaniy katika kitabu cha ‘Sirru Al Asraar’ anasema: “Elewa Allaah Akuwafikishe kwa Anachokipenda na kuridhia, Allaah Aliumba roho ya Muhammad kwanza kutokana na nuru yake na uzuri wake, kama alivyosema Allaah: Nimeumba roho ya Muhammad kutokana na nuru ya uso wangu…”

na huo ni uongo dhaahir na kumsingizian Allaah ambacho Hajakisema.

Aidha wanadai kuwa siku ya kuzaliwa kwake Mtume (صلي الله عليه وسلم) ni siku bora kuliko hata usiku wa Laylatul Qadr, na wanadai kuwa roho ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) huhudhuria katika maulidi na huwa anazungumza na mawaliiy.

Kwa ujumla, mambo mengi yamezushwa katika Dini hii kwa kumzushia Mtume (صلي الله عليه وسلم) mambo ambayo mengine tumeshindwa kuyaandika katika safu hii kutokana na kutunza heshima ya kipenzi chetu Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم)

Ndugu zangu Waislamu, tumpende Mtume (صلي الله عليه وسلم) ukweli wa kumpenda, tumuingize katika maisha yetu, awe ni kiongozi wetu, ruwaza yetu, mshauri wetu, hakimu wetu, mwalimu wetu, tuyafundishe mafundisho yake kwa walimwengu wote, na tuuthibitishie ulimwengu kuwa, Mtume Muhammad (صلي الله عليه وسلم) ni Mtume aliyetumwa kwa watu wote na ni rehma kwa walimwengu wote.

Tunayo Dhimma kubwa ya kuhakikisha kuwa mafunzo ya Mtume (صلي الله عليه وسلم) yanafahamika vyema kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu, na njia nyepesi ya kufanikisha hilo ni sisi wafuasi wa Mtume (صلي الله عليه وسلم) kumpenda Mtume wetu ukweli wa kumpenda, na kuyaingiza mafundisho yake katika maisha yetu ya kila siku

 

………………………………………………….

Mjue Mtume Wako صلى الله عليه وآله وسلم Vizuri Uzidi Kumpenda

بسم الله الرحمن الرحيم

www.alhidaaya.com

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad,

Tumeona juhudi nyingi zinazofanywa na makafiri katika nyakati mbalimbali za kumtia kasoro na kumdhalilisha Mtume wetu mpenzi صلى الله عليه وآله وسلم bila shaka Muislamu yeyote anaathirika sana na kupata machungu na maudhi ya kutukanwa kipenzi chetu. Pamoja na kuwa mashambulizi ya kumtia dosari yamefanywa na yanaendelea kufanywa kila kukicha, lakini kila mashambulizi hayo yanapotokea, ndipo hisia na mapenzi ya Waislam wengi yanapofumuka zaidi na kuimarika kwa kipenzi chao Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم .

Matukio ya kutukanwa Mtume wetu na kudhalilishwa na kutuhumiwa, hayakuanza leo na hayakuanza kwake, ni kama vile wakati aliposingiziwa Mama wa Waumini ‘Aaishah رضي الله عنها na wanafiki wa Madiynah wakiongozwa na ‘Abdullaah bin Saluul aliyemsingizia uovu Mama wa Waumini ‘Aaishah رضي الله عنها katika kisa cha Ifk (uzushi/uongo) ambacho kilisababisha kuteremshwa Aayah tukufu za kumsafisha na uzushi huo muovu kuwa ametembea na Swahaba Swafwaan bin Al-Mu’attwal. Na hizo aya tokea siku zilizoteremshwa zama hizo zinasomwa hadi  leo, na zitaendelea kusomwa kila mahali, Misikitini, nyumbani, nyoyoni mwa Waislamu mpaka siku ya Qiyaamah kumsafisha Bibi ‘Aaishah Mama wa Waumini katika sifa chafu na ovu aliyozuliwa nayo na ambayo hadi sasa kuna wengi bado wanamtukana na hali wanadai wao ni Waislam. Katika tukio hilo Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

((إِنَّ الَّذِينَ جَاؤُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ وَالَّذِي تَوَلَّى كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ)) 

((Hakika wale walioleta uongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa)) [An-Nuur: 11]

Kutokana na mafundisho hayo tuliyoyapata kutokana na kisa cha kusingiziwa mama wa waumini, nasi tunaamini kuwa kumepatikana kheri mbalimbali kwa tukio hili la kudhalilishwa Mtume wetu mpenzi صلى الله عليه وآله وسلم. Tumeona jinsi Waislam walivyoungana katika tumkio hilo na kugomea kununua bidhaa za hao Makafiri na pia kuandamana, kuandika barua kwa viongozi wao na mengi mengine ambayo yamesababisha khasara kubwa za mali kwa hao makafiri na pia kusheheneza khofu katika nafsi zao hadi sasa hivi wanatapatapa hawajui la kufanya! Na hayo ndiyo mapenzi ya dhati na umoja wa kweli. Hakika kwa uchache tumeonyesha jinsi tunavyompenda kipenzi chetu na jinsi tunavyoithamini dini yetu. Na bila shaka kungepatikana khasara kubwa kwa hao makafiri kama viongozi wa nchi za Waislam wangekuwa na misimamo thabiti na mikali zaidi katika tukio hili! Basi na tuzidi kumtambua huyu kiumbe bora kabisa umuhimu wake kwetu, tabia zake na wema wake ili tuzidi kuongeza mapenzi yetu kwake.

Hakuna sentensi itakayoweza kuelezea mema aliyokuja nayo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na nafasi yake katika ulimwengu huu na athari zake ambazo hazitoweza kufutika hadi siku ya mwisho.

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

((لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ))

 

((Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho)) [Al-Ahzaab: 21]

UMUHIMU WAKE KWETU

1.     Mtume wa mwisho Waislamu tunaamini mitume yote walioletwa kabla na ujumbe wa Allaah سبحانه وتعالى tokea Adam عليه السلام hadi ‘Iysa عليه السلام kisha ndio Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye katumwa kwa ajili ya Umma huu wa Kiislamu tunaojifakharia nao. Hakuna tena baada yeye Mtume mwingine atakayekuja hadi siku ya Qiyaamah, na Qur-aan ndio kitabu cha mwisho kabisa ambacho kimekamilisha vitabu vyote vya nyuma vilivyoteremshwa mbinguni na Mitume yake.

2.    Wa kwanza atakayefufuliwa kutoka kaburini siku ya Qiyaamah.

3.    Wa kwanza atakayevuka As-Swiraat.

4.    Wa kwanza atakayeingia peponi na sisi Umma wake tutafuatia kabla ya Umma nyingine zote.

5.    Ameletwa kama ni Rahma kwa ulimwengu wote.

6.    Hatajwi jina lake ila anaswaliwa (anaombewa rahma).

7.    Swalah zetu hazitimii ila baada ya kumtaja yeye kwa kumswalia.

8.    Amekuja na miujiza mikubwa, kama Qur-aan, Israa Wal-Mi’iraaj na miujiza mingi mingine tunayoisoma katika Siyrah yake.

9.    Imaam wa Mitume yote.

10.           Amefutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia na ya mbele yake.

11.           Ni Mtume pekee atakayeweza kutuombea siku ya Qiyaamah. Atakapokuwa amesujudu chini ya ‘Arshi Ataambiwa: “Ewe Muhammad! Inua kichwa chako na omba unalotaka utapewa”. Atasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم “Umma wangu, Umma wangu, Ewe Mola Umma wangu”

12.           Allaah سبحانه وتعالى na Malaika Wake wanamswalia.

13.           Kumuona kwake katika ndoto ni kumuona hakika.

14.           Baina ya nyumba yake na Minbar yake ni kipande cha pepo ‘Rawdhatul-Jannah’.

15.           Amepewa Al-Kawthar (Mto wa peponi).

16.           Aliyepata wafuasi wengi kuliko Mitume yote mingine.

17.           Kiumbe bora kabisa na bwana wa mwanzo na wa mwisho.

18.           Kwa sababu ya heshima kubwa Aliyopewa na Allaah سبحانه وتعالى ni Mtume pekee asiyetajwa au kuitwa kwa jina lake katika Qur-aan, wengine wote wametajwa au kuitwa kwa majina yao.

19.           Amepewa wasila na fadhila na makazi matukufu Peponi.

20.           Siku ya Qiyaamah, watakapokanusha watu wa Mitume ya nyuma kuwa Mitume yao hawakuwafikishia ujumbe, Umma wake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم (Sisi Waislamu) utashuhudia  kuwa Mitume wamefikisha ujumbe wao kutokana na dalili tuliyoipata katika Qur-aan.

TABIA ZAKE

Na si mwengine aliyemsifia kiumbe hiki bali ni Mwenyewe Mola Mtukufu Muumba wa mbingu na ardhi kwa kusema:

((وَإِنَّكَ لَعَلى خُلُقٍ عَظِيمٍ))

((Na hakika wewe una tabia tukufu)) [Al-Qalam: 4]

Swahaba Sa’ad bin Hishaam alipomuuliza Mama wa Waumini ‘Aaishah رضي الله  عنها kuhusu tabia yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alijibu:

كان خلقه القرآن. ألست تقرأ القرآن (( وَإِنَّكَ لَعَلى خُلُقٍ عَظِيمٍ )) أبي داود والنسائي

Tabia yake ilikuwa ni Qur-aan, kwani husomi katika Qur-aan ((Na hakika wewe una tabia tukufu?)) [Abu Daawuud na An-Nasaaiy]

Jina lake pekee linatosha kuelezea tabia zake kwani Muhammad maana yake ni “Mwenye kusifiwa”.

Kwa hiyo bila shaka anamiliki tabia njema zilizokamilika ambazo hakuna mtu yeyote mwingine aliyemiliki, ni cheo cha daraja ya juu kabisa hakuna atakayeweza kufikia.

Khuluqa yake ya mwanzo iliyojulikana kabla ya kupewa utume ni ukweli na uaminifu hata akapewa jina na kujulikana kwa kuitwa ‘Asswaadiqul-Amiyn’ (Mkweli Muaminifu).

Alikuwa mpole, mwenye huruma kwa kila mtu hata kwa walio dhaifu kama masikini. Upole wake haukuwa kwa binaadamu tu bali hata kwa wanyama. Alikuwa mwenye bashasha, mkarimu, mvumilivu wa maudhi yanayomfika, alipokuwa akinyanyaswa alikuwa mwepesi wa kusamehe hata kama ni kutoka kwa mtu mjeuri kabisa na ingawa alikuwa ana uwezo wa kulipiza.

Hajapata hata siku moja kutukana au kutamka maneno mabaya. Mazungumzo yake yote yalikuwa ni ya maana yenye kufahamika.

Ni mwenye heshima, mwenye haya, hata ilibidi wakati mwingine kwa shida ya haya zake ilibidi Allaah سبحانه وتعالى Amsemee badala yake, kama siku ya harusi yake na Bibi Zaynab bint Jahsh wakati Maswahaba walibakia kuzungumza baada ya karamu naye alikuwa anataka kupumzika na mkewe:

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَى طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ إِنَّ ذَلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ وَاللَّهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ))

 

((Enyi mlioamini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapoitwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu Hastahi kwa jambo la haki)) [Al-Ahzaab: 53]

UNYENYEKEVU WAKE

Alikuwa mnyenyekevu kabisa, akichanganyika na kila mtu akiwa Mwarabu au kabila lolote ikiwa ni mweupe au mweusi akiwa ni tajiri au masikini, watu wazima au watoto, hata watoto alikuwa akiwasikiliza na kuzungumza nao. Akicheza na vijukuu vyake na kuwaachia hata wakati akiswali wakimpandia juu ya mgongo wake.

Hakuwa akivaa nguo za fakhari za kumtambulisha utukufu wake au kumtofautisha na Maswahaba zake, wala hakuwa anaishi katika nyumba ya fakhari, wala kumiliki fenicha au vitu vya fakhari. Kitanda chake kilikuwa cha kamba.

Hakuwa na matamanio ya dunia, alikinaika nayo. Hima yake kubwa ilikuwa ni akhera tu. Siku moja aliingia ‘Umar رضي الله عنه nyumbani kwake akasema ‘Umar: “Sikuona chochote cha kutazama” nikasema: “Muombe Mola wako kwani Allaah Amewafungulia wafursi na warumi na Amewapa dunia (mali) na wao hawamuabudu Allaah”. Akasema:

((Una shaka ewe Ibnul-Khatwaab, hao ni watu waliotanguliza mapambo katika maisha yao ya dunia)).

Pia alikuwa akisema:

((ما لي وللدنيا، ما أنا في الدنيا إلا كراكب استظل تحت شجرة، ثم راح وتركها)) صحيح سنن الترمذي

((Mimi na dunia ni wapi na wapi? Mimi si katika dunia ila kama mfano msafiri aliyepumzika chini ya mti, kisha akaondoka na kuuacha)) [Sunan At-Tirmidhiy].

Nyumbani kwake ilikuwa inawezekana kupita siku tatu bila ya moto wa kupikia chakula kuwashwa, ilikuwa ni kula tende na maji tu.

Alikuwa akitoa sadaka bila ya kukhofu umasikini, hata alipofariki hakuwa na chochote cha kumiliki wala dirham wala dinaar [Al-Bukhaariy]

Hakujiona kuwa ni mtu bora kuliko Maswahaba na juu ya kwamba ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa haamui jambo peke yake bila ya kuchukua ushauri kwa Maswahaba zake.

UHUSIANO WAKE NA WATU WA NYUMBANI KWAKE

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa ni mpole kwa ahli zake na  akimpa kila mmoja haki yake. Anapokuwa na wake zake hukaa nao na kuzungumza nao na kucheka nao, akicheza na mkewe Bibi ‘Aishah رضي الله عنها kama wakati mmoja alifanya naye mashindano ya kukimbia, mara nyingine alimbeba mgongoni ili atazame wanaume waliokuwa wakicheza mchezo wa vita msikitini.  Unapofika wakati wa Swalah huondoka ili kutimiza ibada hivyo kumpa Mola wake haki Yake, na alikuwa akimpa kila mtu haki yake.

Hakuwa mwenye makuu katika chakula, akila chochote alichopikiwa bila ya kulalamika.

Akisaidia kazi za nyumba kama kufagia na usafi mwingine. Hata na mfanya kazi wake alikaa naye kwa vizuri wala hakuwahi kumkaripia hata siku moja.

HEKIMA ZAKE

Alikuwa mwenye hikma katika kila hali. Anapokabiliwa na mambo mawili alikuwa akichagua lile lililokuwa jepesi maadam tu halikuvuka mipaka ya Allaah سبحانه وتعالى.

Hakujali kutoa hukumu kwa mtu yeyote hata kama ni mwanawe mpenzi maadam ni mkosa, alisema:

((والذي نفس محمد بيده ، لو أن فاطمة بنت محمد سرقت لقطعت يدها)) البخاري

((Naapa kwa Yule Ambaye Nafsi ya Muhammad iko katika mikono yake (Allaah)! Ikiwa Faatimah mtoto wa Muhammad ameiba basi nitamkata mkono wake)) [Al-Bukhaariy]

Bedui mmoja alikwenda msikitini akasimama kukojoa, Maswahaba walitaka kumkatiza na walikuwa tayari kumvamia, lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwakataza na akamuacha amalize haja yake, alipomaliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimuambia:

((إن هذه المساجد لا تصلح لشيء من هذا البول ولا القذر، إنما هي لذكر الله وقراءة القرآن)) رواه مسلم

((Msikiti huu haufai kukojolewa au kuchafuliwa bali ni kwa ajili ya kumkumbuka Allaah na kusoma Qur-aan)) [Muslim]

Maelezo hayo ni mtazamo mdogo tu kutoka katika mwanga mkubwa wa utume wake Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم. Lau kama ni kuelezea yote basi ingelihitaji vitabu na vitabu kuandikwa. Na sio sisi tu Waislamu tuliyemtambua kwa tabia zake hizo bali hata makafiri wangapi waliosoma wasifu wake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم walikubali kuwa hakika Muhammad alikuwa ni bwana wa tabia na ni mtu wa aina ya pekee aliyekamilika kwa kila upande wa sifa.

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atuzidishie mapenzi kwa Mtume wetu صلى الله عليه وآله وسلم na tuwe wenye kufuata tabia na nyendo zake hata tuweze kuwa karibu naye Peponi kama alivyosema mwenyewe:

عن جابر رضي اللَّه عنه أَن رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال : (( إِن مِنْ أَحَبِّكُم إِليَّ ، وَأَقْرَبِكُمْ مِنِّي مَجلساً يَومَ القِيَامَةِ ، أَحَاسِنَكُم أَخلاقا)(( الترمذي حديث حسن

 

Imetoka kwa Jaabir رضي اللَّه عنه kwamba Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم amesema: (Hakika walio vipenzi kwangu na watakaokuwa karibu na mimi siku ya Qiyaamah ni wale wenye tabia njema)) [At-Tirmidhiy – Hadiyth Hasan]

………………………………………..

Tukio la Israa Na Mi’iraaj

Imekusanywa na Ummu ‘Abdillaah

Kutoka katika Vitabu Zaadul Ma’ad na Ar-Rahiyqul Makhtuum

Kutokana na umuhimu wa tukio hili ambalo Allaah سبحانه وتعالى Kalielezea katika Kitabu Chake Kitukufu pale Aliposema:

“Ametakasika Aliyemchukua mja Wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona” [Al-Israa: 1]

na ni Mu’ujizah mkubwa kabisa wa Nabii yetu kipenzi صلى الله عليه وآله وسلم baada ya Mu’ujizah wa Qur-aan Tukufu, kuna haja ya kukieleza tena japo kimekwishaelezwa na kuandikwa na wengi.

Tukio hili adhimu, limeelezwa na wanahistoria kwa kauli mbalimbali wakati hasa lilipotukia:

1.      Inasemekana Israa ilikuwa katika ule mwaka ambao Allaah سبحانه وتعالى Alimkirimu ndani yake Utume, Ameichagua kauli hii Atw-Twabariy.

2.    Inasemekana Israa ilikuwa baada ya kupewa Utume kwa miaka mitano, Kauli hii imepewa nguvu na Al-Nawawiy na Al-Qurtwubiy.

3.    Inasemekana Israa ilikuwa usiku wa ishirini na saba katika mwezi wa Rajab, Mwaka wa kumi wa Utume, Kauli hii imepewa nguvu na mwanachuoni mkubwa Al-Mansuur Forty.

4.    Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa miezi kumi na sita yaani katika mwezi wa Ramadhaan mnamo mwaka wa kumi na mbili wa Utume.

5.    Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja na miezi miwili yaani Muharram mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.

6.    Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja yaani Rabi’u Ath-Thaaniy mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.

Kauli tatu za mwanzo zimepingwa kwa sababu Mama wa Waumini Khadiyjah رضي الله عنها alifariki mwezi wa Ramadhaan mwaka wa kumi wa Utume na kifo chake kilitokea kabla ya kufaradhishwa kwa Swalaah tano na hakuna tofauti kuwa Swalaah tano zilifaridhishwa katika usiku wa Israa. Ama kuhusu kauli tatu zilizobaki hakikupatikana kile ambacho kingetumika kutia nguvu moja katika kauli hizo isipokuwa mtiririko wa Surat Al-Israa, Ambao unafahamisha kuwa Israa ilichelewa sana. Wanachuoni wa Hadiyth wamepokea ufafanuzi wa tukio hili na hapa chini tunauleta kwa ufupi katika maneno yafuatayo:

Ibn Al-Qayyim amesema; “Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم, kwa kauli sahihi, alipelekwa kimwili akiwa amempanda Buraaq, akifuatana na Jibriyl عليه السلام kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Baytul Al-Maqdis, akamfunga Buraaq katika kikuku cha mlango wa Msikiti, Na kisha kuswali pamoja na Mitume, Yeye akiwa Imaam. Baada ya hapo, usiku huo huo kutoka Baytul Al-Maqdis akapandishwa katika uwingu wa Dunia akifuatana na Jibriyl عليه السلام aliyekuwa akibisha hodi kwa ajili yake, akafunguliwa na huko akamuona Aadam عليه السلام baba wa watu wote, akamsalimia, akamkaribisha na akamjibu salaam yake na akaukubali Utume wake. Allaah سبحانه وتعالى Akamuonyesha roho za watu wema zikiwa upande wake wa kuume na roho za watu waovu zikiwa upande wake wa kushoto. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa pili, Jibriyl عليه السلام akaomba kuingia, akafunguliwa na hapo akamuona Yahya bin Zakariya na ‘Iysa bin Maryam عليهما السلام, akakutana nao, akawasalimia, na wao wakamjibu salaam yake, Wakamkaribisha na kisha wakaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa mpaka uwingu wa tatu, hapo akamuona Yuusuf عليه السلام, akamsalimia, naye akamjibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa nne ambako alimkuta Idriys عليه السلام, akamsalimia, naye akamjibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa uwingu wa tano, Na hapo akamuona Haaruun bin ‘Imraan عليه السلام, akamsalimia, naye akajibu salaam yake na kumkaribisha na kuukubali Utume wake.

Baada ya hapo akapandishwa katika uwingu wa sita na akamkuta hapo Muusa bin Imraan عليه السلام, akamsalimia, naye akajibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Alipompita, Muusa عليه السلام alilia na alipoulizwa ni jambo gani linalimliza? Akajibu, “Ninalia kwa sababu kijana amepewa Utume baada yangu, Na katika Ummah wake wataingia peponi kuliko watakaoingia peponi kutoka katika Ummah wangu.” Kisha akapandishwa kwenye uwingu wa saba, ambako alikutana na Ibrahiym عليه السلام, akamsalimia naye akajibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo ndipo akanyanyuliwa na kupelekwa Sidratul-Muntahaa, Kisha akanyanyuliwa hadi Baytul Ma’amuur, naye akapandishwa kupelekwa kwa Allaah Mwingi wa Utukufu, Akasogea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم mpaka umbali wa kiasi cha masafa ya Qawsayn (pinde mbili) au karibu zaidi kuliko hivyo, Allaah سبحانه وتعالى Akayafunua kwa Mja wake yale Aliyoyafunua, Na Akamfaradhishia Swalaah Khamsini. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Akazipokea na kuanza kurejea mpaka alipofika mahali alipo Muusa عليه السلام ambaye alimuuliza; “Umepewa amri ya jambo gani? Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akamueleza, “Ameniamrisha Swalaah Khamsini”, Muusa عليه السلام akamwambia, “Kwa hakika Ummah wako hawataweza kutekeleza jambo hilo, Rejea kwa Mola wako na umuombe Akupunguzie iwe takhfifu kwa Ummah wako”. Akageuza uso na kumuangalia Jibriyl عليه السلام kwa jicho la kumtaka ushauri katika jambo hilo, naye akampa ishara ndio kama ukitaka. Akapanda naye Jibriyl عليه السلام mpaka akafika kwa Allaah سبحانه وتعالى na hali ya kuwa Yeye Yu Mahali Pake; (Tamko hili ni la Al-Bukhaariy). Katika mapokezi mengine, Akampunguzia Swalaah kumi kisha akateremshwa mpaka mahali alipokuwa Muusa عليه السلام na akamueleza idadi ya Swalaah zilizopunguzwa. Muusa عليه السلام akamwambia, “Rejea kwa Mola wako na umuombe Akupunguzie tena. “Inasemekana kuwa hakuacha kwenda na kurudi kwa Muusa عليه السلام na Allaah سبحانه وتعالى mpaka Swalaah zikabaki tano. Muusa عليه السلام akamtaka arejee kwa Allaah tena na kuomba kupunguziwa, Hapo Mtume akajibu; “Kwa hakika ninamuonea hayaa Mola wangu na sasa mimi ninaridhia na ninakubali Swalaah nilizopewa.” Alipokwenda umbali kidogo, Alilingania mlinganiaji; “Nimezipitisha faradhi Zangu na nimewapunguzia waja Wangu.”

Ibnul Qayyim amejadili kuhusu suala hili la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kumuona Mola wake, Allaah Aliyetukuka mwenye Utukufu na kisha akayataja maneno ya Ibn Taymiyah kuhusu suala hili. Matokeo ya utafiti ni kuwa, “Kumuona Allaah سبحانه وتعالى kwa macho ni jambo ambalo halikuthibiti kabisa. Hiyo ni kauli ambayo haikusemwa na yeyote katika Maswahaba. Na kile tunachokisema kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimuona Allaah سبحانه وتعالى moja kwa moja. Ni kuwa alimuona kwa moyo si kwa macho, Kauli ya kwanza haipingani na ya pili.” Kisha akasema: “Ama kuhusu kauli yake Allaah سبحانه وتعالى katika Suratu An-Najm (53: 8).

“Kisha akakaribia (kwa Mtume) na akateremka.”

Huko siko kule kukaribia ambako kumetajwa katika kisa cha Al-Israa, Kwani kukaribia ambako kumo katika Suratu An-Najm, “Ni kukaribia kwa Jibriyl عليه السلام na kusogea zaidi kama alivyosema Mama wa Waumini ‘Aaishahرضي الله عنها na Ibn Mas’uud رضي الله عنه. Mtiririko wa maneno unafahamisha juu ya maana haya; “Amekukaribia na kusogea sana.” Katika Hadiyth ya Al-Israa, Kuna maana kuwa kukaribia huko ni kukaribia kwa Mola Mtukufu Aliyetukuka na kuwa karibu kwake zaidi. Hakuna kupingana katika Surat An-Najm. Lakini kutajwa huko ndani yake ni kuwa yeye alimuona mara nyingine mbele ya Sidratul-Muntahaa, Na huyo ni Jibriyl عليه السلام.

Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم alimuona Jibriyl عليه السلام katika sura yake halisi mara mbili; ya kwanza hapa duniani na mara nyingine katika Sidratul-Muntahaa na Allaah سبحانه وتعالى Ndiye Mjuzi zaidi.

Lilituka lile tukio la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kupasuliwa tena kifua chake kwa mara ya pili. Kwa ujumla katika safari hii aliona mambo mengi; miongoni mwa hayo ni kule kuletewa maziwa na pombe na kuchagua maziwa badala ya pombe, Na pakasemwa, “Umeongozwa katika fitrah na umechagua na kupata fitrah, Ama kwa hakika laiti ungechukua pombe Ummah wako wote ungepotea, “Katika safari hiyo alionyeshwa mito minne huko peponi, Mito miwili iko nje na mito miwili iko ndani. Mito miwili iliyo nje ni mito ya Nail (Nile) na Furaat (Euphrates), Na maana ya mambo hayo ni kuwa ujumbe wake utafanya makazi yake katika majanga yenye rutuba katika Nail na Furaat na  watu wake ndio watakaokuwa wasimamizi wa da’awah ya Kiislaam, Kizazi baada ya kizazi, na si kuwa maji ya mito miwili hiyo yanachimbuka kutoka peponi.

Alionyeshwa Malaika muangalizi wa moto wa Jahannam ambaye hacheki, mwenye uso usio na furaha wala bashasha. Alionyeshwa pepo na moto. Alionyeshwa walaji wa mali za yatima kwa dhulma, Waliokuwa na midomo kama ya ngamia, Wanatupiwa midomoni mwao vipande vya moto kama mawe na kisha kutolewa katika tupu zao za nyuma.

Alionyeshwa walaji wa ribaa waliokuwa na matumbo makubwa yaliyowafanya wasiweze hata kuondoka mahala walipokuwepo. Alipita na kuwaona watu wa Fir’awn wakionyeshwa moto na hali wakipita wakiukanyaga.

Alionyeshwa wazinifu, Mbele yao kulikuwa na nyama iliyonona vizuri na pembeni mwao kulikuwa na nyama duni iliyooza yenye uvundo. Wakawa wanakula ile nyama duni iliyooza yenye uvundo, na wanaiacha ile nzuri iliyonona. Alionyeshwa wanawake wanaonasibisha waume zao watoto ambao si wao (watoto wa zinaa) hawa walikuwa wametundikwa kwa matiti yao. Na aliona msafara wa kibiashara wa watu wa Makkah wakati wa kwenda na wakati wa kurudi kwake, Na aliwafahamisha watu hao juu ya ngamia aliyewatoroka na alikunywa maji yao yaliyokuwa yamefunikwa na hali ya kuwa wao wamelala na kisha akakiacha chombo kikiwa kimefunikwa na jambo hilo ndilo likaja kuwa dalili (hoja) ukweli wa madai yake asubuhi ya usiku wa Israa.

Ibnul Qayyim alisema. “Kulipopambazuka Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم akiwa kwa jamaa zake aliwaeleza yote Aliyoonyeshwa na Allaah Mtukufu Mwenye Kushinda, Miongoni mwa miujiza Yake mikubwa. Makuraishi walipinga na hawakutaka kabisa kuamini khabari hizo. Katika kutafuta ukweli wa maelezo yake walimtaka awaeleze ulivyo Msikiti wa Baytul Al-Muqaddas. Kwa uwezo wake Allaah سبحانه وتعالى Akamdhihirishia hiyo Baytul Al-Muqaddas machoni mwake, akawa anawaelezea alama zake moja baada ya nyingine na wakashindwa kukanusha kwa vile alikuwa akiwaambia ukweli. Mwisho akawaeleza kuhusu ule msafara wa wafanyabiashara aliokutana nao wakati wa kwenda na kurudi; akawaeleza ni lini msafara huo unategemea kufika; akawaeleza kuhusu ngamia aliyeuongoza msafara huo, Na mambo yakatokea kama alivyowaeleza. Hata baada ya kujulishwa yote hayo Ma-Quraysh walizidi kukanusha na kukufuru. Abu Bakr رضي الله عنه ameitwa “Swiddiyq” ‘Msadikishaji’ kwa sababu ya kulisadikisha tukio hili.

Yapo maelezo mafupi na marefu yaliyokuja katika kueleza sababu ya safari hii. Ipo pia kauli ya Allaah سبحانه وتعالى Mwenyewe inatosha kabisa kueleza sababu ya safari hii, Pale Aliposema:

“Ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu” (17:1).

Na huu ni utaratibu wa Allaah سبحانه وتعالى kwa Mitume, Pahala pengine ndani ya Qur-aan Anasema:

“Na namna hivi Tulimuonyesha Ibraahiym ufalme wa mbingu na ardhi (kuwa ni wa Mungu), Na ili awe miongoni mwa wenye yaqini.” [Al-An’aam: 75].

Na Alisema kumwambia Muusa عليه السلام:

“Tukuonyeshe miujiza (mingine) mikubwa mikubwa.” [Twaahaa: 23].

Na ameweka wazi makusudi ya huko kuonyeshwa, “Ili awe ni miongoni mwa wenye yaqini.” Kwa hivyo ni wazi basi kuwa elimu ya Mitume katika kumjua Mola wao inatokana na kuiona kwa macho miujiza Yake na kwa njia hiyo kuwa na yaqini na Allaah سبحانه وتعالى kwa kiasi kisichokuwa na mfano. Ni ukweli ulio wazi kuwa jambo la kujionea si sawa na la kusikia, Na hii ndio sababu Mitume عليهما السلام walivumilia mengi katika njia ya Allaah سبحانه وتعالى mambo ambayo si rahisi kuvumiliwa na watu wa kawaida. Nguvu zote za kidunia mbele ya Mitume ni kama ubawa wa mbu hawatishiki nazo hata chembe, Hata wanapofanyiwa vitimbi na wakati mwingine kuteswa.

Bila shaka msomaji ataona kuwa katika suratul Israa Allaah سبحانه وتعالى Amekitaja kisa cha Al-Israa katika Aayah moja tu, Kisha Akaingia katika kutaja fedheha za Mayahudi na maovu yao, Na kisha Akawazindua kwa kuwaeleza kuwa hii Qur-aan inaongoza kwenye mambo yanayohitaji misimamo madhubuti kabisa. Inawezekana msomaji akadhania hizi Aayah mbili hazina uhusiano wowote, Jambo hili si kweli, maana kwa maneno haya Allaah Mtukufu Anaashiria kuwa kwa hakika Israa ni tukio lilitokea Baytul Al-Maqdis na kuwa Mayahudi watanyang’anywa cheo cha kuwaongoza wanaadamu kutokana na matendo yao maovu ambayo wameyafanya. Matendo ambayo hayakubakisha nafasi ya wao kubakia katika cheo hicho na kuwa Allaah سبحانه وتعالى Atakihamisha cheo hicho kwa vitendo na kumkabidhi Mjumbe Wake Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم ambaye atamkusanyia vituo viwili vikuu vya Da’awah ya Ibrahiym عليه السلام. Wakati umefika wa kuhamishwa kwa uongozi wa kiroho kutoka Ummah ulioijaza historia yake kwa udanganyifu, Khiyana, Madhambi na uadui kwenda katika ummah mwingine utakaoaminika kwa wema na kheri. Mtume wa Ummah huo hakuacha kuwa anayesifika na wahyi wa Qur-aan inayoongoza kwenye msimamo ulio sahihi.

Kwa vipi utahama uongozi huu hali ya kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anazunguka katika majabali ya Makkah hali ya kuwa ni mwenye kufukuzwana kupigwa na watu wa kabila lake? Suala hili linaibua ukweli mwingine ambao ni kuwa mzunguko wa kwanza katika Da’awah hii ya Kiislaam umekaribia kufika mwisho na kukamilika, Na baada ya hapo utaanza mzunguko wa kwanza katika mapito yake. Kwa sababu hiyo ndio maana tunaona kuwa baadhi Aayah zinakusanya mambo yanayohusu makhofisho ya wazi na makemeo ya kutisha dhidi ya Mushirikina.

“Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.

“Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja Wake.” [Al-Israa: 16-17].

Pamoja na Aayah hizi zipo nyingine zilizowaweka wazi Waislaam na zinazoendelea kuwawekea misingi ya maendeleo na kanuni zake na vyanzo vyake ambavyo hujenga jamii ya Kiislaam. Kama vile tayari wamekwishafika kwenye ardhi iliyo tayari, waliyapanga vizuri mambo yao kwa pande zote na wakaunda umoja wenye mshikamano madhubuti.

Katika jamii yao, hali kadhalika kulikuwepo na Ishara ya kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم atapata makimbilio na mahali pa amani ambako yatatulizana mambo yake na makimbilio hayo ndiyo yangekuwa kituo cha wito wake katika pande zote za dunia. Hii ni moja ya siri miongoni mwa siri za safari hii yenye kubarikiwa.

Tukio hili, ambalo kwa Muislam mwenye Iymaan barabara, hata kama lisingelikuwepo, Iymaan yake bado ingekuwa imara vilevile, ni tukio la kihistoria lenye kuzidisha kuujua uwezo wa Allaah سبحانه وتعالى na Utukufu Wake mkubwa usio na mithali. Ni tukio lenye mafunzo mengi ya kiimani na kiitikadi; ndani yake tumeona kumepatikana faradhi ya Swalaah, kumejulikana adhabu mbalimbali za matendo maovu ya hapa ulimwenguni, na hilo litaweza kutusaidia sana sisi kujiepusha na maovu hayo ili tusiishie kutumbukia ndani ya adhabu hizo kali. Tumeona utukufu na uzito wa Maswahaba kama Abu Bakr رضي الله عنه, na imetuzidishia heshima kubwa juu ya watukufu hao na kujua nafasi yao kubwa katika moyo wa mbora wa viumbe, kipenzi wa macho yetu, Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم. Tuchukue mazingatio yanayopatikana humo na kuyafanyia kazi katika maisha yetu na si tukio hili liwe la kuhadithiwa tu na watu kukusanyana kukisherehekea inapofika mwezi wa Rajab ambao kama tulivyoona mwanzoni kuna utata wa tukio hilo kuwa katika mwezi huo

Leave a comment