MASHAIRI

NIWAPE ZAWADI GANI WAZAZI BABA NA MAMA

Nasomeka Mtandaoni, kuomba zenu hekima

Swali hili ni makini, laniumiza mtima

Naitafuta yakini, nisijefanya hujuma

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Mlipo maburuhani, mliyepewa karama

Nawaomba ihsani, nisije kwenda mrama

Niipate ahueni, moyo upate tuama

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Wazazi ndio kiini, fika niliposimama

Miezi tisa tumboni, alipata tabu mama

Baba yupo mashakani, mke kuvuka salama

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Wazo lapita kichwani, niwapeleke Dodoma

Wafike kule Bungeni, wabunge kuwatazama

Wajifunze kitu gani, majibu yamenigoma

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Ufisadi “namba wani”, wafanye tuso watuma

Hadi miaka sitini, mafao kuja yachuma

Nani atatuauni, katika hii hujuma

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Niwapeleke mbugani, wanyama kuwatazama

Twiga farasi wa kusini, wanasafirishwa wima

Waziri madarakani, avuna asicholima

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Ulaya na Marekani, wafike baba na mama

Niwapandishe ndegeni, wakamuone Obama

Nimegutuka bongoni, wazo hilo sio jema

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Kuwapeleka ni shani, iliyojaa adhama

Kule Hija ibadani, ni Makkati Mukarama

Awatakase Manani, Mola wetu ni karima

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Nikiwa msikitini,dua naiomba njema

Naonyesha shukrani, kwa malezi yao mema

Kunilea kiimani, mengi yamewasakama

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Mapengo wa visiwani, wewe ni bingwa daima

Nymkomogi Bayani, kuwakilisha Mrima

Mnitoe mashakani, majibu mukiyatuma

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Hapa ndiyo kituoni, Mkutubi kadi tama

Nimeshafika mwishoni, hekima ni kusimama

Kalamu naweka chini, nimshukuru Karima

Niwape zawadi gani, wazazi baba na mama.

Leave a comment