Watu saba wafariki katika ajali ya boti Nungwi

ImageWatu saba wamefariki dunia kufuatia ajali ya kuzama kwa boti ya mizigo na abiria iliyokuwa ikitokea Pangani Mkoani Tanga ikielekea Nungwi kisiwani Unguja.

Boti hiyo iliyojulikana kwa jina la Sunrise ilizama majira ya saa nane na nusu usiku wa kuamkia leo kufuati upepo mkali pamoja na mawimbi yaliyopelekea kuzama kwa chombo hicho huku kikiwa kimebeba abiria na mizigo.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Unguja Nd, Ahmada Khamis amesema miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo watatu kati yao ni watoto na watu wazima wane.

Aidha amesema kuwa, jumala ya watu 20 wameokolewa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Kivunge huku wengine 11 wakiwa hawajulikani walipo.

Pia amesema kuwa jeshi la Polisi likishirikiana na kikosi cha wanamaji wamepeleka vyombo vya uokozi katika eneo ilipotokea ajali hiyo ili kuwatafuta ambao bado hawajaonekana.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa abiria walionusurika katika ajali hiyo Bw, Pandu Ali Shaha amesema chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali ulioambatana na mawimbi yaliyoingiza maji ndani na hatimae chombo hicho kupinduka na kuzama.

“Maji yaliingia ndani na sisi tukiyatoa kutokana na kuongezeka kwa mawimbi maji nayo aliongezeka na yakatushinda kuyatoa na mwisho chombo kilizama” alisema Bw, Pandu.

Nae mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh, Pembe Juma Khamis amewataka wasafiri wa baharini pamoja na wavuvi kufuata maagizo ya mamlaka ya hali ya hewa kutokana kutoa taarifa kuhusiana na hali mbaya ya bahari ili kuweza kuepuka maafa.

Boti hiyo ilikuwa imebeba jumla ya watu 38 ambao kati yao abiria ni 33 na mabaharia watano ambao wote wamepatikana wakiwa hai.

 

Wahamasishaji watakiwa kutoa elimu juu ya kupambana na ukatili wanaofanyiwa wanawake na watoto

ImageMkuu wa mkoa wa kaskazini pemba Mh, Dadi Faki Dadi amewataka wahamasishaji wa maendeleo ya jamii kutoka jumuiya ya wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba  kuwaelimisha wananchi ili watambue umuhimu wa  kupambana na ukatili wanaofanyiwa wanawake na watoto.

 Hayo ameyasema huko shengejuu wilaya ya wete wakati wa hafla ya kukabidhi baiskeli 50 zenye thamani ya shilingi milioni sita na nusu kwa wahamasishaji maendeleo ya jamii zilizotolewa na jumuiya hiyo kwa ufadhili wa shirika la ACTIONAID.

Aidha amesema kuwa ni vyema wahamasishaji hao kuendelea kutoa taaluma ili kujenga uwelewa kwa jamii pamoja kutambua wajibu wao katika kutetea na kulinda haki za msingi za wanawake na watoto.

Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza haja kwa wahamasishaji hao kuvitumia vyombo vya sheria katika kudai haki na kuacha tabia ya kusuluhisha migogoro inyojitokeza katika shehia zao.

Mapema mratibu wa mradi huo Bi Nadra Subeti Ali amesema kuwa mradi huo una lengo la kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake na watoto  na kuhakikisha kuwa haki zao za kulindwa na kuishi kwa amani na utulivu zinathaminiwa.

Watoto walioajiriwa mitaani kurejeshwa mashuleni

ImageMwakilishi wa shirika la kimataifa la kuhudumia watoto kanda ya zanzibar  Nd, Mubarak Maaman  amesema shirika hilo lina mpango wa kutokomeza ajira mbaya kwa watoto kwa kuweka mipaka itakayowafanya watoto hao waendelee na masomo.

Akifunga mafunzo kwa Wandishi wa habari wa vyombo mbalimbali huko ukumbi wa elimu mbadala Rahaleo amesema, mpango huo utasaidia kupunguza ajira mbaya zinazopelekea madhara mbalimbali yanayoathiri kiwiliwili na akili .

Aidha amesema kuwa shirika la kuwahudumia watoto linafanya kazi ya kuwabadilisha tabia na kuwarejesha mashuleni watoto hao kwa kushirikiana na  serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taasisi mbalmbali  kwa kuwapa ushauri nasaha

 Nd, Mubarak amefahamisha kuwa katika mikakati ya mradi huo ni kuweka mahakama ya watoto ambayo itakuwa inashughulikia kesi za watoto waliochini ya umri miaka kumi nane

 Nae mratibu wa kupambana na ajira mbaya kwa watoto kutoka wizara ya kazi uwezeshaji wananchi  kiuchumi  na ushirika  Bi Fatma Mussa Omar amesema katika kupunguza utumikishwaji wa watoto wanatarajia kupata  sheria ambayo itawawezesha kufanya uchunguzi na kuwatambua wenye kuwatumikisha watoto hao kwa  kuwachukulia hatua za kisheria .

Mradi wa huo unafadhiliqwa na umoja wa ulaya na utekelezajiwa wake unaendeshwa na shirika la kuwahudumia watoto kwa kushirikiana na TAMWA ,COWPZ,PIRO na KUKHAWA.

Miche elfu kumina mbili ya asili kuoteshwa

ImageIdara ya misitu na mali zisizorejesheka Zanzibar imeandaa mpango maalum wa kuzalisha miche elfu kumi na mbili  ya asili ambayo iko hatarini kutoweka hapa Zanzibar.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi msimamizi wa vitalu wa idara hiyo huko Maruhubi Nd, Rashid Nassor Rashid amesema kuwa kutokana na kuwepo ukataji ovyo wa miti ya asili kuna hatari ya kutoweka kwa miti hiyo hivyo idara hiyo imeona ipo haja ya kuzalisha miche ya miti hiyo

Ameitaja miti hiyo kuwa ni pamoja pilipili doria, mizambarau, muibuyu, mikonge , midoriani pamoja na milingoti.

Aidha amesema kuwa miche hiyo inatarajiwa kupandwa katika sehemu mbali mbali kutokana na uwasili wake na sehemu inayomea zaidi zikiwemo sehemu za vianzio vya maji, barabarani, pamoja na kwenye mashamba ya serikali

Aidha amefahamisha kuwa idara itaendelea kutoa elimu kuhusiana na ukataji wa miti licha ya baadhi ya wananchi kuendelea kukata miti hiyo bila ya kufuata taratibu za kisheria.

Kamishna wa chuo cha Mafunzo awataka maafisa wa jeshi hilo kujiwekea mipango katika utendaji wa kazi,

Kamishna wa chuo cha mafunzo zanzibar Nd, Khalfan Hassan Choum amewataka maafisa na wapiganaji wa jeshi hilo kujiwekea mipango ya utendaji ili kuleta ufanisi wa kazi zao.

Amesema mipango na utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea itasaidia kuleta ufanisi na kufanikisha malengo waliyojiwekea.

Kamishna Choum ameyasema hayo alipokua na mazungumzo na maafisa na wapiganaji wa jeshi hilo huko makao makuu ya chuo cha mafunzo Kilimani mjini Zanzibar.

Aidha amewataka maafisa hao kuongeza mashirikiano katika kuwajibika kwenye sehemu zao za kazi ili kuimarisha nidhamu ya jeshi sambamba na kuondoa matendo maovu yanavyojitokeza kwa baadhi  maeneo.

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa gereza huko Hanyegwamchana kamishna Choum amesema ni vyema wapiganaji hao kuwa na ushirikiano na maofisa wa kada mbalimbali ili kuona ujenzi huo unakamilika kama ilivyokusudiwa

 

MATOKEO YA MTIHANI ZANZIBAR YANAPOFANANA NA WAZIRI SHAMUHUNA

ImageWakati Zanzibar ikijiandaa kujipapatua na makucha na uonevu wa baraza la mitihani la Taifa Tanzania (NECTA), dalili za utayari huo hazioneshi kutosha au kufikia kiwango kinachotakiwa hapa kwetu. Hii ni mfano wa mtu anaejitayarisha kuanza maisha mapya ya kujitegemea au ya ndoa ilhali binafsi hajafanya matayarisho muhimu ya jambo hilo.

Nasema kuwa matayarisho yetu ya kujitegemea kuwa na Baraza huru, letu wenyewe la mitihani ni duni na hayajarekebishwa. Kuna dalili za wazi kwamba Elimu yetu na maamuzi makuu yahusuyo mustakabli wa Elimu kuwa hufanywa kwa misingi ile ile ya kisiasa za kibinafsi zaidi kuliko usiasa wa maendeleo ya kitaifa kwa ujumla.

Usiasa huu kwa kiwango kikubwa unachangiwa na mfumo uliopo. Mfumo ambao sehemu nyeti kabisa za nchi hii hukabidhiwa watu ama wasio na uwezo au wasio na nia njema ya kuwaletea watu maendeleo bila ya kuwabagua au kuwagawa.

Tunatambua kuwa Serikali yetu ipo katika sera ya umoja wa kitaifa, lakini moja kati ya mzaha mkubwa iliofanya katika uteuzi wa mawaziri ni katika Wizara ya Elimu. Tukubali kuwa Wizara ya Elimu ni moja ya Wizara nyeti kabisa katika nchi yetu, lakini kwa muda mrefu Wizara hii imekuwa ikifeli na kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu.

Wizara yetu ya elimu imejaa ubinafsi na ubaguzi wa kivyama na umajimbo, achilia mbali uzembe na ufisadi uliokithiri. Katika hali kama hii uteuzi wa viongozi wakuu wa Wizara hii unahitaji watu wenye roho, moyo na imani ya kweli sambamba na uwezo wa kuongoza Wizara kama hii. Na hili linawezekana kwani tumeona nini Serikali imekifanya pale SUZA kwa kumuweka Profesa Rai kuondoa usiasa katika utendaji. Hili linawezekana pia kufanywa Wizara ya Elimu. SUZA Inang’ara sasa!

Sina shaka tunatambuwa kuwa uteuzi wa Waziri Harun Ali Suleiman ndio uliouwa kabisa uhai wa Wizara ya Elimu. Kwa Waziri Haroun, tulishuhudia uhaba wa walimu uliokifu na malalamiko makubwa ya walimu nchini. Bahati mbaya, kuondoka kwa Waziri Haroun akaja Ramdahan Abdala Shaaban, ikawa ni zaidi ya bure. Juzi tumeletewa Shamuhuna kuja kulifunika jeneza la Elimu ya watoto wetu hapa visiwani.

Uteuzi wa Shamuhuna wizara ya Elimu uliwaumiza wengi wanaomjua yeye kama yeye. Mheshimiwa ni mtu mwenye chuki ya asili dhidi ya Uunguja na Upemba. Pia ni bingwa wa kuanzisha migogoro na masuala yenye utata, kukoroga mambo na kufanya sanaa ya kila aina anapotaka kuharibu na kutimiza lake. Na hili ndio sasa limejitokeza katika matokeo ya mitihani, hasa ya kidato cha pili.

Matokeo ya kidato cha pili, ambayo ndio kweli muhimu kwa watoto wetu. Ni muhimu kwamba hapo huwa wengi wanaoshindwa kuendelea, huwa ndio mwsiho wa safari zao kimasomo. Matokeo ya kidato cha pili ya mwaka huu yana mshabaha mkubwa na Waziri Shamuhuna mwenyewe. Yaani yamefanana kwa sura na tabia alizonazo Waziri. Maana kama yeye angekuwa baba, na matokeo ya mwaka huu yakawa mwana, basi tungesema amejizaa, kopi kwa kopi! Hatuhitaji hata kipimo cha vinsaba(DNA)

Matokeo yetu mwaka huu yamefanana mno na Waziri kwanza, kwa kuonesha sura ya kuwa na upendeleo ambao unahitaji utafiti wa muda mrefu (Survey) ili uweze kututhibitishia kuwa ulikuwa wa haki na usawa. Na kama hauna upendeleo basi pia tutahitaji kujuwa kwanini jadweli ya matokeo yote imelalia upande mmoja tu wa nchi na kuacha kwengine? Tuanze na moja moja.

Mwaka huu wanafunzi bora wote watatu darasa la saba na kumi, wote wanatoka Unguja. Hii ni ajabu ya Karne. Tena istoshe, wote wanatoka mjini  Magharibi. Hapa hoja hii inaleta mushkeli wa dhana yangu ya kwanza ya kutokuwepoo kwa usawa yaani upendeleo, au dhana yangu ya pili, ya wa hakuna usawa kwa sababu ya kutotowa huduma na usimamizi sawa wa huduma za Elimu nchini. Taswira hii ya ni ya ‘Kishamuhuna’(Shamuhunaism) zaidi. Maana tangu Mapuri hili halikuwepo!

La pili, kama ukiangalia kiwango cha ufaulu mwaka huu ni kibaya mno. Yaani katika watahiniwa 19,679, waliofaulu ni asilimia 56.9% tu yaani wanafunzi 11, 195, huku wengine 8,484 wakisubiri kudura ya mungu kujua hatma ya maisha yao. Hii ni hatari.

Katika nchi kama hii ambayo haina miundo mbinu mingi na huduma za kuendeleza vijana wake, idadi ya wanafunzi kama hawa wanaofeli kwa mwaka ni hasara kwa taifa. Lakini pia hili ni matokeo ya uteuzi unaoangalia maslahi ya wanasiasa na kivyama zaidi kuliko maendeleo ya utaifa.Na pia hapa sina shaka hili ndio hasa lengo ambalo lilipelekea Mheshimiwa Shamuhuna kuwekwa pale. Yaani kwa lugha nyepesi, tukikataa kukaangwa na NECTA, tujipike wenyewe hapa hapa kwetu.

Kama nilivyotarajia, usanii ni sehemu kubwa ya viongozi wetu wa kisiasa akiwemo waziri wetu wa Elimu. Kama utayaangalia matokeo yetu mwaka huu na maamuzi yaliyofanywa utaona wazi wzi kuwa kuna usanii au kuwafanya watu wapuuzi.Kwa mfano tunaambiwa kuwa matokeo ya mwaka huu yameongezeka kwa asilimia 0.8%. Hivi hili kweli ni jambo la kusema kweli hili? Hivi hili ni ongezeko gani, na kwa kipimo gani hasa ukichukulia idadi ya wanafunzi ya mwaka jana ilikuwa ndogo zaidi kuliko ya mwaka huu. Hii aslimia inatoka wapi na inamaanisha nini kitaalamu? Usanii.

Jengine, tunaambiwa kwamba wanafunzi wapato 1340 hawakufanya mtihani kwa sababu zisizojulikana. Nakubali kwamba katika hao kuna waliofariki, waliohama, wanaoumwa, na sababu nyenginezo lakini ni jukumu la serikali kufatilia kwanini vijana wote hawa hawakufanya mtihani? Pia baada ya kufanya hivyo walikuwa waeleze iwapo vijana hao watapewa tena fursa ya kufanya tena, jambo ambalo ni haki yao kisheria. Hili hatuambiwi. Kunani?

La ajabu mno, ambalo pia kwa Waziri shamhumuna halinishangazi kwani nalo anafanana nalo kabisa ni hili la maamuzi magumu aliyochukuwa kwa skuli alizozitaja kuwa ‘tiro’. Mheshimiwa amezitaja shule kama Bwefum, Umbuji, Uzi, Ubago, Pongwe pwani, Michamvi na mtende kwa Unguja kuwa madarasa yao yatafungwa. Kwa Pemba kisiwa panza, Makoongwe na Ndagoni pia madarasa yao yatafungiwa.

Suali langu linakuja hapa. Hivi shule ikifanya vibaya huwa kosa la shule hio pekee bila Wizara kuhusika? Isitoshe, kama shule hizo zimefanya vibaya hatuoni kama ni busara tungepitisha watendaji kuuliza kuna matatizo gani hadi yakajiri hayo? Au na hili si la busara? Kama hayo yote siyo, hivi kuzifungia shule hizi ndio tushatauwa tatizo la kufanya vibaya katika masomo na mitihani?

Maana mwaka huu tumefungia skuli nane, na mwakani 10. Hata akiondoka Shamuhuna itakuwa hakuna shule hata moja itakayobaki wazi. Na hapa ndipo tutakapokuja kusema kuwa Ilani ya chama ya uchaguzi ya mwaka 2010-2020 imefikiwa kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi. Na bila shaka huku ndiko waziri Shamuhuna anakotupeleka!
Tungoje tuone!

SMZ yaanza kufanyia kazi mapendekezo ya kamati ya kulichunguza Baraza la Manispaa,

ImageSerikali ya mapinduzi zanzibar imeanza kutekeleza mapendekezo ya kamati ya baraza la wawakilishi iliyoundwa kuchunguza utendaji wa baraza la manispaa kwa kumuondoa madarakani mkurugenzi na mhasibu wa baraza hilo .

Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji huo Waziri wa nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk . Mwinyihaji Makame amesema Mkurugenzi wa Baraza hilo ameondolewa katika wadhifa wake na mhasibu amehamishiwa taasisi nyingine.

Amesema mbali na hatua hizo serikali pia imepeleka suala la watendaji hao katika Ofisi ya Mwanasheria mkuu kupata ushauri wa kuwachukulia hatua za  kisheria zaidi.

Aidha Dk, Mwinyihaji amesema serikali pia inapitia vielelezo vya aina ya makosa dhidi ya wafanyakazi waliotajwa kwenye kamati hiyo ili kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Wakati huo huo serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshauriwa kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali katika taasisi za serikali na mashirika ya umma ili kuepuka hujuma znizo jitokeza katika taasisi hizo.

Akitoa majumuisho ya ripoti ya uchunguzi wa shirika la umeme. Mwenyekiti wa kamati ya kuchunguza na kudhibiti hesabu za serikali na mashirika ya umma Mh, Omar Ali Shehe amesema iwapo mapendekezo ya ripoti hiyo hayatafanyiwa kazi wananchi watapunguza imani kwa utendaji wa taasisi za serikali..

Ripoti hiyo ya uchunguzi yenye mapendekezo 14 imekabidhiwa kwa spika wa baraza la wawakilishi mh. Pandu Ameir Kificho kuiwasilisha serikalini kwa ajili ya hatua za utekelezaji.

Raza akabidhi vifaa kwa Jeshi la Polisai,

ImageWatendaji wa jeshi la polisi nchini wameshauriwa kuendeelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ili waweze kuungwa mkono na wananchi katika kulinda amani na utulivu wa nchi.

Ushauri huo,umetolewa na Mwakilishi wa jimbo la Uuzini Mh, Mohamed Raza wakati akikabidhi vifaa vya ujenzi na michezo vyenye thamani ya shilingi milioni 5  kwa watendaji wa jeshi hilo huko makao makuu ya polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda.

Mh, Raza amesema kuwa jeshi la polisi ni kiungo muhimu   cha kudumisha   amani katika jamii hivyo wanatakiwa kuzidisha juhudi  za kiutendaji katika utekelezaji wa  majukumu yao kwa uadilifu. 

Aidha amefahamisha kuwa lengo la kutoa vifaa hivyo ni miongoni mwa kutekeleza  ahadi  alizozitoa kwa jeshi hilo ili kuhakikisha askari wanafanya kazi katika mazingira mazuri yatakayowasaidia kutoa huduma bora na endelevu kwa jamii.

Nae  Kamishna msaidizi wa polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja Ahmada  Abdallah Khamis ametoa shukrani zake kwa Mwakilishi huyo juu ya msaada alitoa na kuahidi kuwa utatumika kwa shughuli iliyokusudiwa  ili ofisi za jeshi hilo ziwe za kisasa zinazoendana na taswira ya askarin wake.

Pia amesema jeshi hilo limekuwa na ushirikiano mkubwa na wananchi katika kupambana na harakati mbalimbali za uharifu na matukio mengine ya uhalifu ili kuhakikisha zanzibar inazidi kuwa kitovu cha amani duniani.

 

Watoto 70 kupatiwa tiba ya macho hospitalikuu Mnazi mmoja,

ImageJumla ya watoto 70 wenye matatizo ya macho wanatarajia kupatiwa matibabu ya macho katika hosptali kuu ya mnazimmoja.

Matibabu hayo yatakayo chukua kipindi cha wiki moja yatajumuisha watoto kuanzia siku moja hadi miaka 15 ambapo watafanyiwa upauaji na huduma nyengine.

Mkuu wa kitengo cha macho Zanzibar Dk Slim Mohammed Mgeni amesema wagonjwa wengine kumi wenye matatizo zaidi ya macho watapelekwa hospitali ya Muhimbili Dar es salaam kwa uchunguzi wa kina.

Dk, Slim amefahamisha kuwa  mpango huo wa matibabu ya macho kwa watoto utaendelea kila mwaka na kuwataka wazee kutumia fursa hiyo kuwapeleka watoto wao kupatiwa matibabu hayo.

Nao wazazi wa watoto wanaopatiwa huduma hiyo wameshukuru hospitali ya Mnazimmoja kwa kushirikiana na madaktari wa Muhimbili kutoa matibabu hayo kwa watoto wao.

 

Waalimu washauriwa kuwaandalia wanafunzi ziara za kimasomo,

Meneja wa Zala Park Bw Mohammed Ayoub amewataka walimu nchini kuwa na utamaduni wa kuwafanyia wanafunzi ziara mbalimbali za kimasomo ili kuwajengea uwezo wa kujua mambo yanayo husiana na  historia ya nchi.

Akizungumza na shirika la utangazaji zanzibar amesema wakati umefika kwa walimu hao kuweka mikakati imara ili kuona wanafunzi wanafanyiwa ziara kama hizo na kuweza kufahamu mambo mbalimbali yalimo ndani ya nchi.

Bw, Ayoub amesema kuwa lengo la kuweka sehemu za kihistoria ni kutoa taaluma mbalimbali kuhusiana na historia, hivyo tabia ya kuwaandalia wanafunzi ziara kama hizo kutawafanya waweze kufanya vizuri katika mitihani yao pamoja na kukuza kiwango cha elimu hapa nchini.

Aidha amefahamisha kuwa kuna baadhi ya walimu hawapendi kuwafanyia wanafunzi ziara za kimasomo, hivyo kupelekea wanafunzi hao kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao jambo ambalo hurudisha nyuma juhudi zao..

Hivyo amesema katika kuhakikisha sekta ya elimu ya inakuwa nchini ni vyema kuwa na mashirikiano baina ya wanafunzi na walimu wao ili kuweza kukuza maendleo ya elimu na kupata wataalumu wazuri hapo baadae

 

Dk, Shein aipongeza Kamati ya Mapinduzi Cup.

ImageRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na Kamati ya mashindano ya ‘Mapinduzi Cup’ na kupongeza juhudi  walizozichukua katika kufanikisha mashindano hayo yaliyoyafanyika katika kusherehekea  miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi karibuni. 

Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamati hiyo chini ya mlezi wake, Balozi Seif Ali Idd pamoja na Wahisani waliochangia mashindano hayo ambapo pia, uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) nao ulikuwepo.  

Katika maelezo yake, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Kamati hiyo kwa kuendeleza mashindano hayo  ambayo yamefana kwa kiasi kikubwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mohammed Raza ambaye pia, ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini.

Dk. Shein mbali ya pongezi kwa  kufanikiwa kwa mashindano hayo pia, alitoa pongezi kwa timu ya ‘Azam FC’kwa kupata ushindi kwa mara ya pili wa mashindano hayo na kupelekea kombe kubakia katika udongo wa Tanzania .

Alisema kuwa ushindi huo umeipa heshima kubwa Tanzania na kusisitiza kuwa michezo hujenga mshikamano, udugu na maelewano makubwa miongoni mwa jamii kwani ni sehemu ya maisha.

Dk. Shein alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika Kamati hiyo kutokana na uaminifu mkubwa ulioonesha wakati wa matayarisho ya mashindano kupitia kwa wahisani ambao walimeonesha moyo mkubwa wa kuyasaidia mashindano hayo pamoja na kuisaidia nchi hiyo.

Alieleza kuwa hatua kama hiyo inaweza kusaidia katika kuendeleza mambo mbali mbali ikiachiliwa mbali mashinadno ya mpira lakini kubwa kuliko yote ni uaminifu.

Katika maelezo yake hayo, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika michezo mbali mbali hasa mpira wa miguu hivyo kuna haja ya kujiandaa vizuri zaidi katika mashindano hayo hapo mwakani ambapo sherehe za Mapinduzi zinatimiza nusu karne.

Aliunga mkono rai ya Kamati hiyo kupitia Balozi Seif kwa azma yake ya kukutana na Ubalozi wa China kwa lengo la kuialika timu kutoka nchini humo na yeye akasisitiza iwapo kuna haja ya kuyanogesha zaidi mashindano hayo naye yuko tayari kuialika Vietnam nayo kuleta timu yake kwani tayari Zanzibar imeshajenga uhusiano mwema na nchi hiyo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya kujiandaa katika mashindano hayo kitimu kwa kutoa mialiko sehemu mbali mbali zikiwemo ndani na nje ya Bara la Afrika pia, ni vizuri Kamati hiyo kwa kushirikiana na ZFA ikaangalia uwezekano wa kuweka nyasi bandia katika uwanja wa Aman mjini Unguja ili uweze kuchezeka vizuri.

Alisema kuwa Serikali iko tayari kuiunga mkono Kamati hiyo  ili kufanikisha azma yake hiyo huku akisisitiza kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kurudisha heshima yake katika michezo hasa mpira wa miguu kwani Zanzibar ina historia katika medani ya soka.

Nae Balozi Seif  Idd, alitoa pongezi zake kwa Kamati hiyo na uongozi wake na kueleza kuwa mashindano hayo yamekuwa kivutio cha watazamaji wengi na kupelekea kunogesha sherehe hizo na kueleza haja kwa Kamati hiyo kuwa Washajihishaji wa michezo hapa Zanzibar .

Balozi Seif alisema kuwa mikakati maalum imewekwa katika kuhakikisha mashindano yajayo hapo mwakani yanakuwa ya aina yake kwa kuzishirikisha timu nyingi huku akieleza nia yake ya kuzungumza na Balozi wa China ili kuleta timu kutoka nchini humo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk nae alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa azma yake ya kuimarisha michezo huku akisisitiza kuwa busara za Rais ndizo zilizoleta mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kuipa fursa Kamati hiyo ili iendelee kufanya kazi za kuandaa mashinadano hayo.

Waziri Mbarouk, alimuhakikishia Dk. Shein kwamba Wizara yake, imo katika juhudi za  kuhakikisha migogoro ndani ya ZFA inapatiwa ufumbuzi ili soka la Zanzibar lizidi kuimarika.

Mapema  Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mohammed Raza alimueleza Dk. Shein kuwa Kamati hiyo imefanya kazi kwa mashirikiano makubwa huku akimueleza jinsi ilivyojipanga katika mashindano hayo hapo mwakani kwa kualika timu kutoka sehemu mbali mbali zikiwemo za Afrika Mashariki na Kati, Afrika Magharibi na kwengineko.

Mhe. Raza alieleza jinsi wahisani waliochangia mashindano hayo walivyuoonesha moyo wao mkubwa katika kutoa michango yao huku akimueleza Rais kuwa Kamati hiyo haina deni hata moja kutokana na mashindano hayo pamoja na kueleza jinsi Kamati inavyofikiria kutafuta waamuzi kutoka nje ya nchi katika mashindano yajayo.

Katika hafla hiyo pia, Dk. Shein aliwakabidhi vyeti maalum wahisani waliofanikisha mashindano hayo wakiwemo Shirika la Bandari Zanzibar, Benki ya Watu wa Zanzibar, Hassan & Sons, Royal Furniture and Décor Ltd, Zanzibar Ocean Views Ltd, Zanzibar Aviation Services (ZAT), United Petroleum Ltd, Zan Air Ldt.

Wahisani wengine ni  Pemba Misali Beach Resort na Zanzibar Insurance Corporation. Pia, Dk. Shein alimkabidhi tunzo maalum iliyoandaliwa na Kamati hiyo Rais wa ZFA. Bwana Amani Ibrahim Makungu kwa mchango wake mkubwa katika mashindano hayo.  

Kwa maelezo ya Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Bi Sharifa Khamis Salim alizitaja timu nane ambazo zilishiriki katika mashindano hayo ambayo timu ya Azam FC iliibuka mabingwa.

Timu nyengine zilizoshiriki mashindano hayo ni Tusker kutoka Kenya, Mtibwa suger, Simba, Jamhuri, Miembeni, Costal Union na Bandari Zanzibar ambapo timu ya Yanga na Al-Ahli ya Misri zilijitoa katika mashindano hayo.

Na Rajab Mkasaba (IKULU).

 

Jumuia ya uhifadhi Mazingira Zanzibar yataka kuundwa kwa kamati ya Mazingira ya baraza la Mapinduzi.

ImageJumuiya ya maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira Zanzibar (CODECOZ), imesema wakati umefika wa kuanzishwa kwa kamati ya mazingira ya Baraza la Mapinduzi kama sheria ya mazingira ya mwaka 1996, ilivyoelekeza.

Akizungumza kwenye mafunzo ya siku mbili, kwa viongozi wa asasi za kiraia zinazojishughulisha na utunzaji mazingira, huko kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi, katibu mkuu wa CODECOZ kaptein mstaafu Hamaza Makame Omar, alisema sheria hiyo inaagiza kuwe na chombo hicho.  

Amesema tokea kuanzishwa kwa sheria hiyo miaka wa 17 sasa, bado serikali haijaamua kuunda chombo hicho, ambacho kwa mujibu wa sheria hiyo, kitakua ndio chombo cha juu kabisa na cha kukata rufaa iwapo kutajitokeza jambo na kushindikana ngazi za chini.

Kepteni Hamza alisema, sheria hiyo ambayo ilikuja baada ya kutanguliwa na sera ya mazingira ya mwaka 1992, pia iliagiza kuwe na mfuko wa taifa wa mazingira kwa maendeleo endelevu.

Amefafanua kuwa, mfuko huo kwa mujibu wa sheria hiyo, amabo hadi leo hii haujanzishwa, utakuwa na madhumuni ya kuwezesha utekelezaji wa sheria hiyo, ili kulinda na kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa vilpengele vyote vya sheria.

 Aidha katibu mkuu huyo wa CODECOZ, alizidi kueleza kuwa, chombo chengine kilichoolekezwa kuanzishwa kwa mujibu wa sheria hiyo namba 2 ya mwaka 1996, ni vitengo vya mazingira katika taasisi zote za umma ambapo, ameleza hilo lipo kwa kiwango kidogo. 

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Bw Jabu Khamis Mbwana, alisema suala la kuhifadhi na kuyalinda mazingira sio jukumu la idara ya mazingira pekee, bali kila mmoja linamgusa.   

Wakichangia mada mbali mbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo, washiriki hao kutoka Wilaya za Mkoani na Micheweni, wameelezea kusikitishwa kwao na kutokuwepo kwa uwino wa kutiwa hatiani kwa waharibifu mazingira.  

Mafunzo hayo ambayo yaliwashirikisha viongozi 40 wa asasi, kutoka Wilaya za Mkoani na Micheweni, yameandaliwa na jumuia ya maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira Zanzibar (CODECOZ), na kufadhiliwa na mpango wa msaada wa kimaendeleo wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP).  

 

Walimu watakiwa kushirikiana na serikali za wanafunzi.

Walimu nchini wametakiwa kuwa na mashirikiano mazuri na serekali za wanafunzi ili kukuza na kuendeleza elimu nchini.

Hayo yameelezwa na katibu wa umojawa serekali za wanafunzi wa zanzibar (USEWAZA) Nd, Salum Muhammedi Salum wakati alipo tembelea umoja wa serekali ya wanafunzi na walimu wa skuli ya kikungwi huko  skulini kwao.

Aidha amesema kua hakuna sababu ya baadhi ya skuli kuvunjwa serekali ya wanafunzi kwani serekali hiyo ina wahamasisha wanafunzi katika sualazima la elimu.

Kwa upande wake Afisa wa huduma za Elimu kwa shule za msingi mwalimu Suleiman Takadiri amesema walimu kushirikiana na serekali za wanafunzi kutasaidia kuongezeka kwa kiwango cha upasishaji wa wanafunzi nchini.

Nae mwenyekiti wa serekali za wanafunzi Zanzibar Nd Abubakari Hemed Abdalla amesema lengo kuu la usewaza ni kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wanafunzi kwa kuzingatia mila na desturi za wazanzibari.