Maalim Seif Sharif Hamad aiagiza Wizara ya Kazi kusimamia utaratibu wa waajiri binafsi

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa  maonyesho ya nne ya biashara na huduma katika viwanja vya Amaan, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, “May day”.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa maonyesho ya nne ya biashara na huduma katika viwanja vya Amaan, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, “May day”.

Hassan Hamad (OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameiagiza Wizara ya Kazi kusimamia utaratibu wa waajiri binafsi, ili kuhakikisha kuwa wanawapatia zote wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na malipo ya muda wa ziada.

Amesema serikali kwa upande wake imekuwa ikiendeleza utaratibu wa kuwapa malipo hayo wafanyakazi wake, lakini malalamiko mengi yamekuwa yakijitokeza kwa taasisi binafsi.

Maalim Seif ameeleza hayo viwanja vya Amaan mjini Zanzibar, wakati akifungua maonyesho ya nne ya biashara na huduma, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani “Mei day”, yanayotarajiwa kufikia kilele chake kesho.

Kuhusu maonyesho hayo Maalim Seif amesema ni muhimu katika kujifunza mbinu za kibiashara na kubadilishana uzoefu kwa wajasiriamali.

“Maonyesho ya biashara  na huduma yana faida kubwa sana kwa wanaoonesha bidhaa, lakini pia yana faida kubwa kwa wateja ambao wanahitaji kujua bidhaa au huduma za aina gani zinapatikana wapi. Pia ni nafasi ya wateja kupata kujua na kulinganisha unafuu wa upatikanaji wa huduma hizo, kati ya watoaji tofauti”, alisisitiza Maalim Seif.

Amefahamisha kuwa katika maonyesho kama hayo ya biashara, watu hupata fursa ya kipekee ya kubadilishana mawazo na uzoefu katika shughuli za uzalishaji, ununuzi na biashara kwa jumla, nahatimaye kuondoka wakiwa na mawazo na upeo mkubwa zaidi wa kibiashara na kiuchumi kutokana na mawazo na uzoefu walioupata kwa wengine.

Hata hivyo amesema jambo la muhimu kwa wazalishaji na watoa huduma ni kuhakikisha kuwa wanazalisha bidhaa za viwango vya juu na kutoa huduma bora zitakazokwenda sambamba na ushindani wa kibiashara uliopo.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif amezishauri taasisi za Umma kujipanga ili ziweze kushiriki kikamilifu katika maonyesho kama hayo kuanzia mwakani, 2014.

Mapema akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Kazi, Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Haji Omar Kheir, amesema lengo la maonyesho hayo ni kukuza ajira kupitia vyama vya ushirika.

Katika risala yao ya maonyesho, wafanyakazi hao wamesema wanakabiliwa na tatizo la sehemu maalum ya kufanyia maonyesho, na kuiomba serikali kuwasaidia kupata sehemu hiyo.

Maonyesho hayo yamevishirikisha vikundi 48 vya wajasiriamali kutoka Unguja na Pemba.

Maalim Seif aiomba Canada kuwekeza katika miradi mbalimbali Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, ofisini kwake Migombani. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, ofisini kwake Migombani. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameihakikishia Canada kuwa Zanzibar ina maeneo mazuri ya kuwekeza na kuwaomba wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza katika Nyanja tofauti zikiwemo ujenzi wa hoteli kubwa za kitalii, kumbi za mikutano na uvuvi wa bahari kuu.

Amesema Zanzibar ina mahitaji makubwa ya uwekezaji katika maeneo hayo, na kwamba hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa taifa na kunyanyua kipato cha wananchi.

Akizungumza na balozi wa Canada nchini Tanzania balozi Alexandre Leveque ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema serikali imelenga kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza miradi mbali mbali ya kiuchumi.

Aidha Maalim Seif ameiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kuleta wataalamu wa Afya na walimu wa sayansi, ili kupunguza tatizo la wataalamu hao nchini.

Amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta hizo, lakini bado zina upungufu wa wataalamu wakiwemo madaktari wenye sifa, pamoja walimu wa masomo ya sayansi.

Amesifu mchango wa nchi hiyo hasa katika sekta za afya na elimu na kutaka isichoke kutoa misaada yake katika kusaidia kunyanyua uchumi wa Zanzibar.

Kwa upande wake balozi Alexandre amesema Canada imekuwa ikihamasisha wawekezaji binafsi, na kuahidi kuwahamisha kuja kuwekeza Zanzibar.

Kuhusu upatikanaji wa wataalamu wa Afya na walimu wa Sayansi, balozi huyo amesema atawasiliana na mamlaka zinazohusika, ili kupata wataalamu wakiwemo wa kujitolea, watakaoweza kuja kufanya kazi  katika maeneo hayo.

Amesema Canada inajivunia uhusiano wa muda mrefu uliopo kati yake ya Zanzibar, na kwamba uhusiano huo utaendelezwa kwa maslahi ya pande hizo mbili.

Hassan Hamad (OMKR)

Mataifa ya G20 yashauriwa kuwekeza katika Mataifa ya Afrika Mashariki (EAC)

Imewekwa na Nassor Khamis

Mwenyekiti wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni (aliyeshika Kofia) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wenzake wa jumuiya hiyo mara baada ya kumaliza Mkutano wao wa 11 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ngurdoto Mkoani Arusha. Kushoto ya Rais Museveni ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni.Kulia ya Rais Museveni ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana Pierre  Damien Habumuryemi pamoja na Rais wa Burundi Bwana Pierre Nkurunziza.
Mwenyekiti wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni (aliyeshika Kofia) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wenzake wa jumuiya hiyo mara baada ya kumaliza Mkutano wao wa 11 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Ngurdoto Mkoani Arusha. Kushoto ya Rais Museveni ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyemuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni.Kulia ya Rais Museveni ni Waziri Mkuu wa Rwanda Bwana Pierre Damien Habumuryemi pamoja na Rais wa Burundi Bwana Pierre Nkurunziza.

Mataifa yanayoendelea  kupiga hatua za haraka za Kiuchumi Ulimwenguni ya G. 20 yameshauriwa kuwekeza ndani ya Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki { EAC } ili kuunga mkono harakati za Kiuchumi za Mataifa hayo.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Yoweri Kaguta Museveni  wa Uganda katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.  

Rais Museveni alisema Mataifa hayo yenye muelekeo mzuri wa Kiuchumi yanaweza kuongeza nguvu zao katika kusaidia miradi ya Miundo mbinu ya Bara bara ,Mawasiliano na hata Sekta binafsi.

Alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imelenga kunyanyua maisha ya Wananchi wake kwa kuimarisha Sekta zisizo rasmi kwa vile uwezo wa Serikali hizo katika kutoa ajira hasa kwa Vijana bado ni mdogo.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alitolea mfano Taifa lake la Uganda ambalo limejizatiti katika kuimarisha nguvu za sekta binafsi ili kupunguza wimbi la vijana wengi wanaomaliza masomo yao ambao hubaki wakizurura bila ya utaratibu wa kufanya kazi.

“ Vijana popote pale walipo ndio nguvu kazi ya Taifa. Hivyo bado upo umuhimu wa kuwaandalia mazingira mazuri yatakayotoa fursa ya kuyatumikia vyema Mataifa yao “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Museveni wa Uganda.

Akiwahutubia Viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi,   Waziri Mkuu wa Rwanda Bw. Pierre Damien, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar  pamoja na Watendaji wao Rais Museveni alimpongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyata kwa kujumuika pamoja katika mkutano huo baada ya kuchaguliwa kuiongoza Kenya. 

 Alisema  Wananachi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya wanastahiki kupongezwa kutokana na hatua yao ya kufanya uchaguzi Mkuu katika hali ya amani na utulivu.

Naye akiuhutubia Mkutano huo kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Rais Mpya wa Kenya Bwana Uhuru Kenyata alisema Kenya inaendelea kujivunia kuwa mwanachama wa Jumuia hiyo ya Afrika Mashariki.

Alisema Uanachama huo unasaidia kuendeleza ushirikiano wa ujirani mwema uliopo katika kuimarisha masuala ya Kiuchumi, Forodha, Usafiri wa Anga na hata ule wa Bara bara zinazounganisha Mataifa hayo wanachama.

Bwana Uhuru Kenyata aliwaahidi viongozi wa Jumuiya hiyo kwamba Nchi yake itaendelea kuwa huru kwa mwananchi yeyote wa Jumuia hiyo kuishi au kuwajibika katika shughuli za kiuchumi Nchini mwake kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“ Lengo la waasisi wa jumuiya hii  ni kuona Afrika Mashariki inakuwa moja Kiuchumi,Kibiashara, Fedha, Mawasiliano na hata Ustawi wa Jamii “. Alisisitiza Rais Uhuru Kenya.

Alieleza kwamba Wana Jumuiya ya Afrika Mashariki wana wajibu wa kufanya kazi pamoja katika kuona ushirikiano wa Jumuiya hiyo unaendelea kuwa wa kudumu milele.

Akizungumzia suala la Amani Rais Uhuru Kenyata alisema Nchi hiyo itaendelea kuunga mkono harakati za kuimarisha hali ya ulinzi  ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Bara la Afrika.

Bwana Uhuru Kenyata alieleza kuwa matatizo ya ugaidi, sambamba na masuala ya uharamia yanayoikumba pembe ya Bara la Afrika yanaweza kudhibitiwa endapo nguvu za ushirikiano wa pamoja zitadumishwa ipasavyo.

Mkutano huo wa Wakuu wa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika ya Mashariki umemteua Bwana Charles Kackson Njoroge kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Uteuzi unaotarajiwa kuanza rasmi Tarehe 9 June mwaka huu wa 2013.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Rais Kikwete aongoza maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano

Imewekwa na Nassor Khamis

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya ulinzi na Usalama Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Gwaride katika maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika leo katika viwanja vya Uhuru jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya ulinzi na Usalama Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Gwaride katika maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika leo katika viwanja vya Uhuru jijini Dar es salaam.

Na Salum Vuai, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, leo aliwaongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Sherehe hizo zilifanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wote wa kitaifa nchini, mawaziri wa Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar, viongozi wa ngazi zote na watendaji wakuu pamoja na wananchi mbalimbali.

Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Peter Pinda.

Wengine ni Marais wastaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Mawaziri Wakuu wastaafu Fredrick, Sumaye, Edward Lowasa na John Malecela, Spika wa Bunge Anne Makinda na Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho na viongozi wengine.

Pamoja na mvua ya wastani iliyokuwa ikinyesha mapema asubuhi, wananchi mbalimbali walijitokeza kwa wingi uwanjanihapo kusherehekea Muungano huo wa kihistoria ulioziunganisha nchi za Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, mwaka 1964.

Shamrashamra mbalimbali zilipamba sherehe hizo, likiwemo gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama, halaiki ya muungano wa wanafunzi kutoka Zanzibar na Bara, ngoma za asili, Sindimba kutoka mkoani Lindi, Gonga-Kusini Pemba na Nyaketari kutoka Tarime, Mara.

Aidha, kikosi cha kwaya cha JKT Msange kutoka mkoa wa Tabora, nacho kilishuka uwanjani kuhitimisha maadhimisho hayo, ambapo kilitia fora kutokana na manjonjo ya kiongozi wake aliyekuwa kivutio kikubwa uwanjani hapo.

Mapema baada ya kuwasili uwanjani hapo, Rais Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, alipigiwa mizinga 21 na kukagua vikosi vya gwaride, kabla kupokea saluti ya utii kwa Rais.

Baada ya hapo, vikosi mbalimbali vya gwaride vilipita mbele ya mgeni rasmi na waalikwa wengine, kwa mwendo wa polepole na ule wa haraka, huku vikishangiriwa kwa nguvu na wananchi waliovutiwa na ukakamavu wa wapiganaji hao.

Kwa upande wao, vijana wa halaiki walinogesha sherehe hizo kwa kuonesha sura nne za maonesho, ambayo ni ulinzi, uchumi, afya na utamaduni, na kumalizia kwa sarakasi iliyowafurahisha wageni na wananchi wote waliohudhuria sherehe hizo.

Miongoni mwa maumbo waliyotengeneza na kufurahisha umma, ni maandishi yaliyosomeka “Miaka 49 ya Muungano”, pamoja na “Tusichanganye Kiswahili na Lugha nyengine”.

Tukio jengine lililosisimua hadhira uwanjani hapo, ni maonesho ya ndege za kivita za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), zilizoruka katika anga ya uwanja huo, huku zikitoa moshi wenye ishara ya bendera ya Taifa.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliasisiwa Aprili 26, 1964 kutokana na makubaliano ya Rais wa kwanza wa Tanganyika Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyeyere, na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume.

Sherehe za mwaka huu zinabebwa na kaulimbiu isemayo, “Amani, utulivu na maendeleo ni matokeo ya muungano wetu, tuulinde na kuutunza.

 

CUF yampongeza Fatma Ferej kwa kuteuliwa kuwa mwanamke jasiri Tanzania

Imewekwa na Nassor Khamis

Prof. Lipumba na Maalim Seif wakimpongeza Fatma Ferej kwa kupewa Tunzo ya mwanamke jasiri Tanzania kwa mwaka 2013.
Prof. Lipumba na Maalim Seif wakimpongeza Fatma Ferej kwa kupewa Tunzo ya mwanamke jasiri Tanzania kwa mwaka 2013.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Mhe. Fatma Ferej hakupendelewa kupewa tunzo ya mwanamke jasiri Tanzania kwa mwaka 2013 bali amestahiki kutokana na utendaji wake.

Akizungumza katika hafla maalum ya kumpongeza Mhe. Fatma Fereji kutokana na kupewa tunzo hiyo na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania tarehe 4/3/2013, Maalim Seif amesema Fatma Ferej ni mchapa kazi wa kweli na jasiri katika kutekeleza majukumu yake.

Amesema akiwa msaidizi wake katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais , Fatma Ferej amekuwa akimsaidia kwa karibu hasa katika kufuatilia masuala ya dawa za kulevya, mazingira na maendeleo ya watu wenye ulemavu.

Pia alimsifu kutokana na busara na mashirikiano yake na watendaji wengine wa Ofisi hiyo. “Sijawahi kupokea malalamiko kuwa Mhe. Fatma anawanyanyasa wafanyakazi wake, bali siku zote namuona ni kiongozi mwenye busara na mashirikiano makubwa”, alifahamisha Maalim Seif.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema Tunzo aliyoipata Fatma Ferej imekijengea sifa kubwa chama chake cha CUF.

Prof. Lipumba alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kutowabagua watoto wao na kuwapa fursa sawa za kielimu ili waweze kujiandaa vyema kukabiliana na maisha, sambamba na kuwapa fursa wanawake waweze kushiriki shughuli za kijamii.

Nae Mhe. Fatma Ferej amesema anaichukulia tunzo hiyo kama ni changamoto ya kuzidi ari ya kiutendaji, na kuwataka wanawake wajiamini wanapotekeleza majukumu yao.

Amefahamisha kuwa wakati umefika kwa wanawake kuuthibitishia ulimwengu kuwa wanaweza, na kuondokana na mtazamo finyu kuwa kazi za wanawake ni kukaa jikoni pekee.

Hafla hiyo ya pongezi maalum iliyofanyika hoteli ya Bwawani, iliandaliwa na Jumuiya ya wanawake wa CUF.

Hassan Hamad, OMKR.

Makampuni ya Afrika Kusini kutoa fursa ya ukezaji katika miradi ya maji na umeme Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Makampuni ya Maji na Umeme { Botjheng Water na Megtron } ya Afrika Kusini pamoja Uongozi wa Wizara ya Ardhi , Makazi, Maji na Nishati aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Makampuni ya Maji na Umeme { Botjheng Water na Megtron } ya Afrika Kusini pamoja Uongozi wa Wizara ya Ardhi , Makazi, Maji na Nishati aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Uongozi wa  Makampuni yanayojishughulisha na masuala ya Maji Safi na salama ya Botjheng Water na Megatron kutoka Nchini Afrika Kusini  umeamua kutoa fursa kwa  Zanzibar  katika uwekezaji wa miradi yao ya  Maji na Umeme ili kuviwezesha Visiwa vya Zanzibar kutekeleza miradi yake ya Kiuchumi kwa ufanisi.

Mkurugenzi wa  fedha wa Kampuni ya Maji Bwana Hardus Hattingh alieleza hayo wakati ujumbe wao ulipokutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, makazi Maji na Nishati sambamba na idara zilizohusika na miradi hiyo chini ya uenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Hardus Hattingh alisema ujio wao hapa Zanzibar ni kuangalia  mahitaji halisi ya Huduma za maji pamoja na kufikiria mbinu zinazoweza kusaidia kitaalamu kupunguza tatizo hilo.

Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Maji ya Botjheng Water ya Afrika Kusini alifahamisha kwamba Kampuni yao imelenga kusaidia Mataifa yenye matatizo ya upungufu wa huduma hizo wakiangalia  zaidi Nchi za Bara la Afrika.

“ Tumefuatilia matatizo ya huduma za maji safi na salama pamoja na umeme kwenye Mataifa tofauti na kugundua kwamba tunauwezo wa kusadia kitaaluma sambamba na uwezeshaji “. Alifafanua Bwana Hardus.

Naye Mshauri wa Fedha katika Kampuni ya Umeme ya Megatron kutoka Nchi hiyo ya Afrika Kusini Bwana Johan Oelofse alieleza kwamba Taasisi yao iko tayari kuwekeza hapa Zanzibar wakati wowote kutegemea mahitaji watakayoelezwa.

Bwana Yohan alieleza kuwa Kampuni ya Megatron  iko tayari na uwezo kamili wa kuendeleza miradi ya umeme ambayo mengine imeshaanzishwa katika baadhi ya Mataifa Barani Afrika.

Nao kwa upande wao Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, makazi, Maji na Nishati Nd. Al- Khalil Mirza pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Dr. Garu walisema   matumizi ya huduma ya maji yataendelea kuongezeka  kufuatia  kutanuka kwa sekta ya uwekezaji hapa Nchini hasa katika miradi ya Utalii.

Walisema  Mamlaka ya maji inahitaji kuwa na vianzio vyengine zaidi vya maji ili huduma ya maji ifikie katika asilimia ya kiwango kinachohitajika hasa ndani ya eneo la Mji ambalo bado lina upungufu wa huduma hiyo.

“ Tunaangalia zaidi kuelekeza  mipango yetu katika kuhakikisha eneo la Mji wa Zanzibar ambalo limekabiliwa na idadi kubwa ya wakaazi wake linaondokana na upungufu huo wa huduma ya Maji safi na salama “. Alifafanua Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Dr. Garu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema juhudi za ziada zinafaa kuchukuliwa katika kuona huduma za maji safi ndani ya manispaa ya Zanzibar zinapatikana kwa kiwango kinachoridhisha.

Balozi Seif alisema Mkoa wa Mjini  Magharibi hivi sasa una idadi kubwa ya wakaazi wake inayofikia  Laki 5.9 sawa na asilimia  46% ya wakaazi wote wa Visiwa vya Zanzibar wapatao Milioni 1.3.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Ujumbe wa Makampuni hayo ya Maji na Umeme kutoka Nchini Afrika Kusini kuitumia fursa ya upungufu wa huduma hizo hapa Zanzibar katika  kuwekeza vitega uchumi vyao.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Watendaji wa ZBC watakiwa kutekeleza vyema majukumu yao

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } alipofanya ziara ya ghafla Kituoni hapo Karume House. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.)
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } alipofanya ziara ya ghafla Kituoni hapo Karume House. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.)

Matumaini ya Wananachi katika kupokea na hatimae kuangalia matangazo ya Televisheni kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } yatarejea endapo watendaji wa Shirika hilo kwa kushirikiana na Viongozi wao watajipanga vyema katika kutekeleza majukumu yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ghafla katika Kituo cha Televisheni cha Shirika hilo kilichopo Karume House kuangalia matatizo yaliyopelekea kukosekana kwa matangazo ya Habari Kituoni hapo.

Akizungumza na Uongozi wa Shirika hilo na baadae Watendaji wake Balozi Seif alisema Serikali iliamua kuunda Shirika hilo lengo likiwa ni kuimarisha zaidi matangazo yake pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya mfumo wa utendaji katika sekta ya Habari Duniani.

Balozi Seif alisisitiza kwamba wakati umefika hivi sasa   kwa Shirika hilo kuendeshwa kibiashara, na hilo litafikiwa iwapo Taasisi zinazoendelea na zile zinazotumia na kuhitaji huduma za matangazo za Shirika hilo zitalipa.

“ Sisi Serikalini tumeshaliagiza Baraza la Wawakilishi ambalo liko chini ya Wizara yangu lianze kulipa fedha wakati linapoendelea na vikao vya Baraza katika matangazo yake ya moja kwa moja. Dodoma Shirika la Utangazaji Tanzania TBC wanalipwa na Bunge wakati wanaporusha matangazo yao utaratibu ambao hata sisi wabunge tunachangia suala hilo “. Alifafanua Balozi Seif.

“ Katika kujenga mahusiano mema baina ya Taasisi hizo inaweza kuruhusiwa kutangazwa  bure wakati wa kipindi cha maswali na majibu “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akizungumzia suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaonya watendaji hao kuwepuka tabia ya fitna baina yao na Viongozi jambo ambalo linarejesha nyuma ufanisi wa kazi zao.

Alikemea kwamba Kiongozi ye yote ambae atapenda kutanguliza fitna na majungu mbele aelewe kwamba anajiingiza katika mfumo mbaya wa kazi unaosababisha kuyeyusha haki za wafanyakazi wake.

Hata hivyo Balozi Seif aliwapongeza Watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } kwa utendaji wao wa kizalengo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yao waliyopangiwa.

Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar alisema Vituo vya Matangazo ya Televisheni haviwezi kufanya kazi zake kwa mpangilio wa bajeti kama zinavyofanya Idara nyengine.

Alisema Uongozi wa Shirika hilo umekuwa akitoa Taarifa za maandishi wakati yanapotokea matatizo hasa suala kubwa la vifaa na uharibikaji wa mashine lakini ufumbuzi wake huchukuwa muda mrefu kutokana na mfumo wa matumizi uliopo.

“ Tumekuwa tukiiandikia Wizara kuijuilisha matatizo yetu yanapotokea lakini hatua zinazochukuliwa za kusubiri fedha hupelekea hata vile vifaa vya dharura vikaharibika baada ya kukosa usaidizi wa ziada “. Alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa ZBC Nd. Chande.

Hata hivyo Ndugu Chande alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Shirika hilo tayari umeshachukuwa hatua za dharura kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwasiliana na makampuni yanayotengeneza vifaa vinavyohitajika kituoni hapo kwa wakati huu wa dharura.

Alisema lengo la Shirika hilo katika mpango wake wa kuingia katika matangazo ya Kisasa ya Digital ni kuwa na mashine 10 za kurikodia vipindi zitakazotosheleza kabisa mahitaji ya vitengo vya Habari, Vipindi pamoja na Matangazo.

Kwa upande wao watendaji wa shirika hilo la Utangazaji Zanzibar wameelezea changamoto wanazopambana nazo kituoni hapo ambazo zimekuwa zikirejesha nyuma hamu na utendaji wao wa kazi za kila siku.

Walizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu usafiri wa uhakika wa kufuatilia Vipindi, Habari na hata kurejeshwa majumbani wakati wa usiku, ukosefu wa Bajeti za Vipindi, uchakavu wa Mashine za Matangazo, Haki za Wafanyakazi kama maposho na fedha za likizo pamoja na majungu na fitina baina ya Viongozi na Wafanyakazi.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Balozi Seif azindua mradi wa maji safi na salama katika kijiji cha Vuga Mkadini

Imewekwa na Nassor Khamis

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizindua mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Vuga Mkadini ndani ya Jimbo la Kitope. Nyuma ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya wananchi walioshuhudia uzinduzi huo. (Picha na Hassan Issa wa  - OMPR – ZNZ.)
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizindua mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Vuga Mkadini ndani ya Jimbo la Kitope. Nyuma ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya wananchi walioshuhudia uzinduzi huo. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.)

Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kujitahidi katika kuhakikisha huduma za Maji safi na salama ndani ya Jimbo hilo zinapatikana ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma hiyo Wananchi wake.

Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua mradi wa huduma za maji safi na salama katika kijiji cha Vuga Mkadini kilichomo ndani ya jimbo la Kitope.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Maji ni miongoni mwa huduma muhimu inayopaswa kutumiwa na kila mwanaadamu, hivyo Uongozi huo utachukuwa juhudi ya ziada katika kuona kero za upatikanaji wa huduma hiyo inakuwa ndoto ndani ya jimbo hilo.

Aliwaeleza Wananchi hao wa Kijiji cha Vuga Mkadini kwamba utaratibu mwengine utaangaliwa katika mpango wa kujenga Tangi jengine katika eneo hilo ili lisaidie kukidhi mahitaji ya maji ambayo kwa hivi sasa yanaendelea kuwa ya mgao.

Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi hao kuzingatia maagizo ya Wahandisi katika matumizi ya mashine zinazotumika katika Tangi la Kisima kilichopo Kijijini hapo ili zidumu kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.

Akitoa Taarifa ya uzinduzi wa Mradi wa maji safi na salama wa katika Kijiji hicho cha Vuga Mkadini Katibu wa Kamati ya  maendeleo ya Kijiji hicho Ndugu  Hamad Mwinyi Ramadhan alisema huduma za maji safi ilikuwa ni kilio cha muda mrefu katika kijiji chao.

Nd. Hamadi alisema juhudi za Viongozi wa Jimbo hilo kupitia Mbunge huyo katika harakati za ziada za kujituma zimesaidia kuleta maendeleo ya haraka ndani ya Jimbo  hilo.

“ Ukweli juhudi unazoendelea nazo siku hadi siku, hasa kilio chetu cha ukosefu wa Pump ya kupandisha maji na Switch Control Box zimeleta faraja na kwa kweli tunajisikia raha isiyo kifani “. Alisema Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Vuga Mkadini Nd. Hamad.

Akitoa Shukrani kwa niaba ya Wananachi wa Kijiji hicho Diwani wa Wadi ya Fujoni Nd. Hamad Khamis Hamad amempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif kupitia uratibu wa Mke wake Mama Asha Suleiman Iddi kwa kusimamia vyema maendeleo ya Wananachi wa Jimbo hilo.

Diwani Hamad alisema Wananchi wa Jimbo hilo wamekuwa wakishuhudia usimamizi wa Mbunge Kimawazo na hata uwezeshaji unaoendelea kuleta faraja na neema kwa wananchi hao.

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif tayari ameshauzindua mradi wa Maji safi na Salama wa Kijiji cha Kipandoni uliogharimu shilingi Milioni 2,300,000/-, Kisima cha Maji Mgambo kiligharimu shilingi Milioni 4,000,000/- na mradi wa Vuga Mkadini umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 6,900,000/-.

Miradi yote mitatu imegharimu zaidi ya shilingi Milioni Kumi na Tatu na Laki Mbili { 13,200,000/- }.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Mwekezaji atakiwa kutoa huduma ndani ya mwaka mmoja katika Magofu ya Bweleo

Imewekwa na Nassor Khamis

Moja ya Magofu ya Kihistoria yaliyopo Zanzibar.
Moja ya Magofu ya Kihistoria yaliyopo Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imemuagiza mwekezaji aliyepewa eneo la Magofu ya Kihistoria liliopo Bweleo Wilaya ya Magharibi kuhakikisha kwamba ameshakamilisha shughuli zake za uwekezaji na kuanza kutoka huduma kama alivyoahidi katika mkataba wake ndani ya kipindi cha Mwaka mmoja kuanzia leo.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Mwekezaji huyo Bwana Chandra, Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya watu wa Bweleo, Sheha wa Shehia ya Bweleo, Mkurugenzi Zipa pamoja na  Mkurugenzi Mazingira hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema ameridhika na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Maalum aliyoiteua kuchunguza mgogoro wa eneo hilo Tarahere 28 Oktoba mwaka 20112 kati ya Mwekezaji huyo na wananachi wa Bweleo waliyoiomba Serikali Kuu kumnyang’anya eneo hilo Mwekezaji huyo baada ya kukaa nalo kwa miaka mingi bila ya faida ya Wananchi hao.

Akifafanua baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo Maalum ya kuchunguza mgogoro wa eneo hilo  ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Mh. Abdulla Mwinyi, Balozi Seif alimtaka Mwekezaji huyo kuhakikisha kwamba mradi wake unafaidisha kimapato Wananchi wa maeneo hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema njia pekee ya kuepuka migogoro ndani ya sekta ya uwekezaji ni kwa wananchi wenyewe kuiachia Serikali kuu kutimiza waji wake kwa kutiliana saini ya mikataba na wawekezaji ili kuwepuka ujanja unaopelekea kuleta mzozo hapo baadaye.

“ Moja kati ya suala nililolishuhudia wakati wa ziara yangu mwaja jana katika eneo hilo ni lile lalamiko la wananchi hao la kuzibiwa njia wanayoitumia wakati wanapotoka katika shughuli zao za uvuvi. Hili unapaswa kulichukulia hatua mara moja kwa kushirikiana na Uongozi wa Shehia, Zipa na Mazingira “. Balozi Seif alimuagiza Mwekezaji huyo.

Hata Hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwekezaji huyo Bwana Chandra kwa hatua yake ya kusaidia maendeleo ya Wananachi wa Vijiji vinavyouzunguuka mradi huo na kumuomba asichoke kuendelea kufanya hivyo ili kujenga uhusiano mwema na Wananchi hao.

Balozi Seif aliusisitiza Uongozi wa mradi huo kuwasiliana na Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA }, Mipango Miji pamoja na Idara ya Mazingira ili kuhakikisha kwamba mradi huo unaendeshwa katika misingi iliyokubalika kutekelezwa Kisheria.

Eneo la Magufu ya Kihistoria la Bweleo limekuwa na mzozo wa muda mrefu kati ya Mwekezaji wake Bwana Chandra na Wananchi wa Vijiji vilivyolizunguuka eneo hilo wakidai Mwekezaji huyo kushindwa kuliendeleza kama ilivyokubalika.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar

Wanafunzi wa Laurete International wafanya ziara ya kimasomo “Sober Houses”

Imewekwa na Nassor Khamis

Wanafunzi wa skuli ya Laureate International wakiwa ndani  ya Sobber house ya wanawake Kwa Mchina, walikokwenda kwa ajili ya kujifunza namna na kujikinga na matumizi ya dawa za kulevya.
Wanafunzi wa skuli ya Laureate International wakiwa ndani ya Sobber house ya wanawake Kwa Mchina, walikokwenda kwa ajili ya kujifunza namna na kujikinga na matumizi ya dawa za kulevya.

Wanafunzi na walimu wa skuli ya Laurete International, wamefanya ziara ya kimasomo katika nyumba za kurekebisha tabia kwa vijana walioamua kuachana na dawa za kulevya “sober houses”, na kusema kuwa ziara hiyo imewapa uwezo mkubwa wa kuelewa athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya.

Mkuu wa kitengo cha Sekondari katika skuli hiyo, Mwalimu Moh’d Saleh alisema wamefurahishwa kwa namna wanafunzi wao walivyopokewa na kupatiwa mashirikiano, jambo lililopelekea kuweza kujifunza kwa mafanikio makubwa.

Kufuatia ziara hiyo Mwalimu Mohd ameahidi kuwa walimu na wanafunzi wa skuli hiyo watakuwa mabalozi wazuri wa kuipeleka elimu hiyo katika jamii iliyowazunguka,  ili iwe hatua muhimu ya kampeni ya kuwakinga vijana na utumiaji wa dawa za kulevya.

Wanafunzi na walimu hao walipata fursa ya kufanya majadiliano na vijana walioamua kuachana na dawa za kulevya katika nyumba ya vijana hao iliyoko Bububu pamoja na nyumba wanayoishi vijana wa kike iliyoko Kwa Mchina.

Wametoa wito kwa skuli nyengine kutembelea nyumba hizo ili kujifunza kwa vitendo juu ya sababu zilizopelekea vijana hao kujiingiza katika vitendo hivyo, ili waweze kusaidia mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Hivi karibuni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alizindua kampeni ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya maskulini, na kusema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwapa vijana wengi elimu inayohusiana na dawa za kulevya, na kufikia azma ya serikali na kutokuwepo kabisa kwa matumizi ya dawa za kulevya Zanzibar.

Hassan Hamad, OMKR

Uchaguzi mdogo Jimbo la Chambani

Imewekwa na Nassor Khamis

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jullius Mallaba.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jullius Mallaba.

UCHAGUZI NDOGO JIMBO LA CHAMBANI KUFANYIKA JUNI 16

Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Chambani, Pemba, unatarajia kufanyika Juni 16, mwaka huu.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Salum Hemed Hamis, kufariki dunia  Machi 28, mwaka huu.

Aidha, uchaguzi huo utaenda sambamba na wa madiwani katika Kata 26 za Halmashauri 21, kwa ajili ya  kujaza nafasi zilizoachwa  wazi kufuatia baadhi ya waliokuwa wanashikilia nafasi hizo kujiuzulu, kufukuzwa, kuhama vyama au kufariki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jullius  Mallaba, uteuzi wa wagombea wa kiti cha ubunge utafanyika Mei 17, mwaka huu, kwa kufuatiwa na kampeni  ambazo zitafanyika Mei 18 hadi Juni 15, mwaka huu.

Alisema uteuzi wa uchaguzi mdogo wa madiwani utafanyika  Mei 14, mwaka huu, wakati kampeni zitakuwa ni Mei 15 hadi Juni 15, mwaka huu.

Kata zitakazohusika katika uchaguzi mdogo wa Madiwani  ni Stesheni (Nachingwea), Nyampu-Lukano na Lugata (Sengerema), Genge na Tingeni (Muheza), Ibugule (Bahi), Langiro (Mbinga), Manchila (Serengeti), Iyela (Mbeya), Mbalamaziwa (Mufindi), Runzewe Mshariki (Bukombe) na Mianzini (Temeke). 

Nyingine ni Dalai (Kondoa), Minepa (Ulanga), Makuyuni(Monduli), Bashnet (Babati), Kimandolu, Elerai, Kaloleni na Themi (Arusha), Iseke (Singida), Dongobesh (Mbulu), Ng`ang`ange (Kilolo), Ifakara (Kilombero), Msanze (Kilosa)  na Mnima (Mtwara).

Salim Hemed Hamis alifariki dunia katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipolazwa siku moja baada ya kuanguka ghafla wakati akishiriki katika vikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

WANACHAMA 11 WA CUF WAWANIA UBUNGE JIMBO LA CHAMBANI

WANANCHAMA 11 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejitokeza kuwania ubunge katika jimbo la Chambani, liliko Kisiwani Pemba, kutokana na kifo cha mbunge wake, Salim Hemed Khamis.

Khamis alifariki Machi 28, mwaka huu, siku moja baada ya kuaguka ghafla wakati akihudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa hivi karibuni.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, alisema jana kuwa mpaka jana mchana wanachama hao ndio waliokuwa wamejitokeza na kusema kuwa zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo bado linaendelea.

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi, Mketo alisema bado wanaendelea kujipanga na kwamba yataanza rasmi baada ya Baraza Kuu la chama hicho litakapokaa mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kupitisha jina moja la mgombea.

“Kwa kuwa sisi ndiyo tunaotetea jimbo letu, tunaendelea na taratibu za chama kama zinavyowataka wanachama kuchukua fomu za kugombea, ili Baraza Kuu litakapokaa kuchagua mgombea mmoja na kuanza kampeni kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Juni 16 mwaka huu na kwamba kampeni zinatakiwa kuanza.

CHANZO: NIPASHE & TANZANIA DAIMA

SMZ yaiomba Uingereza kusaidia taaluma ya kuimarisha kilimo cha mwagiliaji maji Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyopo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyopo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Uingereza ina uwezo wa kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Taaluma ya kuimarisha Kilimo cha umwagiliaji Maji ambacho kimepewa msukumo zaidi.

Alisema Serikali imemua kuimarisha Kilimo hicho lengo likiwa kuongeza chakula sambamba na kuwapunguzia umaskini wananchi walio mwengi ambao ni Wakulima.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi  Dianna Melrose hapo Ofisini kwake kwenye Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema zaidi ya asilimia 70 ya Wananchi  wa Zanzibar wako Vijijini wakijishughulisha na harakati za kilimo hali iliyopelekea Serikali kujikita zaidi katika kuimarisha miundo mbinu ya kilimo ambapo umwagiliaji maji ukipewa kipau mbele.

“ Sio mbaya kwa Uingereza  ambayo ina utaalamu mkubwa katika sekta ya elimu ikasaidia Zanzibar kwa vile wananchi wengi wa Visiwa hivi wanaishi kwenye maeneo ya kilimo “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania kwamba Zanzibar pia ina nyengine kadhaa za uwekezaji ikiwemo Viwanda vya usindikizaji matunda ambapo wafanyabiashara wa Uingereza wana nafasi ya kuitumia  Fursa hiyo.

Akizungumzia suala la kukabiliana na maafa yanapotokea Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi ya kuwasiliana na washirika wa maendeleo katika kuijengea uwezo idara ya Maafa ili itekeleze vizuri majukumu yake.

Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na  Zanzibar kukumbwa na ajali za meli mbili za abiria zilizotokea katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na kusababisha maafa makubwa yaliyoleta simanzi miongoni mwa Wananchi.

Mapema Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose alisema Nchi yake itaendelea kushirikiana na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Balozi Dianna alifahamisha kwamba Mataifa hayo mawili yamekuwa yakibadilishana Taaluma katika masuala ya matumizi sahihi ya ardhi sambamba na  utawala bora ili kufanikisha dhana nzima ya demokrasia baina ya Viongozi na Wananchi.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba

Uingereza kuendeleza ushirikiano na Zanzibar

Imewekwa na Nassor Khamis

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi wa Uingereza nchini Tanzania bibi Dianna Melrose, ofisini kwake Migombani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi wa Uingereza nchini Tanzania bibi Dianna Melrose, ofisini kwake Migombani.

Uingereza imeahidi kuendeleza uhusiano wake na Zanzibar katika nyanja mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu, biashara na vita dhidi ya dawa za kulevya.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania bibi Dianna Melrose, ameeleza hayo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ofisini kwake Migombani.

Amesema daima Uingereza itakuwa ikifanya kazi kwa karibu na Zanzibar katika kuhakikisha kuwa inapiga hatua za kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kijamii.

Balozi Dianna amemueleza Maalim Seif kuwa ofisi yake itawasiliana na taasisi zinazohusika nchini Uingereza kwa lengo la kuangalia namna zinavyoweza kuisaidia Zanzibar kupata walimu wa masomo ya Sayansi, jiografia na Kiingera, ili kupunguza tatizo la wataalamu wa masomo hayo.

Pia ameahidi kuwasiliana na wataalamu wa ubalozi kuona jinsi wanavyoweza kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka katika kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na vitendo vya uharamia katika bahari ya Hindi.

Mapema Maalim Seif alimueleza balozi huyo wa Uingereza kuwa Zanzibar bado inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Kiingereza sambamba na upungufu wa wataalamu wa afya, na kuiomba nchi hiyo kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kusaidia utatuzi wa kero hizo.

Kuhusu dawa za kulevya Maalim Seif amesema serikali inaandaa utaratibu wa kuweza kuwabaini wasafirishaji wakubwa wa dawa hizo nchini ili iweze kuwachukulia hatua za kisheria.

“Ukweli ni kuwa wahusika wakuu wa dawa za kulevya ni vigumu kuweza  kuwapata wakiwa na ushahidi kamili kwa sababu wao hawabebi dawa hizo bali wanawatuma vijana kufanya kazi hiyo, lakini tunaweza kutumia utaratibu mwengine kuwabaini na kuwachukulia hatua”, alifahamisha.

Katika mpango huo pia amesema watazibainisha nchi zinazotoka dawa hizo, sambamba na kuimarisha ulinzi katika bahari kuu, ili kufikia lengo la serikali la kuifanya “Zanzibar huru bila ya matumizi ya dawa za kulevya”.

Akizungumzia kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim Seif amesema imepata mafanikio makubwa katika kujenga mazingira bora ya kiuchumi na uwekezaji, pamoja na kuendelea kwa maelewano na mashirikiano miongoni mwa wananchi.

Maalim Seif ametumia fursa hiyo kutuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo bibi Magret Thatcher.

 

Hassan Hamad (OMKR)